Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 7 Sitting 55 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 458 2017-06-28

Name

Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Kumekuwa na Maswali yaliyokosa majibu stahiki kila mara kuhusu suala la mabaki ya mjusi (Dinosaur) yaliyopo Ujerumani, kila linapoulizwa au kuchangiwa hapa Bungeni:-
(a) Je, ni nini kauli ya mwisho ya Serikali kuhusu faida ambayo wananchi wa Mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla watanufaika kutokana na mabaki hayo?
(b) Je, kwa nini Serikali isishauriane na Serikali ya Ujerumani kuboresha barabara na huduma za maji katika Kijiji cha Manyangara katika Kitongoji cha Namapwiya, ambapo mabaki ya mjusi huyo yalichukuliwa?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maswali kuhusu mijusi mikubwa (Dinosaria) iliyochimbuliwa katika Kilima cha Tendaguru, Mkoani Lindi, nchini Tanzania kati ya mwaka 1909 hadi mwaka 1913 na kupelekwa katika Makumbusho ya Elimu Viumbe ya Berlin, nchini Ujerumani, yamejibiwa kwa miaka mingi na wakati tofauti Bungeni ambapo Serikali imekuwa ikitoa ufafanuzi uliokidhi haja katika mazingira yaliyokuwepo wakati maswali hayo yanajibiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika siku za hivi karibuni Wizara yangu imefuatilia suala hili kwa umakini mkubwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kujiridhisha kama ifuatavyo:-
(a) Wazo la kuwarudisha dinosaria nchini halina tija kutokana na changamoto za kiteknolojia na gharama, ikilinganishwa na faida za kuchukua hatua hiyo.
(b) Tanzania iendelee kusisitiza kupata manufaa kutokana na uwepo wa dinosaria wake huko Berlin, Ujerumani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia majadiliano bya kina yaliyohusisha pia wataalam waliobobea katika masuala ya malikale kutoka pande zote mbili, imekubalika kama ifuatavyo:-
i. Serikali ya Ujerumani itendesha shughuli za utafiti zaidi huko Tendaguru na katika maeneo jirani, ili kuwezesha uchimbuaji wa mabaki ya dinosaurian wengine yanayoaminika kuwepo katika maeneo hayo.
ii. Serikali ya Ujerumani itawezesha kuanzishwa kwa kituo cha makumbusho, ili shughuli za utalii zifanyike katika eneo hilo na kuvutia watalii kutoka nchini na nje ya nchi.
iii. Serikali ya Ujerumani itafadhili zoezi la uimarishaji idara inayohusika na malikale katika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam na kuwezesha upatikanaji wa watalaam wa kutosha wa fani husika, ili kuendeleza utalii wa malikale nchini. Hivyo, uboreshaji wa barabara na miradi ya maji anaouzungumzia Mheshimiwa Mbunge utakuwa sehemu ya mafanikio ya shughuli za utalii katika eneo linalozungumziwa.