Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 5 Water and Irrigation Maji na Umwagiliaji 42 2018-04-09

Name

Ajali Rashid Akibar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. AJALI R. AKBAR) aliuliza:-
Je, nini hatma ya Mradi wa Maji wa Makondeko?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ajali Rashid Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeandaa mpango madhubuti katika kuhakikisha inaboresha huduma ya maji kwa wananchi wanaohudumiwa na Mradi wa Maji wa Kitaifa wa Makonde. Katika kufikia lengo hilo, Wizara inatekeleza mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza kazi za muda mfupi, Wizara imefanya ununuzi wa mabomba ya urefu wa kilometa 24 kwa ajili ya kukarabati baadhi ya maeneo yaliyochakaa sana yenye kipenyo cha inchi mbili hadi sita, kwa maeneo ya Makote hadi Nanguruwe, Nanda hadi Kitangali, Chihangu hadi Mnyambe, Ghana Juu hadi Lukokoda na Mahuta hadi Nanywila. Aidha, ununuzi wa pampu kumi umefanyika ambazo zitafungwa katika vyanzo vitano vya kuzalisha na kusambaza maji. Matayarisho ya ulazaji wa mabomba na ufungaji wa pampu yanaendelea.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda wa kati Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo (CRIDIF) kutoka Afrika ya Kusini wametekeleza ukarabati wa visima sita ambavyo vimeongeza uzalishaji wa maji kutoka lita miloni 6.72 hadi lita milioni 11.88 kwa siku katika chanzo cha Mitema.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa CRIDIF wanaendelea na upembuzi yakinifu kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ambayo itahusu ununuzi na ujenzi wa bomba kuu kutoka chanzo cha Mitema kwenda Nanda la urefu wa kilometa
8.56 lenye kipenyo cha inchi 12; ujenzi wa mtandao wa usambazaji kutoka Nanda kwenda Kijiji cha Mtopwa na ukarabati na ujenzi wa matanki ya maji katika Vijiji vya Mtopwa, Nanywila na Mtavala.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa muda mrefu, Serikali imepanga kutumia kiasi cha dola za Kimarekani milioni 84 kutoka mkopo wa masharti nafuu wa Serikali ya India ambazo zitatumika kufanya ukarabati wa mradi mzima. Kwa sasa majadiliano kwa ajili ya kusaini mkataba wa kifedha yanaendeea kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya India.