Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 30 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Mifugo na Uvuvi 258 2018-05-16

Name

Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Primary Question

MHE. ALLY S. UGANDO (K.n.y. MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA) aliuliza:-
Wananchi wa Kata za Mwaseni, Mloka, Ngoroko na Kipungila Wilayani Rufiji waliruhusiwa kuingia ndani ya Hifadhi ya Selous na kuvua samaki na hivyo kuinuka kiuchumi. Baada ya marekebisho ya mipaka ya hifadhi wamezuiwa kuingia kwenye hifadhi na wakati mwingine wanatendewa vitendo kinyume na sheria.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani kusaidia wananchi wa maeneo hayo ili waweze kupata kipato?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani kurejesha amani kati ya vijiji vinavyozunguka maeneo ya mipaka ya hifadhi na watumishi wa hifadhi?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 1990 Pori la Akiba la Selous lilianzisha Mpango wa Ushirikishwaji Jamii zinazozunguka pori hilo katika uhifadhi chini ya mradi ulioitwa Selous Conservation Programme (SCP). Katika kutekeleza mpango huo, wananchi wa jirani waliruhusiwa kuvua samaki ndani ya Pori la Akiba la Selous kwa ajili ya kitoweo baada ya kuombwa na wananchi wa Vijiji vya Kata za Mwaseni na Ngorongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kibali hicho kilisitishwa baada ya kuwepo ukiukwaji wa masharti yaliyotolewa ambapo baadhi ya wanavijiji waliingia ndani ya hifadhi bila kujisajili au kujiandikisha na kuvua samaki kwa ajili ya kufanya biashara kinyume na kusudio la kibali hicho. Aidha, baadhi ya wanavijiji walitumia fursa hiyo kufanya ujangili ndani ya pori kwa kuingia na silaha walizoficha ndani ya mitumbwi yao na kuua tembo, faru na wanyamapori wengine. Kutokana na sababu hizi, Serikali haina mpango wa kuruhusu uvuvi katika Pori la Akiba Selous. Nashauri Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na Serikali kuelimisha wananchi kuvua katika mabwawa yaliyo nje ya hifadhi pamoja na kuhamasisha ufugaji wa samaki kibiashara ili kujipatia kitoweo na kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuimarisha mahusiano mema kati ya wahifadhi na jamii inayozunguka maeneo yanayohifadhiwa itaendelea kuhakikisha inatoa elimu kwa jamii na kushirikiana nayo kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo.