Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ahmed Juma Ngwali (3 total)

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, fedha zilizotolewa na wahisani ni zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa kipindi cha miaka mitano; je, ni fedha kiasi gani zilizopelekwa Zanzibar na kwa miradi ipi kwa lengo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi? (Makofi)
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, kuna harufu kubwa ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha hizi za wahisani, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kuliambia Bunge hili Tukufu ni hatua gani hadi sasa zimechukuliwa na Serikali katika kukabiliana na ufisadi huo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Ngwali kwa swali lake zuri na jinsi ambavyo amebobea katika mambo ya mazingira na ndiyo maana swali lake hapa limekuwa refu sana. Kwanza katika hizo fedha shilingi bilioni 224 ambazo nimezitaja, tumepeleka Zanzibar zaidi ya sh. 17,234,056,000.80. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi ambazo tumezipeleka Zanzibar ni 7.7% ya fedha zote ambazo zilipokelewa na wafadhili, ambazo ni zaidi ya kiwango kilichowekwa cha General Budget Support cha asilimia 4.5. Kwa miradi ipi? Tumepeleka kwa miradi mingi Zanzibar.
Moja, ni mradi ule wa Kilimani ambapo tunajenga makingio, lakini na Kisiwa Panza, pia pamoja na miradi mingine ya upandaji mikoko kwenye maeneo hayo kwa maana ya Kilimani pamoja na Kisiwa Panza. Tunapanda mikoko pamoja na kujenga kuta na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ameuliza kwamba Ofisi hii imechukua hatua gani kwa ufisadi uliozungumzwa, hasa katika hotuba ya Kambi ya Upinzani wakati ule akiwasilisha hapa. Tuliahidi siku hiyo hapa Bungeni kwamba tutafuatilia tujue ukweli wa tuhuma hizi ukoje.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie kwamba tarehe 12 tulishamwagiza Chief Internal Auditor wa Ofisi yetu kufanya mapitio ya matumizi ya fedha za kuhimili mabadiliko ya tabianchi zilizotolewa kutoka muda ule wa mwaka 2010 mpaka mwaka 2015 ili kujua uhalali wa matumizi yake. Kazi hiyo imeanza na itamalizika baada ya siku 30 tu. Kwa hiyo, Bunge hili litapata taarifa nini kilichojiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama taarifa ile itakuwa imekwenda vizuri, maana yake hakuna ubadhirifu wowote, tuwapongeze watumishi wetu kwa kazi nzuri waliyoifanya, lakini kama tutagundua kwamba kuna ufisadi wa aina yoyote, nilihakikishie Bunge hili kwamba hakuna atakayepona wala atakayechomoka, tutachukua hatua kali stahili.
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa fedha za Mfuko wa Jimbo hazijawahi kukaguliwa Zanzibar na kwa kuwa hakuna utaratibu wowote kwa sababu Hazina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haiwezi kukagua Hazina ya Zanzibar.
Je, fedha za Mfuko huu wa Jimbo zitakaguliwa lini
na kwa utaratibu gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, fedha ya Mfuko wa Jimbo uko utaratibu kwamba hizi zinazoingia Bara na zile zinazoingia Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, hili kuna utaratibu wa wazi kule Ndugu yangu Mheshimiwa Ngwali nadhani tukifanya consultation na wenzetu kutoka Baraza la Wawakilishi tutakuja kuona ni jinsi gani wanafanya kule utaratibu mzima wa usimamizi wa fedha katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kwamba Baraza la Wawakilishi litakuwa linafanya kazi yake kwa mujibu wa utaratibu unaotakiwa, ili fedha hizi ziweze kutumiwa kama inavyokusudiwa. (Makofi)
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa sababu tumetoka katika siasa ya uchumi na tumeingia katika sera mpya ya demokrasia ya uchumi, naomba niuize kwamba Serikali imejipanga vipi katika kuandaa wataalam katika kuhakikisha hiyo dhana halisi ya kufikia hiyo demokrasia ya uchumi inafikiwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nauliza kutokana na hali mbaya za Balozi zetu ambazo kila mmoja anaelewa nadhani kwamba Balozi zetu hazipo katika hali nzuri, Serikali imejipanga vipi kupeleka bajeti na kuhakikisha kwamba bajeti hiyo inatosha kwa ajili kuhudumia Balozi ili waweze hasa hiyo mikakati kwa ajili ya kutekeleza hiyo diplomasia ya uchumi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kuhusu Wizara imejipangaje katika kuandaa wataalam ambao wataweza kutekeleza diplomasia ya uchumi; kama tulivyokuwa tumeeleza katika hotuba yetu ya bajeti, katika mpango wetu wa bajeti, katika kila Kitengo cha Wizara tumeweka sehemu ambayo inaangalia mafunzo ya watumishi wetu na katika kila kitengo inaangalia kwamba ina idadi ya watumishi wangapi na wangapi watatakiwa kwenda kwenye training na training hizo zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, mafunzo haya yanafanywa nje na ndani ya nchi. Kuna semina mbalimbali, wanahusishwa katika ushiriki wa Mikutano yetu ya Kimataifa, lakini vilevile wanapelekwa katika training ni za muda mrefu na zile za muda mfupi.
Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema katika utekelezaji wa diplomasia ya kiuchumi, haihusishi tu Wizara ya Mambo ya Nje, hili ni suala mtambuka, linagusa Wizara nyingine za kisekta na hata tunapojadili miradi ambayo imetafutwa kwa fursa kwa kupitia Wizara yetu, tunahusisha pia Wizara za kisekta na katika Wizara za kisekta tunatumia pia wataalam katika Wizara husika pamoja na Wizara yetu. Kwa hiyo, tumejipanga vizuri kama Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika suala la pili ambalo linahusu mkakati wa kusimamia na kuhakikisha kwamba bajeti iliyopangwa inakwenda; sisi kama Wizara tunajua kwamba tunawajibika, tunajua kuna watu ambao wanafanya kazi kwa ajili ya Serikali hii na kazi yetu kubwa kama Wizara ni kuhakikisha kwamba bajeti ambayo tumeiomba na imepitishwa katika Bunge hili inakwenda kwa wakati na tutakuwa tunaendelea kufuatilia.
Mheshimiwa Spika, pia katika siku zijazo tutaendelea pia kuliomba Bunge hili kuhakikisha kwamba wanapitisha bajeti ambayo tunaiomba ili kuhakikisha kwamba tunatekeleza hii diplomasia ya uchumi kwa ukamilifu zaidi.