Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 24 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 198 2019-05-09

Name

Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAWA A. GHASIA) aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa reli kutoka Mtwara – Mbambabay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma utaanza?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa awali (feasibility and preliminary design) wa ujenzi wa reli kutoka Mtwara – Mbambabay kupitia matawi ya Mchuchuma-Liganga zenye urefu wa kilometa 1,092. Mshauri Mwelekezi wa kifedha na uwekezaji (transaction advisor) tayari amepatikana, mkataba na mshauri wa uwekezaji unatarajiwa kusainiwa ifikapo Juni, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mshauri wa Uwekezaji atakuwa na jukumu la kuunadi mradi huu kwa wawekezaji mbalimbali, ikizingatiwa kuwa mradi huu unatekelezwa kwa utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP). Hii ni katika kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa reli nchini kwetu. Hivyo, baada ya kukamilika kwa utaratibu wa kumpata mwekezaji kwa njia ya PPP, ujenzi wa reli hii utaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa hata sasa tumekuwa tukipokea wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika reli hii ambapo tumekuwa tukiwaelekeza kufuata sheria na taratibu za ununuzi kwa miradi inayotekelezwa kwa mfumo wa PPP. Taratibu hizo zinawaelekeza kuandaa na kuwasilisha wazo lao (proposal) la kufanya uwekezaji kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambalo litawasilishwa katika Wizara yetu baada ya kuwa wamejiridhisha. Aidha, baada ya kuchambuliwa kwa kina na Wizara, litawasilishwa katika kitengo cha PPP kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uchambuzi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kitengo hicho, wakimaliza uchambuzi na kuridhia, mwekezaji atatakiwa naye kufanya upembuzi yakinifu wake ambao baadaye utalinganishwa na upembuzi yakinifu uliofanywa na Serikali kabla ya kukamilisha taratibu za uwekezaji.