Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 8 Sitting 6 Water and Irrigation Maji na Umwagiliaji 79 2017-09-12

Name

Dr. Jasson Samson Rweikiza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Vijijini

Primary Question

MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Kuna mradi mkubwa wa maji wa siku nyingi pale Maruku (Kyolelo) ambao miundombinu yake mikubwa kama matanki, mabomba chini ya ardhi na vyanzo vyake ni vizuri lakini kutokana na uchakavu mradi huo hautoi maji; mradi huo ulikuwa ukihudumia vijiji vitano katika Kata za Kanyangeneko na Maruku; kukarabati miundombinu iliyochakaa inaweza kugharimu kiasi kidogo cha fedha kama shilingi milioni 500 kwa kuhudumia vijiji vitano wakati mradi mmoja kwa kijiji kimoja wa miradi inayoendelea unagharimu zaidi ya shilingi milioni 800.
Je, Serikali haioni ni busara kuukarabati mradi huu haraka?

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi wa Maji wa Maruku- Kanyangereko ni miongoni mwa miradi iliyoanza kujengwa baada ya Tanzania Bara kupata Uhuru mwaka 1961. Mradi ulijengwa na ulikamilika mwaka 1977 na kuanza kutoa huduma. Mradi huu ulikuwa ukiendeshwa na Serikali chini ya usimamizi wa Idara ya Maji ngazi ya Mkoa. Hadi kufikia mwaka 1983, mradi ulikuwa unafanya kazi lakini ulisimama kwasababu ya wananchi kutochangia fedha za uendeshaji na matengenezo ikiwa ni pamoja na kuhujumiwa kwa miundomibu ya mradi. Aidha, wananchi hawakupewa elimu ya kutosha ya kutambua kuwa mradi huo ni wa kwao na wanatakiwa kuutunza.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri imewasilisha maombi Wizarani ya kukarabati mradi huu kupitia miradi ya maji iliyoko kando kando ya Ziwa Victoria itakayofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la maendeleo ya JICA.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba imepanga kutekeleza mradi huu kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II) na inatarajiwa kuwa mradi huu utaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.278 kimetengwa kwa ajili ya Halmashauri ya Bukoba. Ukarabati wa mradi huo utatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha.