Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ahmed Juma Ngwali (2 total)

MHE. AHMED JUMA NGWALI aliuliza:-
Tanzania iko kwenye mikataba mbalimbali na ushirikiano katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kama Green Climate Fund (GCF), Adaptation Fund (AF), Last Developed Countries Fund (LDCF), UNEP na kadhalika.
Je, Serikali imepokea fedha kiasi gani toka kwa wafadhili kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi tangu mwaka 2010 hadi 2015?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ahmed Juma Ngwali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea fedha kutoka kwenye Mifuko iliyo chini ya Mikataba ya Mabadiliko ya Tabianchi na ushirikiano wa nchi wafadhili kiasi cha jumla ya Dola za Marekani 89,099,139.87, Euro 10,518,018.50, Shilingi za Tanzania 2,784,382,109/= kwa mchanganuo ufuatao:-
(i) Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, kiasi cha Dola za Marekani 1,324,200.32 zilipokelewa kuanzia mwezi Februari, 2013 hadi Oktoba, 2015. Jumla ya gharama zote za mradi huu ni Dola za Marekani 5,008,564 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Novemba, 2012 hadi Oktoba, 2017.
(ii) Mfuko wa Nchi Maskini Duniani (Least Developed Countries Fund) chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi kiasi cha Dola za Marekani 1,056,851.24 zilipokelewa kuanzia Juni, 2012 hadi Machi, 2017. Gharama zote za mradi huu ni Dola za Marekani 3,356,300.00 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Novemba, 2012 hadi Oktoba, 2017.
(iii) Jumuiya ya Ulaya (European Union) Awamu ya Kwanza mwaka 2010 hadi 2013 zilipokelewa Euro 1,975,025.00 Awamu ya pili ziliidhinishwa Euro 8,542,993.50, utekelezaji umeanza kwa mwaka wa 2014 ambao utakamilika mwaka wa 2018.
(iv) Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP), kiasi cha sh. 2,543,882,695/= zilipokelewa kuanzia Aprili, 2012 hadi Juni, 2015 wakati zilizoahidiwa zilikuwa ni Dola za Marekani 2,000,820,000.00.
(v) Serikali ya Norway kiasi cha Dola za Marekani 85,929,553.31 zilipokelewa kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2015.
(vi) Serikali ya Japan kupitia UNDP ilitoa kiasi cha Dola za Marekani 971,533 na Sh. 1,400,070,145 kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2013.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kiwango cha kubadilisha fedha kwa sasa, fedha hizi ni sawa na sh. 224,314,313,555.30 ambapo sh. 7,017,510,977.40 zilipokelewa Ofisi ya Makamu wa Rais na sh. 217,296,802,577.90 zilipokelewa moja kwa moja na wadau wengine wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zilipatikana baada ya kuandaa miradi kwa kuzingatia uwezo wa vipaumbele vya vyanzo vya fedha husika. Aidha, pamoja na fedha hizi, baadhi ya wafadhili hutoa fedha zao moja kwa moja kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, taasisi au sekta husika na asasi zisizo za kiserikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali limekuwa refu kulingana na lilivyoulizwa. Ahsante.
MHE. AHMED JUMA NGWALI aliuliza:-
Tanzania ilibadilisha Sera yake ya Kibalozi ili kuendana na mazingira ya sasa ya kiuchumi duniani kwa maana ya kujiwekeza katika Diplomasia ya Uchumi (Economic Diplomacy).
(a) Je, ni lini Tanzania ilibadili Sera yake ya Mambo ya Nje ya awali na kujielekeza katika Sera ya Diplomasia ya Uchumi?
(b) Je, mwenendo ukoje kati ya sera hii na ile iliyokuwepo awali?
(c) Je, ni vigezo au vipimo gani vinavyotumika kupima Balozi zetu katika utekelezaji wa sera hii ya Diplomasia ya Uchumi.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Juma Ngwali, Mbunge wa Wawi, lenye vipengele (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mara baada ya Tanzania kupata uhuru mwaka 1961 na hata baada ya Muungano mwaka 1964, Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania iliweka msisitizo zaidi kwenye masuala ya kisiasa hususan kupigania uhuru wa nchi za Afrika zilizokuwa zinatawaliwa na wakoloni, kupanga ubaguzi wa rangi na ukoloni mamboleo.
Mheshimiwa Spika, ushiriki wa Tanzania kwenye masuala ya uhusiano wa Kimataifa kabla ya mwaka 2001 uliongozwa na matamko mbalimbali ya Viongozi Wakuu wa nchi na nyaraka kama vile Waraka wa Rais Namba 2 wa mwaka 1964. Tanzania ilifanikisha jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa na kujijengea heshima mbele ya jamii ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha jukumu la kuzikomboa nchi za Afrika kutoka katika makucha ya ukoloni na vilevile kutokana na mabadiliko yaliyotokea duniani katika medani za kisiasa na uchumi ikiwemo kwisha kwa vita baridi, kuibuka kwa utandawazi, dhana ya demokrasia na uchumi wa soko, Tanzania ililazimika kubadili mwelekeo wa sera yake ya mambo ya nje.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, mwaka 2001 Serikali ilitunga sera mpya ya mambo ya nje ambayo imeweka msisitizo kwenye diplomasia ya uchumi. Sera hiyo ndiyo inayoendelea kutekelezwa hadi hivi sasa.
(b) Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu kwenye kipengele (a), sera ya awali ya mambo ya nje ilijikita zaidi katika masuala ya kisiasa ambapo Tanzania ilishiriki kikamilifu kutafuta ukombozi wa nchi nyingi za Bara la Afrika.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sera ya Mwaka 2001 ya Mambo ya Nje ambayo utekelezaji wake umelenga zaidi kupata manufaa ya kiuchumi kutokana na mahusiano yake na nchi nyingine duniani, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la watalii waliotembelea nchi yetu; ongezeko kwenye biashara ya nje na uwekezaji, pamoja na kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na misaada ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, licha ya kuwa sera ya sasa imejikita katika masuala ya kiuchumi, bado Tanzania inashirikiana na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa katika kulinda amani na usalama katika nchi mbalimbali duniani.
(c) Mheshimiwa Spika, vigezo vinavyotumika kupima utendaji wa Balozi zetu ni pamoja na namna Balozi anavyotimiza majukumu yake kama yanavyoainishwa katika OPRAS na Mpango Kazi wake wa mwaka pamoja na kutekeleza kwa weledi majukumu yake kama kuvutia wawekezaji kutoka nje, kutafuta masoko ya bidhaa zetu, kuvutia watalii, kutafuta teknolojia sahihi na rahisi, kutafuta misaada ya maendeleo na mikopo ya masharti nafuu na kuendelea kujenga sifa nzuri ya nchi yetu na mambo hayo yamewekwa katika kitabu chao cha Ambassador’s Handbook.