Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 5 Sitting 2 Good Governance Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu 16 2016-11-02

Name

Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Primary Question

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:-
Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi matukio ya majanga na maafa kama mvua za mawe pamoja na matetemeko ya ardhi yameanza kutokea mara kwa mara na mara zote Serikali imekuwa haina maandalizi ya kifedha na vifaa vya kusaidia wahanga kwa muda mfupi na muda mrefu na badala yake imekuwa ikitegemea zaidi wasamaria wema wa Mataifa mengine:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali imekuwa haisaidii kifedha na vifaa zaidi ya kuhamasisha wasamaria wema wasaidie na wenyewe kubaki na jukumu la kupeleka wataalam kama Madaktari na kuratibu misaada pekee?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isianzishe Mfuko wa Maafa Kitaifa ambao utakuwa unachangiwa wakati wote kwa njia endelevu?

Name

Dr. Abdallah Saleh Possi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali inatambua kuwa ni wajibu wake kusaidia wananchi pindi wanapokumbwa na maafa yanayoharibu mfumo wa maisha ya kila siku. Katika kutekeleza wajibu huo Serikali imekuwa ikitoa misaada ya aina mbalimbali kwa waathirika wa maafa ikiwemo vyakula, malazi, vifaa vya kibinadamu na huduma za afya.
Vilevile Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kununua mahitaji ya dharura ya kibinadamu pamoja na kurejesha miundombinu iliyoharibika. Aidha, katika jitihada za kuhakikisha kuwa misaada inawafikia wananchi kwa haraka Serikali tayari ina maghala ya maafa yenye vifaa mbalimbali vya kukabiliana na maafa katika Kanda sita nchini.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema ifahamike kuwa suala la kukabiliana na maafa ni mtambuka na haliwezi kuachwa mikononi mwa Serikali peke yake kwani wakati mwingine maafa yanakuwa ni makubwa sana hivyo kuhitaji juhudi za pamoja baina ya Serikali, wadau wa maendeleo na wananchi katika kuyakabili na kurejesha hali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo Serikali ilileta Muswada wa Sheria ya Maafa uliopitishwa na Bunge lako Tukufu na kuwa Sheria Namba 7 ya mwaka 2015 ambayo pamoja na mambo mengine inaelekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Maafa na pia, Kifungu 31 kinaainisha vyanzo vya mapato vya Mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa wadau wa maendeleo pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Serikali katika harakati zake za kujiandaa, kukabili na kurejesha hali, ili kuhakikisha jamii yetu inakuwa salama zaidi dhidi ya majanga mbalimbali.