Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na naunga na wenzangu wote….

SPIKA: Kwa wale wengine wasiomfahamu huyu ndio Mbunge wa Kigoma Mjini eeeh! Si mnaelewa.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, naungana na wenzangu waliotangulia kuutambua utukufu wa Mungu katika kutuweka hapa, naungana pia na wenzangu kukishukuru Chama cha Mapinduzi na wapiga kura wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mjadala unaohusu hotuba ya Rais wetu ni mjadala wenye kusudio kubwa moja la kutafsiri dira hii aliyoitoa Rais wetu katika utekelezaji wa kazi za Serikali na Taifa kwa ujumla. Kama ulivyosikia wazungumzaji waliotangulia na wengine hakuna anayekosoa wala kupinga, maana yake wote tunaikubali kwamba hii ni dira ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimepata bahati kuanza kazi za uongozi wa siasa toka kipindi cha mwisho cha Mwalimu alipokuwa anamalizia nafasi yake ya uongozi.

Kwa hiyo, nimepata nafasi ya kujifunza kutoka kwa Mwalimu, kwa Mzee Mwinyi, Hayati Mzee Mkapa na Mzee wetu Jakaya Mrisho Kikwete. Kwa hiyo, wazee wote hawa kwa kweli walikuwa na vipawa mbalimbali ambavyo vimelifikisha Taifa letu mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme juu ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, huyu mtu amepewa uthubutu wa aina yake haogopi, hakuna mtu alifikiri kwamba unaweza ukawa Rais usiende nje kupiga magoti kwa wakubwa hawa halafu ukaongoza nchi vizuri, lakini ametufikisha hapo na sasa tunaamini unaweza ukaongoza Taifa la Tanzania bila kwenda kupiga magoti huko nje na shughuli zikaenda. Ni Rais ambaye amekuwa na uwezo mkubwa wa kutafsiri nadharia katika vitendo katika muda mfupi, anaamua jambo hili lifanyike na muda mfupi wananchi wanaona jambo limefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatuna jambo kubwa katika haya tunayozungumza zaidi ya kuonesha kwamba hotuba yake ni dira kwa Taifa letu. Katika kipindi cha miaka ya 1990, Chama chetu cha Mapinduzi kilijikita katika sera ya kutaka kulitoa Taifa letu kuwa Taifa lenye uchumi tegemezi na kulileta kwenye uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea. Tumekwenda hivyo katika kipindi chote, lakini sasa tunauona mwanga, mwanga huu tunauona hapa tulipofikia kwenye hatua ya kuwa kwenye uchumi wa kati kwenye kipindi kifupi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachokusudia kusema hapa ni kwamba sekta ya viwanda ambayo sasa imetupiga tafu (imesaidia) kubwa ni lazima tuiongezee kasi na katika kuiongezea kasi ni kuiongezea kasi katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji, wenzangu wengi wameshalieleza. Lakini niseme kwa upande wa Mkoa wetu wa Kigoma, sisi tunaweza tukasaidia sana Taifa letu kuondokana na fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje na Serikali imeanza na Waziri Mkuu huyu Mheshimiwa Kassim Majaliwa amekuwa ndio askari wa mstari wa mbele wa kuhakikisha zao la michikichi linalimwa, linakuzwa na ikiwezekana linavunwa na kusaidia kuondokana na tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto tuliyonayo, kulima ni mchakato mrefu, na mabenki yetu mengi si rafiki kwa mkulima, miaka mitatu ya kutunza mchikichi mpaka uanze kuzaa ni changamoto kwa wakulima wetu. Kwa hiyo, Serikali iangalie uwezekano wa kutumia fedha, mfuko sijui wa kilimo kwanza kuwapa kama ruzuku wale wakulima ili waweze kusaidia kulima na tuweze kuondokana na tatizo la kuagiza mafuta kutoka nje. Mafuta ambayo siyo tu ni gharama, lakini ni hatari kwa maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka niliseme ni lile ambalo Mheshimiwa Rais amelisema katika ukurasa wa 27 wa hotuba yake nalo linahusu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nimesikia kengele naunga mkono hoja mengine tutachangia katika mpango ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii, lakini niseme kidogo sisi Wabunge ambao tumeingia kwa mara ya kwanza tunatumia njia mbili hapa kujifunza namna shughuli za Bunge zinavyoendeshwa. Ya kwanza ni hii ya kusoma kwenye Kanuni na nini na nyingine ni kuwaangalia wale wazoefu waliokuja hapa siku nyingi namna wanavyoendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niseme kwamba ninayo masikitiko. Wapo baadhi ya wazoefu wanachangia Mpango hapa wanasimama tangu ameanza mpaka anamaliza anakosoa tu halafu hasemi tufanyeje. Nilitaka kusema hilo kwa kweli sioni kama ni jambo jema ambalo sisi tunajifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa maono yangu mimi Serikali ya CCM na inawezekana Serikali ya nchi nyingine yoyote duniani ingependa kuwafanyia wananchi wake kila jambo wanalotaka, kinachozuia kufanya hivyo ni uwezo. Ndiyo maana tuko hapa leo kupitia mipango kuona kupanga ni kuchagua, lipi litangulie lipi lisubiri kutokana na uwezo wetu. Kama tunataka tuongeze zaidi lazima tuseme tunapataje uwezo wa kufanya zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nishauri kidogo kwenye eneo la ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP). Nimeangalia katika Mpango huu, ni miradi nane tu ambayo imewekwa katika Mpango wa PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wa kwanza ni Kiwanda cha Dawa; mwingine ni Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi; Hoteli ya Nyota Nne; Uwanja wa Mwalimu Nyerere; usambazaji wa gesi asili; Reli ya Standard Gauge Tanga – Arusha – Musoma na Mtwara – Mbambabay; Mwingine ni hosteli ya Chuo cha Biashara Kampasi za Dar es Salaam na Dodoma; na Chuo cha Uhasibu Kampasi ya Dar es Salaam na Mbeya; na wa mwisho ni mradi wa Kiwanda cha Kutengeneza Simu. Hii ndiyo miradi katika mpango mzima wa mwaka ambayo imeingia kwenye PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na PPP ndilo eneo ambalo lingeweza kutusaidia kushirikisha sekta binafsi katika kutekeleza mambo mengi ya Serikali. Kwa mfano leo hii usafiri wa Reli ya Kati kutoka Kigoma kuja Dar es Salaam, wasafiri wanaotakiwa kusafiri kila siku ya treni wanaoondoka ni asilimia 25 tu, asilimia 75 ya wasafiri wote wanabaki kwa ajili ya kukosa mabehewa. Kwa nini katika mpango huu tusingeingiza mabehewa kwenye PPP, wapo Watanzania wafanyabiashara ambao wangeweza kununua mabehewa ya treni yakafungwa. Sasa hivi injini hizi zinakokota mabehewa chini ya uwezo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda pale Stesheni ya Kigoma zaidi ya mara nne, mara tano. Injini inaondoka imefunga mabehewa nane yenye capacity ya kubeba mabehewa 30, mabehewa hakuna na mabehewa ya mizigo vilevile tatizo. Wakati mwingine yanakosekama mabehewa mpaka yanasababisha mfumuko wa bei ya saruji na bidhaa nyingine za viwandani zinazotoka Dar es Salaam kuja maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango atakapokuja hapa atueleze namna anavyoweza kuongeza wigo kwenye PPP. Naamini kabisa wapo Watanzania kama watu wanaweza wakanunua mabasi 115 wanashindwaje kununua behewa mbili, tatu au nne za treni akaingia katika utaratibu huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya afya vilevile bado tunaweza tukaingia kwenye utaratibu wa PPP. Nimeangalia sasa hivi kwenye hospitali zetu, tuna wodi za kawaida zile za msongamano na kuna wodi ambazo zimepewa grades; grade one na grade two. Wodi zile kukaa wodini siku moja acha huduma nyingine, unachajiwa kati ya shilingi 25,000 mpaka shilingi 40,000. Hiki ni kiwango cha lodge za kawaida za mjini ambazo mtu anaweza akakaa. Ukiwaambia wafanyabiashara wakujengee majengo hayo kwenye hospitali, watajenga tutaigia kwenye utaratibu wa PPP…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kilumbe, naona hii kengele bwana sijui ina matatizo gani. (Kicheko)

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Ina hiyana, lakini hakuna shida. Ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nataka niseme kwamba sina kawaida sana ya kuzungumzia mambo hasa ninayoona yananitia uchungu kwa watu ninaowafahamu vizuri na hasa Wabunge wenzangu, lakini mnapofika mahala mnataka kutengeneza chombo ni lazima mkubali kwamba, kama yuko mtu anapasua mtumbwi ili mzame, basi bora azame yeye lakini chombo kiendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge tuliomo humu tumeletwa na vyama vyetu kupitia kura za wananchi, vyama vyetu vina katiba na miongozo, chama kikongwe kama CCM kina mpaka Kanuni za Maadili na Uongozi, zinazoonyesha miiko, zinazoweka makatazo na utaratibu. Kwa bahati mbaya, niseme kwa mfano Shahidi Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Gwajima, labda muda wake wa kuwepo kwenye CCM umekuwa ni mfupi sana, labda mambo haya hajapata nafasi nzuri ya kuyasoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si hilo tu, tukishachaguliwa tukifika hapa, hatuanzi kazi mpaka tubebe Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tuape kuitii, kuitetea kwa mujibu wa sheria. Katiba hiyo inayo mambo ambayo yanatutaka lazima tuyafanye kwa sababu tumeapa, unashangaa na unajiuliza na unapata shaka, hivi hawa wenzangu wanapata nafasi ya kupita hii miongozo. Kama wangefahamu vizuri nadhani tusingefika huku tulipofika. Alipoanza Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Gwajima, alianza kama anatoa ushauri hivi, akaeleza kuhusu hizo chanjo na nini, halikuwa jambo baya na wakati huo Rais wetu mpendwa alikuwa ameunda Kamati ya Wataalam kumshauri kuona namna ya kuliendea jambo la kupambana na COVID. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata kama unaamua kumshauri Rais, Katiba ulioapa nayo Ibara ya 37 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoeleza majukumu ya Rais, inaonyesha kwamba Rais yuko huru katika kazi yake, halazimiki kufuata ushauri, ukimpa anaweza akauchukua au asiuchukue na atatimiza wajibu wake. Kama Rais alikua ameshaunda Kamati ya Wataalam hana lazima ya kusikiliza ushauri wa Askofu, maana jambo lenyewe la ugonjwa ni la kitaalam.

Mheshimiwa Spika, tuache Katiba na miongozo ya chama, ndugu yetu huyu ni mtumishi wa Mungu, Askofu, imeshafika mahali jambo liko kwenye mamlaka ya Rais analishughulikia, unawezaje kufika mahali ukaanza tena kuhoji, kwenda mbele kuchochea watu, hasomi hata Biblia yenyewe inasemaje? Kwamba mtii mamlaka maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ya Kanuni, ya Katiba yamempita na ya Biblia yamempita? Si hilo tu hata sisi tunaoamini katika Uislamu imeandikwa atwiu-Allah, waatwiu rasuli wauli-l-amri minkum, kwamba tumtii Mwenyezi Mungu, tumtii Mtume na tuwatii wenye mamlaka miongoni mwetu. Huu aliouonesha mwenzetu siyo utii kwa mamlaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya, tunapokuwa hapa ni vizuri tujue viwango vyetu, umeingia siasa jana, Ubunge una miezi sijui sita au tisa, lakini hata huko kwenye Biblia, si tuyaishi maneno ya Bwana Yesu. Ukialikwa kwenye harusi usikae viti vya mbele, maana mwenye harusi anaweza akaja na watu muhimu akakupeleka nyuma, kaa viti vya nyuma ili kama yeye atakuona wa muhimu akulete mbele maana ajikwezae hushushwa na ajishushae hupandishwa na haya maneno hayajui? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa amekuja hapa Mheshimiwa Gwajima amekaa viti vya mbele, hata sisi tuliokaa siku nyingi humu kwenye chama hiki tunamwangalia, lakini basi umefika mahali umekaa viti vya mbele, unaanza tena kupiga mawe kiti cha bwana harusi na sisi tukuangalie tu haiwezekani. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge karibu wengi ambao tumekutana huko nje tunazungumza juu la tukio hili la mwenzetu, kila mmoja anasema kwa kweli huyu bwana kafanya vibaya. Sasa ukiwauliza mbona hamkemei, wanasema hapana tunaogopa, atapanda madhabahuni kwenda kutuchapa pale kutukashfu. Mheshimiwa Gwajima, Mbunge mwenzangu, mimi nimejitoa kama dhabihu, nipeleke kwenye madhabahu siku ya jumapili, nichape ujuavyo, lakini mwachie Mama Samia na Serikali yake wafanye kazi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, narudia tena nimejitoa, nikwambie kwa nia ya kukurekebisha kama Mbunge mwenzetu, twende pamoja, ukiamua kwenda kutumia jukwaa la Mungu badala ya kuongoza kondoo kuanza kuwasema watu, endelea hivyo ila ujuwe Mungu anakupa muda. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja.

SPIKA: Haya malizia.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, mimi nimechukulia wito wa mama yetu na juhudi alizozifanya Mheshimiwa Rais wetu, tena nimenukuu maisha ya Nabii Nuhu, alipoona watu wake wanatenda makosa mengi kwa Mungu na Mungu akamletea ufunuo kwamba, mimi nataka kugharikisha, alikwenda akawasihi watu wote, jamani tutengeneze safina tupande, Mungu analeta gharika kutokana na makosa tuliyofanya, sasa tujisalimishe tukae kwenye safina. Wako baadhi ya watu mpaka ya wa familia yake walimpinga. Kilichotokea gharika ilikuja na wote waliompinga waliangamia. Mama ametutaka tuchanje na akatuomba kwa hiari anayetaka achanje, asiyetaka aache, sisi tulioamua kuchanja tunasubiri safina iwe tayari, wale ambao wamekataa litakapotokea gharika ya Mungu shauri yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi kweli angekuwa Mheshimiwa hayati Magufuli ndiyo Rais leo, Mheshimiwa Gwajima angeweza kusema hayo aliyoyasema? Wakati wa mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka wa 1979, alikuwepo Mjumbe mmoja wa Halmashauri tena Mjumbe wa Kamati Kuu na alikuwa Mkuu wa Idara ya Organization, namkumbuka alikuwa mtu wa kwetu, mzee wetu, ameshatangulia mbele ya haki, Mungu amuweke mahali pema, alikua anaitwa Tuwakali Karangwe. Iliwekwa karantini ya kipindupindu alipokwenda kule Kigoma akakuta ma- barrier watu wanazuiwa wasiende huku kwa imani tu ya kutaka watu wala sio kwa kiburi, akawaambia fungueni watu waende wakapate huduma, kipindupindu kikaathiri watu wakafa, alilazimika kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu anachochea watu wasichanjwe na kushambulia wale wanaohamasisha na wanaoleta chanjo, katika CCM hii ninayoijua adhabu bado.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, nakitaka chama kiangalie vizuri adhabu hii. Ahsante sana. (Makofi)
THE FIRE AND RESCUE FORCE (AMENDMENT) ACT, 2021
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Sura ya 427 kama Muswada ulivyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri na mapendekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda niipongeze Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na pia kumpongeza Mwenyekiti na Kamati nzima ya Bunge ya Ulinzi na Usalama. Kwa kweli, jambo hili limekuwa ni jema na limekuja kwa wakati ambapo majanga ya moto yanachukua kasi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nilikuwa natazama wakati ndugu yangu Mheshimiwa Zahor anatoa ufafanuzi juu ya suala zima la kuwa jeshi kamili, maana zamani ilikuwa inajulikana kama Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, sasa ni Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri wenzetu wanaosimamia jeshi hili watazame changamoto moja kubwa ya kuitwa jeshi, tusitazame tu haja ya kuitwa jeshi. Vitendo vya matukio ya moto yanatokea halafu wanakwenda pale wakiwa hawana maji, siyo vitendo vya jeshi, ni vitendo vya kikosi. Sasa mnakwenda kwenye jeshi, ni lazima myaangalie mambo hayo. Hakuna jeshi linaweza likawa linafanya uzembe wa kiasi hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka kujielekeza katika Kifungu Namba 11(a)…

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda. Watu wengi wanashindwa kuelewa. Vyombo hivi vinapokwenda kuzima moto, vinakwenda vikiwa vimekamilika na vina maji ndani ya magari yao. Changamoto inapatikana, pressure inayotumika ku-discharge maji kwenye magari haya ni kubwa mno. Inachukua muda mchache sana maji yale kuweza kwisha na baadaye kuonekana gari imekuja bila maji. Ndiyo maana sheria hii sasa inaweka kipengele cha kulinda fire hydrants ambazo ndiyo sehemu sasa ya kuweza kupata rescue ya kuchukua maji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, siyo kwamba magari haya yanakwenda kuzima moto bila maji, hiyo, siyo kweli. Magari yanakwenda na maji na ukakamavu upo wa kutosha, tatizo yana-discharge maji kwa pressure kubwa yanakwisha upesi. Nakushukuru. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mwenyekiti nimeipokea ingawa haiendani na taarifa halisi zilizoko kwenye Umma wa Watanzania. Tunaarifiwa na vyombo vya Habari hivyo, nasi hatuendi kwenye matukio yote; na sijamsikia Mwenyekiti anasimama kupinga taarifa hizo za vyombo vya Habari. Kwa hiyo, haisaidii sana hapa Bungeni. Marekebisho haya ya sheria hayahusiani na hilo; hilo nilikuwa nimeweka tu kwamba, tunapozungumza jeshi, tutazame dhima ya jeshi badala ya ilivyokuwa kikosi.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu hasa inaanzia kwenye Kifungu cha 11(a) ambacho kimeongezwa kwenye Muswada huu ambacho kinawapa nafasi sasa Askari wa Zimamoto kutumia silaha. Katika hoja hii, kutumia kwao silaha kumeelezwa humu kwenye Muswada huu kwamba ni kwa lengo la kulinda miundombinu ya jeshi ambayo ni hayo magari, sehemu za kuhifadhia maji na maeneo mengine. Sasa lazima niseme kwamba iwe wazi au iongezwe zaidi kwamba hata kulinda mali za wananchi maeneo wanapokwenda kufanya uokoaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipengele hiki kilichoko kwenye Muswada kinazungumzia miundombinu ya jeshi. Kwamba, wanapewa silaha kwa ajili ya miundombinu ya jeshi. Nataka pale ikiwezekana waongeze, “pamoja na kulinda mali katika maeneo yanayofanyiwa shughuli za ukoaji wa moto.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo nataka nilichangie katika hili ni suala la Kifungu Namba 22 ambacho kinataka sasa majengo yote yenye urefu kutoka usawa wa ardhi kwenda juu mita 12 yanayojengwa, michoro yake ipitishwe kwenye Jeshi la Zimamoto kwa ajili ya kuzingatiwa kwa vifaa vya zimamoto katika majengo hayo. Jambo hili naona ni jema na zuri, lakini kitu kimoja tu ambacho nataka niombe, tumekuwa na tatizo la urasimu katika ofisi zetu. Kuna watu wanataka kujenga majengo haya, watapeleka zimamoto, anaambiwa acha hapa, utarudi wiki ijayo uje uchukue. Huyu mtu anatakiwa aende Mipango Miji, anatakiwa aende kwa Bwana Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mawazo yangu ambayo nataka kushauri ni kwamba, Jeshi hili la Zimamoto lihusike katika kuangalia mambo haya, lakini lihusike pale ambapo Kikao cha Kamati ya Mipango Miji kinapokaa kupitisha building permit, ndipo nao waalikwe kuhudhuria. Kwa sababu wakati mwingine kunatokea mpaka upotevu wa nyaraka. Unapeleka michoro yako ya jengo, unataka kwenda kuichukua, wanasema hiki hakionekani, hiki hakionekani kwa sababu, kimekaa muda mrefu kwenye ofisi mojawapo. Sasa wote wakutane kwenye Kikao cha Mipango Miji kinachotoa building permit watazame michoro hapo na wakubaliane au kutokukubaliana na mchoro huo wakiwa kwenye kikao cha pamoja badala ya mwananchi kuzunguka ofisi moja moja anatembeza nyaraka hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo ndio mambo ya msingi niliyoyaona.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda. Mita 12 ndiyo ghorofa tatu? Mita 12!

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Kuanzia ghorofa tatu.

SPIKA: Inafika hapo eeh! Maana tusije tukasema mita 12 halafu kumbe ni hapa karibu karibu tu.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, kwenye sheria humu wamesema mita 12, hawakusema ghorofa ngapi.