Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Abdulhafar Idrissa Juma (1 total)

MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya kuridhisha kiasi ya Naibu Waziri, lakini vitendo vya udhalilishaji na uhalifu katika Wilaya ya Magharibi “A” ambapo Jimbo langu la Mtoni lipo, lakini pia na kituo hicho cha polisi tunachokizungumzia kipo, vimekuwa vikiongezeka sana.

Sasa je, nini kauli ya Serikali katika wakati huu wa vitendo vikiongezeka na kituo kimefungwa nini kauli ya Serikali juu ya mapambano yake ama inafanya nini kuhakikisha kwamba vitendo hivi vya uhalifu na udhalilishaji unapungua?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdul-Hafar Idrissa Juma, Mbunge wa Jimbo la Mtoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimuambie Mheshimiwa Abdul kwamba nipo tayari kufuatana na yeye kwanza kwenda kukiona kituo hicho, lakini pia nipo tayari kwenda kukaa na uongozi wa Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Mjini ili lengo na madhumuni kuweza kufanya nao mazungumzo, ili ikiwezekana baada ya kujiridhisha tuone namna ambavyo tunaweza tukakifungua kituo hiki na kikaendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nipo tayari kwenda kukaa na wananchi kuweza kuwaambia maneno mazuri ambayo yatawapa imani ya kuendelea kuwa amani na salama na utulivu katika Jimbo lao. Lakini kikubwa nimuambie kwamba hili suala lake aliloliuliza la kuongezeka kwa matukio haya ya udhalilishaji katika Mkoa huu, katika Jimbo lake na katika Wilaya hii, Serikali tuna mipango mingi ambayo tumeshaanza kuifanya. Lakini kubwa nimuambie kwamba kwanza tunakwenda kuongeza nguvu kwenye masuala mazima ya ulinzi shirikishi. Ulinzi ambao unawapa nafasi wananchi wenyewe kushiriki katika ulinzi huu wa wananchi wao binafsi na hapa nataka nichukue fursa hii, nimpongeze sana Mheshimiwa Abdul-Hafar amekuwa anafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza amewatafutia kituo hawa walinzi shirikishi, lakini kubwa amewatafutia vifaa vya ulinzi kwa ajili ya kufanya doria zao. Lakini pia anafika wakati anawagawia hata posho ili lengo na madhumuni shughuli za ulinzi katika Jimbo lake ziendelee. Lakini kingine ni doria, misako na operesheni mbalimbali tunaziendesha katika Jimbo hili, ili lengo na madhumuni wananchi waishi kwa amani. Lakini kikubwa ziara za Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa tutajitahidi tuziongeze katika Jimbo hili na maeneo mengine ili lengo na madhumuni wananchi waweze kujua wajibu wao na waishi kwa ulinzi, amani na utulivu. Nashukuru.