Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Regina Ndege Qwaray (1 total)

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa kuna uhitaji mkubwa wa elimu ya mafunzo ya ufundistadi hapa nchini ni nini commitment ya Serikali katika kuhakikisha inaongeza msukumo wa pekee ili vijana wengi wa kike na wa kiume kupata elimu hiyo hususan katika Mkoa wetu wa Manyara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Regina, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Manyara peke yake VETA ina vyuo vifuatavyo: tuna Chuo hiki cha Mkoa cha Manyara, tuna Chuo cha Ufundi Simanjiro, vile vile tuna Chuo cha Ufundi Babati kilichopo Babati Vijijini ambacho kinaitwa Gorowa. Vile vile tunafanya upanuzi katika Chuo cha Wananchi cha Tango ambacho baada ya upanuzi huo zaidi ya wanafunzi 228 wanaweza wakapata udahili. Katika vyuo hivi vyote nilivyovitaja ambavyo viko katika Mkoa wa Manyara jumla ya wanafunzi 1,000 ambao wanaweza kuchukua kozi za muda mrefu na muda mfupi wanaweza wakapatiwa mafunzo katika maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali vile vile kupitia bajeti yake ya mwaka 2019/2020, imepeleka fedha jumla ya shilingi bilioni 48.6 kwa ajili ya kujenga vyuo mbalimbali vya VETA nchini kwa lengo la kuhakikisha kwamba elimu hii ya ufundi inawafikia wananchi wengi na vijana wengi kwa lengo la kupeleka Serikali au nchi yetu katika uchumi wa kati. Ahsante.