Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 44 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 372 2018-06-05

Name

Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Primary Question

MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja sasa ya kuziagiza rasmi Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwezesha Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kutekeleza baadhi ya majukumu yake ili walimu wapate huduma stahiki kwa wakati?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Utumishi wa Walimu ilianzishwa kwa Sheria Na. 25 ya mwaka 2015 ili kuwahudumia walimu wa shule za msingi na sekondari za umma Tanzania Bara. Aidha, Tume ya Walimu ina fungu lake (Fungu 2) linalojitegemea na watumishi wake kupitia wasimamizi wao huripoti moja kwa moja kwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Makao Makuu ya Tume. Hivyo Mamlaka za Serikali za Mitaa hazina bajeti za kuwawezesha uendeshaji wa siku kwa siku wa kazi za TSC zilizoainishwa na sheria kwa kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ziko chini ya mafungu mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Bunge limeiidhinishia Tume ya Utumishi wa Walimu jumla ya shilingi bilioni 12.515; kati ya hizo shilingi bilioni 4.622 ni matumizi mengineyo ili tume ipate vitendea kazi kama magari, samani za ofisi na pia kugharamia vikao vya mashauri ya nidhamu na rufaa. Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu wa Tume, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimewapatia Makatibu Wasaidizi wa Tume katika Wilaya zote nchini Ofisi na baadhi ya vitendea kazi. Serikali itaendelea kuiimarisha Tume ya Utumishi wa Walimu ikiwemo kutatua changamoto za kiutendaji ndani ya wigo wake wa kisheria ili itekeleze majukumu yake vizuri zaidi.