Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 2 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 15 2018-04-04

Name

Mattar Ali Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Primary Question

MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Usafiri wa kutumia bandari ni usafiri muhimu sana na ni wa lazima kwa watu wanaotoka Tanzania Bara kwenda Unguja na Pemba; na zipo kampuni zinazotoa huduma ya usafirishaji lakini hazitoshelezi katika kutoa huduma hiyo muhimu.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kununua meli ili kukidhi mahitaji ya usafirishaji wa watu wetu?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba usafiri wa kutumia bandari ni usafiri muhimu sana na hutumiwa na watu wengi wanaoishi maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi hususan wanaotoka Tanzania Bara kwenda Unguja na Pemba. Ni kweli pia kampuni zinazotoa huduma ya usafirishaji katika maeneo hayo hazitoshelezi katika kutoa huduma hiyo muhimu kulingana na uhitaji wa abiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa mahitaji ya huduma za usafiri wa majini katika maeneo hayo kwetu ni fursa kwa sekta binafsi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kulitambua hilo Serikali imekuwa ikijenga mazingira wezeshi na kuihamasisha sekta binafsi kutoa huduma za usafiri kwa kutumia meli za kisasa kati ya wasafiri wanaotoka Tanzania Bara au kwingineko kwenda visiwa vya Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla juhudi za Serikali zimekuwa zikilenga katika kuhakikisha kuwa wakazi wa maeneo ya mwambao na visiwa vya Unguja na Pemba wanapata huduma za usafiri kwa njia ya maji zilizo salama na hivyo kuwaepusha kutumia vyombo vya usafiri huo visivyokidhi matakwa katika kubeba abiria na mizigo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhamasishaji huo, kwa sasa kampuni ya meli ya Azam ilianza kutoa huduma ya usafiri baina ya Tanga, Unguja na Pemba kuanzia tarehe 29 Januari, 2017 kwa kutumia meli ya kisasa iitwayo Azam Sealink 2. Meli hii inatoa huduma kutokea Tanga kuelekea visiwa vya Unguja na Pemba mara moja kwa wiki. Aidha, kampuni hiyo iko tayari kuongeza safari baina ya Tanga, Unguja na Pemba kwa wiki mara itakapobainika kuwa abiria wanaosafiri katika maeneo hayo wameogezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaipongeza Kampuni ya Meli ya Azam kwa kuitikia wito wa kuanzisha huduma ya usafiri kwa njia ya maji baina ya Tanga, Unguja na Pemba na kuwataka wananchi kuepuka kutumia vyombo vya usafiri wa maji visivyokidhi matakwa katika kubeba abiria na mizigo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kutumia nafasi hii kuendelea kutoa wito kwa wawekezaji wengine kama ilivyo kwa Kampuni ya Meli ya Azam kuwekeza katika vyombo vya kisasa vya usafiri kwa njia ya maji ili kutoa huduma ya usafiri katika maeneo ya mwambao ya Tanzania ikiwamo na Visiwa vya Unguja na Pemba. (Makofi)