Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 14 Sitting 7 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 79 2019-02-05

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Primary Question

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-

Je, Serikali ina mipango ipi ya muda mfupi, wa kati na mrefu ya kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika matengenezo ya miundombinu nchini baada ya ujenzi wake kukamilika?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ramo Matala Makani, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto ya matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja, Serikali ilianzisha Bodi ya Mfuko wa Barabara mwezi Julai, 2000 kwa lengo la kufanya matengenezo mbalimbali ya barabara ya kawaida, matengenezo ya muda maalum, matengenezo ya maeneo korofi na matengenezo ya madaraja. Ili kukabiliana na changamoto za matengenezo ya miundombinu ya barabara baada ya kukamilika kwa ujenzi, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya matengenezo kila mwaka kupitia Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kufanya matengenezo mbalimbali ya barabara nchini. Bajeti ya matengenezo ambayo imekuwa ikiongezeka kila mwaka inatumika kufanya matengenezo ya kawaida, matangenezo ya muda maalum, matengenezo ya maeneo korofi na matengenezo ya madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu ilivyoanzishwa Bodi ya Mfuko wa Barabara bajeti ya matengenezo imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka 2000/2001 zilitengwa Sh.44,436,708,674 na Mwaka wa Fedha 2010/2011 zilitengwa Sh.286,907,000,000 na Mwaka wa Fedha 2018/2019 zimetengwa jumla ya Sh.908,808,000,000. Mfuko huu unaimarishwa kila mwaka ili miundombinu ya barabara na madaraja iweze kutengenezwa na kupitika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inaendelea kudhibiti uzito wa magari kwa kujenga mizani na kupima uzito wa magari kwenye barabara zote za lami zilizokamilika na zinazopendelea kujengwa nchi nzima ili kuzinusuru barabara hizo kutokana na uharibifu mkubwa unaosababishwa na magari yanayozidisha uzito. Mizani inajumuisha mizani ya kudumu, mizani inayohamishika na mizani inayopima magari yakiwa kwenye mwendo, yaani Weigh in Motion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) unaendelea kufanya tafiti mbalimbali kupitia Maabara Kuu ya Vifaa vya Ujenzi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Afrika Kusini, lengo ni kubaini sababu za baadhi ya barabara hapa nchini kuharibika katika kipindi kifupi mara baada ya kukamilika. Wizara kupitia TANROADS tayari imekwishatoa mwongozo wa usanifu wa uchanganyaji wa lami, yaani Guideline for Asphalt Mix Design, unaozingatia mabadiliko ya mifumo ya miundo na vyombo vya usafiri, hali ya hewa na viwango sahihi vya vifaa vya ujenzi wa barabara. Mwongozo huu ulianza kutumika Mwezi Novemba mwaka 2018.