Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 5 Sitting 4 Water and Irrigation Maji na Umwagiliaji 46 2016-11-04

Name

Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Primary Question

MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Manispaa ya Kigoma-Ujiji unaogharimu shilingi bilioni 32 ambao unafadhiliwa na Shirika la KFW la Ujerumani na Jumuiya ya Ulaya ulipangwa kukamilika mwezi Machi, 2015:-
(a) Je, kwa nini mradi huo umechelewa kukamilika kwa mujibu wa mkataba?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani dhidi ya Mkandarasi kwa kuchelewa kukamilisha mradi huo?

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa Manispaa ya Kigoma unaogharamiwa na Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya KFW kwa gharama ya Euro milioni 16.32 sawa na shilingi bilioni 39.13.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mradi huu unaotekelezwa na Mkandarasi Spencon Services Limited ulianza mwezi Machi, 2013 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2015. Hata hivyo, baada tu ya kuanza kwa ujenzi Mkandarasi alichelewa kupewa eneo la ujenzi kutokana na matatizo ya fidia. Hali hii ilisababisha Mkandarasi kupewa nyongeza ya muda wa kazi hadi kufikia mwezi Disemba, mwaka 2015. Pia, kubadilika kwa Menejimenti ya Spencon Services Limited na mtaji mdogo kifedha kumechangia kuchelewa kwa ukamilishaji wa mradi wa maji ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba, 2016 utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia wastani wa asilimia 66.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia masharti ya mkataba Serikali imechukua hatua dhidi ya Mkandarasi ikiwa ni pamoja na kumkata fedha (Liquidated Damages) ya Euro 1,632,315.27 sawa na shilingi bilioni 3.9 ambayo ni asilimia 10 ya mkataba kuanzia mwezi Januari, 2016. Vilevile Mkandarasi ameagizwa kuongeza nguvu kazi, vifaa na pia kufanya kazi muda wa ziada zikiwemo siku za mapumziko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Mkandarasi ameandikiwa barua ya kumfahamisha kuwa Wizara imemweka katika kundi la Non Performing Contractors, (Makandarasi wasioweza kufanya kazi) na Mamlaka zinazohusika za PPRA na CRB zimejulishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, miundombinu ya msingi kama matenki amekwishajenga, pampu zote ameleta, wananchi wa Kigoma Mjini wataanza kupata maji kuanzia mwezi Aprili, 2017.