Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 12 Sitting 7 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 83 2018-09-12

Name

Hassanali Mohamedali Ibrahim

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiembesamaki

Primary Question

MHE. KANALI MST. MASOUD ALI KHAMIS (K.n.y. MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI) aliuliza:-
Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na tatizo la ombaomba wengi na katika baadhi ya maeneo wamejenga miundombinu ya kulala.
Je, ni lini Serikali itachukua hatua ya kuwaondoa
ombaomba katika Jiji la Dar es Salaam?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ibrahim Mohamedali Raza, Mbunge wa Kiembesamaki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wapo ombaomba katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar-es-Salaam kwa sababu vipo vivutio vingi ikiwemo watu wenye imani mbalimbali ambao huwapatia fedha na vitu vingine kama sehemu ya ibada. Kuzagaa kwa ombaomba kimekuwa chanzo kimojawapo cha uchafuzi wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za ombaomba mara kadhaa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam imetekeleza hatua mbalimbali za kuwaondoa, ikiwemo kuwakamata na kuwasafirisha makwao, lakini wamekuwa wakirudi. Mfano mwezi Septemba, 2013 ombaomba 253 na watoto 135 walirejeshwa kwao ambapo watoto 33 walirejeshwa shuleni. Hii inathibitisha kuwa wapo watu wazima wanaotumia watoto kuombaomba. Watanzania wanatakiwa kuzitumia fursa za kupambana na umaskini zilizoandaliwa na Serikali, ikiwemo elimu msingi bila malipo, huduma za afya vijijini na uwepo wa Sheria ya Fedha 2018 inayotoa fursa kwa makundi mbalimbali ya uzalishaji mali kupata mikopo, wakiwemo walemavu. Vilevile watumie uwepo wa ardhi ya kutosha yenye rutuba kama fursa ya kuweza kujitegemea na hivyo, kujikomboa dhidi ya kuombaomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ombaomba wamekuwa wakisababisha watoto wengi kutopata fursa ya kusoma shule au kuwa watoro, nawaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri chini ya usimamizi wa Wakuu wa Mikoa kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama kuwakamata wototo wote ambao badala ya kwenda shuleni huzagaa mitaani wakiombaomba, wakamatwe pamoja na wazazi wao na washtakiwe Mahakamani chini ya Sheria ya Elimu ya mwaka 78 inayokataza utoro na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Kifungu cha 166, 167 na 169A vinavyohusu wajibu wa wazazi na walezi kwa watoto. Aidha, Mabaraza ya Madiwani nayo yanaweza kutunga Sheria Ndogo za kuzuia utoro pamoja na kudhibiti mienendo ya baadhi ya watu kuombaomba.