Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 8 Youth, Disabled, Labor and Employment Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu 63 2016-04-29

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA IKUPA ALEX aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko la ombaomba au utegemezi kwa watu wenye ulemavu nchini:-
Je, ni kwa nini Serikali isiwawezeshe kiuchumi watu wenye ulemavu kwa kuwapa upendeleo wa zabuni za kazi mbalimbali, kama vile kuzoa takataka, usafi wa vyoo, ushonaji na kadhalika kwenye Halmashauri?

Name

Dr. Abdallah Saleh Possi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali namba 61 la Mheshimiwa Stella Alex, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua haki za watu wenye ulemavu kufanya kazi kwa misingi sawa na wengine, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kiuchumi, fursa za ajira na kuwaandalia mazingira wezeshi. Serikali pia inatambua uwepo wa watu wenye ulemavu waliojiajiri wenyewe kupitia makampuni au vikundi mbalimbali ambao wanahitaji kuungwa mkono ili kupambana na utegemezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha upatikanaji wa fursa sawa kwa watu wenye ulemavu katika fursa mbalimbali, zikiwemo fursa za ajira na za kiuchumi, Serikali itaendeleza kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sheria Namba Tisa (9) ya Mwaka 2010 inayoelekeza hatua za makusudi za msingi na wajibu wa kutambua haki za watu wenye ulemavu. Kifungu 34(2) cha Sheria tajwa kinaipa nguvu Serikali kuchagiza upatikanaji wa fursa za ajira kwa watu wenye ulemavu kwa kufuata utaratibu wa kutoa kipaumbele maalum (affirmative action).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu wa pekee Serikali inawasisitiza Watendaji wote kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha tatu (3) cha Sheria Namba Tisa (9) ya Mwaka 2010, maana ya neno kubagua inajumuisha, kukataa bila sababu maalum kutoa kipaumbele maalum kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudie, kwa mujibu wa Kifungu cha tatu (3) cha Sheria Namba Tisa (9) ya Mwaka 2010, maana ya neno kubagua inajumuisha, kukataa bila sababu yoyote kutoa kipaumbele maalum kwa watu wenye ulemavu. Hivyo basi, Watendaji wa Serikali wanawajibika kutoa kipaumbele maalum kwa watu wenye ulemavu katika masuala na fursa mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 58(2) imeelekeza kutengea asilimia 30 ya tenda zote za utoaji huduma kwenye Halmashauri zote nchini kwa makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu.