Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 33 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 285 2018-05-21

Name

Saed Ahmed Kubenea

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Ubungo

Primary Question

MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-
Serikali katika Bunge la Kumi iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ambayo ilidhihirika kuwa na upungufu na baadhi ya wadau waliona kuwa kama sheria ikipita inaweza kuifanya nchi kuwa adui wa matumizi ya mtandao wa teknolojia ya habari na mawasiliano na sheria hiyo sasa inawaathiri watumiaji wa mitandao, kompyuta, simu za mikononi, saa, televisheni na vifaa vingine vinavyofanana na hivyo:-
Je, ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa kuifanyia Marekebisho Sheria hiyo inayobana uhuru wa mwananchi wa kupata habari?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na marekebisho madogo kwenye jibu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Makosa ya Mtandao Na. 14 ya Mwaka 2015 ni sheria adhibu kwa maana ya penal law ambayo inaainisha makosa na adhabu dhidi ya uhalifu unaotendeka mtandaoni. Sheria hii imeanisha makosa yanayotokana na matumizi mabaya ya mitandao na adhabu zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa sheria hii una manufaa makubwa kwani imesababisha kupungua kwa makosa ya mtandao, upatikanaji wa haki pale mtu anapotenda kosa, kwani kabla ya hapo kulikuwa na changamoto katika uainishaji wa makosa na adhabu hali iliyopelekea haki kutopatikana. Pia uwepo wa sheria hii umewezesha kuimarika kwa matumizi salama ya mtandao kama vile, Serikali Mtandao, Elimu Mtandao, Biashara Mtandao na hivyo kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii ni muhimu sana katika nchi yetu na badala ya kuwaathiri watumiaji au wananchi, imesaidia kupunguza uhalifu wa mitandao, kwani wananchi wameanza kujua na kuelewa faida na hasara ya kutumia mitandao. Mfano, wahalifu wanaoiba fedha kwa njia ya mtandao wanashughulikiwa na sheria hii na haki kupatikana tofauti na ilivyokuwa hapo awali, kwani wananchi wengi walikuwa wakipoteza haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za hali ya uhalifu kuanzia Januari hadi Desemba, 2017 iliyotolewa na Jeshi la Polisi inaonesha kuwa uhalifu kwa kipindi hicho ni matukio 4,824 yaliyoripotiwa, ukilinganisha na matukio 9,441 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2016 ambapo ni sawa na upungufu wa asilimia 48.9. Hivyo kwa sasa Serikali haina mpango wa kuleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria hii hadi hapo kutakapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kuwahimiza wananchi kutumia fursa chanya zinazotokana na matumizi sahihi ya mtandao kuliko kutumia mitandao kwa ajili ya kufanya mambo ambayo ni kinyume na sheria za nchi na tamaduni za Kitanzania.