Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula (70 total)

MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:-

Hapa Tanzania kumekuwepo na migogoro mbalimbali ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi, wakulima na wafugaji, hifadhi na wananchi na baina ya wananchi wenyewe:-

(a) Je, Serikali ina mikakati gani ya kupanga matumizi bora na endelevu ya ardhi ili kuondokana na migogoro?

(b) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuondokana na tatizo la maendeleo ya miji kutokuendana na kasi ya ukuaji wa miji?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kuandaa Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi wa mwaka 2013 mpaka 2033. Mpango huu ndiyo kiunzi wa matumizi ya ardhi yaani National Land Use Framework Plan unaotoa maelekezo ya namna ya kupanga maeneo yote nchini kuanzia katika ngazi ya Kanda, Mkoa, Wilaya na Vijiji. Mpango huu umeanza kutekelezwa kupita programu sita za kipaumbele ambazo ni makazi na miundombinu mikuu ya uchumi, kilimo na mifungo, ardhi ya hifadhi na utalii, maeneo ya nishati na madini, mipango ya matumizi ya ardhi kwa ngazi za chini, pamoja na programu ya kuboresha Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi. Kupitia programu hizi, ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii itategwa na hivyo kuondokana na migogoro baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi. Aidha, Serikali imeandaa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi nchi nzima ili kuondokana na migogoro ya ardhi.

(b) Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la wakazi mijini ambako kumepelekea mamlaka za upangaji na uendelezaji miji kushindwa kutoa huduma za kijamii na kiuchumi kwa kiwango stahiki na hivyo kufanya miji yetu kukua kiholela. Katika kukabiliana na changamoto hizi, Wizara yangu imeendelea kuratibu uandaaji wa mipango kabambe ya Majiji na Miji mbalimbali nchini ambayo itatoa muongozo wa uendelezaji wa miji kwa kuzingatia mahitaji mbalimbali na hivyo kuondokana na tatizo la ukuaji wa miji isiyopangwa. Hadi sasa mipango kabambe ya Majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Miji ya Mtwara, Musoma, Iringa, Bariadi, Bagamoyo, Kibaha na Shinyanga iko katika hatua za mwisho za maandalizi na itakamilika kabla ya mwezi Agosti, 2016. Aidha, Mipango Kabambe ya Miji ya Tanga Singida, Tabora, Songea, Morogoro, Sumbawanga, Geita, Njombe na Mpanda ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa mamlaka za upangaji ambazo hazina mipango kabambe kutenga fedha katika bajeti zao ili kuharakisha uandaaji wa mipango kabambe na mipango ya kina itakayotoa mwongozo wa uendeleshaji katika miji yao na hivyo kuzuia tatizo la ukuaji wa miji isiyopagwa.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuza:-
Wanachi wa Mikumi upande mmoja wamebanwa na Hifadhi na upande wa pili ardhi kubwa wamepewa Wawekezaji ambao hawajafanya uendelezaji wowote katika mashamba ya Kisanga, Masanze, Tindiga na hiyo kupelekea wananchi kukosa ardhi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuirudisha ardhi hii kwa wananchi ili waweze kujiletea maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Jimbo la Mikumi ni miongoni mwa maeneo ambayo yana ardhi nzuri kwa kilimo na ambalo pia lina wakulima na wawekezaji wenye mashamba makubwa.
Mheshimiwa Spika, ili kuitwaa ardhi kwa yeyote ambaye ameshindwa kuiendeleza utaratibu ufuatao unapaswa kufuatwa:-
Mheshimiwa Spika, kwanza sheria inataka mmiliki apatiwe ilani ya ubatilisho ya siku 90 na mamlaka (Halmashauri) husika ambapo shamba lipo. Ilani hiyo inatakiwa kueleza masharti yaliyokiukwa na kwa nini miliki yake isifutwe. Vile vile muda huo unampa mmiliki muda wa kuwasilisha utetezi wake kwa mujibu wa kifungu cha 47, 48 na 49 cha Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999.
Pili, muda wa ilani ya ubatilisho utakapokuwa umekwisha mapendekezo ya ubatilisho yatatumwa kwa Kamishna ambapo kama Kamishna atakubaliana na sababu za mapendekezo ya ubatilisho, Kamishna atawasilisha mapendekezo kwa Waziri mwenye dhamana ambaye naye atawasilisha mapendekezo hayo kwa Mheshimiwa Rais na kumshauri afute miliki hiyo.
Mheshimiwa Spika, naishauri Halmashauri husika ifanya ukaguzi wa mashamba yote makubwa yaliyomo ndani ili yale yaliyokiuka sheria hatua zinazofuata zichukuliwe.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. JOSHUA S. NASSARI) aliuliza:-
Shamba Na.112 (Ex-Arusha Coffee Estate) lililopo Nduruma Wilaya ya Meru lililokuwa likimilikiwa na Tanzania Flowers Ltd. lenye ukubwa wa ekari 721 lilishawahi kufutwa mwaka 2000 na hati ya utwaaji ardhi (Deed of Acquisition) ikasajiliwa 12/6/2001 na aliyekuwa Waziri wa Ardhi wa wakati huo, Mheshimiwa Gideon Cheyo lakini hadi leo wawekezaji hao bado wanazidi kuiuza ardhi hiyo ambayo ilifutwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi wenye shida ya ardhi:-
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya jambo hilo hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ilishawahi kuwaambia wananchi wa maeneo hayo kuwa shamba hilo halimilikiwi na wawekezaji tena?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joshua Samwel Nassari, Mbunge wa Arumeru, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba Na.112 lilikuwa na ukubwa wa ekari 721 na lilikuwa eneo la Nduruma, Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha. Tarehe 14/11/1990 shamba hili lilimilikishwa kwa Tanzania Flowers Ltd. ya Arusha na mnamo tarehe 8/8/1991 na tarehe 2/10/1991 kampuni hiyo ililigawa shamba hilo katika sehemu saba na kuwauzia watu sita tofauti baada ya kufuata taratibu zote za kisheria na sehemu moja yenye ekari 80 iliendelea kumilikiwa na Tanzania Flowers Ltd. Kampuni zilizouziwa zilipewa hati kutokana na hatimiliki mama yenye Na.7320 hili lilifanyika kwa kuzingatia kufungu cha Sheria Na. 83 na 88 cha Sheria ya Usajili wa Ardhi. Mgawanyo wa shamba hilo ulikuwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 6/12/2011, Serikali iliamua kulitwaa eneo linalomilikiwa na Tanzania Flowers Limited lenye Hati Na. 7320 ambalo kwa wakati huo lilikuwa na ukubwa wa ekari 80. Utwaaji huu ulisajiliwa kwa Waraka Na.14316. Hivyo basi, ekari 80 zilitwaliwa kwa ajili ya matumizi ya wananchi, na ardhi hiyo ilisharudishwa kwa Halmashauri Halmashauri ya Arumeru ndiyo wanahusika katika ugawaji wa shamba hilo.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Katika Jimbo la Korogwe Vijijini yako mashamba ambayo tangu yabinafsishwe hayajaendelezwa:-
(a) Je, ni lini mashamba hayo yatagawiwa kwa wananchi kwa sababu hayaendelezwi?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuyatoa kwa wananchi mashamba ambayo hayaendelezwi ili kuwapa fursa ya kuyatumia kwa shughuli za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali namba 67 la Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani, naomba kutoa maelezo ya utangulizi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini kukagua mashamba na kuwasilisha taarifa za ukaguzi na hatua stahiki. Mashamba yatakayobainika kwamba hayajaendelezwa ilani ya ubatilisho zitatumwa na Wakurugenzi husika kwa umilikishaji. Baada ya kipindi cha siku 90 kumalizika Halmshauri zitatakiwa kuleta mapendekezo ya ubatilisho Wizarani.
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ukaguzi uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, umebaini kuwepo kwa shamba lisiloendelezwa la Mwakijubi Farm linalomilikiwa na Ndugu Chavda. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ameanza kufanya taratibu za ubatilisho wa milki kabla ya kuwasilisha mapendekezo Wizarani.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ugawaji wa mashamba kwa wananchi hufanyika baada ya taratibu za ubatilisho kukamilika na kupata kibali cha Mheshimiwa Rais. Taratibu za ubatilisho zinapokamilika mashamba haya hurejeshwa katika Halmashauri husika ili yapangiwe matumizi mengine ikiwemo kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yetu sasa baada ya taratibu za ubatilisho kukamilika na maeneo haya kukabidhiwa kwenye Halmashauri, Halmashauri watapanga matumizi kulingana na uhitaji wa eneo husika ikiwa ni pamoja na matumizi ya kilimo. Kwa sasa, wakati zoezi la ubatilisho linafanyiwa kazi, tunaomba wananchi waendelee kuvuta subira mpaka hapo mchakato wa ubatilisho utakapokamilika.
MHE. HUSSEIN M. BASHE (K.n.y. MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU) aliuliza:-
Kifungu na 97(1)(b) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kinamtaka mwekezaji kabla hujaanza shughuli za kujenga mgodi ili kuzalisha madini ni lazima ahakikishe kwamba anawasilisha na kutekeleza mpango wa fidia, ujenzi wa makazi mapya na kuwahamishia wananchi waliopisha ujenzi huo kwenye makazi mapya yaani “compensation, reallocation and resettlement plan” kulingana na matakwa ya Sheria ya Ardhi.
Je, ni lini Serikali itarekebisha Sheria ya Ardhi ili iendane na matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Namba103 la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ardhi yenye madini pamoja na kutawaliwa na Sheria ya Madini Na. 14 ya mwaka 2010 pia hutambuliwa na Sheria mama za sekta ya ardhi. Kwa kutambua hilo, kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Madini kinatoa tafsiri ya mmiliki halali wa ardhi (lawful occupier) kuwa ni mtu ambaye anamiliki ardhi chini ya Sheria ya Ardhi Na. 4 na 5 za mwaka 1999. Hivyo, ni wajibu wa wamiliki wa migodi kuhakikisha kwamba wanatekeleza masharti ya Sheria ya Madini na Sheria ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ardhi Na. 4 na 5 za mwaka 1999 kifungu cha 3(1)(f) vinabainisha kwamba ardhi ina thamani na kwamba thamani hiyo inazingatiwa wakati wowote katika mapatano yoyote yanayoathiri maslahi hayo. Sheria hizi zinasisitiza kwamba lazima ardhi ilipwe fidia kamili kwa bei ya soko, haki na kwa wakati kwa yeyote ambaye ardhi yake imetwaliwa. Aidha, katika Kanuni za Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999, Kanuni ya 10 ya “The Land (Compensation Claims) Regulations” ya mwaka 2001, inaelekeza kuwa fidia lazima iwe ya fedha lakini Serikali inaweza kutoa fidia katika muundo wa kitu kimoja kati ya hivi au vyote kwa pamoja:-
(a) Kiwanja kinacholingana na kile kilichotwaliwa;
(b) Jengo au majengo yanayolingana na yale yaliyotwaliwa;
(c) Mimea au mbegu; na
(d) Kutoa nafaka na vyakula vya msingi kwa wakati maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999, imezingatia matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Hivyo, kwa sasa hakuna sababu ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi ili iendane na Sheria ya Madini katika suala la ulipaji wa fidia.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiendeleza zoezi la bomoa bomoa katika maeneo tofauti hapa nchini. Zoezi hili limekuwa likiwaathiri wananchi kiuchumi na hata kisaikolojia kwa kuwaacha wakiwa hawajui waelekee wapi:-
Je, kwa nini Serikali isiwafidie wananchi hawa ukizingatia kwamba wakati wanajenga, Serikali ilikuwa inawaona, lakini haikuchukua hatua stahiki?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali namba 109 la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Mwingwi, kama ifuatavyo:-
SPIKA: Wingwi. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali namba 109, naomba kutoa maelezo yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, suala la bomoa bomoa katika maeneo tofauti hapa nchini limesababishwa na sababu zifuatazo:-
(1) Ni wananchi kuvamia kwenye maeneo hatarishi na oevu kinyume cha sheria;
(2) Ni kuvamia maeneo au viwanja vya watu wengine au maeneo ya wazi na ya umma bila kufuata utaratibu;
(3) Ni kujenga ndani ya hifadhi ya barabara, misitu, mbuga, mikoko, fukwe, kingo za bahari na mito; na
(4) Ni kujenga majengo kwenye maeneo yaliyopangwa bila kufuata taratibu.
Mheshimiwa Spika, mambo yote manne niliyotaja hapo juu na mengine yanayofanana na hayo yanasimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 na Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, bila kuathiri maana iliyopo katika Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya 2004, Kifungu cha 55 na 57 cha Sheria hii, vimeeleza wazi na kutoa katazo la kutoruhusu mtu yeyote kufanya shughuli zozote za kibinadamu za kudumu ndani ya mita 60 ambazo zinaharibu au kwa asili yake inaweza kuathiri ulinzi wa mazingira ya bahari au kingo za mito, mabwawa au miamba ya asili ya ziwa.
Aidha, Sheria hii pamoja na mambo mengine, imekataza shughuli zozote zinazohusisha kuchepusha au kuzuia mto, ukingo wa mto, ziwa au mwambao wa ziwa, ufukwe au ardhi oevu kutoka mkondo wake wa asili au kukausha mto au ziwa. Vile vile imeeleza wazi kuwa mtu yeyote anayekiuka masharti hayo anakuwa ametenda kosa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na sheria tajwa hapo juu, Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007 inaeleza na kufafanua kwa upana namna bora ya kusimamia ardhi yote ya Mijini kuwa, ―Sheria itaweka utaratibu wa maendelezo endelevu ya ardhi katika maeneo ya Mijini, kulinda na kuboresha huduma pamoja na kutoa vibali vya uendelezaji wa ardhi na kudhibiti matumizi ya ardhi katika masuala yanayohusiana na hayo.‖
Mheshimiwa Spika, wananchi wote watakaovunjiwa nyumba zao kwa sababu ya kutofuata sheria au kuvunja sheria au sababu nilizozitaja awali, hawatalipwa fidia.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Wilaya ya Lushoto ni miongoni mwa Wilaya kubwa na Kongwe nchini ambapo ina takribani watu laki tatu lakini haina Mahakama ya Ardhi hivyo Wananchi hufuata huduma hiyo hadi Wilaya ya Korogwe licha ya kwamba majengo tunayo:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha Mahakama hiyo katika Wilaya ya Lushoto ili kuwapunguzia adha wananchi wake wanaofuata huduma hiyo Wilayani Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Shekilindi naomba Waheshimiwa Wabunge wafahamu kuwa, lengo la Serikali la kuunda Mabaraza ya Ardhi katika kila Wilaya ni kusogeza huduma za utatuzi wa migogoro ya ardhi karibu na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua hilo, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali kupitia Wizara yangu kupitia Gazeti la Serikali Namba 545 ilitangaza kuanzisha jumla ya Mabaraza 47 ambayo yataundwa nchini likiwemo Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu na unyeti wa utatuzi wa migogoro ya ardhi katika Wilaya Kongwe ya Lushoto tarehe 6 Julai, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alizindua rasmi Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Lushoto. Kuanzia tarehe hiyo, Baraza limeshaanza kutoa huduma kwa wananchi wote wa Wilaya ya Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa kutupatia jengo kwa ajili ya uanzishwaji wa Baraza hilo. Vilevile nitoe wito kwa Wakurugenzi wote nchini kuharakisha kutoa majengo kwa ajili ya ofisi za Mabaraza ili huduma hii muhimu iweze isogezwe karibu na wananchi na kuweza kupunguza kama siyo kumaliza kabisa kero mbalimbali za migogoro ya ardhi nchini.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE (K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Malangali ndani ya Wilaya ya Wanging‟ombe na wafanyakazi wa Hifadhi ya Mpanga?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali namba 422, la Mheshimiwa Neema William Mgaya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Nabu Spika, Hifadhi Mpanga au Kipengere lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 1,574 kwa mara ya kwanza ilitangazwa kuwa hifadhi mwaka 2002 kupitia Tangazo la Serikali (GN) Namba 483.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Oktoba10, 2012 Serikali ilitangaza tena Hifadhi hii kuwa Aifadhi ya Akiba, tangazo ambalo lilioneshwa kuwa kijiji hiki kipo ndani ya hifadhi na hivyo kusababisha mgogoro kati ya wanakijiji, wafanyakazi wa hifadhi pamoja na hifadhi yenyewe kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Wanging‟ombe mwezi Februari, 2016, aliunda Tume ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu. Pamoja na timu hiyo, Wizara yangu itakutana na Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wote kwa lengo la kufanya mapitio ya matangazo yote mawili ili kupata tafsiri sahihi ya mipaka ya Hifadhi na kijiji kisha kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jambo hili ni nyeti, naomba kuahidi kulifanyia kazi mapema iwezekanavyo mara baada ya vikao vya Bunge lako Tukufu kumalizika.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Wakazi wa Kichangani katika Wilaya ya Mpanda Mjini hawajawahi kupata hati kwa ardhi wanayomiliki:-
Je, ni lini wananchi wa maeneo hayo watapatiwa hati zao hasa ikizingatiwa kuwa zimechukua muda mrefu sana na haijulikani hatma yao ni nini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 416 la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, umilikishwaji wa viwanja katika eneo la Kichangani katika Wilaya ya Mpanda ulifanyika kwenye maeneo ambayo upimaji wake ulikuwa bado haujakamilika. Ili wananchi hao waweze kupewa hatimiliki taratibu za upimaji wa maeneo hayo zinapaswa kukamilishwa kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu umekuwa ukifanywa na Halmashauri nyingi hapa nchini na ulilenga kupunguza mfumuko wa makazi holela mijini. Hata hivyo, baada ya Wizara yangu kubaini kuwa kuna maeneo mengi nchini ambayo yamemilikishwa bila upimaji wake kukamilika hivyo kuwakosesha haki na fursa wananchi kupata hati kutokana na upimaji kutokamilika. Wizara yangu imeingilia kati na kuzitaka Halmashauri zote nchini kuainisha maeneo yote ambayo yako katika demarcation ili upimaji wake ukamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wizara yangu tayari imetangaza zabuni kwa ajili ya kukamilisha upimaji huo na wazabuni mbalimbali wameshawasilisha zabuni na kufanya kazi hiyo na taratibu za kumpata mzabuni mwenye sifa zinaendelea. Aidha, tunapenda kutoa wito kwa Halmashauri zote nchini ikiwemo Wilaya ya Mpanda kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha upimaji ambao haujakamilika katika maeneo yao yote ambayo yataguswa katika mpango huu wa Wizara.
MHE. SOPHIA M. SIMBA (K.n.y. MHE. ANATROPIA L. THEONEST) aliuliza:-
Kuna mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa Kipunguni „A‟ na Kipunguni Mashariki dhidi ya Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Jijini Dar es Salaam. Wananchi hao wanapinga uthamini uliofanywa na fidia kidogo kwa kikundi cha watu wachache, huku wengine wakizuiwa kuendeleza maeneo yao?
(a) Je, ni lini Serikali itaenda kumaliza mgogoro huo uliodumu tangu 2007?
(b) Je, Serikali ipo tayari kuwapa fidia ya kiwango cha soko wananchi waliozuiwa kuendeleza maeneo yao na kuendelea kubaki maskini kwa muda wote huo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 417 la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Kipunguni “A” na Kipunguni Mashariki pamoja na maeneo ya Kipawa pamoja na Kigilagila ni maeneo yaliyotwaliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mwaka 1997. Uthamini wa maeneo haya ulifanywa na Kampuni ya Tanvaluers and Property Development ambayo ni kampuni binafsi ya uthamini na ilifanya mwaka 1997. Hata hivyo, malipo ya fidia hayakuweza kufanyika kwa wakati. Mwaka 2011 Serikali iliamua kuanza kuwalipa wananchi hao fidia kwa kuanza na eneo la Kipawa na Kigilagila.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuwa Sheria iliyotumika kufanya uthamini huo ilikuwa ni ile ya Utwaaji Ardhi ya mwaka 1967 yaani (The Land Acquisition Act of 1967) ambayo ilipwaji wa fidia ulipaswa kuzingatia yafuatayo:-
(i) Maendelezo pekee (yaani majengo na mazao katika eneo);
(ii) Kiwanja mbadala; na
(iii) Riba ya 6% kwa kila mwaka pindi malipo yanapocheleweshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2010 wananchi hao walifungua kesi Mahakama Kuu wakipinga kulipwa fidia kwa kutumia sheria ya zamani, wananchi walishindwa kesi hiyo, kwani mchakato wa utwaaji wa eneo hilo ulianza ndani ya Sheria ya zamani ya Utwaaji Ardhi na sio Sheria mpya ya mwaka 1999 ambayo ilianza kutumika mwaka 2001. Sheria hii mpya inataka malipo ya fidia yalipwe kwa kuzingatia yafutayo:-
(i) Thamani ya ardhi;
(ii) Thamani ya maendelezo;
(iii) Posho za makazi, usumbufu na usafiri; na
(iv) Riba ya kiwango cha soko pale malipo yanapocheleweshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hukumu hiyo stahili ya wananchi hao ni fidia ya maendelezo, viwanja mbadala na riba ya 6% kwa mwaka mpaka pale malipo yatakapofanyika kama ilivyobainishwa katika Sheria ya Utwaaji Ardhi ya mwaka 1967. Mnamo mwaka 2011 wananchi wa maeneo ya Kipawa na Kigilagila walilipwa fidia yenye wastani wa shilingi bilioni 18. Wananchi wa eneo la Kipunguni bado hawajalipwa fidia zao. Serikali kupitia mamlaka ya viwanja vya ndege ipo katika mkakati wa kutafuta fedha hizo ili kuwalipa wananchi stahiki zao.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE (K.n.y. MHE. LUCY S. MAGERELI) aliuliza:-
Matatizo ya migogoro ya ardhi na mipango miji ni suala nyeti sana linalohitaji kutazamwa sana katika zama hizi; na hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aligawa ramani za maeneo ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam lakini zoezi hilo halikufanikiwa kutokana na kukosa mkakati ulioambatana na matumizi ya ramani hizo:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ramani hizo zinapatikana kwa nchi nzima ili kusaidia kuongoza matumizi ya ardhi katika miji mingi nchini?
(b) Waziri Mkuu aliyepita, Mheshimiwa Mizengo Pinda alisema, Serikali ingeuza Government Bond ili kupata fedha za kugharamia mradi huu. Je, agizo hilo limefikia hatua gani katika utekelezaji?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 418 la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) yote kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007, kifungu cha 21(1) kinaeleza kwamba mipango yote iliyoidhinishwa na Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji kwa maana ya Mipango Miji ya jumla (Master plan) na ile ya kina (michoro ya mipango miji) itahifadhiwa na mamlaka husika ya upangaji kwa maana ya Halmashauri ya Jiji, Manispaa, Miji na Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli matatizo ya migogoro ya ardhi na mipango miji ni suala nyeti sana linalohitaji kupatiwa mtazamo wa kipekee. Ni kweli hivi karibuni niligawa ramani za maeneo ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam na zoezi hilo lilifanyika kwa lengo la kuwawezesha viongozi wa ngazi za mitaa kushiriki kikamilifu katika udhibiti wa ujenzi holela na uvamizi wa maeneo ya umma, maeneo ya wazi na yale yaliyohifadhiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu ina jukumu la kuhakikisha kuwa michoro yote ya mipango miji iliyoidhinishwa na Wizara inatumiwa kwenye Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa na nakala zake kupelekwa katika Halmashauri husika na mamlaka hizo zina jukumu la kuweka michoro hiyo hadharani ili umma uweze kuona na kulinda maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Serikali kuuza bond ili kupata fedha za kugharamia mradi huu, suala hili halijatekelezwa, badala yake kila Halmashauri inaelekezwa kutumia vyanzo vyake vya ndani vya mapato kwa kushirikiana na sekta binafsi. Hii ni kutokana na Sheria ya Mipango Miji inayotoa fursa kwa wamiliki binafsi wa ardhi kuandaa mipango ya matumizi kwa mujibu wa sheria.
MHE. EMMANUEL P. JOHN aliuliza:-
Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi huko Kiteto baina ya wakulima na wafugaji:-
(a) Je, ni lini Serikali itaipatia Kiteto Mahakama ya Baraza la Ardhi ili kesi nyingi ziweze kusikilizwa hapo Kiteto?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kupima ardhi yote ya Kiteto ili kila mtu afahamu mipaka ya eneo lake ili kuepusha mwingiliano wa maeneo usio wa lazima, itafanya hivyo lini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 231 la Mheshimiwa Emmanuel Papian John, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu naomba nifanye sahihisho dogo kwenye jibu la msingi isomeke mwaka 2015/2016 na siyo 2016/2017 kama ilivyoandikwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu sasa Wabunge wafahamu kuwa lengo la Serikali la kuunda Mabaraza ya Ardhi katika kila Wilaya ni kusogeza huduma za utatuzi wa migogoro karibu na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara iliahidi kuunda Mabaraza nane likiwemo Baraza Nyumba katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kiteto ametoa jengo ambalo tayari limeshafanyiwa ukaguzi ili kubaini mahitaji. Wizara imekwisha nunua samani za ofisi na hata sasa inaendelea na taratibu za upatikanaji wa watendaji. Taratibu hizo zitakapokamilika baraza litaanza kazi mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, Novemba, 2014, kikosi kazi cha kushughulikia mipaka ya maeneo katika Wilaya ya Kiteto kiliundwa. Kikosi kazi hicho kilijumuisha wataalam kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI; Ofisi ya Takwimu; Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wataalam kutoka Halmashauri ya Kiteto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zilizofanyika zilikuwa ni kurekebisha mipaka ya vijiji 10; Kijiji cha Loltepes, Emart, Enguserosidan, Kimana, Kinua, Nhati, Nemalock, Ndirigishi, Krashna na Taigo) katika eneo lililokuwa limegombewa kuzunguka hifadhi ya Emboley Murtangos kukamilisha mipango shirikishi ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 10 ni pamoja na kupima mashamba 2,110 katika vijiji vitatu, Kijiji cha Loltepes mashamba 385; Kimana mashamba 1,250; na Nemalock 475 na kutoa elimu iliyolenga kutatua migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Kiteto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii ni kazi endelevu na itakamilika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:-
Kumekuwa na Migogoro mingi ya ardhi mjini na vijijini inayotokana na kutopima na kupanga matumizi bora ya ardhi:-
(a) Je, Serikali imejipangaje kupunguza au kumaliza migogoro ya ardhi?
(b) Je, lini Serikali itaandaa mipango Kabambe (Master plans) mijini na vijijini lili kuainisha matumizi bora ya ardhi na kuondoa migogoro ya ardhi nchini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), napenda kutoa maelezo mafupi ya vyanzo vya migogoro kama ifuatavyo:-
Utwaaji wa ardhi bila fidia stahiki; taasisi za umma na binafsi kuwa na maeneo au mashamba makubwa bila kuyaendeleza na kuyalinda; utata wa mipaka kati ya vijiji na wilaya pamoja na hifadhi; uvamizi wa viwanja na mashamba; kutokuwepo kwa mipango ya matumizi ya ardhi;ongezeko kubwa la idadi ya watu na shughuli mijini na vijijini katika ardhi ile ile na kutoheshimu sheria na mipango ya matumizi ya ardhi na shughuli za makundi ya watu wengine kama vile wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupunguza na kutatua migogoro ya ardhi, Wizara imekuwa ikitekeleza mambo yafuatayo:-
(i) Kuandaa kitabu cha orodha ya migogoro ya Nchi nzima kinachoainisha vyanzo vyake ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa;
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI:
(ii) Kuwasiliana na Wizara zinazohusika na kilimo, mifugo na uvuvi; maliasili na utalii pamoja na TAMISEMI ili kutatua migogoro mtambuka;
(iii) Kuandaa matumizi ya ardhi katika vijiji na miji ambako migogoro ya ardhi imekuwa ikijitokeza na kusambaza miongozo inayohusu sera na sheria za ardhi;
(iv) Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kuainisha viwanja na mashamba yasiyoendelezwa ipasavyo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa;
(v) Kuimarisha mfumo wa ki-electronic katika kutunza kumbukumbu;
(vi) Kuimarisha ofisi za kanda ili kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi;
(vii) Kuanzisha Mfuko wa Fidia ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utayarishaji wa mipango kabambe ya miji, Wizara imekuwa ikitekeleza mambo yafuatayo:-
(i) Kuunda na kukamilisha program ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi Tanzania itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2015 mpaka 2025;
(ii) Wizara inasaidiana na Halmashauri za Wilaya na miji 18 kwenye program ya Urban Local Government Supporting Program katika utayarishaji wa mipango kabambe; na
(iii) Kujadiliana na Benki ya Dunia ili kuharakisha zoezi la utayarishaji wa mipango kabambe katika miji mingine 30 ya Tanzania bara.
MHE. ZAINAB M. VULU (K.n.y MHE. ALLY S. UNGANDO) aliuliza:-
Kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais kutaka kumaliza kabisa urasimu wa upatikanaji wa hati za kimila na hati za ardhi mpaka sasa bado ni tatizo kwa Wilaya ya Rufiji:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Afisa Ardhi Mteule?
(b) Je, Serikali haioni kwamba ina kila sababu ya kupeleka vifaa vya kisasa vya kupima viwanja na mashamba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kawaida, Afisa Mteule na ni Mwajiriwa katika halmashauri husika. Kabla ya kuteuliwa kuwa Afisa Ardhi Mteule, mapendekezo ya uteuzi huanzia katika halmashauri husika kutoa pendekezo ambalo linawasilishwa kwa Katibu Tawala wa Mkoa husika ambaye na yeye ataliwasilisha pendekezo hilo kwa Kamishna wa Ardhi. Pendekezo litakapowasilishwa kwa Kamishna wa Ardhi, Kamishna atafanya uteuzi wa Afisa Mteule Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji afuate utaratibu huo nilioueleza hapo awali ili halmashauri yake iweze kupata Afisa Mteule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inatambua umuhimu wa kupima viwanja na mashamba hapa nchini. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imekuwa ikiziagiza halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji. Aidha, katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa vifaa hivyo, Wizara kupitia Benki ya Dunia ipo katika mchakato wa kununua vifaa vya upimaji ambavyo vitasambazwa katika Kanda nane za Wizara yangu ili halmashauri zote zilizopo ndani ya kanda hizo ziweze kunufaika.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH (K.n.y. MHE. HASSAN S. KAUNJE) aliuliza:-
Kuna migogoro ya ardhi iliyosababishwa na upimaji na ugawaji wa ardhi kwa ajili ya makazi na ujenzi wa taasisi katika Kata ya Rasbura eneo la Mitwero.
Aidha, watumishi wa Idara ya Ardhi walijigawia ardhi kinyume na taratibu na kuiuza kwa manufaa yao. Pia wananchi wanalalamikia fidia na utwaaji wa maeneo makubwa tofauti na michoro iliyomo kwenye nyaraka zilizothibitishwa na Wizara kwa matumizi ya taasisi za umma au binafsi:-
Je, Serikali ipo tayari kufanya uchunguzi au uhakiki wa zoezi zima la upimaji na ugawaji wa viwanja katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na.375 la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Mitwero lililoko katika Kata ya Rasbura ni moja ya maeneo ambayo upimaji wa viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali katika Manispaa ya Lindi umefanyika. Kwa kawaida, upimaji wa viwanja popote hufanyika kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi pamoja na Sheria ya Mipango Miji na kanuni zake ambazo huelekeza upimaji na fidia stahiki kwa eneo husika kabla ya kutwaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba pamoja na kuwepo kwa utaratibu huu wa kisheria wa upimaji na ugawaji viwanja, yapo malalamiko mbalimbali yaliyojitokeza wakati Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ikiwa inatekeleza mradi wa upimaji viwanja katika eneo la Mitwero. Miongoni mwa malalamiko hayo ni wananchi kulipwa fidia ndogo, ucheleweshaji wa malipo ya fidia na utaratibu usioridhisha wa ugawaji wa viwanja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kushughulikia malalamiko ya wananchi wa Mitwero, nilitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi kwamba washirikiane na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Kusini katika kuyashughulikia malalamiko hayo ikiwemo kurejea uthamini wa maeneo na maendelezo ambayo hayakuthaminiwa wakati Halmashauri ikitekeleza mradi huo ili walalamikaji walipwe stahiki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi watakaobainika kukiuka maadili ya Utumishi wa Umma pamoja na ukiukwaji wa miiko ya taaluma zao, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, (TAMISEMI) tutachukua hatua zinazostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara yangu kwa kushirikiana na Manispaa ya Lindi imeshafanya uhakiki na wote waliokuwa na madai yameanza kushughulikiwa kwa kulipwa fidia zao stahiki.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwamilikisha na kutoa Hati za Kimila kwa wananchi wa Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nachingwea ina jumla ya vijiji 127, hadi kufikia mwaka 2007 vijiji 104 vilikuwa tayari vimefanyiwa upimaji. Kati ya hivyo 104, vijiji 99 tu ndiyo vilikuwa vimepata vyeti vya vijiji na hapo vijiji 22 ndiyo vilikuwa vimewekewa mpango wa matumizi bora ya ardhi. Mwaka 2009 Vijiji vya Mbondo, Nakalilonji na Nahimba vilikuwa katika mchakato wa kuandaliwa Hati Miliki za Kimila pamoja na ujenzi wa Masijala ya Ardhi kwa ufadhili wa MKURABITA ambao haukukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa kukamilisha wananchi na kutoa Hati za Haki Miliki za Kimila ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Ardhi Na. 5 ya mwaka 1999 na Kanuni zake. Hati na Haki Miliki za Kimila siyo tu zinawahakikishia wananchi usalama wa miliki zao bali pia huwawezesha wananchi kuzitumia kama dhamana za mikopo pale wanapohitaji kukidhi vigezo vya mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi zinazofanywa na Halmashauri mpaka sasa ni kutenga fedha katika bajeti zao ili kukamilisha zoezi la utoaji wa hati 1,170 ambazo hazikukamilishwa na MKURABITA. Aidha, Halmashauri imejiwekea mkakati wa kutayarisha hati nyingine 1,170 na kuzigawa kwa wananchi wa Vijiji vya Mbondo, Nakalonji, Nahimba na Namatunu ifikapo 2017. Jukumu la Halmashauri za Wilaya ni kutenga fedha katika bajeti zao ili kuwezesha utoaji wa hati za haki miliki za kimila kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Ofisi ya Mbunge wa Nachingwea kwa kuwezesha pia kufanikisha zoezi la uandaaji wa Hati Miliki za kimila katika Kijiji cha Namatunu kwa kutumia fedha za Mfuko wa Jimbo ambapo mpaka sasa jumla ya hati 66 zimeandaliwa. Nitoe rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kutenga fedha katika bajeti zao ili wananchi wote wenye uhitaji katika Halmashauri zetu waweze kupata haki ya kumiliki ardhi zao ili kuinua pia vipato vyao.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatumia wataalam wake katika kupanga Miji na kuondokana na ujenzi holela unaoendelea nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu imeshaanza kushughulikia jambo hili kwa kuhakikisha kuwa katika kila Kanda tulizoanzisha tunapeleka wataalam wa kutosha wa fani zote. Hii yote ni kuhakikisha kuwa usimamizi wa uendelezaji miji nchini unakuwa katika viwango vinavyokubalika. Aidha, pamoja na jitihada hizo bado tuna changamoto kubwa ya uhaba wa maeneo yaliyopangwa na kupimwa nchini ambayo pia ni chimbuko la ujenzi holela katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hii, Wizara yangu imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na:-
(i) Kuandaa program ya miaka mitatu ya kuandaa mipango kabambe ya Miji, Manispaa na Halmashauri za Miji yote Tanzania. Utayarishaji wa mipango kambambe ya Miji ya Mwanza, Musoma, Singida, Kibaha, Tabora, Iringa na Mtwara upo katika hatua za kutangazwa katika gazeti la Serikali ndani ya siku 90 ili watu waweze kutoa maoni yao.
Katika Jiji la Dar es Salaam zoezi hili bado halijakamilika lakini pia katika Jiji la Arusha zoezi hili halijakamilika kwa sababu zile Halmashauri hazikuelewana kwa hiyo, inabidi wakae waridhie. Aidha, katika mwaka wa fedha 2015, Wizara yangu pia ilitoa wataalam wa Mipango Miji kusaidia utayarishaji wa mipango kabambe katika Miji ya Iringa, Mtwara na Shinyanga. (Makofi)
(ii) Vilevile, Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi kinapimwa nchi nzima na Serikali imeshaanza kufanya upimaji katika Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi kupitia mpango wa Land Tenure Support Progamme.
(iii) Kuruhusu makampuni binafsi ya Mipango Miji kushiriki katika kutayarisha mipango kabambe na mipango ya kina katika miji yote nchini.
(iv) Wizara pia ilitoa wataalam katika zoezi la urasimishaji makazi katika Manispaa ya Kinondoni katika Kata za Kimara na Saranga na katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete katika Kata ya Tandala. Katika mwaka huu wa fedha Wizara yangu inatarajia kupeleka wataalam katika Halmashauri za Manispaa ya Sumbawanga, Lindi, Kigoma Ujiji, Singida, Musoma na Tabora kwa ajili ya kuwezesha zoezi kama hilo.
(v) Vilevile kuzijengea uwezo Halmashauri nyingine ili ziweze kurasimisha maeneo yao kwa kutumia wataalam wake. Hii ni utekelezaji wa program ya miaka mitano ya urasimishaji wa maeneo ambayo hayajapangwa, ambapo Wizara yangu imeandaa mwongozo wa namna ya kufanya urasimishaji, mwongozo utakapokamilika utasambazwa katika Halmashauri zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai kwa Halmashauri zote kuandaa mipango kabambe ya maeneo ambayo yamefikia hadhi ya kuanzishwa kuwa miji ili upimaji ufanyike mapema kwa lengo la kuepusha ujenzi holela. Aidha, kwa maeneo ambayo yamejengwa kiholela Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri na wananchi wa maeneo husika tutaendelea kuboresha kwa kuyarasimisha kwa kadri ya mahitaji. (Makofi)
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITILE (K.n.y MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO) aliuliza:-
Miji mingi nchini inakabiliwa sana na uhaba wa Maafisa Ardhi na Maafisa Mipango Miji.
(a) Je, ni kwa nini Serikali isianzishe utaratibu wa kuajiri Maafisa hawa moja kwa moja wanapohitimu Vyuo Vikuu?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isichukue jukumu la kununua vifaa vya kupimia ardhi kama vile darubini, GPS na kadhalika na kuvisambaza kwenye Miji yetu ikiwemo Mji wa Kasulu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna upungufu mkubwa wa wataalam katika sekta ya ardhi na tafiti zinaonesha kwamba hadi kufikia Machi, 2016 idadi ya wataalam wa sekta ya ardhi kwa maana ya Maafisa Ardhi, Mipango Miji na Wapima Ardhi, Wathamini na Mafundi Sanifu katika Halmashauri 161 ilikuwa ni 1,087 ukilinganisha na mahitaji ya wataalam 3,040. Idadi hii ni sawa na asilimia 36 ya mahitaji kamili ya watumishi hao. Tafsiri ya mapungufu haya imekuwa ikionekana katika kiwango kidogo cha upangaji, upimaji na umilikishwaji wa ardhi iliyopimwa mijini na vijijini.
(a) Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu wa kuajiri maafisa moja kwa moja wanapohitimu Vyuo Vikuu, Serikali imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo. Mathalani katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2016/2017 Wizara yangu imeomba kibali cha kuajiri watumishi wapya 252 katika sekta ya ardhi. Kama kibali hicho cha kuajiri kitapatikana basi nina uhakika pengo litapungua ingawa ni kwa kiasi kidogo.
Hata hivyo nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuliona hili na nimwahidi kuwa Serikali imechukua wazo lake na pia itaendelea kulifanyia kazi.
(b) Mheshimiwa Spika, kuhusu ununuzi wa vifaa vya upimaji, Wizara yangu tayari imetenga kiasi cha shilingi bilioni nane katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kununua vifaa vya upimaji ambavyo vitasambazwa katika ofisi zetu za Kanda na hata hivyo Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji ndizo zenye dhamana ya kusimamia upimaji wa ardhi kwenye maeneo yao, hivyo zinapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya upimaji. Aidha, katika kukabiliana na upungufu wa vifaa vya upimaji, Wizara imekuwa ikinunua vifaa vya kupimia ardhi na kuvisambaza kwenye Halmashauri kila fedha zinapopatikana.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Shamba la Mkonge la Hale Mwakinyumbi lilimilikiwa na Chavda Ltd. lakini Serikali ililitoa shamba hilo kwa wananchi wa Hale kwa matumizi yao lakini hulimwa huku wakiwa na wasiwasi kila wakati.
Je, kwa nini Serikali isiwakabidhi rasmi wananchi wa Hale shamba hilo ili wawe na utulivu wanapoendelea na shughuli zao za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 95 la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shamba la Mwakinyumbi ni shamba linalomilikiwa na Kampuni ya Mwakinyumbi Sisal Estates Ltd. ya M/s Chavda. Bwana Chavda alinunua shamba hili kwa Mamlaka ya Mkonge Tanzania wakati wa awamu ya kwanza ya ubinafsishaji wa mashamba ya mkonge mwaka 1985 na 1988.
Mheshimiwa Spika, wakati wa ubinafsishaji sehemu ya shamba hili lilitolewa kwa wananchi wa vijiji vya Mwakinyumbi Stesheni na Hale kwa ajili ya makazi na kilimo cha mazao ya chakula. Shamba hili limeacha kuzalisha tangu mwaka 1994 baada ya kutelekezwa na mmiliki.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 20 Julai, 2016 nilifanya ziara Mkoani Tanga na katika ziara hiyo nilitembelea mashamba ya Mwakinyumbi, Magunga, Magoma na Kwashemshi yaliyopo katika Wilaya ya Korogwe. Katika kulikagua shamba la Mwakinyumbi, tulibaini kuwa shamba hili limevamiwa na wananchi na taasisi mbalimbali kwa shughuli za kilimo na uchimbaji kokoto.
Mheshimiwa Spika, tayari Wizara yangu ilishatoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kuanza utaratibu wa ubatilisho wa miliki hiyo. Hata hivyo, katika kutekeleza maelekezo haya mnamo tarehe 5 Agosti Halmashauri ilituma ilani ya siku 90 ya kusudio la kufuta miliki ya shamba hilo.
Mheshimiwa Spika, ili wananchi wa Korogwe waweze kukabidhiwa sehemu ya shamba hilo rasmi kupitia Halmashauri yao, taratibu za ubatilisho lazima zikamilishwe. Ninatoa rai kwa wananchi wa Korogwe kuwa na subira wakati Serikali inashughulikia suala hili.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako Tukufu, nitoe rai pia kwa Halmashauri zote nchini kuendelea kuainisha mashamba pori na viwanja vilivyotelekezwa ili mchakato wa kisheria wa kufuta milki zake ufanyike kwa wakati na kuondoa migogoro inayozidi kushamiri siku hadi siku.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Suala la Mpango Miji ni jema na mtu aliyepimiwa ardhi na kupata hati ya eneo lake huweza kutumia hati hiyo kukopa kirahisi lakini gharama za kupima ardhi ni kubwa sana kiasi kwamba wananchi walio wengi wanashindwa kupima maeneo yao.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kupunguza gharama za upimaji ardhi ili wananchi wengi zaidi waweze kupima maeneo yao na kuyaongezea thamani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 12 la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji wa ardhi hapa nchini unafanywa na Wapima wa Ardhi wa Serikali walioajiriwa na Serikali na Wapima Binafsi walioajiriwa na Bodi ya Wapima Ardhi na kupewa leseni za biashara ya upimaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Serikali, gharama za upimaji rasmi kwa sasa ni shilingi 300,000 kwa hekta ya shamba moja na kiwanja kimoja. Gharama hizi zilipunguzwa na kuridhiwa na Bunge lako Tukufu kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ambapo kabla ya hapo zilikuwa shilingi 800,000 kwa hekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kubwa za upimaji zinatokana na sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Halmashauri nyingi hazijajengewa uwezo wa wataalam na vifaa na jukumu la kuajiri wataalam na kununua vifaa ni la Halmashauri yenyewe hivyo upungufu wa vifaa pamoja na wataalam ni mkubwa kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili ni kwamba gharama za vifaa vya upimaji ni kubwa sana na upatikanaji wa seti moja ya kawaida ya upimaji kwa kutumia darubini ni shilingi milioni 18 kwa seti moja na GPS ni shilingi milioni 48. Ukubwa huu wa gharama na vifaa husababisha wapima wengi kutokuwa na uwezo wa kununua vifaa na hivyo kutegemea kukodi kwa gharama kubwa hivyo kufanya pia upimaji kuwa ghali ili kuweza kurejesha gharama za vifaa kwa sababu ni vya kukodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ongezeko la gharama za upimaji nchini, Serikali ina mpango wa kusogeza huduma zote zinazotolewa Wizarani kwenda kwenye kanda. Hatua hii itawezesha kanda hizo kujengewa uwezo na hivyo kuchangia kupunguza gharama. Katika kuzijengea uwezo, Serikali inategemea kununua vifaa vya upimaji katika mradi wa World Bank na kuvigawa katika kanda zake ambavyo vitasaidia Halmashauri katika kanda husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nitoe rai kwa Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji pamoja na kuajiri wataalam wa kutosha katika kada hii ya upimaji na wengine wa sekta ya ardhi ili kuondokana na gharama kubwa za kukodisha vifaa hivyo kutoka katika taasisi binafsi.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Je, ni kwa nini Serikali imekuwa hairudishi katika Halmashauri zetu 30% ya mauzo ya viwanja?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara yangu haikuwahi kuwa na utaratibu wa kurudisha asilimia 30 za mauzo ya viwanja kwa Halmashauri, kwa sababu mauzo ya viwanja hufanywa na Halmashauri husika wanapokuwa na mradi wa viwanja katika maeneo yao na Wizara hupokea ada ambazo zinahitajika kisheria katika uandaaji wa hati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 30 ya fedha ambazo zilikuwa zinarejeshwa Halmashauri ni kodi ya ardhi ambapo katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara ilipeleka mgao wa Sh. 3,541,212,774.01 kwa Halmashauri zote nchini na Halmashauri ya Babati ilipokea jumla ya Sh. 24,138,421.39.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Wizara imekuwa inakumbwa na changamoto kadhaa katika kurejesha asilimia 30 ya fedha za makusanyo. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na:-
(i) Halmashauri nyingi kutotuma taarifa za makusanyo kwa wakati ili kuiwezesha Wizara kufanya ulinganisho wa kiasi kilichopokelewa na kile kilichokusanywa.
(ii) Baadhi ya Halmashauri kutumia fedha za makusanyo kabla ya kuziwasilisha kwenye akaunti ya makusanyo ya maduhuli inayosimamiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
(iii) Wizara kupatiwa mgao mdogo wa fedha unavyopokelewa Wizarani kutoka Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imeondoa utaratibu wa marejesho ya retention ya asilimia 30 ya makusanyo ya fedha zote zinazoingia katika Mfuko Mkuu wa Hazina. Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaangalia namna bora ya kuweka utaratibu wa utoaji wa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa sekta ya ardhi katika Halmashauri zetu.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Wananchi waliojenga nyumba katika maeneo ambayo hayajapimwa wanapopata kesi hasa kwenye Mahakama ya Wilaya wanatakiwa kutoa Hati au Ofa lakini kwa kukosa nyaraka hizo ndugu au jamaa wanakosa kudhaminiwa:-
Je, Serikali haioni kuwa iko haja ya kupandisha thamani ya makazi ya wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 52 la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli maeneo mengi katika majiji na miji takribani asilimia 70 ya wakazi wake hayana miliki salama na kwa hali hiyo kukosa uhalali wa kutumika kama dhamana kuwadhamini ndugu zao pale wanapokuwa na mashauri katika Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa ardhi kama rasilimali inayoweza kuwasaidia wanyonge kujikwamua kiuchumi na kutumika kama dhamana katika mashauri ya Mahakama na shughuli nyingine za kiuchumi, Wizara yangu imefanya mambo yafuatayo:-
(i) Kuandaa program ya Kitaifa ya miaka mitano (2015 – 2020) ya kurasimisha makazi yaliyojengwa kiholela na kutoa hati miliki kwa wamiliki wake. Awamu ya kwanza ya urasimishaji wa makazi ambayo imeanza katika Kata za Kimara na Saranga katika Jiji la Dar es Salaam ambapo nyumba au viwanja 6,000 vitapimwa na kumilikishwa kwa wananchi katika kipindi cha miezi sita kuanzia Juni mpaka Disemba, 2016. Awamu ya pili itahusisha upimaji na umilikishaji wa nyumba au viwanja katika Manispaa tano za Jiji la Dar es Salaam za Kinondoni, Ilala, Temeke, Ubungo na Kigamboni) ambapo viwanja 299,000 vitapimwa.
(ii) Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri za Musoma, Tabora, Singida, Kigoma, Ujiji, Sumbawanga na Lindi mwezi Septemba 2016 imefanya tathmini ya maeneo ya urasimishaji ambapo jumla ya viwanja/nyumba 50,200 zimebainishwa kuweza kurasimishwa katika mwaka wa fedha 2016/2017. Kimsingi zoezi hili ni endelevu kwa nchi nzima na litaendelea pia kulingana na upatikanaji wa rasilimali utakavyokuwa unaruhusu.
(iii) Kuandaa progam ya miaka kumi (2015 – 2020) ya kupanga na kumilikisha kila kipande cha ardhi. Program hii ambayo itaratibiwa na Wizara yangu, itahusisha wadau wengine zikiwemo sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la urasimishaji makazi holela litaongeza thamani ya kila kipande cha ardhi kwa kuwapatia wakazi husika hati miliki baada ya kupanga maeneo yao. Aidha, litaongeza ulinzi wa ardhi na kupunguza migogoro ya ardhi na litarahisisha pia utoaji huduma muhimu za kijamii kwa kuainisha maeneo ya huduma na kuhakikisha huduma muhimu zilizokuwa zinakosekana zinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tumeshaanza kukabidhi hati katika Mkoa wa Morogoro, Mtaa wa Bingwa Kisiwani ambapo hati 28 zimetolewa na Mwanza eneo la Buhongwa hati 18 zimetolewa. Jumla ya hati miliki 46 zimetolewa kufikia tarehe 30/10/2016 ambazo imekuwa chachu kwa wananchi wengi katika maeneo mengine.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-
Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kupunguza gharama za upimaji viwanja ambazo ni kubwa sana ili kumwezesha kila Mtanzania kupata huduma hiyo na kuondoa migogoro ya ardhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe kwanza maelezo ya awali kwa sababu swali hili juzi limejibiwa, liliulizwa pia na Mbunge wa Mbozi. Kwa hiyo, majibu nitakayoyatoa pengine yanaweza yakafanana na yale yale kwa sababu swali linafanana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji wa ardhi hapa nchini unafanywa na wapima ardhi wa Serikali walioajiriwa na Serikali na wapima binafsi waliosajiliwa na Bodi ya Wapima Ardhi na kupewa leseni za biashara ya upimaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Serikali, gharama za upimaji rasmi kwa sasa ni Sh. 300,000/= kwa hekta moja ya shamba na pia kwa kiwanja kimoja. Gharama hizi zilipunguzwa na kuridhiwa na Bunge lako Tukufu mwaka 2015/2016 ambapo kabla ya hapo zilikuwa Sh. 800,000/= kwa hekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kubwa za upimaji zinatokana na sababu zifuatazo:-
(i) Halmashauri nyingi nchini hazijajengewa uwezo wa wataalam na vifaa. Jukumu la kuajiri wataalam na kununua vifaa ni la Halmashauri zenyewe ila upungufu wa vifaa na wataalam ni mkubwa kwa nchi nzima.
(ii) Gharama za vifaa vya upimaji ni kubwa. Ili kupata seti moja ya kawaida ya upimaji kwa kutumia total station ni shilingi milioni 18 na seti moja ya GPS ni shilingi milioni 48. Ukubwa huu wa gharama za vifaa husababisha wapimaji wengi kutokuwa na uwezo wa kununua vifaa na hivyo kutegemea kukodi kwa gharama kubwa na hivyo kufanya pia upimaji kuwa ghali ili kuwezesha kurejesha gharama za vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ongezeko la gharama za upimaji nchini, Serikali ina mpango wa kusogeza huduma zote zinazotolewa Wizarani kwenda kwenye kanda. Hatua hii itawezesha kanda hizo kujenga uwezo na hivyo kuchangia kupunguza gharama. Katika kuzijengea uwezo, Serikali inategemea kununua vifaa vya upimaji kupitia mradi wa Benki ya Dunia na kuvigawa vifaa hivyo kwenye kanda ambavyo vitasaidia Halmashauri katika kanda husika na hivyo kuwafikia Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, nitoe rai kwa Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji pamoja na kuajiri wataalam wa kutosha katika kada hii ya upimaji na wengine wa sekta ya ardhi ili kuondokana na gharama kubwa za kukodisha vifaa hivyo toka kwenye taasisi binafsi.
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:-
Je, ni nini umuhimu wa kuwa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 78 la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya hapa nchini yanaundwa na kusimamiwa na kifungu cha 22 cha Sheria ya Mahakama ya Ardhi Namba 2 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Spika, umuhimu wa kipekee wa Mabaraza haya ni suala zima la utatuzi wa migogoro yote itokanayo na matumizi ya ardhi nchini kwa karibu zaidi ukilinganisha na vyombo vingine vya kutatua migogoro. Hivyo, Mabaraza haya yana umuhimu mkubwa sana katika kuleta amani na muafaka katika maeneo mengi yenye migogoro ya watumiaji wa ardhi nchini.
Mheshimiwa Spika, umuhimu mwingine ni kutatua migogoro yote ya ardhi kwa haraka na kwa njia rafiki na shirikishi kwa kuwa Mabaraza haya yako karibu na wananchi wa eneo husika.
Mheshimiwa Spika, umuhimu huu umejidhihirisha katika utendaji wake. Kati ya Oktoba, 2004 mpaka kufikia Oktoba, 2016 jumla ya mashauri 131,470 yalipokelewa na kati yake mashauri 100,744 yameamuliwa na mashauri 32,176 bado yanaendelea.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia walimu kupata mikopo ya muda mrefu na yenye riba nafuu ili waweze kujenga nyumba bora za kuishi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa viti maalum kama ifuatavyo:-
Serikali inao Mfuko wa mikopo ya nyumba kwa watumishi wa Serikali inaowezesha watumishi kupata mikopo ya nyumba wakiwemo walimu. Mikopo hiyo inaweza kurejeshwa ndani ya miaka 30 lakini kabla ya mtumishi kustaafu. Masharti makuu ya kupata mkopo huo ni mhusika kuwa na hati ya kumiliki ardhi pamoja na uwezo wa kurejesha mkopo anaohitaji na kubakia na angalau theluthi moja ya mshahara wake kwa matumizi mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 1995 mpaka 2016 jumla ya walimu 95 walipata mikopo yenye jumla ya shilingi 892,254,796.50. Walimu hao ni kutoka Mikoa ya Dodoma, Tabora, Mwanza, Morogoro, Pwani, Bukoba, Musoma na Dar es Salaam.
Aidha, Serikali kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Bima ya Afya pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa imeanzisha Watumishi Housing Company mwaka 2013. Lengo kuu la kuanzisha kwa Kampuni ya Watumishi Housing ni kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya kuuzia watumishi wa umma na mashirika yake. Kampuni hii tayari imefanya makubaliano na Benki tano za biashara ili zitoe mikopo ya kununua nyumba kwa watumishi kwa masharti nafuu. Benki hizo ni Azania, CRDB, NMB, BOA na Exim.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watumishi Housing Company imeingia pia makubaliano na Mamlaka ya Elimu ya Sekondari kujenga nyumba zipatazo 240 katika mikoa 23 ya Tanzania Bara. Hivi sasa ujenzi wa nyumba 90 kwa ajili ya walimu unaendelea katika Mkoa ya Mtwara - Nanyumbu, Tandahimba na Liwale, Mkoa wa Morogoro - Kilosa, Jiji la Tanga - Mkinga, Pwani - Msata na Rufiji pamoja na Jiji la Dar es Salaam - Wilaya ya Ilala eneo la Mvuti na Singida eneo la Mkalama na pia katika Mikoa ya Simiyu na Shinyanga.
Aidha Wizara yangu kupitia mortigage financing chini ya TMRC na BOT imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 374,515,110,203 kwa wananchi 4,065 wakiwemo walimu kupitia mabenki 54 yaliyopo nchini.
MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:-
Wananchi wa Mloganzila waliopisha ujenzi wa MUHAS hawakulipwa fidia ya ardhi au angalau “mkono wa kwaheri” na wapo wenye madai ya „kupunjwa‟ fidia ya maendelezo:-
(a) Je, ni lini wananchi hao watapewa malipo yao kama Serikali ilivyoahidi?
(b) Je, ni kwa namna gani Serikali imeshughulikia madai ya mapunjo ya fidia ya maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya kuwalipa fidia ya hisani au mkono wa heri iliyotolewa na Serikali mnamo tarehe 20 Mei 2015 italipwa baada ya kupata fedha. Malipo haya hayajafanyika kutokana na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia ililipa kiasi cha Sh. 8,067,904,700 kwa ajili ya fidia ya maendelezo katika ardhi kwa wananchi 1,919 katika kipindi cha mwaka 2008 mpaka 2010. Aidha, mwaka 2011 Serikali ilitenga kiasi cha sh. 1,610,374,700 kwa ajili ya fidia ya wananchi 619 waliosalia. Fedha hizi zililipwa kama fidia ya maendelezo kwa wananchi waliokuwa wamewekeza ndani ya shamba ambalo lilikuwa mali ya Serikali. Serikali haidaiwi mapunjo kwa kuwa fidia ilishalipwa kwa mujibu wa Sheria.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Kufunguka kwa mawasiliano ya barabara za Tabora, Nzega, Tabora - Manyoni na Tabora - Kigoma kumeleta maendeleo ya kukua kwa Mji wa Tabora na kuongezeka shughuli za uwekezaji na ujenzi wa nyumba za makazi na biashara:-
Je, ni lini Serikali italeta Msajili wa Hati za Viwanja Tabora ili aweze kuidhinisha hati za viwanja kwa wakazi na wawekezaji kwa kuwa kwa sasa huduma hizo hazipo Mkoani Tabora?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Msajili wa Hati Msaidizi ameshateuliwa kwa kuzingatia Kifungu Na. 4 cha Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sura Na. 334. Tangazo la uteuzi lilitolewa katika Gazeti la Serikali la tarehe 16, Desemba, 2016, Toleo Na. 52.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Msajili Msaidizi ameshawasili kituoni. Aidha, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu mpaka sasa Wizara imeshapeleka Wasajili wa Hati katika Ofisi zote za Kanda. Rai yangu kwa Halmashauri zote nchini ni kuongeza kasi ya upimaji, upangaji na umilikishaji wa ardhi ili wananchi waweze kupatiwa hati za umiliki wa maeneo yao.
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:-
Je, ni nini umuhimu wa kurasimisha ardhi kwenye maeneo ambayo hayajapimwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, urasimishaji wa ardhi maana yake ni kutambua miliki za wananchi kwenye maeneo yaliyoendelezwa bila kupimwa kisheria. Matokeo ya urasimishaji ni kutoa hatimiliki na kuweka miundombinu ya msingi kama vile barabara, maji, mifereji ya maji ya mvua na
ikiwezekana kuweka majina ya mitaa. Kwa kawaida, urasimishaji ni zoezi shirikishi limalowezesha wananchi kukubaliana mipaka ya viwanja, kufungua njia na kutoa maeneo ya huduma za jamii kama vile shule, vituo vidogo vya polisi, makaburi, zahanati na maeneo ya wazi.
Mheshimiwa Spika, umuhimu wa kurasimisha maeneo haya ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza, urasimishaji unatoa fursa kwa wananchi kutumia ardhi kupitia nyaraka za umiliki wa ardhi kama vile hati, kuweka dhamana ya mikopo katika taasisi za fedha, mahakama.
Mheshimiwa Spika, la pili ni kuongeza thamani ya ardhi au nyumba husika (value addition) iwe kwa kuweka dhamana (collateral) rehani, upangishaji na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, tatu ni kuboresha makazi hususan kwa kuweka miundombinu ya msingi ili kurahisisha usafiri, kupunguza madhara yatokanayo na majanga mbalimbali kama vile mafuriko na moto. Kwa upana wake urasimishaji ni dhana inayochangia kupunguza umaskini.
Mheshimiwa Spika, nne ni kutoa uhakika wa milki ya ardhi na hivyo kuwa kivutio kwa mazingira ya uwekezaji. Kwa mfano, maeneo mengi ambayo yamerasimishwa, kumekuwa na uwekezaji wa shughuli za kiuchumi kama vile mahoteli, maduka, shule, hospital na maeneo ya burudani na kadhalika Mheshimiwa Spika, tano vilevile ni kupunguza migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa, urasimishaji si jibu la kudumu la kuzuia ujenzi holela mijini bali ni utayarishaji wa mipango kabambe ya miji yetu ambayo ikienda sambamba na uimarishaji wa usimamizi na uthibiti wa uendelezaji miji itaweka ustawi mzuri wa mandhari ya nchi yetu na hivyo kufanya nchi yetu kuwa sehemu nzuri ya kuishi.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE Aliuliza:-
Nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ni za muda mrefu na zimekuwa chakavu sana na nyingine zimeanza kubomoka.
(a) Je, ni lini Serikali itafanya operesheni kubaini uharibifu ulioko kwenye nyumba hizo?
(b) Je, ni lini Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya kukarabati au kujenga upya nyumba hizo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Savelina Silvanus Mwijage, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambazo ni za muda mrefu na kati ya hizo zipo zilizo katika hali chakavu ambazo idadi yake si kubwa sana ukilinganisha na nyumba zilizo katika hali nzuri kimatengenezo. Ili kuhakikisha nyumba zote zinakuwa katika hali nzuri na bora kimatengenezo, Shirika limeweka mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba nyumba zote zilizo katika hali ya uchakavu zinafanyiwa ukarabati mkubwa na kwa nyumba ambazo kiwango cha ukachakavu ni kikubwa sana (beyond repair) shirika limeweka utaratibu wa kuzivunja na kuendeleza upya viwanja hivyo kwa kujenga majengo ya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba la Taifa limefanya uhakiki wa nyumba zake zote na kubaini hali halisi ya kila nyumba na kuweka mpango wa kuzifanyia ukarabati nyumba hizo kwa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 shirika lilitenga takriban shilingi bilioni 11, kwa ajili ya kuzifanyia ukarabati nyumba zake ambapo hadi Machi, 2017 jumla ya nyumba 2,451 zilikuwa zimekwishafanyiwa ukarabati mkubwa kupitia bajeti hiyo. Aidha, idadi ya nyumba zilizofanyiwa ukarabati mkubwa inatarajiwa kuongezeka ifikapo mwisho wa mwezi Juni, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, shirika linatarajia kumaliza kuzifanyia ukarabati nyumba zote katika Mwaka wa Fedha 2017/2018. Hata hivyo, ni vema ikafahamika kuwa matengenezo ya nyumba ni kazi endelevu kwa shirika, hivyo bajeti ya matengenezo itaendelea kutengwa kila mwaka ili wapangaji wa nyumba za shirika waendelee kuishi katika nyumba na mazingira bora.
MHE. HAWA A. GHASIA (K.n.y. MHE. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kupima ardhi yote ya Tanzania na kuipangia matumizi yaliyo bora kufuatia kuwepo kwa tatizo kubwa la migogoro ya ardhi kati ya wakulima, wafugaji na Mamlaka ya Hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuondoa migogoro ya ardhi kote nchini na ili kufikia azma hiyo, Serikali imeandaa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa programu
hii, kila kipande cha ardhi nchini kitapangiwa matumizi na kupimwa, hali ambayo itaondoa mwingiliano baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi na hivyo kupunguza uwezekano wa kuibuka kwa migogoro ya ardhi. Mpango huu utasaidia ardhi yote kutunzwa na watumiaji husika na kuhifadhi maliasili zilizopo katika mazingira kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, pia jamii inayozunguka maeneo
hayo yaliyohifadhiwa itawezeshwa kutambua mipaka yao na kuwa na mipango ya matumizi ya ardhi na kudhibiti uvamizi wa maeneo ya hifadhi. Aidha, utekelezaji wa programu hii utajenga uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda ardhi inayomilikiwa dhidi ya uvamizi wowote, kuwezesha kukabliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, kuboresha makazi ya wananchi na kuleta usalama na ustawi wa maliasili za Taifa.
Mheshimiwa Spika, programu ya kupanga, kupima
na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini itahusisha Halmashauri zote 181 nchini na imepangwa kufanyika katika kipindi cha miaka kumi kwa awamu ya miaka mitano kwa kila awamu kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.
Aidha, programu hii itakuwa na miradi mikubwa miwili ambayo ni miradi ya upimaji wa kila kipande cha ardhi vijijini na mradi wa upimaji wa kila kipande cha ardhi mijini.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa programu hii kwa awamu ya kwanza, umeanza kupitia Mradi wa Land Tenure Support Program ambao unatekelezwa katika Wilaya tatu za mfano katika Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga ambayo hadi sasa jumla ya mipaka ya vijiji 50 imeshapimwa na kazi ya uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi, upimaji wa vipande vya ardhi na utoaji wa hatimiliki za kimila, unaendelea.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Tatizo la makazi duni kwa wananchi husababisha afya mbovu na hivyo kupunguza nguvu ya uzalishaji.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata makazi bora?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Hali Halisi ya Miji Tanzania iliyoandaliwa na Mtandao wa Miji nchini (Tanzania Cities’ Network - TACINE) ya mwaka 2014, wastani wa kiwango cha ujenzi holela katika miji saba ya Tanzania Bara na Manispaa ya Zanzibar ilibainika kuwa ni asilimia 67 ya maneno yaliyojengeka. Mengi ya maeneo haya hayana miundombinu na huduma za msingi kama vile maji safi na salama, barabara na mifereji ya maji ya mvua na udhibiti wa maji taka na taka ngumu. Hali hiyo husababisha mafuriko, milipuko ya magonjwa, mazalio ya mbu na inzi, na mandhari mbaya ya kuishi yanayopelekea afya duni na kupunguza nguvukazi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali imeandaa programu na mikakati mbalimbali kukabiliana na hali hiyo kama ifuatavyo:-
(i) Programu ya Kitaifa ya Kurasimisha Makazi Holela Nchini ambayo inalenga mwaka 2013 mpaka 2023 inayolenga kurasimisha makazi mijini na kutoa fursa kwa maeneo kupangwa, kupimwa na kumilikishwa na kisha kutoa huduma za msingi na miundombinu.
(ii) Programu ya Kitaifa ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Kila Kipande cha Ardhi ya mwaka 2015 mpaka 2025 inayolenga, pamoja na mambo mengine, kuzuia kudhibiti ujenzi holela ambao husababisha kuwepo kwa makazi duni; na
(iii) Kuandaa mipango Kabambe katika Miji (Master Plans) kwa miji 30 kwa kushirikisha Halmashauri za miji na Wilaya itakayosaidia kusimamia na kudhibiti uendelezaji miji. Hadi sasa Mipango Kabambe ya Arusha, Mwanza, Singida, Tabora, Mtwara, Kibaha, Musoma, Korogwe na Songea imeandaliwa na makampuni binafsi na ipo katika hatua za mwisho za maandalizi.
Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa mamlaka na Serikali za mitaa kutenga fedha za kutosha katika bajeti zao kila mwaka kwa ajili ya kuongeza kasi ya kupima, kupanga na kumilikisha ardhi katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kupata makazi bora.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Jimbo la Tabora Mjini hususan katika Kata za Mpera, Malolo, Mbugani na Ng’ambo (Kidongo Chekundu) kuna migogoro ya muda mrefu ya ardhi na bomoa bomoa ya nyumba za wananchi.
Je, Serikali inafanya juhudi gani kuhakikisha inamaliza migogoro hiyo ya ardhi ambayo ni kero ya muda mrefu kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA, MAENDELEO NA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama Ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwepo na migogoro ya ardhi mingi baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi katika Jimbo la Tabora Mjini hususani katika kata za Mpera, Malolo, Mbugani, Ng’ambo na Kidongo Chekundu. Migogoro mingi inahusiana na madai ya fidia, kuingiliana kwa mipaka, kutozingatiwa kwa taratibu za uendelezaji, uvamizi wa maeneo yaliyopangwa kupimwa na kumilikishwa na miliki pandikizi.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na migogoro hiyo Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya urasimishaji wa maeneo yote ambayo yalikuwa yamevamiwa na kujengwa kiholela ili kuweka miundombinu ya huduma muhimu katika maeneo hayo. Vilevile Serikali imeimarisha ushirikishaji wa sekta binafsi katika kuanga na kupima viwanja kwa kushirikiana na wananchi ambapo makampuni binafsi ya upangaji na upimaji yaliyosajiliwa yameshaanza kufanya kazi ya kupanga na kupima katika maeneo ya Uledi, Kariakoo na Inala. Aidha, Mpango Kabambe wa Mji wa Tabora, (Tabora Master Plan 2015 - 2035) utatoa dira ya upangaji usimamizi na uendelezaji wa ardhi katika mji wa Tabora.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu pia imekuwa ikisisitiza Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha uwepo wa fedha kwa ajili ya kulipia fidia kabla ya kufanya zoezi la uthamini wa mali kwa ajili ya utoaji wa ardhi ili kuzuia uwezekano wa kuibuka kwa migogoro ya ardhi inayohusiana na fidia. Aidha, wamiliki wa ardhi wamekuwa wakishirikiana na makampuni binafsi ya upangaji na upimaji katika hatua zote za upangaji na upimaji wa viwanja katika maeneo yao ili kuhakikisha kuwa maslahi ya pande zote yanalindwa.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Kumekuwa na ujenzi wa nyumba za ghorofa kando kando ya barabara kuu na Serikali ndiyo inatoa vibali vya ujenzi huu ambapo baada ya muda maghorofa hayo yanaweza kubomolewa na mwenye jengo kulipwa fidia.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuainisha maeneo yenye mipango ya maendeleo ili kuepuka gharama kubwa ya kulipa fidia?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MANDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na ujenzi wa nyumba za ghorofa na za kawaida kando kando ya barabara kuu na barabara nyingine. Kasi ya ujenzi wa nyumba hizo huchochewa na kuimarika kwa miundombinu hususan barabara za kiwango cha lami. Uimarishaji wa barabara za lami huvutia wawekezaji kujenga nyumba za biashara, vituo vya mafuta, mahoteli pamoja na makazi. Hali hii ni ya kawaida katika uendelezaji miji kwa kuwa uboreshaji miundombinu hususan barabara hupandisha thamani ya ardhi katika eneo husika na kuvutia ujenzi wa majengo ya ghorofa.
Mheshimiwa Spika, ili kupunguza uwezekano wa kubomoa au kulipa fidia maeneo yaliyoendelezwa kwa ujenzi wa nyumba za ghorofa, Serikali imejiwekea mikakati ifuatayo:-
(i) Kuanisha meneo yote ambayo yameiva kiundelezaji upya (areas ripe for redevelopment) ili kuoanisha matumizi ya sasa na ya baadaye.
(ii) Kupanga maeneo hayo ili uendelezaji wake uendane na thamani ya ardhi na kuboresha sura ya miji. Mipango kina ya uendelezaji maeneo haya ni kama vile Kariakoo, Kurasini, Temeke, Msasani, Oysterbay, Magomeni na Ilala.
(iii) Kwa upande wa miji mingine, upangaji wa maeneo haya unazingatiwa katika utayarishaji wa mipngo kabambe (master plan) ya miji husika.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa nyumba za ghorofa kando ya barabara kuu hauna budi kufuata taratibu za mipango miji, uhandisi, mazingira na masharti ambayo muendelezaji hupewa katika kibali chake cha ujenzi. Natoa rai kwa taasisi zenye mamlaka ya kutoa vibali vya ujenzi ambazo ni Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa pamoja na Majiji kuzingatia masharti ya uendelezaji wa miji ili kuzuia uwezekano wa kubomoa maghorofa na kulipa fidia.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Lengo la Serikali ni kuwainua kiuchumi wananchi maskini vijijini hasa wanawake ambao hawana dhamana ya kuweka benki ili waweze kupata mikopo kwa sababu nyumba nyingi za vijijini hazina Hatimiliki ambazo zingeweza kutumika kama dhamana benki.
Je, Serikali inawasaidiaje wananchi na hasa wanawake kwa kuzungumza na benki ili zikubali kukpokea Hatimiliki za kimila kama dhamana ya mikopo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa Hatimiliki za kimila ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999 na kanuni zake. Utoaji wa hati za Hakimiliki ya kimila ulianza mwaka 2004 Wilayani Mbozi na baadae uliendelea katika Wilaya zingine ambapo hadi sasa takribani hati za Hakimiliki za kimila 400,761 zimekwishatolewa kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 18(1) cha Sheria ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999, hati za Hakimiliki za kimila zina hadhi sawa kisheria na hati inayotolewa na Kamishna wa Ardhi. Hadi sasa hati za Hakimiliki za kimila zimewezesha wananchi kupata mikopo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 59 kutoka taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo NMB, CRDB, TADB, Stanbic Bank, Meru Community Bank, Agricultural Trust Fund Bank, SIDO, NSSF na Mfuko wa Pembejeo katika Wilaya ya Mbozi, Iringa, Babati, Bariadi, Arumeru, Mbarali, Manyoni, Kilombero, Bagamoyo, Mbinga na Tandahimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, baadhi ya taasisi za fedha zimekuwa hazikubali kupokea hati za Hakimiliki ya kimila kama dhamana kwa wananchi kupata mikopo. Sababu ambazo zimekua zikitolewa na taasisi hizo ni pamoja na baadhi ya maeneo kutokuwa na thamani au ardhi husika kutoendelezwa; vikwazo katika kuuza dhamana pale mkopaji anaposhindwa kurejesha mkopo kutokana na sharti la kutaka ardhi iuzwe kwa mkazi wa kijiji husika na baadhi ya wamiliki wa ardhi kutokuwa na sifa za kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hizo, Wizara yangu kupitia marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 yanayoendelea inaangalia uwezekano wa kuondoa vikwazo vinavyozuia uuzaji wa dhamana pale mkopaji anaposhindwa kurejesha mkopo pamoja kuzungumza na taasisi za fedha kuwa hati ya Hakimiliki ya kimila ina hadhi sawakisheria na hati inayotolewa na Kamishna wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, wananchi hawana budi kuyaendeleza maeneo yao hususani yale yaliyopatiwa hati za Hakimiliki za kimila ili kuyaongezea thamani na hivyo kuzishawishi taasisi za fedha kuyakubali maeneo hayo kama dhamana ya mikopo.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Wananchi wengi Sumbawanga hawana hati miliki; aidha, kumekuwa na changamoto nyingi katika kupata hati hiyo hali inayowafanya wananchi kukata tamaa.-
Je, ni gharama kiasi gani zinazohitajika ili kupata hati miliki?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida hati miliki za ardhi hutolewa kwa utaratibu wa mwombaji kuchangia gharamaza upatikanaji wa hati husika. Utaratibu huu umetokana na matakwa ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 95 ambayo inaelekeza kuwa ardhi ina thamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za kupata hati miliki hutofautiana kutokana na thamani ya ardhi katika eneo linaloombewa hati, ukubwa wa eneo na matumizi yanayokusudiwa katika eneo husika. Kwa mantiki hiyo, gharama za kupata hati miliki hutofautiana kwa kuzingatia vigezo hivyo. Gharama zinazotakiwa kulipwa wakati wa umilikishaji ardhi ni kama ifuatavyo:-
Ada ya upimaji;
(ii) Ada ya uandaaji wa hati ambayo ni shilingi 50,000 ni fixed;
(iii) Ada ya usajili wa hati;
(iv) Ushuru wa stempu;
(v) Gharama za upatikanaji ardhi;
(vi) Ada ya mbele (premium) ambayo ni asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi; na
(vii) Ada ya ramani ndogo (Deed Plan) ambayo ni shilingi 20,000 nayo ni fixed.
Mheshimiwa Naibu Spika, ada ya upimaji, usajili wa hati, ushuru wa stempu na gharama za upatikanaji ardhi hutegemea ukubwa na thamani ya ardhi katika eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwa na uwiano wa gharama za umilikishaji wa ardhi nchini, Wizara imeandaa na kusambaza mwongozo wa ukadiriaji wa bei za viwanja kwa Halmashauri zote nchini. Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini hazina budi kuzingatia mwongozo wa bei elekezi za viwanja uliotolewa ili kuwawezesha wananchi kupata hati miliki kwa gharama nafuu zaidi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Shamba la Kampuni iliyokuwa ikiitwa Tanganyika Packers lenye ekari 45,000 katika Halmashauri ya Itigi limetelekezwa kwa muda mrefu na wananchi wa kata nne (4) na vijiji 12 wamekuwa wakilitumia kwa kilimo na ufugaji:-
(a) Je, ni lini Serikali itapendekeza kwa Mheshimiwa Rais kufutwa kwa hati hiyo?
(b) Je, ni lini Serikali italirudisha rasmi shamba hilo kwa Halmashauri ya Itigi ili lipangiwe matumizi kwa ajili ya wakulima na wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba lenye hati namba 15467 na ukubwa wa ekari 45,000 lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi lilimilikishwa kwa Kampuni ya Tanganyika Packers Limited mwaka 1955 kwa muda wa miaka 99 kwa matumizi ya ufugaji (cattle holding).
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba limezungukwa na Vijiji vitatu vya Kitaraka, Doroto na Kaskazi ambavyo wananchi wake kupitia uongozi wa vijiji wamekuwa wakikodishwa maeneo ya kilimo na ufugaji kutokana na shamba hilo kutoendelezwa na Mwekezaji kwa muda mrefu. Baada ya Mwekezaji kushindwa kutimiza masharti ya uendelezaji wa shamba hili, Serikali ililitaifisha shamba hili pamoja na majengo yaliyokuwa ndani yake na kuliweka chini ya uangalizi wa msajili wa Hazina. Aidha, kwa nyakati tofauti kupitia vikao vya viongozi na wananchi, Serikali imekuwa ikikataza wananchi kuvamia shamba hili kwa kuwa ni mali halali ya Serikali kwa ajili ya mipango ya uwekezaji lakini wananchi wamekuwa wakikaidi makatazo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, shamba hili ni mali halali ya Serikali hivyo wananchi waliovamia na kufanya maendelezo ndani ya shamba hili ni kinyume na taratibu na hivyo wasitishe shughuli zao mara moja. Serikali inaendelea kuandaa mpango wa uwekezaji utakaoleta tija ya maendeleo kwa Taifa hasa kwa wananchi wanaozunguka shamba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Itigi katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Tayari walishaleta maombi Serikalini kwa Msajili wa Hazina kwa lengo la kutaka kuingia ubia na Mwekezaji ili kuliendeleza shamba hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inayafanyia kazi maombi hayo na itatoa taarifa kamili baada ya kukamilisha tathmini ya faida na hasara zitakazotokana na uwekezaji unaopendekezwa. Natoa rai kwa viongozi wa Serikali za Vijiji na Kata kuacha kugawia wananchi eneo hilo kwa mtindo wa kuwakodisha kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za sheria ya nchi.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Manispaa ya Mtwara Mikindani ina migogoro mikubwa ya ardhi inayokaribia kusababisha uvunjifu wa amani:-
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kutatua migogoro hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali Na. 50 la Mheshimiwa Mftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kumekuwepo changamoto ya kuibuka kwa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua na jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kuwa migogoro hiyo inapungua au inamalizika kabisa.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo, Wizara iliwataarifu Waheshimiwa Wabunge kuwasilisha taarifa za migogoro iliyopo katika maeneo yao. Aidha, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya waliombwa kuwasilisha taarifa za mashamba makubwa yaliyotelekezwa na migogoro iliyopo katika mikoa yao kupitia barua yenye Kumb. Na. EA 171/438/01 ya tarehe 21 Desemba, 2015.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea taarifa za migogoro kutoka katika maeneo mbalimbali, Wizara imekuwa ikiyapitia hayo na kutatua migogoro kama ilivyowasilishwa kutoka kwa viongozi wa maeneo husika.
Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Mtwara, Wizara ilipokea taarifa za migogoro mbalimbali ikiwemo migogoro mikubwa. Kati ya iliyopokelewa ilikuwa ni mgogoro wa Shamba la Chumvi, maarufu kama Libya; mgogoro wa Mjimwema na Tangila, maarufu kama UTT; mgogoro wa mipaka baina ya wakazi wa Mtepwezi na Jeshi la Magereza Lilungu; mgogoro kati ya wananchi wa Mangamba na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege; na mgogoro baina ya wananchi wa Mbae Mashariki na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mheshimiwa Spika, kuhusu mgogoro katika eneo la Libya, wananchi walifikisha suala hilo Mahakamani na sasa shauri hilo lipo katika Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara kama Shauri la Madai Na. 7 la mwaka 2014. Kwa upande wa mgogoro wa UTT, mgogoro huu nao ulifikishwa Mahakamani kama Shauri la Madai Na. 8 la mwaka 2015 ambapo wananchi 723 wanadai fidia Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara na wapo tayari kuiondoa kesi hiyo Mahakamani endapo watalipwa fidia hiyo. Aidha, shauri hili litakuja Mahakamani kwa ajili ya usuluhishi wa mwisho tarehe 18, Septemba, 2017.
Mheshimiwa Spika, kwa maeneo mengine nchini ambayo yalitembelewa na timu ya wataalam wa kisekta iliyoundwa kuchunguza vyanzo vya migogoro ya ardhi na kupendekeza namna ya kuzitatua, Serikali itahakikisha kuwa migogoro yote inatatuliwa kwa wakati kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya Kampuni ya Highland Estate Mbarali na wananchi wanaolizunguka shamba hilo kwa kuwa mwekezaji amekuwa akipora ardhi kwa wananchi na kusababisha uvunjifu wa amani kwa muda mrefu sasa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, shamba linalomilikiwa na Kampuni ya Highland Estate awali lilikuwa likimilikiwa na Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula kuanzia mwaka 1978. Baada ya upimaji kukamilika 1981, shamba hilo liliendelea kumilikuwa na NAFCO kwa Hati Na. 327–DLR. Tarehe 18 Agosti, 2008 shamba hili liliuzwa na Serikali kwa Kampuni ya Highland Estate Ltd.
Mheshimiwa Spika, mgogoro wa shamba la Highland Estate unahusu tafsiri ya mipaka baina ya shamba hilo na vijiji vya Mwanavala, Ibumila, Imalilo, Songwe, Urunda, Ubaruku, Utyego, Mbarali, Mpakani, Mkombwe, Mwakaganga, Ibohola na Nyelegete.
Mheshimiwa Spika, hatua za awali za utatuzi wa mgogoro huu zinahitaji kupata tafsiri sahihi ya mpaka wa shamba kulingana na ramani ya upimaji iliyoidhinishwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na vijiji vinavyozunguka shamba hilo. Zoezi la kutafsiri mipaka baina ya shamba na vijiji husika limeshaanza kufanyiwa kazi na wataalam wa Ofisi ya Mkuu wa wa Mkoa wa Mbeya, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbarali pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kwa kushirikiana na wanakijiji husika isipokuwa wanakijiji wa kijiji cha Nyelegete ambao wamesusia zoezi hili.
Mheshimiwa Spika, juhudi za kutatua mgogoro huu bado zinaendelea kufanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kwa kuwahimiza kijiji cha Nyalegete kutoa ushirikiano kwenye utatuzi wa mgogoro huu ili uweze kumalizika.
Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kutoa ushirikiano kwa wataalam wa sekta ya ardhi katika maeneo yao ili kuharakisha utatuzi wa migogoro ya ardhi hususan inayohusiana na mipaka ya mashamba. Aidha, napongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa utaratibu wake wa kusikiliza kero za wananchi ikiwemo kutatua migogoro ya ardhi mara mbili kwa kila mwezi.
MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:-
Msongamano wa magari, ujenzi holela, miundombinu duni ya maji taka na kadhalika katika miji mikubwa hapa nchini vinatokana na udhaifu wa upangaji wa matumizi bora ya ardhi (poor land use planning).
Je, Serikali imejiandaa vipi kuendesha zoezi la Mipango Miji na matumizi bora ya ardhi katika miji mipya ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu Namba 7(1) cha Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007 kinaelekeza kuwa jukumu la upangaji na uendelezaji miji lipo chini ya mamlaka za upangaji ambazo ni Halmashauri za Majiji, Manispaa Miji, Wilaya na Mamlaka za Miji Midogo. Kutokana na umuhimu wa kuwa na Miji iliyopangwa kiuchumi na kijamii, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo uandaaji wa mipango kabambe itakayotumika kuongoza, kusimamia na kudhibiti uendelezaji wa Miji pamoja na urasimishaji wa makazi yasiyopangwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Hadi kufikia Oktoba 20, 2017 maandalizi ya mipango kapambe ya miji 29 nchini ilikuwa imefikia katika hatua mbalimbali. Maeneo hayo ambayo tayari mipango yake ipo katika hatua mbalimbali ni Majiji ya Mwanza, Da es Salaam, Arusha na Tanga na kwa upande wa Manispaa tunayo Mtwara - Mikindani, Iringa, Musoma, Tabora, Singida, Sumbawanga, Songea, Shinyanga, Morogoro, Lindi, Bukoba, Moshi, Mpanda na Kigoma Ujiji. Kwa upande wa miji midogo ni Kibaha, Korogwe, Njombe, Bariadi, Geita, Babati, Ifakara, Mahenge, Malinyi, Tunduma na Mafinga. Kati ya maeneo hayo, mipango kabambe kwa Manispaa ya Mtwara - Mikindani, Musoma, Iringa na Singida imeshaidhinishwa na kuzinduliwa na hivyo imeanza kutumika rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uandaaji wa mipango kabambe hufanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo makampuni ya upangaji na upimaji ardhi yaliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria, wamiliki wa ardhi, taasisi za Serikali, watu binafsi na asasi za kiraia pamoja na taasisi, zinatoa huduma mbalimbali za miundombinu kama vile TANESCO, TANROADS na Mamlaka za Maji Safi na Maji Taka. Utekelezaji wa mipango hiyo husaidia kutatua changamoto zilizopo na hatimae kuwa na miji iliyopangwa na yenye mtandao mzuri wa miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango kabambe wa Mji wa Njombe unaandaliwa na Kampuni ya CRM Land Consult ya Dar es Salaam kupitia programu ya Urban Local Government Strengthening Program iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Hadi sasa rasimu ya kwanza ya mpango kabambe ya mji huo imeandaliwa na hatua inayofuata ni kuwasilisha rasimu hiyo kwenye mikutano ya wadau kwa ajili ya kupokea maoni na mapendekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa wito kwa mamlaka za upangaji ambazo hazina mipango kabambe, kuanza maandalizi ya mipango hiyo pamoja na kongeza kasi ya kupanga maeneo mapya, kurasimisha makazi yasiyopangwa na kudhibiti uendelezaji holela kwa kushirikiana na makampuni yaliyosajiliwa kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa sheria.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Kutokana na uvamizi wa ardhi katika maeneo ya mashule, masoko na zahanati.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha upimaji wa maeneo hayo?
(b) Je, kutokana na ukubwa wa gharama za upimaji, kwa nini zoezi la upimaji lisitolewe bure kwa taasisi za umma kupitia Halmashauri hizo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya shule, soko, zahanati, vituo vya afya, hospitali, vyuo, ofisi za Serikali, vituo vya polisi, mahakama, maeneo ya majeshi, hifadhi za misitu na wanyama na maeneo ya makumbusho hutengwa maalum kwa ajili ya matumizi ya umma na shughuli mbalimbali za Serikali. Maeneo yote haya yapo chini ya usimamizi na uangalizi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa au Serikali Kuu. Hata hivyo, maeneo mengi kati ya hayo yamekuwa yakisimamiwa na taasisi za Serikali bila kupimwa wala kuwa na hatimiliki badala yake yamekuwa yakimilikishwa kwa utaratibu wa kupewa government allocation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu pamoja na kwamba umekuwa ukifanywa kwa nia njema, umetoa mwanya kwa wananchi wenye nia ovu kuyavamia, kuyamega na kuyaendeleza maeneo ya Serikali kinyume na utaratibu. Ili kuhakikisha kuwa changamoto ya uvamizi wa maeneo ya umma unakomeshwa, Serikali kupitia Wizara yangu iliagiza kuwa maeneo yote ya umma, yapimwe na yamilikishwe kwa taasisi husika kupitia barua yenye Kumb. Na. AB225/30/305/01 ya tarehe 7 Septemba, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuitikia wito huu baadhi ya taasisi za Serikali ikiwemo TBA, Hazina na TANROADS zinaendelea kuyatambua maeneo yake na kuyamilikisha maeneo wanayoyasimamia. Nitoe rai kwa Wakuu wote wa taasisi za umma kuhakikisha wanakamilisha zoezi hili mapema na kwa maeneo ambayo yamevamiwa ni vema wavamizi wakaondoka kwa hiari yao na wasisubiri mkondo wa sheria uwakumbe. Aidha, nampongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Tabora na timu yake kwa kutekeleza agizo la Waziri kwa vitendo na ni vema Wakuu wote wa Mikoa wengine wakachukua hatua ili kuondoa wavamizi kwenye maeneo yote ya umma.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama elekezi za huduma za upimaji ambazo kwa mara ya mwisho zilifanyiwa mapitio mwaka 2016 siyo kubwa kama inavyodhaniwa kwa kuwa upimaji wa ardhi hufanywa kwa misingi ya kurejesha gharama pakee. Gharama hizo hujumuisha vifaa vya upimaji, shajara, usafiri, matengenezo ya vifaa na mawasiliano ya kitaalam. Aidha, kukamilika kwa mtandao wa upimaji (Taref 11) tutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za upimaji nchini.
Mheshimia Mwenyekiti, natoa rai kwa taasisi zote za Serikali nchini kuhakikisha zinapima na kumilikishwa maeneo yao ili kuwa na miliki salama kwa kuwa ulinzi wa ardhi wanayomilikishwa ni jukumu la taasisi husika. Aidha, taasisi zote za umma nchini zinahimizwa kutenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kuharakisha upimaji wa maeneo yote wanayoyasimamia.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-
Kumekuwa na upandaji holela wa gharama za pango kwa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kudhibiti upandaji holela wa pango ambao unaathiri wananchi wengi kutokana na kipato chao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba la Taifa linaendeshwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na miongozo ya Serikali. Aidha, masuala ya upingaji wa kodi huongozwa na Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na sheria iliyoanzisha Shirika la Nyumba la Taifa Na. 2 ya mwaka 1990 kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005. Sheria zote mbili zimeweka viwango ambavyo mmiliki wa nyumba ikiwemo Shirika la Nyumba la Taifa anapaswa kuzingatia katika ukadiriaji wa kodi za pango. Miongoni mwa vigezo hivyo ni ukubwa wa nyumba, mahali nyumba ilipo, hali ya nyumba na kodi za Serikali zinazolipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kurekebisha viwango vya kodi ya nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa husimamiwa na bodi ya wakurugenzi ambayo imepewa mamlaka ya kisheria ya kusimamia kodi ya pango pamoja na kuidhinisha viwango vya kodi vitanavyotozwa kwa wapangaji wa nyumba za Shirika la Nyumba. Tangu mwaka 1990 shirika limefanya marekebisho ya kodi kwa miaka 6; 1994, 1999, 2001, 2005, 2007, 2008 na 2011.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na marekebisho hayo, bado viwango vya kodi ya pango kwa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa ni kati ya asilimia 42 hadi 80 ya viwango vya soko. Kwa mfano, eneo la Masaki Shirika la Nyumba la Taifa hutoza kodi ya shilingi 1,700 kwa kila mita ya mraba wakati bei ya soko katika eneo hilo ni kati ya shilingi 12,000 hadi 30,000 kwa mita mraba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara ya mwisho Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa iliidhinisha viwango vipya kwa kutoza kodi kwenye nyumba za shirika mwaka 2011 ambavyo ndivyo vinatumika mpaka sasa. Utaratibu wa kupandisha kodi kwa sasa hufanyika pale mkataba wa mpangaji unapomalizika na mpangaji kuomba kuhuisha mkataba wake. Ieleweke kuwa kodi zinapanda kwa mujibu wa sheria na pale mkataba wa mpangaji unapomaliza muda wake.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA,aliuliza:-
Kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi nchini inayosababisha uvunjifu wa amani miongoni mwa wananchi na hata katika baadhi ya maeneo migogoro hiyo imesababisha vifo;
(a) Je, Serikali imechukua hatua gani kutatua migogoro hiyo?
(b) Kwa kuwa Maafisa Ardhi wengi ndiyo chanzo cha migogoro hiyo, je, ni Maafisa Ardhi wangapi wamechukuliwa hatua kwa kusababisha migogoro hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu kwanza kwa sababu ni mara ya kwanza mwaka huu niwatake heri ya mwaka mpya wote na tumshukuru Mungu kwamba tunaendelea kulijenga Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa migogoro ya ardhi nchini na tayari imeweka mikakati mbalimbali ya kuitatua na kuzuia uwezekano wa kuibuka migogoro mipya. Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na:-
(i) Kutoa elimu kwa watendaji wanaohusika na utatuzi wa migogoro ya ardhi kuanzia ngazi za Serikali za Mitaa hadi Serikali Kuu na kuzifanyia marekebisho sera na sheria mbalimbali zinazosimamia sekta ya ardhi;
(ii) Kuboresha Mabaraza ya Ardhi na kuyaongezea watumishi pamoja na vitendea kazi;
(iii) Kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ya wilaya na vijiji; na
(iv) Kutekeleza mkakati wa kupima kila kipande cha ardhi nchini na kuboresha mifumo ya kutunza kumbukumbu za ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara imeanzisha utaratibu wa kushughulikia migogoro ya ardhi ambapo Mheshimiwa Waziri akiambatana na wataalam wa sekta ya ardhi amekuwa akikutana na wananchi papo kwa papo na kutatua migogoro na changamoto zinazowakabili kwa mfumo ambao tunaita Funguka na Waziri wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi kwa namna moja ama nyingine husababisha pia na watendaji wa sekta ya ardhi wasio waaminifu; lakini Serikali imeendelea kuwachukulia hatua maofisa hao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2014/2015 na 2016/2017, watumishi wanne wamesimamishwa kazi baada ya kufikishwa Mahakamani kutokana na ukiukwaji wa maadili ya Utumishi wa Umma; watumishi 16 walifukuzwa kazi kwa makosa mbalimbali ya kiutendaji; na watumishi 19 waliandikiwa barua za onyo na kutakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa watendaji wa sekta ya ardhi walio chini ya usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Wizara imekuwa ikishirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika kuhakikisha kuwa hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya watendaji hao ambao wamekuwa wakisababisha migogoro kutokana na kutowajibika au kukiuka masharti ya ajira zao.
MHE. JULIUS K. LAZIER aliuliza:-
Hivi karibuni Serikali ilitoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa kusimamia urejeshwaji wa mashamba makubwa ambao hayakuendelea yakiwemo ya Wilaya ya Monduli.
Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kufuta mashamba 25 katika Wilaya ya Monduli ambayo mchakato wake kwa ngazi ya Halmashauri umekamilika?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer Mbunge wa Monduli kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia maelekezo ya Serikali kwa mikoa kusimamia urejeshwaji wa mashamba yasiyoendelezwa nchini, Wizara yangu imekuwa ikipokea mapendekezo ya kubatilisha miliki za mashamba na viwanja ambavyo wamiliki wake wakiuka masharti ya kumiliki ardhi kwa kutoendeleza, kutelekeza au kuendeleza kinyume na masharti au kutolipa kodi ya pango la ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ilifanya ukaguzi kwa mashamba 25 ambayo yalikuwa hayajaendelezwa. Katika ukaguzi huo ilibainika kuwa kati ya mashamba yaliyokaguliwa, mashamba 12 hayakuwa na nyaraka kamili za umiliki, kwa maana ya barua ya toleo au hati na hivyo kutokuwa halali kwa kubatilishwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri iliwasilisha mapendekezo ya kufutwa mashamba 13 tu na Wizara yangu imekamilisha utaratibu wa kubatilisha miliki za mashamba hayo yote 13 yaliyopo katika maeneo ya Mswakini Juu, Lolkisale na Maserani yenye ukubwa wa jumla ya ekari 131,873.35 Mashamba haya yamerejeshwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuandaliwa mpango wa matumzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nichukue fursa hii kuwakumbusha Halmashauri kuwa maeneo yanayorejeshwa kwao wakumbuke kuwa na mpango mzuri wa matumizi ikiwepo kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji pamoja na matumizi mengine ya wananchi. Hata hivyo hadi leo Wilaya na Mkoa hawajaleta mapendekezo rasmi ya kutumia ardhi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inaendelea kupokea na kushughulikia mapendekezo ya kubatilisha milki za mashamba mengine kutoka Halmashauri mbalimbali nchini baada ya wamiliki kupewa ilani kwa mujibu wa sheria.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Wilaya ya Muheza imetenga eneo sehemu ya Chatur kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za NHC za bei nafuu na baadae kuuziwa wananchi na NHC walishalipia eneo hilo. Je, ni lini ujenzi huo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi, Mbunge wa Muheza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba la Taifa linatambua kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kuna mahitaji makubwa ya nyumba. Utekelezaji wa mradi wa nyumba Muheza unakwenda sambamba na mpango wa Shirika wa kujenga nyumba za bei nafuu katika Wilaya mbalimbali hapa nchini. Kwa sasa Shirika la nyumba tayari limeingia makubaliano na Halmashauri ya Muheza ili kujenga nyumba 10 katika makubaliano yaliyofanyika tarehe 29 Septemba, 2017 baada ya Halmashauri kuridhia rasmi ramani ya nyumba ambazo zilipendekezwa. Aidha, Halmashauri imeshalipa malipo ya awali kiasi cha shilingi milioni 100 ikiwa ni sehemu ya malipo ya nyumba hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba lina eneo lenye ukubwa wa ekari 83 katika eneo la Chatur. Kwa sasa watalaam wa Shirika la Nyumba wako katika eneo la mradi wakiandaa mpango wa kina kwa matumizi ya viwanja (site plan). Baada ya kukamilisha kwaundaa mpango wa kina wa matumizi ya ardhi, Shirika la Nyumba litajenga nyumba 20 kwa gharama nafuu ambapo nyumba 10 ni kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na nyumba nyingine 10 zitauzwa kwa wananchi wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa halmashauri nyingine kuiga mfano wa Halmashauri ya Muheza pamoja na halmashauri zingine ambazo tayari zimekwisha faidika na huduma hiyo zikiwemo Halmashauri ya Busokelo, Uyui, Momba, Geita na kwingineko ambao kwa kiasi kikubwa wamepunguza tatizo la makazi kwa wafanyakazi wao. Kwa Halmashauri ambazo zilijengewa nyumba lakini hawajanunua nyumba hizo kwa sasa soko liko wazi kwa mwananchi yeyote kununua nyumba hizo.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-
Kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu sana unaohusu eneo lenye ukubwa wa ekari 357.5 Boko Dovya – Kawe – Kinondoni baina ya wananchi na watu wanaojitambulisha kuwa wamiliki halali wa eneo hilo maarufu kama SOMJI; wananchi katika hatua mbalimbali wamepeleka malalamiko Serikalini kuanzia ngazi ya Wilaya, Wizara ya Ardhi na hata kwa Waziri Mkuu lakini mpaka sasa hakuna utatuzi uliofanyika.
Je, hatua gani zimeanza kuchukuliwa ili kero hiyo ya muda mrefu imalizike?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali namba 17 la Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, awali shamba hili lililokuwa na ukubwa wa ekari 366 Mbweni maarufu kama Somji Farm lilipimwa na upimaji namba E7/37F na kupewa namba ya upimaji 10,917 ya tarehe 15 Agosti, 1959. Baada ya upimaji shamba lilimilikishwa kwa Ndugu Hussein Somji pamoja na Ndugu Munaver Somji mwaka 1961 na baadae kuandaliwa hati iliyosajiliwa kwa namba 14,573 ya kipindi cha miaka 99.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya shamba hilo, ekari 5.8 zilitwaliwa kwa matumizi mahususi ya Serikali mwaka 1975 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 670 la tarehe 30 Mei, 1975. Aidha, sehemu iliyobaki yenye ekari 357.5 ilitwaliwa na Serikali tena mwaka 2002 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 617 la tarehe 27, Septemba, 2002 kwa ajili ya kutumika katika mradi wa viwanja 20,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo eneo hilo halikuingizwa kwenye mradi kutokana na sehemu kubwa kuwa imevamiwa na wananchi. Pamoja na uvamizi huo, wamiliki wa awali walifungua mashauri mahakamani dhidi ya Serikali kupinga eneo lao kutwaliwa; shauri la Kikatiba namba moja la 2003 na shauri la Kikatiba namba 40 la 2010. Uwepo wa mashauri haya ulikwamisha juhudi za Serikali kushughulikia mgogoro huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni mara kadhaa imekaa na wahusika kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha wamiliki wa awali kulipwa fidia stahiki kwa fedha iliyopatikana kutokana na wanachi ambao watatakiwa kurasimishiwa maeneo waliyojenga.
Hata hivyo changamoto iliyopo ni katika kumilikisha makubaliano haya kwa wananchi kupitia kamati yao waliyounda, kutokuwa tayari kuchangia gharama za kurasimisha eneo hilo. Jitihada zaidi za wadau wengine akiwemo Mbunge zinahitajika katika kuwaelimisha wananchi kupitia Kamati yao kuwa tayari kushiriki katika upatikanaji wa ufumbuzi wa suala hili.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Ardhi ikipimwa huwa na thamani na hivyo kuwafanya wamiliki kupata mikopo katika taasisi za kifedha na kuwekeza katika uchumi. Katika Jimbo la Tarime Mjini ni Kata mbili tu za Bomani na Sabasaba ndizo ambazo ardhi yake imepimwa kwa asilimia 75 kati ya kata nane zilizopo, hii inatokana na upungufu mkubwa wa wataalam wa kupima ardhi.
Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam wa kutosha ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tarime kuweza kupima ardhi kwa kata sita zilizosalia ili wananchi wa Tarime Mjini waweze kunufaika na ardhi yao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, swali lake Na. 359 kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kupanga na kupima ardhi nchini kwa manufaa ya wananchi wake. Halmashauri ya Mji wa Tarime ina wataalam wa ardhi wanne tu ambao ni Afisa Mipango Miji, Afisa Ardhi, Mchora ambaye ni Mrasimu Ramani na Mthamini Mali. Idadi hii ni ndogo ukilinganisha na kasi ya ukuaji wa Mji wa Tarime kwa sasa. Tatizo hili si kwa Mji wa Tarime pekee bali ni tatizo linalozikabili karibu Halmashauri zote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kutekeleza azma ya kupanga na kupima kila kipande cha ardhi kwa nchi nzima, ikiwemo kusajili makampuni binafsi ya kupanga ardhi, yenye weledi wa kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. Hadi sasa tuna jumla ya makampuni 36 ya kupanga miji na makampuni 65 ya kupima ardhi yamesajiliwa ili kuongeza kasi ya upangaji na upimaji wa ardhi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa inaandaa utaratibu wa kuwatumia wataalam wa sekta ya ardhi kutoka katika maeneo yenye watumishi wa kutosha kufanya kazi katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa watumishi na hivyo kuharakisha kasi ya upangaji na kupima ardhi nchini. Halmashauri ya Mji wa Tarime ni mojawapo ya maeneo yanayotarajiwa kunufaika na utaratibu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu pia inaendelea kuzihimiza Halmashauri zote nchini kutenga fedha za kutosha katika bajeti zao kwa ajili ya kuajiri wataalam wa sekta ya ardhi wanaokidhi mahitaji na hivyo kuongeza kasi ya kupanga na kupima ardhi katika maeneo yao.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-
Taarifa ya Idara ya Upimaji wa Ramani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inalitaja eneo la Chisinjisa lililopo Wilaya ya Manyoni kuwa ndipo alama pekee ya katikati (center point) ya Tanzania inapatikana.
• Je, ni lini Serikali italitambua rasmi eneo hili na kulitangaza katika Gazeti la Serikali?
• Je, Serikali haioni umuhimu wa kuendeleza na kulitangaza eneo hili ili kuvutia utalii wa ndani na nje kama chanzo cha mapato?
NAIBU WAZIRI WA ARIDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali namba 474 kutoka kwa Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hakuna taarifa rasmi za kitaalam zilizobainisha kwamba Kijiji cha Chisinjisa ndipo alama pekee ya katikati (center point) ya Tanzania pamoja na wenyeji wa eneo hilo kudai kuwepo kwa alama hiyo eneo la Sukamahela.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Idara ya Upimaji na Ramani inakusudia kufanya utafiti wa kina kwa kutumia elimu ya jiometriki (geometics) ili kubaini eneo rasmi ambalo alama ya katikati (center point) ya Tanzania inapatikana.
Mheshimiwa Spika, baada ya utafiti huo kukamilika eneo la katikati ya Tanzania litatangazwa katika Gazeti la Serikali. Aidha, mamlaka zinazohusika na masuala ya utalii zitaliendeleza eneo husika ilikuvutia utalii wa ndani na nje kama zinavyofanya nchi nyingine duniani na kuongeza mapato ya Serikali.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA aliuliza:-
Je, nini sera ya Serikali katika kubadilisha mandhari ya maeneo ambayo ni squatter au ya wazi kwa kuwekeza katika majengo ili kuwa na makazi ya kisasa kwa ajili ya wananchi kwa kutumia ardhi iliyopo katika eneo husika?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali namba 475 la Dkt. Mary Mwanjelwa, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kifungu namba 4.1.4.2 cha Sera ya Taifa ya Makazi ya mwaka 2000 kinaelekeza kuwa maeneo yaliyojengwa bila kupangwa na kuwekewa huduma za msingi yaboreshwe na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na asasi za kijamii. Kwa maeneo yaliyojengwa bila kupangwa na kupimwa lakini yapo katikati ya miji (prime areas) hususan katika Jiji la Dar es Salaam, Wizara imeandaa rasimu ya mkakati wa uboreshaji wa maeneo hayo kwa kutumia dhana ya kukusanya ardhi (land pooling). Utekelezaji wa dhana hii utawawezesha wananchi wa maeneo husika kupata makazi bora na pia kupata ardhi kwa ajili ya uwekezaji mpya.
Mheshimiwa Spika, dhana ya kukusanya ardhi inalenga kuboresha maeneo hayo kwa kujenga majengo makubwa ya ghorofa ili kuweza kuwapatia makazi mbadala wakazi wa maeneo husika katika eneo hilo hilo, na pia kupata eneo la uwekezaji utakaojumuisha ujenzi wa majengo ya kibiashara kama vile maduka makubwa (super markets and shopping malls), makazi ya maghorofa ambayo mengi yanakuwa na apartments, hoteli, huduma za kijamii, maeneo ya wazi, maeneo ya burudani na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, rasimu hiyo kwa awamu ya kwanza inapendekeza kufanya ukusanyaji wa ardhi katika maeneo ya Manzese, Vingunguti, Buguruni, Msasani, Keko, Namanga, Mikocheni na Kawe.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza:-
Je, ni nini faida ya hati miliki za kimila?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Mwamoto kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa fungu la 18, 28 hadi 47 la Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba tano ya mwaka 1999 hati ya hakimiliki za hati ya kumiliki ardhi kwa kuzingatia mila na desturi kwa raia wa Tanzania na ina hadhi sawa na hakimiliki nyingine inayotolewa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna faida nyingi za hati za hakimiliki ya kimila, miongoni mwa faida hizo ni pamoja na kuwa na usalama wa miliki, kupunguza migogoro baina ya watumiaji ardhi, kutumika kama dhamana katika taasisi za fedha na vyombo vya kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Machi, 2018 jumla ya hatimiliki za kimila 56,506 zimeandaliwa katika maeneo mbalimbali nchini. Wananchi katika maeneo hayo wamenufaika kiuchumi kutokana na mikopo waliyoipata katika taasisi za kifedha kwa kutumia hati za hatimiliki za kimila kama dhamana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Juni, 2017 kiasi cha shilingi bilioni 59.2 zimekopeshwa kwa wananchi kwa kutumia hati za hakimiliki za kimila kama dhamana kutoka mabenki na taasisi za kifedha. Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja NMB PLC, CRDB PLC, Stanbic Bank, SIDO, PSPF, Agriculture Trust Fund, Meru Community na Mfuko wa Pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika miradi ya utoaji hati za hakimiliki za kimila inayoendelezwa katika maeneo yao ili ziweze kuwanufaisha kwa ustawi wa kiuchumi na kijamii.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali haisemi ukweli Bungeni juu ya fidia kwa wananchi wa Mtwara Mjini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro mkubwa wa fidia uliopo sasa katika Manispaa ya Mtwara Mikindani unahusu eneo la Mjimwema na Tangira unaotokana na upimaji wa viwanja 10,000 uliotarajiwa kufanywa kwa njia ya ubia baina ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, pamoja na Taasisi ya UTT- PID mwaka 2003. Upimaji huu haukufanyika kama ilivyopangwa kutokana na amri ya kusitishwa kwa miradi yote ya upimaji wa viwanja ambavyo Halmashauri mbalimbali zilikuwa zikishirikiana na UTT-PID iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI mwaka 2004.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na katazo hilo, Manispaa ya Mtwara Mikindani iliendelea kuomba kibali cha kuendelea na mradi huo, kwa kuwa shughuli mbalimbali tayari zilikuwa zimeshafanyika zikiwemo uthamini kwa ajili ya fidia. Baada ya ufuatiliaji, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilitoa kibali cha kuendelea na mradi huo kwa barua yenye Kumb. Na. GB.2013/234/01/117 ya tarehe 2/09/2016.
Hata hivyo mwishoni wa mwaka 2017 Taasisi ya UTT- PID ilikiri kutoweza kuendelea na mradi huo kutokana na ukosefu wa fedha uliosababishwa na taratibu za utekelezaji wa mradi huo kuchukua muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Januari, 2018 Baraza la Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani liliamua kuendelea na mradi huo kwa kuwapimia wananchi maeneo yao na kisha kuwapa viwanja kulingana na ukubwa wa maeneo yao na hatimaye kuwamilikisha kisheria badala ya kusubiri fidia ambayo kimsingi haipo. Jumla ya shilingi milioni 170 zilitengwa katika bajeti ya Halmashauri kwa ajili ya kugharamia zoezi la upimaji na ufunguzi wa barabara za msingi katika eneo la mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa eneo la Tangira katika Kata ya Mitengo waliridhia kuendelea na utaratibu wa kupimiwa viwaja katika mashamba yao. Mpaka sasa jumla ya viwanja 1,212 vimepimwa. Aidha, jumla ya viwanja 2,800 vinatarajiwa kupimwa katika eneo la Mjimwema Kata ya Magengeni. Kwa maeneo mengine upimaji wa viwanja utaendelea baada ya kukamilika kwa majadiliano baina ya Serikali na wananchi ambao ni wamiliki wa asili wa mashamba husika.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Kwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la upimaji wa viwanja kwenye Manispaa mbalimbali nchini.
• Je, kwa nini wananchi wanalazimishwa kuuza maeneo hayo kwa Manispaa na kulipwa bei ndogo badala ya kufanya zoezi hilo kwa ubia?
• Kwa sababu maeneo hayo mengi ni mashamba, je, Serikali haioni kufanya hivyo kunasababisha Watanzania kukosa kazi maana asilimia 75 ni wakulima?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007 inaelekeza kuwa eneo lolote likishatangazwa kuwa ni eneo la upangaji yaani planning area linapaswa kupangwa kwa kuzingatia Sheria ya Upangaji Mijini. Wananchi wanaokutwa kwenye maeneo hayo wanatakiwa kutambuliwa, kuelimishwa na kushirikishwa katika hatua zote za upangaji hadi umilikishaji. Pia Sera ya Ardhi ya mwaka 1995, Sheria ya Upimaji wa Ardhi Namba 4 na Namba 5 za mwaka 1999 na kanuni zake za mwaka 2001 na Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na kanuni zake na miongozo yake, zinaelekeza Mamlaka za Upangaji kufanya upangaji na upimaji kwa kushirikisha wadau wote muhimu katika kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Aidha, Sheria ya Utwaaji Ardhi Namba 47 ya mwaka 1967 pamoja na mambo mengine inazingatia mamlaka za upangaji miji uhalali wa kutwaa ardhi iliyopangwa na inayohitaji kupangwa kutoka kwa wamiliki na kuwalipa fidia kwa kufuata miongozo ya ulipaji fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera na Sheria za Ardhi zinaelekeza umuhimu wa kutathmini ardhi na maendelezo ya wananchi waliokutwa nayo na kulipwa fidia sambamba na kupima na kumilikisha kwa makubaliano yatakayoridhiwa na pande zote mbili bila kuathiri sheria. Hata hivyo uzoefu unaonesha kuwa mamlaka za upangaji hupenda kutumia njia ya kulipa fidia ya Ardhi na maendelezo hali ambayo imeleta malalamiko mengi kutoka kwa wananchi. Serikali inazielekeza mamlaka zote za upangaji kutowalazimisha wananchi kutumia njia moja ya kulipa fidia na badala yake wananchi washirikishwe kuchagua njia wanayoona inafaa kati ya kuingia ubia au kulipwa fidia.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote ambayo yametangazwa kuwa ni maeneo ya upangaji yaani planning area yanapaswa kuendelezwa kwa kuzingatia Sheria ya Upangaji Mijini. Ni kweli kuwa kuna maeneo yanayotwaliwa na kuingizwa kwenye mpango ya kuendelezwa kimji ambayo ni mashamba ya wananchi. Mamlaka za Upangaji kwa kuwashirikisha wananchi wenye maeneo hayo hupanga matumizi mbalimbali yakiwemo makazi, kilimo cha mjini, viwanda vidogo vidogo, masoko, biashara kubwa na ndogo, huduma mbalimbali za kijamii kwa kutegemea maendeleo ya kimji na matakwa ya sheria. Kwa hatua hii wananchi huwa na fursa ya kupata kazi za kuwaingizia kipato kwa kupata viwango vya matumizi watakayo pendelea.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi walio kwenye vijiji vilivyopo kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kuwarahisishia upatikanaji wa vitabu vya usajili Wilayani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA YA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba tano ya mwaka 1999 kifungu la 21 na Kanuni ya 36, kila kijiji chenye mpango wa matumizi bora kwa ardhi inapaswa kuwa na daftari la usajili wa ardhi ambalo linatunzwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji. Daftari la usajili ni daftari ambalo hutumika kusajili hati za hakimiliki za kimila zinazotolewa katika ardhi ya kijiji husika. Utoaji wa hatimiliki za kimila hutanguliwa na zoezi la uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi ambayo inalenga kuboresha mipango ya matumizi ya ardhi katika kijiji kwa kuondoa mgongano wa matumizi katika ardhi za vijiji pamoja na kuiongezea thamani ardhi hiyo kuifanya kuwa ni mtaji hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwepo na changamoto za upatikanaji wa madaftari ya usajili wa ardhi katika baadhi ya Halmashauri kutokana na uhaba wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuchapisha madaftari hayo. Katika kutatua changamoto hiyo, Wizara imekuwa ikisadiana na Halmashauri kuzipatia madaftari ya usajili wa ardhi wakati wa kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi. Hata hivyo, Wizara imeanza kutoa hati za hakimiliki za kimila kwa kutumia mfumo wa kielektroniki katika Wilaya ya Kilombero, Ulanga, Malinyi, Mkoani Morogoro. Teknolijia hii itakapoenea katika maeneo yote nchini itaondoa kabisa mahitaji ya madaftari ya usajili wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninahimiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kuchapisha madaftari ya usajili wa ardhi wakati tunasubiri teknolojia ya utaji wa Hatimiliki za kimila kwa njia ya kielektroniki kuenea katika nchi nzima.
MHE. NURU A. BAFADHILI aliuliza:-
Shule za Serikali na shule binafsi zina mitaala tofauti, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuwa na mfumo mmoja wa mitaala?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nuru Awadhi Bafadhili, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala hutolewa kwa lengo la kuweka mwongozo mpana wa viwango vya utoaji elimu kwa kuzingatia idadi ya masomo yatakayofundishwa, umahiri utakaojengeka, njia za ufundishaji na kujifunzia, vifaa vya ufundishaji, upimaji, ufuatiliaji na tathmini za mtalaa husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtalaa unaotumika katika shule za Serikali na shule binafsi ni mmoja na wanafunzi wote wanaosoma shule hizo hupata umahiri unaofanana. Aidha, mtalaa ambao ni tofauti ni ile mtu inayotumika katika shule chache za kimataifa (international schools) zilizopo nchini. Mitalaa hii ya kimataifa imeruhusiwa ili kukidhi mahitaji ya raia wa kigeni wanaoishi hapa nchini.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-

Ili kuharakisha upimaji na urasimishaji wa ardhi na makazi, Serikali iliruhusu kampuni binafsi kufanya kazi hiyo katika maeneo mbalimbali.

(a) Je, ni lini kampuni zinazofanya kazi hiyo zitatoa hati za ardhi au leseni za makazi kwa wananchi?

(b) Je, ni vikwazo gani vinakabili zoezi hilo na Serikali inachukua hatua gani kuviondoa ili kuzisaidia kampuni hizo kumaliza kazi hiyo kwa haraka?

(c) Je, ni lini Serikali itakamilisha mpango kabambe (masterplan) mpya ya Jiji la Dar es Salaam ili uwe dira katika upangaji, upimaji na urasimishaji?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, umilikishwaji wa ardhi hufanywa kwa mujibu wa Sheria Na.4 ya mwaka 1999 ambayo inampa Kamishna wa Ardhi mamlaka ya kutoa hati au leseni za makazi. Hivyo, lengo la kusajili makampuni ya upangaji na upimaji ardhi ni kuongeza kasi ya upangaji na kupima ardhi nchini lakini hati miliki za ardhi hiyo hutolewa na Kamishna baada ya mwananchi kulipa gharama za umilikishaji zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kimingi kwa sasa hatuna kikwazo au vikwazo vinavyokabili zoezi la urasimishaji ardhi nchini zaidi ya changamoto ya mwitikio mdogo wa wananchi katika maeneo mbalimbali. Awali zoezi hili lilikuwa linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ramani za msingi (base maps), uhaba wa vifaa vya kisasa vya upimaji, matumizi ya teknolojia duni, baadhi ya wananchi kutokuwa tayari kulipia gharama ya ardhi kwa ajili ya miundombinu na uelewa mdogo kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuondoa changamoto hizo, Serikali iliweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa picha za anga katika Jiji la Dar es Salaam na KIbaha na kuandaa ramani za msingi (base maps) mpya za mwaka 2016, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya upimaji, kuongeza mtandao wa alama za msingi za upimaji yaani control points, usimikaji wa mfumo wa ILMIS kwa ajili ya kurahisisha umilikishaji na uhamasishaji wa wananchi kuhusu zoezi la urasimishaji.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, rasimu ya mwisho ya mpango kabambe ya Jiji la Dar es Salaam imekamilika na nakala za kielektroniki za rasimu hiyo zimesambazwa kwa wadau kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni yao. Aidha, rasimu ya mpango huo imewekwa kwenye tovuti ya Wizara www.lands.go.tz ili kwezesha wadau kutoa maoni yao. Kwa sasa Mtaalam Mwelekezi anafanya mawasilisho ya rasimu hiyo katika mikutano ya hadhara (public hearing) katika Mamlaka zote za Upangaji za Jiji la Dar es Salaam ili kuapata maoni ya wananchi.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI) aliuliza:-

Kumekuwa na utaratibu wa Serikali kuchukua maeneo kwa wananchi na kuahidi kuwalipa, lakini huchukua muda mrefu kuwalipa.

Je, Serikali haioni kuwa kufanya hivyo ni kuwanyima wananchi haki yao ya msingi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ulipaji wa fidia hufanyika kwa mujibu wa Sheria Namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria Namba 5 ya mwaka 1999. Sheria hizi zinaelekeza kwamba pindi Serikali au mamlaka nyingine inapotwaa maeneo ya wananchi, wanatakiwa kulipa fidia stahiki, kamili na kwa wakati. Pamoja na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 Serikali ilitunga Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini Namba 7 ya mwaka 2016 ambayo imeelekeza kuwa pindi uthamini unapofanyika waliothaminiwa mali zao wanapswa kulipwa ndani ya miezi sita. Baada ya miezi sita tozo yaani prevailing interest rate in commercial banks inapaswa kuongezwa kwenye malipo ya madai ya fidia husika. Aidha, baada ya kupita kwa kipindi cha miaka miwili toka uthamini wa awali ufanyike, sheria inaelekeza pia, uthamini wa eneo hilo utafanyika upya.

Mheshimiwa Spika, licha ya taratibu za ulipaji wa fidia kuwekwa wazi katika sheria, kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi katika maeneo mbalimbali kuhusu ucheleweshaji wa malipo ya fidia. Katika kutatua changamoto hizo Wizara imeandaa mwongozo unaozitaka taasisi zote zinazotaka kuchukua mali za wananchi kuwasilisha uthibitisho wa uwezo wa kulipa fidia kabla ya kuidhinishiwa kwa taarifa za uthamini wa mali unaotarajiwa kuchukuliwa. Aidha, mwaka 2016 Wizara ilizindua Mfuko wa Fidia ya Ardhi utakaosaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza katika ulipaji wa fidia. Mfuko huo umepewa jukumu la kuratibu malalmiko ya ulipaji fidia na kusimamia malipo yote ya fidia yanayofanywa na watu au taasisi binafsi, ili kuhakikisha kuwa viwango vinavyotumika ni vile vilivyokubaliwa kwa wakati huo.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa changamoto ya ucheleweshaji wa malipo ya fidia imepatiwa ufumbuzi kwa kiasi kikubwa. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa changamoto hii inafikia mwisho ili kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa wananchi.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Serikali iliahidi kuanzisha Baraza la Ardhi la Wilaya ya Mbulu. Aidha, wataalam wa Serikali walifika Mbulu na kukabidhiwa majengo kwa ajili ya Baraza hilo katika Mji wa Dongobesh na Mheshimiwa Mbunge akachangia shilingi milioni tatu za kuongeza miundombinu.

Je, ni lini Baraza la Ardhi la Wilaya ya Mbulu litaanzishwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hadi sasa tuna jumla ya Mabaraza 97 ambayo yameundwa, ambapo kati ya hayo Mabaraza 53 yanatoa huduma na Mabaraza 44 likiwemo Baraza la Mbulu hayajaanza kutoa huduma kutokana na changamoto za uhaba wa rasilimali watu. Ili Baraza liweze kuanza kufanya kazi linahitaji kuwa na angalao Mwenyekiti mmoja, Katibu Muhtasi, Msaidizi wa Kumbukumbu, Msaidizi wa Ofisi, Dereva na Mlinzi.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Serikali imeipatia Wizara Wenyeviti 20 ambao ni wajiriwa wapya. Wenyeviti tisa kati ya hao ni kwa ajili ya kuongeza nguvu katika maeneo hayo yaliyoelemewa kwa wingi wa mashauri katika Wilaya za Mbulu, Sumbawanga, Kibondo, Kigoma, Temeke, Bukoba, Mwanza, Musoma na Ulanga. Wenyeviti 11 kwa ajili ya mabaraza 11 ambayo hayana Wenyeviti katika wilaya za Ukerewe, Maswa, Kilosa, Same, Kyela, Shinyanga, Lindi, Iramba, Nzega, Lushoto na Tunduru. Taratibu za mafunzo ya awali zinafanywa ili Wenyeviti hawa waweze kupangiwa vituo na kuanza kazi katika Mabaraza hayo ambayo yana uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba Baraza la Mbulu linaanza kufanya kazi mapema iwezekanavyo, Wizara imeshatuma barua kwenda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara kupata mapendekezo ya wananchi wenye sifa, ili Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aweze kufanya uteuzi wa Wazee wa Baraza la Ardhi na Nyumba kwa Wilaya ya Mbulu.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zitakazopata Wenyeviti wapya wa Mabaraza kutuma mapendekezo ya Wajumbe wa Mabaraza kwa wakati, kila wanapotakiwa kufanya hivyo, ili wananchi wasikose huduma kwa kukosekana Wajumbe wa Baraza. Aidha, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanashauriwa kuangalia uwezekano wa kutoa maeneo ya ofisi kwenye majengo yaliyo katika hali nzuri ili kurahisisha uanzishwaji wa Mabaraza katika Wilaya ambazo Mabaraza hayajaanza kazi.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-

Migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya za Mvomero na Kilosa Mkoani Morogoro inaendelea kugharimu maisha ya watu, mifugo pamoja na uharibifu wa mazao.

Je, Serikali imejipanga vipi katika kutafuta suluhu ya kudumu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika Wilaya za Mvomero na Kilosa, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri husika imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ya vijiji na Wilaya kwa ajili ya kuainisha matumizi mbalimbali ikiwemo suala la kilimo na ufugaji; kupima mipaka ya vijiji na kuiwekea alama za kudumu; kupima vipande vya ardhi za wananchi na kuwapatia hati za hakimiliki za kimila, lakini pia kubatilisha miliki za mashamba yasiyoendelezwa na kuyapangia matumizi mengine na kufanya ziara za mara kwa mara katika maeneo yenye migogoro ili kuyapatia ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizo Wizara inaelekeza mradi wa majaribio ya kuwezesha umilikishaji wa ardhi ya vijiji (Land Tenure Support Program) katika Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi. Mradi huu unatarajiwa kusambaa (ku-scale up), katika Wilaya zingine za Mkoa wa Morogoro zikiwemo Wilaya za Mvomero na Kilosa. Lengo la kukamilika kwa kazi hii ya uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi, upimaji wa mipaka na vijiji na upimaji wa vipande vya ardhi na kukamilisha kumilikisha wananchi na hivyo kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wananchi katika Wilaya ya Kilosa na Kilombero kuendelea kuheshimu Sheria za Ardhi, hususan kufuata mipango ya matumizi ya ardhi iliyoainishwa na hivyo kuondoa uwezekano wa kuibuka kwa migogoro isiyokuwa ya lazima.
MHE. RUTH H. MOLLEL aliuliza:-

Ardhi ni rasilimali ya msingi katika nchi yoyote duniani na tamaa ya kupora ardhi imesababisha migogoro na vita:-

(a) Je, Serikali ilitenga bajeti kiasi gani kuanzia mwaka 2010 – 2015 kwa ajili ya kupima matumizi ya ardhi?

(b) Je, kati ya kilometa za mrada 945,000 za Tanzania ni eneo kiasi gani limepimwa hadi Disemba 2015?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda nijibu swali la Mheshimiwa Ruth Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa nabu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Namba 6 ya Mwaka 2007, uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ni jukumu la mamlaka za upangaji ambazo ni Tume ya Taifa ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi kwa ngazi ya Taifa, Halmashauri za Wilaya pamoja na Halmashauri za Vijiji. Serikali imekuwa ikitenga fedha za kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka wa Fedha 2010 na 2011 hadi 2014/2015, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ilitenga na kutumia kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuandaa na kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, wadau wa maendeleo wamekuwa wakiziwezesha mamlaka za uandaaji kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi imekuwa ikiboreshwa mwaka hadi mwaka. Kati ya mwaka 2015 hadi 2018 Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ilitenga jumla ya shilingi bilioni 6.3 kwa ajili ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi nchini. Kati ya fedha hizi kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kimetumika kati ya mwaka 2015/2016 na 2017/2018 na kiasi cha bilioni tano kimetengwa kwa bajeti ya Tume kwa Mwaka 2018/2019.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ardhi ya Tanzania imegawanyika, katika aina tatu ambazo ni ardhi ya kawaida, ardhi ya hifadhi na ardhi ya vijiji. Hadi sasa kuna takribani vipande vya ardhi 2,000 vilivyopimwa ambavyo vinakadiriwa kuwa na ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 141,750 sawa na asilimia 15 ya eneo la nchi. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea na uboreshaji wa kumbukumbu za ardhi ikiwemo takwimu za upimaji ardhi kupitia mfumo unganishi wa kutunza kumbukumbu za ardhi, yaani ILMIS.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa eneo la ardhi ya nchi lililopimwa linaongezeka. Mojawapo ya mikakati hiyo ni mkakati wa kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini ulioanza kutekelezwa mwaka 2016 kupitia programu mbalimbali ikiwemo Programu ya Kuwezesha Umilikishaji wa Ardhi, yaani Land Tenure Support Progamme, katika Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi Mkoani Morogoro. Ni matarajio ya Wizara kuwa, kupitia mkakati huu idadi ya vipande vya ardhi vilivyopimwa itaongezeka na hivyo kupunguza eneo la nchi ambalo halijapimwa.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA) aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa shamba la Efatha Mkoani Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu wa matumizi ya Shamba Na. 48/1 la Malonje kati ya mmiliki ambaye ni Mdhamini wa Efatha na wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hili, hususan Vijiji vya Songambele, Sikaungu na Msanda Muungano. Madai ya wananchi hao ni kuwa sehemu ya shamba hili imeingia ndani ya vijiji vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo awali Shamba la Malonje lilikuwa likimilikiwa na Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo likiwa halina upimaji ambapo lilipimwa mwaka 1997 likiwa na ukubwa wa hekta 15,000. Mwaka 2007 shamba hili liligawanywa ambapo hekta 10,000 ziliuzwa kwa wamiliki ambao ni Efatha Ministry na hekta 5,000 zilizobaki zilipimwa vitalu na kugawiwa wafugaji. Mwaka 2010 baada ya kupokea malalamiko na kuyafanyia kazi, ilibainika kuwa upimaji wa vijiji uliofanyika umeingiliana na mipaka ya shamba husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa, imefanya jitihada mbalimbali za kumaliza mgogoro huo. Baada ya jitihada hizo kutozaa matunda, tarehe 7 Novemba, 2017 nilikutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma ya Efatha na baadhi ya Watendaji wake kwa lengo la kukubaliana namna bora ya kumaliza mgogoro huu ili kuboresha mahusiano ya ujirani mwema kati ya mmiliki na wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hilo. Wizara yangu ilipendekeza kwamba Efatha iridhie kuachia sehemu ya ardhi ya shamba yenye ukubwa wa ekari 8,392.9 na kuigawa kwa wananchi wa vijiji husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Bodi ya Wadhamini kukaa, waliridhia kutoa ekari 3,000 kwa Vijiji vya Songambele, Sikaungu na Msanda Muungano kwa maana ya kila kijiji kigawiwe ekari 1,000. Hata hivyo, Kijiji cha Sikaungu kimekataa kupokea ekari hizo kwa kuwa wao wanataka kiasi cha ardhi kama ilivyoonekana kwenye vyeti vyao vya ardhi ya kijiji.

Aidha, majadiliano bado yanaendelea kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Efatha na Serikali ya Kijiji cha Sikaungu. Baada ya majadiliano hayo kukamilika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri itasimamia upimaji wa ardhi hiyo.
MHE. RHODA E. KUNCHELA aliuliza:-

Serikali iliahidi kumaliza migogoro ya ardhi kwa kupima maeneo ya wananchi mapema ili kuepuka bomoa bomoa bila fidia:-

Je, ni lini jambo hilo litafikia mwisho?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba kila kipande cha ardhi nchini kinatambuliwa, kinapangwa na kinapimwa. Katika kutekeleza azma hiyo, Wizara imenunua vifaa vya kisasa vya upimaji ambavyo vimesambazwa katika kanda zote nane na vinatumiwa na Hamashauri zote ili kurahisisha na kuharakisha upimaji wa maeneo ya wananchi na kutoa hatimiliki za ardhi. Vile vile Wizara inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa kupima kila kipande cha ardhi nchini ambapo awamu ya kwanza ya mkakati huu inatekelezwa kupitia Mradi wa Majaribio wa Kuwezesha Umiliki wa Ardhi (Land Tenure Support Programme) unaotekelezwa katika Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi katika Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetoa kiasi cha shilingi 6,400,000,000 kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa 25 kwa ajili ya kupima, kupanga na kumilikisha ardhi. Halmashauri hizo ni Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Halmashauri ya Sumbawanga, Manispaa ya Shinyanga na Iringa, Halmashauri za Miji ya Makambako, Njombe, Kondoa, Nzega, Kahama, Bariadi na Halmashauri za WIlaya za Misungwi, Sengerema, Geita, Nzega, Bukombe, Magu, Chato, Ukerewe, Busega, Simanjiro, Gairo, Songea, Namtumbo na Itilima. Serikali inaendelea kutafuta fedha katika vyanzo mbalimbali ili jambo hili lifikie mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na utekelezaji wa kupima kila kipande cha ardhi nchini, Wizara imeendelea na utekelezaji wa Programu ya Kurasimisha Makazi yasiyopangwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiana na makampuni binafsi ya kupanga na kupima ardhi yaliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria. Lengo la Serikali ni kuhakikisha maeneo yote yanapangwa na kupimwa ili kukidhi mahitahi ya sasa na ya baadaye na hivyo kuzuia uendelezaji holela ambapo husababisha migogoro na adha kwa wananchi ikiwemo bomoa bomoa ya makazi yasiyo rasmi.
MHE. ANTONY C. KOMU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya mara kwa mara ya kuyapima upya mashamba yaliyotaifishwa wakati wa Azimio la Arusha ambayo hivi sasa yamebadilishwa matumizi na kujengwa Shule, Zahanati, Hospitali, Makazi na kadhalika?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antony Calist Komu, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mashamba kadhaa nchini yaliyotaifishwa wakati wa Azimio la Arusha. Baadhi ya mashamba hayo yaligawiwa kwa mashirika na taasisi za Umma kwa ajili ya kuyaendeleza hususan kwa kilimo cha kahawa na mkonge.

Hata hivyo, baadhi ya mashamba hayo yamebadilishiwa matumizi na yamekuwa yakitumiwa na wananchi kwa matumizi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ikiwemo makazi, shule, zahanati, hospitali na kadhalika. Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri mbalimbali nchini, imeendelea kuyakagua, kuyaandalia mipango ya matumizi ya ardhi na kupima upya baadhi ya mashamba hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mashamba ambayo Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri imeyaandalia mpano wa matumizi ya ardhi ni pamoja na Kihuhwi Estate, Sagulas Estate, Lewa Estate, Bombwera Estate, Geiglitza Azimio, Kilapula pamoja na Kibaranga yote ya Mkoa wa Tanga. Mashamba mengine ni New Msovero Farm, Mvumi Farms/Estate Kilosa pamoja na Luipa Estate yaliyopo Mkoani Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi jukumu la kuandaa mipango ya matumizi ya mashamba hayo ni la Halmashauri husika yalipo mashamba hayo. Hivyo, ninaagiza Halmashauri zote nchini kuendelea kukagua mashamba yaliyotaifishwa wakati wa Azimio la Arusha ili yaandaliwe mipango ya matumizi ya ardhi na kupimwa.

Aidha, natoa rai kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga bajeti kwa ajili ya kupanga na kupima mashamba husika ili yaweze kutumika kwa tija kulingana na mahitaji halisi ya sasa.
MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Handeni ambao wanakosa ardhi ya kuendesha shughuli zao za kilimo kwa sababu ya kumilikiwa na wachache?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa mashamba uliofanyika katika kipindi cha 2018/2019 Wilayani Handeni ulibaini kuwepo kwa mashamba manne makubwa yenye hekta 7,279.26 ambayo hayajaendelezwa ipasavyo na hivyo kupelekea baadhi ya mashamba hayo kuvamiwa na wananchi. Serikali inaendelea na utaratibu wa ufutaji wa miliki za mashamba hayo yaliyokiuka masharti ya uendelezaji ambapo wamiliki wanne wameshatumiwa ilani zao ubatilisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya miliki hizo kubatilishwa, ardhi husika itaandaliwa mipango ya matumizi ikiwemo ya kilimo na ufugaji na kugawia kwa wananchi wenye uhaba wa ardhi. Aidha, mipango hiyo itazingatia utengaji wa ardhi ya akiba (land bank) kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa wananchi kutumia ardhi yao kwa tija kwani ardhi haiongezeki wakati idadi ya watu, mifugo na shughuli za uzalishaji zinahitaji ardhi zinaongezeka. Vilevile, viongozi wa Vijiji na Kata waache tabia ya kuwagawia ardhi kwa mtindo wa kuwakodisha wananchi kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu na sheria za nchi yetu.
MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:-

Je, ni muda gani mchakato wa kuandaa hatimiliki unatakiwa kukamilika kwa mujibu wa sera na taratibu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuthamini umuhimu wa kuwapatia wananchi hatimiliki kwa muda mfupi, Wizara yangu pamoja na uwepo wa sera na sheria za ardhi inao Mkataba wa Huduma kwa Mteja (Client Service Charter) ambao unaweka bayana kuwa ndani ya siku thelathini tangu nyaraka zifikishwe Ofisi ya Kanda kutoka Halmashauri, hatimiliki husika inapaswa kuwa imekamilika kwa hatimiliki za kawaida (analog system). Aidha, kwa upande wa hatimiliki zitolewazo kwa njia ya mfumo unganishi wa kielektroniki (ILMIS) ulioanza kufanya kazi katika Wilaya ya Kinondoni na Ubungo, hatimiliki inapaswa kuwa imekamilika ndani ya siku saba tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu ndiyo imepewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa sheria za ardhi ambapo pamoja na mambo mengine inahakikisha kuwa wananchi, taasisi, makampuni au mashirika yanamilikishwa rasilimali hii adhimu ya ardhi kwa kupatiwa nyaraka za umiliki. Nyaraka hizo ni Hati ya Hakimiliki ya Kimila ambayo hutolewa kwa ardhi ya kijiji na Hatimiliki ya kupewa ambayo hutolewa kwa ardhi ya kawaida na ya hifadhi. Hati hizi zikishasajiliwa hukabidhiwa kwa wahusika ili wazitumie katika kujiletea maendeleo na kuwahakikishia usalama wa miliki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa watumishi wa sekta ardhi nchini kuhakikisha kuwa wanakamilisha taratibu zote za umilikishaji kwa wakati. Aidha, napenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa Wizara yangu itaendelea kuboresha taratibu za utoaji wa huduma hii muhimu ikiwemo kupunguza muda wa upatikanaji wa Hatimiliki na kuwasogezea huduma katika ngazi za mikoa.
MHE. MARY D. MURO (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENAN) aliuliza:-

Je, ni lini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litajenga nyumba za bei nafuu ambazo wananchi wenye hali ya chini wataweza kununua?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekuwa likitekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba kwa kufuata Mpango Mkakati wa Miaka 10 unaoanza 2015/2016 - 2024/2025. Pamoja na Shirika kutekeleza mpango mkakati huo, Shirika limekuwa na miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa kipato cha chini wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za nyumba hizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo gharama kubwa ya kununua ardhi, riba ya mikopo na gharama za uwekaji wa miundombinu katika maeneo ya miradi. Ili Shirika liweze kujenga nyumba za gharama nafuu hususani kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini, mamlaka husika zinatakiwa kuwezesha upatikanaji wa ardhi, uwepo wa miundombinu ya umeme, maji, barabara na riba nafuu ya mikopo ya taasisi za fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika ziara Mkoa wa Mtwara aliagiza kuwa Halmashauri zote nchini zitoe ardhi kwa Shirika la Nyumba la Taifa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na pia taasisi zinazohusika na miundombinu ziweke miundombinu hiyo kwenye maeneo ya miradi ya shirika ili kupunguza gharama ya nyumba hizo. Kufuatia utekelezaji wa maelekezo hayo, bei ya nyumba katika baadhi ya miradi imeshuka kwa kiasi kikubwa. Mfano, bei ya nyumba katika mradi wa Chatur, Wilaya ya Muheza imeshuka mpaka shilingi milioni 24.6 ikilinganishwa na bei ya miradi ya awali mfano Ilembo, Katavi ambayo ilikuwa inauzwa milioni 30.6; Mlole Kigoma milioni 34.2; na Mtanda, Lindi milioni 33.6. Tunatoa rai kwa Halmashauri zingine za Miji na Wilaya kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais ili waweze kujengewa nyumba za gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi, shirika linadhamiria kujikita zaidi katika ujenzi wa nyumba za kupangisha ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wasio na uwezo wa kununua nyumba. Kwa kuanzia nyumba hizo za kupangisha zitajengwa katika Jiji la Dodoma eneo la Chamwino ili kukidhi mahitaji yaliyopo hususan kwa watumishi wa Serikali.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-

Serikali imeruhusu urasimishaji wa makazi katika maeneo mbalimbali Nchini ikiwemo Jiji la Mwanza isipokuwa maeneo ya Kata ya Isamilo, Mbugani, Mabatini na Igogo.

Je, ni lini Serikali itawamilikisha wananchi hawa maeneo yao kwa kuwa wameishi katika maeneo haya kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendele ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na zoezi la urasimishaji wa makaziyasiyopangwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni utekelezaji wa kifungu namba6.4.1(iii) cha Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 ambacho kinatamka kwamba;

“Maeneo ya makazi holela isipokuwa yale yaliyojengwa kwenye maeneo ya hatarishi hayatabomolewa bali yataboreshwa na kuwekewa huduma za msingi”.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jiji la Mwanza urasimishaji wa makazi unafanyika katika kata mbalimbali zikiwemo Kata za Isamilo na Mbugani. Katika Kata ya Isamilo urasimishaji umefanyika katika Mitaa ya Msikiti, SDA pamoja na National ambapo michoro ya mipangomiji miwili yenye jumla ya viwanja 3,444 imeandaliwa, viwanja 560 vimepimwa na viwanja 101 tayari vimemilikishwa. Aidha, Katika Kata ya Mbugani urasimishaji umefanyika katika Mitaa ya Nyashana na Kasulu ambapo michoro miwili ya mipangomiji yenye jumla ya viwanja 1001 iliandaliwa na viwanja 395 vimepimwa na vipo katika hatua ya umilikishaji.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kufanyika urasimishaji katika mitaa hiyo, maeneo mengine ya kata za Isamilo, Mbugani, Igogo na Mabatini hayajafanyiwa urasimishaji wa makazi kutokana na sehemu kubwa ya maeneo hayo kuwa hatarishi; ambayo yapo kwenye milima yenye miteremko mikali zaidi ya asilimia 15. Hivyo maeneo hayo hayakidhi vigezo vya kurasimishwa kwa kuwa ni hatarishi kwa maisha ya wananchi na mali zao pamoja na ugumu wa kuyafikika kwa barabara.

Mheshimiwa Spika, Mpango Kabambe wa Jiji la Mwanza 2015/2035 umeainishabaadhi ya maeneo ya Kata za Mbugani, Isamilo, Pamba, Nyamagana, Mkuyuni na Igogo kuwa ni maeneo yanayotakiwa kuendelezwa upya (redevelopment) kwa kuzingatia hali halisi ya miinuko na ujenzi hatarishi uliofanyika. Kwa sasa wamiliki wamakazi hayo watatambuliwa na kupatiwa leseni za makazi (formalization)wakati wakisubiri uendelezwaji mpya wa maeneo hayo.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-

(a) Je Ikama ya Wataalam wa Ardhi Katika Halmashauri za Wilaya ni ipi na ni lini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru itafikia kiwango hicho?

(b) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kurudisha eneo la Hekari takribani 2,000 za Shamba Pori la Nambarapi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili nayo irejeshe ardhi kwa Wananchi wa Vijiji husika kikiwemo Kijiji cha Nambarapi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ramo Makani Mbunge wa Tunduru Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimimiwa Spika, kwa mujibu wa viwango vya utendaji vya mwaka 2015, ikama ya Wataalam wa ardhi katika Halmashauri za Wilaya Maafisa Ardhi watatu, wanatakiwa Wapima Ardhi watatu, Maafisa Mipangomiji watatu, Wathamini watatu na Mafundi Sanifu Upimaji pamoja na Maafisa Ardhi Wasaidizi wanne. Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa sasa ina watumishi wanne katika Sekta ambao ni Maafisa Mipangomiji wawili, Mpima Ardhi mmoja na Afisa Ardhi Msaidizi mmoja. Serikali inaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya watumishi wa Sekta ya Ardhi ili kufikia kiwango kinachohitajika na hivyo kuongeza ufanisi. Aidha, Wizara itawapanga upya watumishi wa Sekta ya Ardhi ili kuwa na uwiano wenye tija.

Mheshimimiwa Spika, sehemu ya (b) ya swali lake shamba hili linatambuliwa kama “Shamba Namba 69 Nambarapi” na lina ukubwa wa hekta 774 ambazo ni sawa sawa na (ekari 1,913). Mwaka 2003 kulianza kujitokeza migogoro wa kugombea ardhi ya shamba hili hali iliyosababisha kufunguliwa kwa Shauri namba 03 la mwaka 2016 katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Tunduru. Shauri hili lilikuwa kati ya TAMCU Ltd dhidi ya wananchi wanne (Hassan Mussa Ismaili, Ismail Mussa Ismail, Sophia Mussa Ismail na Said M. Ndeleko. Katika Shauri hili Chama cha Ushirika Wilaya ya Tunduru kilipata ushindi. Pamoja na ushindi wa TAMCU Ltd, wananchi wa kijiji cha Nambarapi waliomba ardhi katika shamba hilo kwa TAMCU ambapo ekari 1,000 zilimegwa na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na kugawa kwa wananchi. Hivyo, sehemu ya shamba iliyobaki ni mali ya chama cha Ushirika Wilaya ya Tunduru yaani (TAMCU Ltd).
MHE. QAMBALO W. QULWI (K.n.y. MHE. SUSAN A. LYIMO) aliuliza:-

Je, Serikali inasema nini kuhusu ucheleweshaji wa kupata hati za kumiliki ardhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa hapo awali kulikuwepo na malalamiko ya ucheleweshaji wa upatikanaji wa hatimiliki za ardhi. Sababu kubwa iliyosababisha changamoto hiyo ni kuwepo kwa Kamishna mmoja tu kwa nchi nzima aliyeruhusiwa kutia saini hati kwa nchi nzima, hali hiyo ililazimu rasimu zote za hati kuwasilishwa Makao Makuu ya Wizara. Hata hivyo, tangu mwaka 2018 mpaka sasa Wizara imefanikiwa kuanzisha jumla ya Kanda 8 za usimamizi wa ardhi kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali ikiwemo hiyo. Utoaji wa hatimiliki za ardhi, upelekaji wa huduma za ardhi katika Ofisi za Ardhi za Kanda pamoja na kutumia mfumo wa kielektroniki katika utoaji wa huduma zimeondoa kwa kasi kubwa changamoto ya kuchelewesha utoaji wa hatimiliki kwa wanachi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kuanzishwa kwa Ofisi za Kanda, Wizara imejenga Mfumo Unganishi wa Kutunza Kumbukumbu za Ardhi (Integrated Land Management Information System). Mfumo huu unalenga kurahisisha, kuharakisha na kupunguza gharama za utoaji huduma za ardhi. Kwa sasa tayari mfumo huo umeanza kutoa hatimiliki za kielektroniki katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na Ubungo. Aidha, Serikali imekamilisha ufungaji wa mfumo huo katika Ofisi za Ardhi za Manispaa ya Ilala, Kigamboni na Temeka na utaanza kutumika kuanzia Julai 01, 2019. Serikali inaendelea na utaratibu wa kusimika mfumo huu katika halmashauri zote nchini kwa awamu.
MHE. CECILIA D. PARESSO Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuyagawa kwa wananchi mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji katika Kata za Daa na Oldeani, Wilayani Karatu ambayo hayaendelezwi huku wananchi wakikosa ardhi kwa ajili ya makazi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, ni mara yangu ya kwanza kusimama toka Bunge la Kumi na Mbili limeanza, naomba unipe fursa na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema, lakini nimshukuru sana Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini tena katika kipindi hiki cha pili, kunipa dhamana ya kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Aidha, niwashukuru Wanailemela wote walionipa fursa hii ya kuweza kuwatumikia kwa miaka mingine mitano na kwa leo nitoe pole kwa msiba mkubwa wa Mkuu wa Shule ya Bwiru, shule ya ufundi, Ndugu Elias Kuboja ambaye amefariki dunia. Nawapa pole Wanailemela.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshinia Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya kazi ya uhakiki na ukaguzi wa mashamba makubwa nchini ili kubaini uzingatiwaji wa masharti ya umiliki yaliyotolewa. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kubatilisha milki za mashamba ambayo wamiliki wamekiuka masharti ya uendelezaji. Katika kipindi cha miaka mitano (2015 – 2020) jumla ya mashamba 45 yenye jumla ya ekari 121,032.243 yalibatilishwa kutokana na waliokuwa wamiliki kushindwa kutekeleza masharti ya umiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata za Daa na Oldeani Wilaya ya Karatu, kuna mashamba 25 ambayo yalimilikishwa kwa wawekezaji kwa ajili ya shughuli mbalimbali hususan kilimo na ufugaji. Taarifa za awali za uhakiki zinaonesha kuwa mashamba hayo yameendelezwa kwa viwango tofauti ambapo mashamba tisa yameendelezwa kwa wastani wa asilimia 50. Sehemu nyingine ya mashamba hayo imejengwa miundombinu ya barabara na huduma za jamii kama vile shule, nyumba za kulala wageni, viwanda, vituo vya watalii na kadhalika. Kwa sasa Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa kina wa mashamba yote na kuchukua hatua kwa wamiliki ambao wameshindwa kutimiza masharti ya umiliki.
MHE. FELISTA D. NJAU Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa hati kwa Wananchi wa Meko na Basihaya baada ya maeneo hayo kupimwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Meko liko katika Kata ya Kunduchi Manispaa ya Kinondoni awali eneo hilo lilitengwa kwaajili ya machimbo ya kokoto. Baada ya machimbo kufungwa Manispaa ilidhamiria kupima viwanja kwa ajili ya Kituo cha Biashara. Hata hivyo upimaji haukufanyika kutokana na eneo hilo kuwa limevamiwa na wananchi. Mwaka 2017 Manispaa ya Kinondoni ilimaliza mgogoro na wavamizi kwa kuruhusu wananchi wapimiwe viwanja katika eneo hilo kupitia mpango wa urasimishaji wa makazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha ilikubalika kuwa wananchi watapimiwa viwanja katika maeneo yale waliyoyaendeleza na maeneo yaliyo wazi yatapangwa na kupimwa viwanja vya matumizi ya umma. Kazi ya upimaji ilianza tarehe Mosi Januari, 2019 na kukamilika tarehe 20 Januari, 2021 na jumla ya viwanja 840 vimepimwa na hatua ya umilikishaji zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Basihaya lipo katika Kata ya Bunju, Mtaa wa Basihaya ambako kuna Vitongoji vya Chasimba, Chatembo, Chachui ambavyo kwa sehemu kubwa uendelezaji wake umefanywa ndani ya ardhi inayomilikiwa na Kiwanda cha Saruji cha Wazo. Wamiliki wa Kiwanda cha Wazo walipeleka malalamiko Mahakamani baada ya kuona eneo lao limevamiwa. Mahakama kupitia Shauri Na. 129 la mwaka 2008 kati ya Haruna Mpangao na wenzake 932 dhidi ya Tanzania Portland Cement ilitoa uamuzi kuwa wananchi waliovamia katika eneo hilo waondolewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ardhi ilichukua jitihada za kufanya majadiliano na mwekezaji ili kuangalia namna bora ya kutatua mgogoro huo ambapo iliamua wananchi walioendeleza katika maeneo hayo wasiondolewe bali walipe gharama ambazo atapewa mwekezaji ili akanunue eneo lingine kwa ajili ya kupata malighafi za kutengeneza saruji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshawapimia viwanja waendelezaji wote katika eneo hilo ambapo jumla ya viwanja 4,000 vimepatikana na kila mwendelezaji atatakiwa kulipia gharama zitakazotumika kumlipa mmiliki wa kiwanda. Wizara inaendelea kufanya majadiliano na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Wazo kuhusu gharama na fidia ya eneo lililoendelezwa na wananchi.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA Aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje katika kupanga matumizi bora ya ardhi kwa Vijiji vyote nchi nzima ili kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bryceson Magessa Tumaini, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya Mwaka, 2007 Sura ya 116 Kifungu cha18, kimebainisha Mamlaka za Upangaji kuwa ni Halmashauri za Vijiji, Wilaya na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ngazi ya Taifa na Mkoa. Jukumu la uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji ni la Halmashauri za Vijiji na Wilaya. Wizara ya Ardhi kupitia Tume ya Mipango ina jukumu la kuwajengea uwezo, kusimamia na kuratibu Mamlaka za Upangaji na sekta mbalimbali katika utekelezaji wa mipango hiyo.

Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi, jitihada mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa na Serikali ili kuhakikisha vijiji vyote nchini vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Jitihada hizo ni pamoja na zifuatazo: -

Kwanza, ni kutenga bajeti kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini, kupitia Mamlaka za Upangaji na hivyo kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi.

Pili, kushirikisha wadau mbalimbali wa kimkakati wa matumizi ya ardhi, kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji mbalimbali nchini.

Tatu, kuendelea kuhamasisha Halmashauri za Wilaya na Mikoa kutenga bajeti ya uandaaji wa mipango wa matumizi ya ardhi katika vijiji kwenye maeneo yao.

Nne, kushirikiana na vyuo vinavyofundisha masuala ya ardhi ikiwemo Chuo cha Ardhi, katika uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Tano, kubuni miradi ya kimkakati itakayowezesha uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi nchini.