Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Pauline Philipo Gekul (38 total)

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na nimshukuru Mheshimiwa Silinde ku-share na mimi dakika chache ili na mimi niweze kutoa maoni yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niunge mkono asilimia mia moja hotuba za Kamati zetu zote mbili. Wamezungumza mambo mazuri ya kujenga na naamini Mawaziri wanasikiliza ili wakayafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pale Mheshimiwa Silinde alipoishia kuhusu TIB Bank kwamba hawa wadaiwa wanatukwamisha, fedha hizo zisitufikie maeneo mengine. Basi sasa kama Bunge tuazimie kwa nguvu zote kwamba hili litekelezwe na tuwafahamu hawa watu na waweze kulipa hizi fedha ili ziendelee kusaidia maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala ambalo nilitaka kulizungumzia siku ya leo, ni asilimia tano ya akina mama na vijana. Naungana na maoni ya Kamati kwamba walete marekebisho ya sheria kwa vile ule ni mwongozo umeshashindikana. Nilikuwa kwenye Kamati ya TAMISEMI kipindi kilichopita tulilisimamia hili sana lakini Wakurugenzi hawapeleki.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na upungufu huo, jambo ambalo nahitaji kuishauri Serikali siku ya leo ni kwamba kwanza ule mwongozo una upungufu. Kwa mfano, wazee wa jinsia ya kiume wao hawapati zile fedha, akina mama wazee wanapata upande wa wanawake na vijana pia wanapata lakini wazee wa jinsia ya kiume (me) hawapati. Nimepita kwenye Jimbo langu na kila nilipopita wazee walilalamika kwamba hawanufaiki kabisa na mfuko huu na wenyewe wanaomba wapate hizo fedha kwa sababu sio wazee wote wenye wake na wenye watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naunga mkono mapendekezo ya Kamati kwamba marekebisho yafanyike au ule mwongozo sasa tuuache. TAMISEMI kupitia miscellaneous amendment kama ni muswada mzima mtuletee ili na hao wazee wapate fedha hizo tofauti na sasa ambavyo wanahangaika kupata upande wa TASAF wakati TASAF haifiki maeneo yote. Pia mnafahamu TASAF kila baada ya miaka mitatu ndiyo wanabadilisha zile kaya maskini kwa hiyo hawa wazee hawatafikiwa. Kwa hiyo, hili mtuletee na naunga mkono kabisa mapendekezo ya Kamati ili na wazee wa jinsia ya kiume (me) waingie wapate hizo fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kukazia siku ya leo ni suala la safari za Wakurugenzi. Kwa kweli Wakurugenzi mliotuletea hawakai kwenye Halmashauri zetu, akitoka kwa DC yuko kwa Mkoa wa Mkoa, akitoka kwa Mkuu wa Mkoa yuko kwa RAS. Ametoka kwa RAS anarudi kwa DAS ametoka hapo anaenda kwa OCD, ametoka kwa OCD yuko kwenye safari anasafiri Dar es Salaam au Dodoma, hawakai kabisa kwenye vikao vyetu. Wizara upande wa TAMISEMI muwaandikie basi muwape miongozo kwa sababu hawakai na ndiyo maana baadaye wanapoanza kutumbuliwa wanashangaa kama yale madudu yalifanywa na watu ambao waliwakaimisha wao. Kwa hiyo, niunge mkono maoni ya Wabunge wenzangu ambao jana walizungumza kwamba kuna tatizo kubwa sana kwa Wakurugenzi wetu, muwape mafunzo lakini wakae kwenye vikao vyetu vya Halmashauri waweze kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kuzungumza siku ya leo ni suala la madeni katika Halmashauri zetu. Mlivyotuletea Waraka wa Elimu Bure, kiukweli Serikali hampeleki pesa. Shule ya watoto 300 au 400, mnapeleka shilingi 200,000, huko huko wanunue mipira kwa ajili ya michezo, huko huko fedha za administration. Niliuliza swali kwa Waziri Mkuu jamani hiki kitu mfanyie review kwa hali ya kawaida shule zetu kuna madeni na Halmasahuri hizi zinadaiwa wakati huo huo mmechukua vyanzo vikubwa vya mapato. Kodi ya ardhi sasa inakusanywa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina hata zile asilimia 30 hamrudishi tena na ndiyo maana juzi nikasema kama ninyi ni waungwana kaeni chini muangalie zile asilimia 30 ambazo mlitakiwa kuzirudisha na mnafahamu zaidi shilingi bilioni 50 hamkuzirudisha, ni shilingi bilioni 4 tu mmerudisha juzi, basi leteni vifaa vya upimaji ardhi katika maeneo yetu kwa sababu huko kwenye Halmashauri zote kwa hali ya kawaida hawana vifaa hivyo.
Mimi niishauri Serikali acheni kuua Halmashauri zetu, kwanza mmepeleka sasa eti bima ya afya wazee tukawalipie kwa fedha gani? Kodi ya majengo mmechukua, TRA mpaka sasa hawakusanyi mnapoteza tu muda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kodi ya majengo ndiyo hiyo tena inakusanywa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Wakati huo kuna madeni, Waraka wa Elimu Bure unataka tulipie madeni ya walinzi, maji katika shule zetu yameshakatwa kwa sababu Halmashauri haina fedha na fedha hampeleki hebu kaeni chini muangalie hizo Halmashauri mnaziweka upande gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nisisitize, kama mnahitaji kujenga hizi Halmashauri mkumbuke mlifanya decentralization kwa sababu wakusanye, walipe na wasimamie. Leo mnapochukua fedha hizo zote, mnatubakisha na ushuru tukimbizane na mama lishe, bodaboda na bajaji, kwa nini? Mtuachie hizo kodi ndiyo zilikuwa zinatusaidia tuendeshe hizo Halmashauri. Muwa-empower hao Wakurugenzi na Madiwani wetu wasimamie hizo fedha muone kama kazi hazitoenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho jamani leteni pesa za maendeleo, hakuna fedha kabisa. Halafu mnategemea hizo barabara tutachonga na nini? Pia kwenye miscellaneous mnazotuletea kila siku mtuletee ile ya TANROADS asilimia 70 tuiondoe, asilimia 30 ziende kwenye Halmashauri zetu kuchonga hizo barabara haiwezekani. Nilisema kwenye Bunge hili kwamba TANROADS watusaidie kwenye zile asilimia 70 ili tuchonge hizo barabara lakini ile ni wao wenyewe wapende au wasipende. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kunipa nafasi na mimi nitoe maoni yangu katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Pia ninamshukuru Mwenyenzi Mungu kutupa afya njema, sisi wote katika Bunge hili ili kuishauri Serikali.

Pili, niendelee kuwapa pole wananchi wangu wa Jimbo la Babati Mjini kwa msiba ambao tulipata wa wale watoto ambao walipata ajali na Watanzania wote niwape pole, siku ya leo ni mazishi pale mtaa wa Mrara, Mungu awatie nguvu, ni msiba mzito sana ambao kwa kweli ni kazi kuupokea katika mioyo yetu, lakini Mungu atupe faraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, haya ninayochangia ni ambayo naona niyaseme kutoka moyoni mwangu. Naomba niseme neno moja la kiswahili kwamba Wabunge tuko hapa kwa ajili ya kusimamia Serikali, lakini kama hatutaacha unafiki toka moyoni, haya malalamiko ya wanajeshi na wananchi wetu hayawezi kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hili kwa sababu unafiki huu tusipouacha tutaendelea kusema Magereza ya Jimboni kwangu, Polisi wa Jimboni kwangu, Zimamoto wa Jimboni kwangulakini wenye matatizo ni sisi Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii bajeti yake ni shilingi bilioni 930, lakini bajeti ya maendeleo ni shilingi bilioni 40, kati ya shilingi bilioni 940 ndio za maendeleo. Waheshimiwa Wabunge tunaongea hapa kinafki, tunaongea tu kwa kupapasa wakati wa kupitisha vifungu tunaongeaongea tunakwenda kwenye guillotine haya hatuyaongei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatufiki kwenye vifungu, hatuongei kwa dhati ya mioyo yetu na kama tukisimama kuisimamia Serikali niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu pamoja na mimi tuache unafiki. Ikifika saa ya kupitisha vifungu tuitake Serikali waongeze fedha za maendeleo kwa sababu kila Mbunge analalamika kuhusu Polisi kwenye Jimbo lake, Magereza kwenye Jimbo lake, Polisi kwenye Jimbo lake, na Jeshi la Zimamoto kwenye Jimbo lake hawana magari, hawana maji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikifika kwenye kupitisha vifungu tunaenda mtu anatoa shilingi baadaye anarejesha kishkaji, wakati fedha hazipo huku kwenye maendeleo. Kwa hiyo, ni aibu Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo inalinda Tanzania, fedha za maendeleo shilingi bilioni 40 wakati wanajeshi wanakaa kwenye mabanzi, kwenye bati ndiyo nyumba zao. Unafiki huu utatupeleka pabaya. Mimi ninawaomba Waheshimiwa Wabunge leo, bajeti hii isipite wanongezewe fedha wanajeshi hawa na magereza na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe pole Mheshimiwa Waziri wetu Kivuli Mheshimiwa Godbless Lema, jana alibaguliwa kule Arusha na maeneo mengine. Nimtie moyo tu kwamba ubaguzi huu siyokwa sisi peke yetu, ubaguzi huu upo hata kwa wanajeshi wetu. Nitoe mfano, Jeshi la Magereza katika bajeti hii, hivi tunavyoongea nimeona kwamba Jeshi la Magereza hawajawahi kusikilizwa mambo yao. Niwape mfano, Mheshimiwa Rais mwaka jana mwezi Novemba, alizungumza kuhusu duty free hizi bidhaa ambazo zinapelekwa kwenye majeshi yetu, akasema hizi fedha badala ya kuwaletea vinywaji tutakuwa tunawaletea kila baada ya miezi mitatu shilingi 300,000. Ninavyoongea hapa Jeshi la Magereza hawajawahi kupewa fedha hizi, lakini majeshi mengine wamepewa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri utuambie kwa nini mnabagua Jeshi la Magereza. Jeshi la Polisi mmewapa Januari, Aprili mmewapa awamu mbili. Jeshi la Wananchi mmewapa mwezi wa Novemba, Desemba, awamu mbili. Jeshi la Magereza hamjawahi kuwapa hizi fedha,kwa nini mnawabagua jeshi hili? Wakati Jeshi la Magereza ndiyo linakaa na wananchi ambao wanaonewa, wanabambikiziwa kesi, wanawalinda wahalifu, wanakaa na watu kule wanawavumilia. Wengine hawa mahabusu na wafungwa mnawapeleka kule.

Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikikuambia hawana hata uniform, hawana hata nguo, mnawapeleka mnawafunga. Wafungwa wetu katika magereza nilifanya ziara katika Gereza la Babati, mtu mzima unakwenda pale unapewa suruali na shati la juu tu hakuna nguo nyingine yoyote ni mfungwa huyo! Jeshi hili wanakaa na watu hawa wasiokuwa na nguo mnawapa suruali tu na shati la juu, nguo zingine pull neck na nguo za ndani hamuwapi, halafu watu hawa hawapewi fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mnaita Jeshi la Magereza mnawapenda, mnawasikiliza, hata kwenye nyumba kwenye kitabu cha development nimekwenda, nyumba zote ambazo mnakwenda kujenga mnafanya renovation ni nyumba za polisi, sina tatizo na polisi wetu lakini Jeshi la Magereza mmewasahau kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie kwa nini ubaguzi huu mnaotufanyia sisi, sasa mnaupeleka kwenye majeshi yetu? Mtakuwa salama vipi? Wewe ni mfungwa mtarajiwa kaka yangu, kesho na kesho kutwa, utakuwa mahabusu pia, uko hapo tu wengine walikuwa hapo na wengine walishaondoka unafahamu, usicheze na Jeshi la Magereza wapelekeeni mahitaji yao na hizi pesa mlizowaahidi muapelekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo niliseme, hizi shilingi bilioni 40 ambazo ninasema tusipoacha unafiki, ndiyo hizi ambazo zinatakiwa ziende kwenye maendeleo. Wafungwa na mahabusu wapate magodoro. Gereza la Babati wafungwa wetu na mahabusu wanalala kwenye magodoro kama slice za mikate. Wanaunganishaunganisha vipande vya magodoro halafu havitoshi wanalala chini. Ukitaka kwenda kupeleka pale mlolongo ni mrefu mpaka uende Magereza Makao Makuu. Mkuu wa Gereza pale hatakuruhusu kupeka hivyo vitu mpaka uandike barua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama mnaleta mlolongo kwa nini hamnunui vitu hivyo? Magodoro hamnunui, uniform hampeleki lakini pia hata chakula ration wanazokula hazitoshelezi! Mtuambie ni kwa nini hizi fedha za maendeleo msiongeze kwa sababu kila mmoja ni mfungwa na mahabusu mtarajiwa. Hakuna magodogo huko.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwigulu alifika babati, alifika pale Jeshi la Polisi, nashukuru alienda pale rangi ikapigwa pigwa kwa sababu alienda pale, lakini nilimweleza masuala ya Gereza la Babati, hali ni mbaya na Magereza ya nchi nzima hali ni mbaya, hata magodoro hakuna. Ni vizuri tukakubaliana kwamba fedha hizi ziongezwe.Mfano, Jeshi la Magereza wanatakiwa nyumba 10,526 asilimia 71 hizi nyumba hazipo.Achilia mbali Magereza wanakokaa, lakini asilimia 71 ya Jeshi la Magereza hawana hizo nyumba.Polisi hawana hizo nyumba, Wilaya tano tu ndiyo mmeweka katika bajeti hii. Hivi kweli Waheshimiwa Wabunge tukae tu tunalalamika, kwamba jimboni kwangu, jimboni kwangu, nafikiri hili tulichukue kama Wabunge. Kwamba Wizara hii tunataka fedha za development angalau hata bilioni 200 ili tuache kelele za nyumba za Polisi wetu, tuache nyumba zetu za Magereza zijengwe, vinginevyo mnatuachia mzigo mkubwa sana na hili halitokubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la Magereza Wilaya moja kutokuwa na Gereza. Mfano, Babati pale tuko Makao Makuu ya Mkoa, lakini wenzetu wa Hanang’ hawana gereza tunaletewa mahabusu, gereza la Babati sasa lina watu zaidi ya 400 wafungwa pamoja na mahabusu, wanakaa mahabusu wa Hanang’ wiki tatu hawapelekwi Mahakamani, OCD wa Babati na wa Hanang’ hawana mafuta, Polisi wetu hawa wamewaachia mzigo mkubwa sana, kwenye ziara zao wakubwa wakija pale, wanawaambia watafute magari, wanaanza kuomba matairi yako wapi, mafuta yako wapi, hata fedha hawapeleki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanashindwaje kujenga Gereza Hanang’ wanarundika pale, watu wanasukumana pale, chakula hakitoshi, hawapelekwi Mahakamani, wanakosa haki zao. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu, naomba nifahamu na atuunge mkono kwa kweli, siyo baadaye aseme hela hazitoshi wakati anajua Hanang’ hakuna gereza, Babati msongamano ni mkubwa kwenye Gereza letu la Wilaya. Atuambie ni lini la Hanang’ litajengwa ili wananchi wa Babati wanapoingia kwenye lile Gereza, wasisongamane kiasi hicho kwa sababu hizi fedha hazitoshi na yeye atuunge mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine suala la Zimamoto. Jeshi la Zimamoto wanafanya kazi nzuri na wanakusanya…

TAARIFA...

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nisaidie tu kulinda muda wangu. Naomba nipokee taarifa ya Mheshimiwa Nagu ni dada yangu, naomba tu nikwambie dada ulikuwa haujalisemea ndiyo maana mpaka leo hakuna Gereza, kwa hiyo acha nikusaidie mdogo wako nikusemee.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niseme machache katika Wizara hii muhimu sana kwa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba Mwongozo ulioombwa asubuhi na Mheshimiwa Waitara kuhusu Sekretariet ya KUB kuondolewa Bungeni ni Mwongozo ambao hautakiwi kuendelea kupewa siku. Hili suala linatakiwa lijadiliwe kwa dharura ili haki itendeke katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa afya ya Bunge hili ni vizuri mkafanya maamuzi mapema ili hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani iwepo Bungeni na Watanzania watendewe haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nategemea kubomoka sana. Sasa kabla sijabomoka, naomba nishauri machache ambayo nikibomoka baadaye hamtonisikia. Naomba nishauri kuhusu suala la TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba mna barabara nchi hii za kilometa 108,000 vijijini na mijini, lakini TARURA hii mpaka leo kwenye shilingi bilioni 230 mmewapelekea shilingi bilioni 98, wamejenga kilometa 4,000 tu kati ya 34,000. Naomba majibu, ni kwa nini tunatengeneza vitu halafu pesa hampeleki? Kuna uhalali gani wa ninyi kuendelea tu kwamba bajeti nzuri wakati ukweli ni kwamba fedha hazipo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nishauri tu kwa nia njema. Mfuko wa Bima ya Afya sasa hivi mtu mmoja hawezi akapata ile Bima kubwa akatibiwa kwenye Hospitali ya Rufaa kama Muhimbili na maeneo mengine, ni lazima awepo kwenye group. Naomba nishauri, ile Bima ya shilingi 76,000 muifanye kwa mtu mmoja mmoja angalau wananchi watibiwe, siyo lazima wawe kwenye group ili isaidie Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, nishauri kuhusu suala la elimu bure. Mmeanza elimu bure, elimu bila malipo, sijui kitu gani na kitu gani. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku- wind-up atuambie fedha za walinzi, maji, umeme wameziweka wapi? Kwa sababu kwa sababu walinzi wameacha shule zetu na madawati yanaibiwa na hata fedha za elimu bure bado hawajaziongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nashauri kuhusu mikopo ya vijana na akinamama. Wamefanya jambo jema kuondoa riba ya asilimia 10, ni jambo jema wala hatukatai. Hata hivyo, ni nani aliyewalalamikia kwamba tatizo ni riba? Tatizo ni Halmashauri kutokutenga fedha. Katika bajeti hii iliyopita, kati ya shilingi bilioni 61 ni shilingi bilioni 15 tu zimepelekwa, 9% ndiyo zimetengwa kwa vijana na akinamama. Tatizo siyo riba, tatizo ni fedha hazipelekwi na Halmashauri hawana vyanzo. Badala ya ku-tackle tatizo, mnakuja na maneno mazuri mazuri ya kufurahisha Watanzania, ham-solve tatizo! Atuambie kwa nini fedha hazipelekwi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, wazee wamewasahu. Wamewapatia walemavu, it is okay, nami nawapongeza; lakini akinamama na vijana wamebakiwa na asilimia nne nne. Ushauri wangu ni kwamba wachukue 2% wawapatie wazee ili na wao katika nchi hii waone kwamba wamewakumbuka, maana kipindi cha Awamu iliyopita ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete waliambiwa watapewa hata token amount kwa mwezi. Mpaka leo hawapewi, lakini hata kwenye hizi fedha hawakumbukwi. Sasa wawatengee na wao 2%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nibomoke. Utawala Bora katika nchi hii tunapoongea msituone maadui. Hii Tanzania ni ya kwetu sote. Tunatamani kila Mtanzania mmoja wetu aheshimike kwa nafsi yake, atendewe haki kwa nafasi yake; kila mmoja awajibike kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi hii ambazo tumejiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mbunge mmoja wa Mkoa wa Manyara anasema kifua kinamuuma. Wakati anachangia asubuhi, anasema mimi kifua changu kimejaa, kinauma, naomba tu mengine niya-save kwenye kifua. Naomba nisiumie kifua, leo nibomoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Wakuu wa Mikoa ambao mmekuwa mkiwateua bila kuangalia ame-serve kwenye public service kwa muda gani mnawatoa kwenye Vyama vya Siasa, mnawaleta mnawapa nafasi za kuongoza Halmashauri na Wilaya zetu, wamekuwa wakifanya mambo ya ajabu haijawahi kutokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kwa Tunduma, siyo kwa Mkoa wetu wa Manyara, siyo kwa Hanang ambako hata mzee wetu, Mama Nagu anawekwa ndani, lakini ni Wakuu ambao wamekuja kufanya kazi ya siasa, siyo kazi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lilitokea tatizo kubwa sana katika Mkoa wetu wa Manyara. Stendi ya mabasi ambayo Mheshimiwa Waziri anasema kwamba tukusanye ushuru, ilikabidhiwa CCM mwaka huu. Stendi ya mabasi ambayo Halmashauri tunakusanya ushuru wa zaidi ya shilingi milioni 10, imekabidhiwa CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 13 Januari, 2018 tuliitwa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Kamati ya Fedha, Kamati ya Ulinzi na Usalama DC, pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa. Tukaambiwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kuanzia hivi ninavyoongea na ninyi hapa tulipo, tumekaa tangu asubuhi na siku ile Mheshimiwa Lukuvi alikuja, akatuacha pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu asubuhi tumekaa, saa
8.00 anakuja anatuita anasema, nimeagizwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nendeni mkakabidhi Stendi Kuu ya Mabasi ya Babati kwa CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe. Huyo ni mama yangu, sina sababu ya kumjibu. Naomba niendelee tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyoitwa tukatakiwa tukabidhi stendi, labda nimsaidie tu, yeye haingii kwenye Baraza la Madiwani la Mji wa Babati. CCM hawajawahi kuomba kumilikishwa stendi, hata ombi tu, acha kumilikishwa, hawajawahi kuomba. Kwa hiyo, kilichotokea, tukatoka hapo tukarudi kwenye Halmashauri yetu. Terehe 2 Machi, wakati tumeondolewa hapo hatukuruhusiwa hata kuhoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipohoji Barua ya Mheshimiwa Rais iko wapi? Tulijibiwa, Mheshimiwa Mkuu wa MKoa akasema, Mheshimiwa Mbunge, sifanyi masuala ya kitoto. Nikamwambia, Mheshimiwa Rais kama anataka kukabidhi stendi CCM, anaandika kwako. Tuoneshe hata tuone. Akasema atatuletea kwenye Baraza la Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Baraza la Madiwani, hatukuletewa barua wala Kumbukumbu Namba ya Barua ya Rais ya kukabidhi stendi, mali ya wananchi kwa CCM. Tukakatazwa kujadili kwenye Baraza la Madiwani. Nchi hii hakuna utawala bora. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyekiti wa Halmashauri akaandika barua tarehe 2 kumtaka Mkurugenzi Baraza Maalum, Waziri wa TAMISEMI anijibu, tangu lini Baraza la Madiwani linakatazwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi akakimbia akaenda kwa Mkuu wa Mkoa, akapeleka barua tarehe 5, anaomba mwongozo kwa Mkuu wa Mkoa kana kwamba hajui kazi yake kama Mkurugenzi. Mkuu wa Mkoa tarehe 6 akajibu akasema haoni mantiki ya Baraza la Madiwani kujadili amri ya Mheshimiwa Rais. Hivi mna utawala bora?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 8 Mwenyekiti akaandika mwezi wa Tatu tunaomba tukae tujadili, hiki ni chanzo kikubwa. Wakasema, shut up. Hakuna kujadili. Tukaomba, Mwenyekiti wa Halmashauri na Madiwani waende kwa wananchi kwamba stendi yetu imepokonywa na CCM. Polisi wakakataza wasiende kwa wananchi wawaambie kilichotokea. Kuna utawala bora? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kubomoka. Sasa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora mnijibu yafuatayo:-

Ni kwa nini barua ya Mheshimiwa Rais ninyi Mawaziri hamkupewa nakala? Kwa nini anaandikiwa Mnyeti? Hierarchy ya information katika nchi hii ninyi ni Mawaziri, kwa nini ninyi hamjaandikiwa, mnijibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kwa nini mmeshindwa kumshauri Mheshimiwa Rais kwamba CCM; maana sisi tulioitwa kwenye Baraza, mchakato wa muda mrefu, walitunyang’anya kwanza uwanja wa wanafunzi ekari nane tukaurudisha. Tena Katibu Mkuu wa TAMISEMI ananisikia yuko humu ndani. Barua yake ikapuuzwa, Mkuu wa Mkoa anasema hatambui barua ya Katibu Mkuu kwamba uwanja ni wa wanafunzi. Tulivyozuia uwanja, wakatunyang’anya stendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini ninyi Mawaziri mnaogopa kumshauri Rais? Kama alivyosema Mheshimiwa Malocha hapa, kwa nini mnaogopa kumshauri Mheshimiwa Rais wakati amelishwa matango pori? Naomba mnijibu, ni kwa nini ninyi mnakubali chanzo kikubwa cha Halmashauri kama hiki kinachukuliwa na ninyi mkiwa mnaangalia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mnijibu yanayoendelea Babati, kwa sababu kengele imelia. Sasa hivi kinachoendelea, CCM walivyokabidhiwa stendi, wale wafanyabiashara ambao wana mkataba wa miaka 31 mpaka 2031 na Halmashauri wameambiwa ninyi sio wamiliki, wapangaji ndio wamemilikishwa. Sasa hivi kuna vita Babati kati ya wapangaji na wamiliki wa vibanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Mawakala wa Halmashauri wanaokusanya ushuru wa Halmashauri walifukuzwa kama mbwa, stendi pale CCM wamepeleka green guard. Huu ubabe wa CCM mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wamepeleka notice wiki ya pili wanaishtaki Halmashauri. Hiyo fidia ya kuwalipa wafanyabiashara kupoteza vibanda vyao tunatoa wapi? Mawakala wameishtaki Halmashauri wamepeleka notice ya mwezi mzima, according to sheria. Wiki ya pili sasa, mnategemea tutalipa hizi fidia kutoka kwenye chanzo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba leo vyombo vya habari, usalama wa Taifa, mkamwambie Rais, Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kwamba Babati kumechafuka. Kwa sababu ninyi mnaogopa kumshauri Rais, tunamtaka Mheshimiwa Dkt. Magufuli aje ajibu Babati, ni kwa nini anachukua stendi ambayo tumemiliki tangu mwaka 2004 mpaka leo wanakabidhiwa CCM? Mungu alivyo mwema, Ofisi ya Mkoa CCM na Wilaya wameanza kupigana kwa sababu ya shilingi milioni 10. Vita vimehamia ndani sasa hivi wanagawana ruzuku. (Kicheko/Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nimesema wafanyabiashara na wapangaji wamegonganishwa; wamiliki wamenyang’anywa, wapangaji wamekabidhiwa vibanda, moto unafukuta, lakini inawezekana hata mali za wafanyabiashara zikachomwa moto kwa sababu waliotolewa wana uchungu na vibanda vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fukuto lingine, CCM wanagawana hiyo ruzuku ya shilingi milioni 10, moto umewaka kati ya mkoa na wilaya, wanapigana vikumbo. Vile vile Halmashauri imeshtakiwa na Mawakala kwa kuvunja mkataba; Halmashauri imeshtakiwa na wananchi kwa stendi yao kukabidhiwa CCM; na Halmashauri imeshtakiwa na wamiliki wa vibanda wenye mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu hii hoja tunaambiwa ni barua ya Rais. Tunaiomba hiyo barua tupewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, group la wazee wa CCM na wananchi wa Babati walikuja kumwona Waziri Mkuu mwezi wa Pili…

T A A R I F A . . .

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, no research, no right to talk. Sisi ndio Baraza la Madiwani tunaopokea maombi ya yeyote anayeomba ardhi awe CHADEMA, awe CCM. Sasa wewe unayeongea huko ulikuwepo kwenye Baraza au kwenye Kamati ya Mipango Miji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawajawahi kuomba wala hawajawahi kumiliki. Naomba record iwe sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuja kumwona Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Halmashauri na Madiwani na wazee; akatukaribisha vizuri miezi miwili iliyopita, akasema atapeleka kwa Mheshimiwa Rais. Mpaka leo hakuna majibu. Maana yake kama inafikia hatua mpaka level ya Waziri Mkuu tunakuja hamtupi majibu, halafu tunaambiwa kuna barua ya Mheshimiwa Rais; hivi barua ya Mheshimiwa Rais kwa rasilimali ya nchi ni siri?
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. PAULINE PHILIPO GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa maoni yangu katika Bajeti ya Serikali iliyokuwa mbele yetu. Naomba nianze mchango wangu kwa kusoma Mwanzo 1:26. Mimi ni Mkristo naomba tu nisome. Inasema: “Mungu akasema na tumfanye mtu kwa mfano wetu.”

Mheshimiwa Spika, mzungumzaji aliyepita sasa hivi alikuwa anazungumzia suala la ushirikishwaji, kwamba halmashauri zetu zishirikishwe na Bajeti ya Serikali ishirikishe yote. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati ametuletea Bajeti yake Alhamisi iliyopita, kuna jambo ambalo si zuri sana masikioni mwa Watanzania. Jambo la kumtukuza mtu mmoja kwamba amefanya, amefanya, amefanya, amefanya. Ameanza ukurasa wa tatu (3) akieleza Mheshimiwa Rais kafanya, kafanya mpaka kujenga ukuta wa Mererani kafanya.

Mheshimiwa Spika, Tanzania ni ya kwetu sote na nchi yetu inaongozwa kwa taratibu na sheria. Bunge inapitisha matumizi ya yeyote, mpaka ya Ikulu tunapitisha. Serikali pia inasimamia kile ambacho Bunge tumepitisha na Mahakama pia wanatusaidia. Kwa hiyo, mimi binafsi naona, hayo ni mawazo yangu, kumtukuza sana Mheshimiwa Rais hatumsaidii. Tuongee ukweli kwamba Watanzania wanalipa kodi, kodi hizi zimetumika zimefanya haya na haya na haya na haya. Tuongee tu ukweli, kwamba Bunge limepitisha Bajeti hii; tena Mheshimiwa Spika juzi uliweka vizuri, ukasema kinacholetwa Bungeni ni mapendekezo, Wabunge sisi tuna- amend, tunarekebisha, tunaweka mawazo yetu, tuna-own pamoja kwa sababu Tanzania ni ya kwetu, kuna watu wanalipa kodi, kuna watu lazima wahudumiwe, lakini kusema kwamba Mheshimiwa Rais amefanya, amefanya; mimi…

T A A R I F A . . .

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee na hapa tunazungumza masuala ya msingi, ni bajeti ya wananchi iko mbele yetu. Kwa hiyo mambo mengine tupunguze tu utani.

Mheshimiwa Spika huu ni ushauri wangu, kwamba ni kweli Rais ameomba kura kwa Watanzania, lakini Rais hafanyi kila kitu. Tusiwe waongo, na tusimtukuze Rais, tumshauri kwa upendo, tumweleze ukweli.

T A A R I F A . . .

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, unajua ukimheshimu mtu muda mrefu sana unaweza ukachoka, ukamvunjia heshima. Huyu mama kuna siku nitachangia Jimbo lake lina matatizo mengi sana. Kuliko majimbo mengine yote, lakini huwa namheshimu sana.

Mheshimiwa Spika naomba niendelee, kwa hiyo naendelea kumheshimu mama yangu. Suala la Rais kafanya, mara elimu bure, mara ukuta, mara hiki. Nchi hii kuna mihimili mitatu, kila mhimili una kazi yake; lakini pia hizi fedha sisi ndio tunaidhinisha. Hata hilo la ukuta wa Mererani ni Kamati zilizopita za Bunge walishauri. Kwa hiyo Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri tu Mheshimiwa Waziri, hatuna sababu ya kumtukuza Mheshimiwa Rais, alishachaguliwa ni vizuri unapoandika…

T A A R I F A . . .

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, ni maamuzi yenu kuendelea kumtukuza lakini hata Mungu katika Mwanzo 1:26 alisema tumfanye mtu kwa mfano wetu. Alihitaji ushirikishwaji, si kutukuza tu mtu mpaka mnapitiliza, ni vizuri mka-moderate, huo ni ushauri wangu.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukiongea sana kuhusu Bajeti delivery na disbursement ya fedha zenu kwa Wizara. Bajeti hii ambayo imetekelezwa ambayo sasa wanatueletea leo wametuonesha kuwa kuna baadhi ya Wizara wamewapa fedha kuliko Wizara nyingine zozote.

Mheshimiwa Spika, mfano, Wizara ya Habari, waliwapa bilioni nane kati ya nne; Tume ya Taifa ya Uchaguzi bilioni mbili kati ya sita; Wizara ya Mambo ya Ndani, bilioni kumi na moja kati ya nne; Ofisi ya Makamu wa Rais bilioni tano kati ya mbili; wakati Wizara ya Maji iliomba bilioni mia sita maji ambayo yanagusa maisha ya Watanzania; kila mmoja wetu, bilioni mia mbili mliwapa kati ya mia sita za development.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukisema kwamba, ni vizuri wakaheshimu maamuzi ya Bunge pale tunapokuwa tumepitisha fedha hizi. Haiwezekani Wizara moja wakaipa zaidi ya asilimia 300 hata Mwaka wa Fedha haujakwisha wakati maeneo mengine hawapeleki fedha. Kwa hiyo ni vizuri, wakaangalia wao wenyewe. Hata Wizara yao juzi wakati wametuletea zaidi ya asilimia 63 wameipa, wametumia sawa, kwa sababu anayekaa na chungu cha ugali ndiye anayekata tonge kubwa, sawa; lakini maeneo mengine hawapeleki fedha na maeneo mengine wanapeleka zaidi ya asilimia 200. Hivi tunawaaminije wa? Kwa hiyo, nahitaji ufafanuzi juu ya hili, kwa nini wanatoa fedha kwa upendeleo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala zima la bajeti hewa, tunapoambiwa hii bajeti ni hewa, ni vizuri tu wakatuelewa. Kwa sababu kazi yetu leo ni kushauri, lakini Watanzania ipo siku wataamua kwamba ninyi mtakaa pembeni na ninyi mtashauri na sisi tutaongoza. Kwa hiyo naomba nizungumze kuhusu bajeti hewa, ni vizuri kwa sababu kila mmoja ana muda wake wa kuchangia. Kila mmoja atashauri, tuna siku saba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Kamati ya Bajeti ambayo wamekaa nayo muda mrefu sana imeshauri, kwamba mpaka sasa wameweza ku-perform kwa trilioni 20, 10 nzima hawawezi ku-delivery kwa muda uliobaki. Ni kwa nini sasa wanatuletea Bajeti ile ile? Bajeti ya sasa hivi wameongeza bilioni mia tano, on top of bajeti ya mwaka jana. Ni kwa nini sasa wanaongeza bajeti wakati wanajua performance yao ni trilioni 20 kati ya hizo zaidi ya 31, 32, ambazo wanaziomba? Kama wao ni waungwana hawataki tuite kwamba bajeti yao ni hewa hata performance hii ambayo wamekaa na Kamati ya Bajeti japo na Hotuba yetu wameikataa hata haya hawayaoni?

Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha, katika fedha ambazo tumezitenga za Development ni trilioni tano tu ndizo wameweza ku-delivery mpaka sasa; hivi wanategemea hii bajeti ambayo wanatuletea kati ya trilioni kumi na moja za maendeleo, tano tu ndizo wamepeleka mwezi mmoja ndio umebaki, hawawezi kufanya, ndiyo maana tunawaambia bajeti hii ni hewa. Ni vizuri wakakubali wakakaa chini wakaiandika upya, tufanye according to kile ambacho tunaweza kukusanya.

Mheshimiwa Spika, TRA wamekusanya mpaka sasa trilioni kumi na mbili, Halmashauri zetu wamekusanya bilioni mia nne kati ya mia sita; lakini wanatuletea wakati wanaona performance ya bajeti hii imefeli. Ndiyo maana tunasema uungwana ni vitendo, wakubali yaishe, kwamba tutumie kile ambacho tunaweza, maana hata mikopo ya wafadhili na zile support tunazopata kwa wahisani zime-drop, fedha haziji. Halafu wanatuletea bajeti ambayo hatuwezi kutekeleza.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda naomba tu nizungumzie masuala ya msingi sasa kwenye halmashauri zetu. Mheshimiwa Waziri tulizungumza sana kuhusu halmashauri kuzi-cripple. Wamefanya halmashauri zetu zimeshindwa kufanya kazi; mzungumzaji aliyepita ameongea vizuri. Walivyopitisha bajeti ya mwaka jana kodi ya ardhi, ushuru wa machinjio na hivi vingine wakaona kwamba wafute na vingine Serikali Kuu ikusanye.

Mheshimiwa Spika, kwa hali ya kawaida fedha haziji kwenye halmashauri zetu; OC haziji na kama zinakuja zinakuja kidogo sana. Wakati huo huo hata ile mikopo ambayo halmashauri ilikuwa inapata riba pia wameondoa riba mimi sina tatizo. Kama nia ni njema pia wangekumbuka hata wazee kwenye mikopo ya asilimia 10; lakini kodi ya majengo, kodi ya mabango, mpaka sasa hawasemi kwamba turudishe kwenye halmashauri zetu. Wanachoendelea kufanya wanaendelea ku-cripple halmashauri zetu wanaondoa mpaka na watumishi; halmashauri hizi wameziuwa.

Mheshimiwa Spika, tuliwashauri mwaka jana hawakusikia, mwaka huu wameendelea na business as usual maana yake ni nini? Itafikia hatua nchi hii kila kitu kita-paralyse kwa sababu halmashauri hizi zilianzishwa kwa mujibu wa sheria. Wanatakiwa waziachie halmashauri zetu vyanzo vyao vya mapato.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri pia bajeti yetu ika-reflect maisha ya Watanzania. Leo tunavyoongea hii bajeti wanayoleta hapa na vigelegele hapa watumishi hawajawagusa, hakuna increment ya salaries kwa watumishi
... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, napenda kuchangia kuhusu gratuity ya Waheshimiwa Wabunge. Kukata kodi gratuity ya Waheshimiwa Wabunge siyo sahihi kabisa kwa kuwa kwa sasa tunakatwa kodi kwenye mishahara yetu. Nashauri wakati wa Finance Bill ondoeni kodi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni lini agizo la Mheshimiwa Rais la kushusha riba katika taasisi za fedha litaanza ili wananchi wetu wakope na wakuze uchumi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, pitieni upya mgawo wa fedha za elimu bure kwani hazitoshelezi kuendeleza shule zetu
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
HE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali na Wizara ituambie ni kwa muda gani wale nyumba zao zilizopigwa (X) zilizopo au zilizokutwa na sheria ya mwaka 2007 zitafidiwa kwa kuwa sasa hawaruhusiwi kabisa kufanya maendeleo yoyote. Ni vyema wakaruhusiwa kufanya ukarabati not ujenzi wa nyumba hizo kwa kuwa hata zikidondoka kwa sasa hawaruhusiwi kukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ng’ombe, punda wanachungwa pembezoni mwa barabara wanasababisha sana ajali, hivyo TANROADS kote nchini watakiwe kuweka doria kwa wanaochunga ng’ombe, punda, mbuzi, kondoo pembezoni ya barabara wachukuliwe hatua kali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, minara ya simu kwenye vijiji vyenye kuwa na tatizo la mawasiliano wasaidiwe upesi kama vile vilivyopo Babati. Mfano, Himiti, Chemchem, Imbilili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgao wa fedha za Mfuko wa Barabara TANROAD; asilimia 70 za fedha za Mfuko wa Barabara upunguzwe hadi asilimia 50 ili wananchi wa Tasime wenye barabara nyingi wasaidiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, all the best brothers.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwakunipa dakika tano angalau niseme machache kwa ajili ya Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli kama kuna Mbunge atasimama kwenye Bunge hili na kusema bajeti ya maji isiongezwe basi huyo Mbunge labda alipata Ubunge kwa kupendelewa na alipewa zawadi tu, hakutafuta kura, lakini kama alikwenda kwa wananchi akaona kero zao hatathubutu akasimama na kusema bajeti hii iziongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja za Wabunge wote wanaosema kwamba ile Sh.50 iongezwe mpaka Sh.100 ili wananchi wetu wapate maji. Wale ambao majimbo yao, mikoa yao ina maji, tafadhali mtuache sisi ambao bado wananchi wetu hawana maji ili tuunge mkono hoja hii ya kwamba fedha ziongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hili kwa sababu mimi niko Jimbo la Babati Mjini lakini nina Kata nzima ya Sigino yenye vijiji vinne haina maji. Asubuhi nilikuwa naongea na Mbunge mmoja ananiambia Mheshimiwa Mbunge inawezekana sana fedha hizi zisiongezwe au zikaongezwa, nikamwambia lakini hebu tupige picha siku moja Wabunge tukae wiki nzima humu ndani tusioge na tusiwe na maji itakuwaje? Akaniambia hivi, tutanunua maji ya Kilimanjaro tutaoga. Nikamwambia okay, una uwezo wa kununua maji ya Kilimanjaro lakini mama na bibi yako uliyemwacha kijijini kule hana uwezo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tusiweke itikadi zetu katika suala hili. Niombe Serikali isikilize kilio hiki cha Wabunge wote kwamba fedha hizi ziongezwe ili wananchi wangu wa kata ya Sigino, Jimbo la Babati Mjini wapate maji. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika, wale akinamama walimvika mpaka na mgoroli akawaahidi kwamba katika bajeti hii fedha zitakwenda katika Vijiji vya Sigino, Singu, Dagailoi na Imbilili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kwenye kitabu zimetengwa shilingi milioni 600 tu hazitatosha, lakini fedha zikiongezwa tutapata shilingi 2,700,000,000 ambazo tumeziomba. Kwa hiyo, niunge mkono kabisa hoja ya Wabunge kwamba fedha hizi ziongezwe na wananchi wa Tanzania wapate maji. Ni aibu, akinamama wanateseka, wanachota maji kongoroni, ndoo zao zinavunjika, wengine wanarudi usiku, wengine wanabakwa, wanahangaika wanatafuta maji halafu sisi wanawake humu ndani tuseme fedha zisiongezwe, inasikitisha sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kabisa Serikali kama mnaona tozo ya mafuta haitoshi twendeni hata kwenye mitandao ya simu, tuna 0.03 ya service charge ambayo siku zote wamekuwa hawalipi. Tumekuwa tukizungumza hata kwenye TAMISEMI hizi fedha haziendi. Hebu Serikali kaeni chini muangalie fedha hizi hata kama ni shilingi 20, 30, 50 tuzipeleke kwenye Mfuko wa Maji ili zipeleke maji kwa wananchi wetu. Wananchihawa wamevumilia kwa miaka hamsini, kwa nini tusiwatendee haki fedha zikaenda wakapelekelewa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sina ugomvi na Mawaziri, wao wamepelekewa asilimia 19, lakini Serikali kama mngepeleka asilimia 100 ya shilingi bilioni 900 ambazo zilipangwa maana yake kero hizi zingepungua. Kwa hiyo pia niombe Waziri wa Fedha pamoja na Serikali kwa ujumla wake Wizara ya Maji wapelekeni pesa. Pamoja na kwamba tunaomba fedha hizi ziongezwe, lakini fedha zile zilizopangwa ambapo miradi iko kwenye mchakato pia ziende.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kwenye Jimbo langu la Babati Mjini, Vijiji vya Haraa na Imbilili tulishampelekea Mheshimiwa Waziri bado kusaini tu mikataba, lakini tunaambiwa zimeenda asilimia 19 tu, bajeti ya Wizara ya Maji ilitakiwa ziende asilimia hata 50, 60, 70 au 80 mbona Wizara ya Ujenzi fedha zimeenda? Kwa nini Wizara ya Maji ambayo inamgusa kila mwanamke katika nchi hii msipeleke fedha?Wangapi waonapita kwenye barabara zenu za lami mnapeleka asilimia zaidi ya 70 au 80 lakini akinamama hawawezi wakapelekewa fedha zao?Kwa hiyo, niunge mkono hoja hii lazima Wabunge tuwe serious kwamba Wizara hii waongezewe fedha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata majibu ya maswali yafuatayo:-

Ni lini Polisi watatoa EFD Machines wanapokusanya faini? Ni lini ombi letu la Magereza Babati kutugawia eneo la makaburi litatekelezwa? Ni lini Serikali itatupa fedha za kumalizia jengo la RPC Manyara? Ni lini Sheria ya Zimamoto itarekebishwa?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, tunaomba mtujengee uwanja wa ndege Manyara Babati pale eneo la Magugu. Pia tunaomba mawasiliano ya simu Kijiji cha Himiti, Chemchem, Imbilili na Babati Mjini.

Mheshimiwa Spika, vile vile tunaomba mwalipe fidia wananchi walio pembezoni mwa barabara za lami mita 12.5 zilizoongezeka. All the best.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kunipa nafasi na mimi nichangie machache katika Wizara yetu hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. (Makofi)

Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetupa nafasi ya upendeleo ya kutupa afya njema sisi Wabunge wa Bunge lako Tukufu ili kuendelea na majukumu yetu ya kulitumikia Taifa Mwenyezi Mungu tunamshukuru sana. (Makofi)

Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini tena na kuniteua kuwa miongoni mwa wasaidizi katika Wizara hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa naomba nimuahidi Mheshimiwa Rais kwamba nimepokea kwa mikono miwili kazi hii na nitaifanya kwa moyo wangu wote kumsaidia Mheshimiwa Waziri na kuisaidia Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Niwashukuru wana Babati kwa jinsi ambavyo wameniamini kuwa Mbunge wao wa Jimbo kwa awamu ya pili. Niwashukuru sana na niwaahidi kwamba nitaendelea kuwa mtumishi mwema kwao na msikivu ili tuweze kufikia yale malengo ambayo tumejiwekea ya maendeleo katika jimbo letu. (Makofi)

Kwa namna ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Innocent Bashungwa amekuwa akitupa ushirikiano katika Wizara yetu, lakini amekuwa akitupa maelekezo mbalimbali ili kutusaidia kufikia malengo ya Wizara yetu pamoja na malengo yaliyoanishwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 - 2025; Mheshimiwa Waziri nakushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani za dhati pia kwa Katibu Mkuu pamoja na timu yetu ya Wizara, Dkt. Hassan Abbas, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Ally Possi pamoja na watendaji wetu wa Wizara na wadau wa Wizara hii wamekuwa msaada kwetu, lakini wamekuwa wakitupa ushirikiano mkubwa sana. (Makofi)

Niwashukuru wadau wote wa sekta hii tumekuwa tukishirikiana kwa karibu lakini pia niwashukuru viongozi wa dini ambao wamekuwa wakiendelea kuombea Taifa letu la Tanzania na kumuombea Mheshimiwa Rais wetu na Watanzania kwa ujumla; nchi yetu imeendelea kuwa salama na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee niwashukuru wale wote wenye mapenzi mema, familia yangu, nawashukuru wanangu nawaona hapo juu Irene pamoja na wenzako kwa maombi ambayo mmekuwa mkituombea mama yenu pamoja na Tanzania na tunawashukuru kwa maombi hayo yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Niwashukuru kwa namna ya pekee Wabunge wote wa Bunge hili waliochangia hoja ya Mheshimiwa Waziri kaka yangu Bashungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maoni mazuri ya Kamati ya Bunge lakini Wabunge walioongea humu ndani ni Wabunge 25, waliotuandikia kwa maandishi ni Wabungu wanne, jumla Wabunge 29 wameweza kuchangia hoja hii iliyoko mezani. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, michango ya Wabunge hawa sisi tumepokea kama Wizara na imekuwa michango ya afya sana kwetu kwa ajili ya kazi hii ambayo ipo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ni Wizara inayogusa ajira za watu, ni Wizara inayogusa hisia za watu, ni Wizara inayoelimisha lakini ni Wizara inayohabarisha Watanzania. Bila vyombo vya habari maana yake taifa letu tunakuwa kwenye giza. Wizara hii imekuwa ikihabarisha inafanya kazi kubwa ya kuunganisha Watanzania. Lakini Wizara hii kupitia michezo ni Wizara ambayo imekuwa ikisaidia Watanzania kujenga afya zetu lakini kuisaidia pia na Wizara zingine na Serikali kwa ujumla kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na afya njema na hata itasaidia pia kupunguza matumizi kwa upande wa Wizara ya Afya kwa bajeti ya dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukuhakikishie kwamba maoni yao yote tumepokea na tutaendelea kuzingatia na kwa sababu ya muda kwa kuwa nina dakika 10 naomba nizungumzie hoja kadhaa ambazo zimewekwa mezani na nianze kuhusu hoja hii ya kukuza michezo katika nchi yetu.

Waheshimiwa Wabunge wamezungumza suala zima la kuhakikisha suala la michezo linapewa kipaumbele. Tunashukuru mnafahamu kazi kubwa inayofanywa na academy mbalimbali kwa ajili ya kukuza vipaji. Sisi kama Wizara tunaona kwamba hili ni la msingi na ndio maana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge Wizara yetu ikishirikiana na Wizara ya Elimu, Wizara ya TAMISEMI, tuliunda Kamati Maalum ambayo pia itapita huko kwenye ngazi za chini kuboresha michezo katika Halmashauri zetu na katika shule zetu za sekondari na za msingi ili vipaji vya Watanzania hawa ambao wanahitaji michezo hii vikuzwe kwa kuwapatia walimu bora, lakini pia mazingira mazuri ya viwanja pamoja na miundombinu ipatikane kwenye ngazi za chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuwahakikishieni kazi hii ambayo mmtupa na maoni ambayo mmetupa kuhakikisha michezo tunaboresha kuanzia ngazi za chini tumeshaanza kufanyia kazi na Kamati hii karibuni inakamilisha pia kupitia combinations mbalimbali ambazo zinafundishwa kwa shule za form five na form six kuhakikisha kwamba watoto wetu hawa ambao wanatoka huku chini, lakini wanafikia kidato cha tano na cha sita waweze pia kusoma masomo ya michezo ambayo tunaishukuru Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Elimu wameshafikia hitimisho kuhusu hili na kuanzia mwakani sasa udahili utafanyika ili hao watoto wetu waweze ku-specialized katika masomo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili Chuo chetu cha Malya pia Waheshimiwa Wabunge katika bajeti hii tunakwenda kukiboresha. Ukiangalia kwenye bajeti yetu ya mwaka huu ambao unaisha mwezi Juni tumetenga zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya Chuo chetu cha Malya na maana yake fedha hizo zitakwenda kule zitaboresha. Lakini kwenye bajeti hiyo ambayo leo tunaomba ridhaa Waheshimiwa Wabunge kwenu Serikali kupitia Wizara hii tumetenga fedha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya Chuo chetu cha Malya. Maana yake hao watoto wakianzia huku chini watakapofika kwenye chuo hiki na masomo ya juu wanakuwa wamebobea katika masuala ya michezo. (Makofi)

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuhakikishieni kazi hii tunaendelea kuifanya vizuri na kusimamia pia michezo kwa wanawake. Tunaomba mtuamini na hili tuendelee kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusu vijana wetu kupata mafunzo kule walipo, tumeshauri sana kuhusu taasisi yetu ya TaSuBa. Tumeshauri pia ndani ya Serikali tuendelee kushauriana na TAMISEMI, Wizara ya Elimu pia kuhakikisha mafunzo ya vijana wetu ya usanii yanapatikana kwa Wilaya zetu kupitia VETA, tunategemea kuanzisha ushirikiano pia na VETA ili vijana wetu wapate mafunzo hayo katika wilaya zao ambako VETA zipo. (Makofi)

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge kwa hili pia itasaidia sana vijana wakipata elimu hawatakuwa wanafungiwa fungiwa maana tumeona pia sio kuwafungia fungia tu ndio kazi yetu, lazima tuhakikishe pia vijana wetu wanapata elimu. Kwa hili tupeane ushirikiano na mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka niende kwenye suala la TBC. Tunashukuru maoni yenu Waheshimiwa Wabunge kwa upande wa kuboresha TBC, lakini pia Wizara yetu inaishukuru Wizara ya Fedha kutupatia fedha za TBC zilitolewa zote kwa ajili ya kuimarisha usikivu katika maeneo mbalimbali ambako usikivu haujafika, ni TBC Television pamoja na redio zake. Nikuhakikishie kwamba Wizara yetu itaendelea kufanya kazi hii na katika bajeti hii pia tunaomba shilingi bilioni tano na tunahakikisha kwamba tutazimamia kwamba fedha hizi zifike kwenye mikoa na wilaya ambazo kwa kweli usikivu bado haujafika. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge kwenye hotuba yetu mmeona kwamba ni maeneo mbalimbali kama Kasulu, Tanga, Ngorongoro, Kahama, Bunda, Karagwe na maeneo mbalimbali usikivu bado tu. Tuwahakikishieni mpaka sasa tumeshafika Wilaya 102 lakini lengo letu ni kufikia Wilaya 119 kati ya 161 kupitia hizi shilingi bilioni tano ambazo mtatupatia Waheshimiwa Wabunge tuwahakikishie tutazimamia na usikivu utapatika kupitia redio pamoja television.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini jingine ni suala la madeni ya TBC; Waheshimiwa Wabunge wameshauri kwamba TBC madeni yao yalipwe. Nikuhakikishie TBC wameshaanza kulipwa madeni yao 1.8 billions zimeshaanza kuingia na Wizara imeshawaandikia wale ambao tunawadai na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la TSN. Tumekaa kwa karibu sana TSN kuangalia kwanza kwa nini makusanyo yao yameanza kushuka. Kuna suala la UVIKO 19 lakini kuna suala pia la mitambo chakavu. Waheshimiwa Wabunge mmelizungumzia hili ndugu zangu, sisi Wizara yetu pamoja na Wizara ya Fedha tunashukuru fedha hizi ambazo TSN ilikuwa inadai zimeanza kulipwa na mmeshauri mtambo ununuliwe. Hili tumeshaanza kulifanyia kazi kwenye zile shilingi milioni 495 ambazo zimeshaingizwa kutoka Hazina tumeshaelekeza mchakato uanze wa ununuzi wa mtambo huu ili TSN sasa waweze kuchapisha magazeti ambayo yana ubora na yaweze kufika kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mtambo utakaponunuliwa maana yake magazeti haya sasa yatakuwa na ubora, lakini pia yatafikia Watanzania kwa wakati. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuwatoe wasiwasi, uhakiki wa madeni unaendelea lakini pia kupitia Wizara ya Fedha, tuishukuru Wizara ya Fedha wamehakiki madeni ya TSN na wameendelea kufuatilia na ndio maana walipohakiki waliamua kutupatia kiasi fulani. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba kazi hii inaendele na TSN watanunua mtambo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa fursa nami nichangie katika Bajeti hii Kuu ya Serikali. Nimshukuru pia Mwenyezi Mungu, huyu Mungu ambaye anatupa pumzi ya uhai bila kuilipa VAT au chochote, ni kwa neema yake tu, namshukuru sana, anatufanya tutimize wajibu wetu tukiwa na afya njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze viongozi wetu kuanzia Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha, Mawaziri na watendaji wa Serikali kwa kuendelea kutumikia Taifa letu kwa upendo na moyo wa uzalendo. Hongereni sana, na sisi tunawaombea pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi hii bajeti, mimi binafsi nilivyoipokea nikawa najiuliza ni nani huyu anakwenda kuthubutu kuipinga bajeti hii? Nitatoa sababu za kutosha tu; kwa sababu naamini Wabunge tunawakilisha wananchi ambao wametutuma, tunaishauri Serikali lakini bajeti hii imekwenda kuonesha vitu vikubwa ambavyo havijawahi kufanyika. Nafikiri siku ya kura kama vile haifiki, tuone ni nani anasema hapana kwenye bajeti hii, na sababu ntazitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wachache wanasema hii bajeti ni ya vitu siyo ya watu, lakini vitu hivi wanavyovisema naomba nivitaje, ambavyo wao wanaona ni vibaya sana kwa Watanzania, vimeorodheshwa ukurasa wa 19 kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri; ni ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara, Dar es Salaam hadi Kibaha, kilometa 19. Wananchi wa Dar es Salaam walikuwa wanahangaika na foleni huko, wanapoteza muda, lakini hiki kwa wengine ni kitu kibaya, haigusi watu, sasa sijui ni watu wapi wanataka waguswe.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vitu wanavyovisema vingine mfano ni ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero. Natoa tu mfano, michele, mipunga ilikuwa inakwama inazamia kwenye ule mto lakini leo daraja limejengwa watu wanasema ni bajeti ya vitu. Bajeti hii ya vitu inayotajwa ni bajeti ambayo inakwenda kutatua tatizo la upungufu wa umeme katika nchi yetu lakini watu wanaona kwamba tunapeleka pesa nyingi huko, ni tatizo, ili viwanda vianze na huku chini wananchi wanufaike na energy ambayo imekuwa ikiwa na upungufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hao watu wanathubutu kubeza hata jitihada za ununuzi wa ndege na vitu vingine. Ukiona watu wamekosa vitu vya kuongea utashangaa wanabaki sasa kuzungumzia mambo madogo madogo, mara wigi, wigi, wigi. Hata hivyo wananchi wetu waliotutuma, naamini wengi tunaowawakilisha huko vijijini hawavai haya mawigi ambayo tunayatetea, wengi wanahitaji maji, umeme na barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili, wanasema milioni 50 hazijatolewa. Nitoe mfano tu, mimi ni wa Babati hapo, ujenzi wa barabara hii kutoka Dodoma mpaka Babati, kilometa zaidi ya 260 ni milioni 50 ngapi kwa vijiji vingapi zimepelekwa kupitia barabara hii tu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi wa maji tu, mfano kijiji change, juzi nimetoka kuzindua huo mradi tukiwa na mwenge pale…

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Taarifa.

MHE. PAULINE P. GEKUL: …ujenzi wa mradi wa maji wa Imbilili wa milioni 600…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gekul, kuna taarifa; Mheshimiwa Salome Makamba.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda nimpe taarifa mzungumzaji kwamba wakati wa kampeni, wakati Chama cha Mapinduzi kinaomba ridhaa ya kuongoza, pamoja na milioni 50 walizoziahidi, waliahidi wataleta barabara, maji na kujenga reli. Kwa hiyo wasipotoshe kwa ku-substitute vitu wanavyojengea wananchi na milioni 50, wapeleke milioni 50 za wananchi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nilikumbusha jana, nimekumbusha na leo; matumizi ya Kanuni ya 68(8), tuisome tunazo nakala, ni taarifa ya namna gani unayoweza kuitoa.

Nasisitiza tena; tuisome Kanuni ya 68(8) matakwa yake. Mheshimiwa Gekul, endelea na mchango wako.

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, natolea mfano Kijiji kimoja tu cha Imbilili cha jimboni kwangu, milioni zaidi ya 600 wamepeleka pale mradi wa maji ambao walikuwa hawategemei katika maisha yao. Hata hivyo, kuna watu wanajificha milioni 50, labda sasa kuna tatizo la kihesabu, Walimu wa hesabu watusaidie, kati ya milioni 600 ambazo wamepelekewa wanakijiji wanakunywa maji na milioni 50 kipi kikubwa? Huo ni mfano tu, ndiyo maana nasema watu hapa tunachanganyana kwa sababu wamekosa vitu vya kuongea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine mtu anasimama kabisa Mbunge anasema bajeti imekuwa haijaongezeka, ya Kenya imeongezeka; so what? Wakati huo huo mtu anasimama tusipotekeleza bajeti ile ya trilioni 32 anakwambia hii bajeti hewa. Hawa watu watatupotezea sana muda, Watanzania wanasubiri tupeleke maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niseme ni kwa nini yeyote humu ndani hatakiwi kusema hapana kwenye bajeti hii. Baada ya kutoa utangulizi huo niende kwenye details za wananchi wetu vitu gani wameguswa, mfano wale wa majimbo ya mijini lakini kwa wananchi wa nchi hii wafanyakazi ni takribani kama milioni moja tu. Wananchi wa Tanzania wengi wao ni wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wadogo, kila mmoja anawakilisha hawa watu kwenye Bunge hili. Unakataaje bajeti hii, la kwanza, Serikali kuondoa Ushuru wa Forodha wa EFD machines kutoka asilimia kumi mpaka sifuri, wafanyabiashara wadogo wadogo walikuwa hizi mashine wananunua kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Serikali imepunguza hili ili wafanyabiashara wapate hizi mashine kwa bei rahisi, kodi ikusanyike, mtu anasema hapana kwenye hii bajeti, nitamshangaa, labda kama hawakilishi wananchi. Kwa sababu hizi mashine zilikuwa zinasumbua, leo Serikali imepunguza hizi gharama ili wapate kwa bei rahisi kodi ikusanyike unakataaje hii bajeti?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili anijibu ambaye anategemea kuikataa hi bajeti; kima cha chini cha kodi kimepunguzwa kwa shilingi 50,000 mpaka 100,000, mtu ambaye mauzo yake si zaidi ya milioni 14 zaidi ya 100,000 imepunguzwa, wananchi wetu wamepunguziwa mzigo wa kodi; mtu anakataaje hii bajeti, hawa wafanyabiashara wadogo wadogo tunaowakilisha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo natamani nijibiwe kwa nini huyu mtu akatae hii bajeti; hawa wafanyabiashara wadogo wadogo walikuwa wanaandaa mahesabu yao mtaji wa kuanzia milioni 20 alikuwa anatakiwa ampate mtu wa CPA amuandalie bajeti yake, lakini sasa hivi ni mpaka mtu mwenye mtaji wa milioni 100, hao wa chini wameachwa ili mitaji yao ikue; unakataaje hii bajeti? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne; Mheshimiwa Waziri ameongeza tena muda wa miezi sita kwa wale ambao walikuwa wanadaiwa riba za kodi mpaka mwezi wa 12 ili walipe zile kodi wanazodaiwa, amewapunguzia mzigo huo. Huyo anayekataa hii bajeti wananchi wake wamepunguziwa huo mzigo ni nani? Labda kama hawawakilishi wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tano, kuanzisha Kitengo cha Ombudsman, cha kupokea malalamiko ya wafanyabiashara ambao walikuwa wanaombwa rushwa, ambao walikuwa wanafungiwa maduka yao, kodi zinadaiwa kwa nguvu. Leo Serikali imeona iandae kitengo maalum kabisa cha kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara pale wanapoonewa. Mtu anasema hataki, maana yake wafanyabiashara wetu waendelee kutozwa kodi kubwa ambayo hawastahili, wafanyabiashara wetu waendelee kuchukuliwa rushwa. Mimi kama Mbunge ninayeongoza Jimbo la Babati Mjini ambalo hawa wafanyabishara wamekuwa wakiteseka nasema bajeti hii haijawahi kutokea. Sasa nasubiri huyo anayekataa kwenye jimbo lake kuna wafanyabiashara au hakuna wafanyabiashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko yote, wafanyabiashara walikuwa wanalia hapakuwa na grace period ya kodi. Unakwenda tu unapewa TIN na kodi unakadiriwa hapohapo, leo Serikali imewapa miezi sita kafanye biashara yako halafu tuje tukukadirie kodi. Halafu mtu unasimama unasema hapana kwenye bajeti hii, labda kama unaongoza fisi, ngedere, siyo binadamu hawa tunaowaongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni bajeti ambayo mimi binafsi sijawahi kuiona. Pia kuna watu walikuwa wamechimba visima vyao, kila mwezi wanalipa Sh.100,000, Serikali imeondoa hiyo, mtu anasema hapana kwenye bajeti hii ili wananchi waendelee kutozwa wapate tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho katika haya mazuri kwa siku ya leo; tozo zaidi ya 54 zile za TFDA, TBS, zimeondoshwa. Kulikuwa na halmashauri inakwenda kukagua biashara ya mama lishe, TFDA wanakwenda kukagua inatozwa mara mbili, wananchi walikuwa wanalalamika. Leo hii Serikali imeondoa tozo zaidi ya 54 halafu eti siku ya kupitisha bajeti mtu anasema hapana. Mimi nafikiri siku hiyo TV zionyeshe kabisa Watanzania watu gani ambao hawataki wananchi wapate maisha nafuu, wawaone kwa haya mazuri atakayesema hapana kwenye bajeti hii, huyo ni adui wa Watanzania na wajasiriamali wadogo wadogo na Watanzania zaidi ya milioni 45.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri siku hiyo TV zionyeshe kabisa Watanzania watu gani ambao hawataki wananchi wapate maisha nafuu wawaone kwa haya mazuri, atakayesema hapana kwenye bajeti hii, huyo ni adui wa Watanzania na wajasiriamali wadogo wadogo na Watanzania zaidi ya milioni 45. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu tu kwa Serikali yangu, nawaomba, suala la watumishi siyo la kwao. Mmelipa madeni, mmeendelea ku-review madeni yao na kuyalipa, kamilisheni hilo la upande wa wafanyakazi. Wasijifanye wao ndio wanabeba, mnafanya mambo mazuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nami nitoe machache katika Muswada ambao uko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika Muswada huu katika Ibara ya Pili kwamba, sheria hii itatumika Tanzania Bara, kwa sababu sheria hii tunayotaka kuitunga sasa katika Muswada ni kwamba, inatumika Tanzania Bara tu, naomba nipate ufafanuzi kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaonesha mambo ya Muungano, ukurasa wa 128.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni Katiba ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Hili jambo ni la pande zote, siyo la upande mmoja tu, lakini jambo la pili ni kile kipengele cha sita, suala zima la uraia, hakuna uraia wa Zanzibar wala wa Tanganyika, tunazungumza masuala ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba nipate justification ya kwa nini sheria hii, Muswada huu ubague Wazanzibari ubaki kwa Tanganyika tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza suala zima la kupata taarifa na huu Muswada umezungumzia hata raia, huyu raia ni wa namna gani. Maana yake ni hatujaangalia kwa mapana ni kwa nini tumewatenga Wazanzibari wasishiriki kama jambo hili ni jema na ndiyo maana kama tunaona Katiba inakiukwa lazima tuseme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema nia ya Muswada huu ni Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 18(d) kwa maana ya kwamba, Katiba hii ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunazungumza suala la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unazungumza raia, unazungumza Katiba na vifungu vyake, kwa nini unakiuka upande wa pili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi naona huu Muswada wa ni wa Kitaifa, huu Muswada usingepaswa kutenga Zanzibar, ulipaswa pia na wenyewe uwe applied kwa sababu raia wa Zanzibar ni Watanzania, anaweza akahitaji kupata taarifa au anaweza akahitaji kufuata zile taratibu ambazo ziko kwenye Muswada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, to be honest, huu Muswada umeletwa kwa makusudi maalum, huu Muswada haujaletwa kwa nia njema ya Ibara ya 18(d) kama alivyosema Mheshimiwa Waziri. Huu Muswada umeletwa kwa ajili ya kufunga watu midomo. Huu Muswada umeletwa kwa sababu ya kuzuia taarifa za Serikali ambazo ni ovu, ambazo mara nyingi zimekuwa zikivuja. Ndiyo maana kama lengo ni jema nisome hiyo Ibara ya 18(d) inasema, “Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Muswada huu umeleta visingizio, umeleta hatua na vikwazo vya Ibara hii ya 18(d). Kimsingi Muswada huu, kwa maoni yangu umekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu Katiba inasema kila mtu anayo haki ya kupewa! Muswada unasema uombe! Huyu raia analazimishwa kwa sheria hii, kama tutapitisha, siyo kupewa kama Katiba inavyotaka, ni kwamba, aombe. Hatua sasa zinaanza kuoneshwa uombe kwa maandishi, uombe sijui kitu gani, mara sijui siku 30, lakini Katiba inasema una haki ya kupewa taarifa wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema mmeleta huu Muswada, mmejisahau tu ni juzi, mlipitisha kwenye Bunge lililopita Sheria ya Whistle Blowers! Mnawafunga sasa midomo wakiwa na taarifa fulani wasizitoe kwa sababu mtawabana kwa sheria hii mtawaambia mliomba wapi? Taarifa za maandishi ziko wapi? Binafsi naona Serikali imekuja na Muswada huu kutimiza na unajua wameshindwa kujificha, tuwe wakweli, mmejianika kwenye Kifungu cha 6(2) kwenye Muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 6(2) kinasema kwamba, taarifa iliyozuiwa inaweza kuzuiliwa kama utolewaji wa taarifa hiyo unaweza kusababisha mambo yafuatayo, mambo mengi sana (a) mpaka (i)! Jambo la kwanza ambalo limenisikitisha (g) inasema, “Kuzuia au kusababisha madhara makubwa kwa Serikali katika kusimamia uchumi.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmejificha hapa, yaani mmejificha kweupe kabisa! kwenye Kifungu cha 6(2)! Halafu lingine mnaandika mnasema kuwezesha au kuhamasisha kufanya kosa! Kuingilia upelelezi unaofanywa na vyombo vya uchunguzi! Kudhoofisha kwa kiasi kikubwa uwezo wamiliki wa taarifa na bla-bla nyingi tu, mmejificha hapo! Mnazuia mambo yenu yasipekuliwe tena! Wale whistle blowers wasitoe tena kama kuna kitu, ufisadi unafanyika katika Serikali hii wasiseme tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao ni wema sana katika Taifa hili, aidha ni wafanyakazi wa Serikali au siyo wafanyakazi wa Serikali, wanapogundua kuna ufisadi mahali wamekuwa wakitoa ushirikiano katika Taifa hili, lakini Muswada huu unakwenda sasa kuwafunga midomo kwa sababu, mnataka msemaji awe tu ni Afisa Habari katika taasisi fulani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wakweli tu, Kifungu cha 16, kuahirisha utoaji wa taarifa, naomba tu ninukuu, “Mmiliki wa taarifa ambaye amepata ombi anaweza kuahirisha kutoa taarifa husika mpaka linapotokea tukio maalum ikiwemo kuchukua hatua za kisheria au kiutawala au mpaka kwisha kwa muda uliowekwa,” tumeweka hapa muda siku 30, lakini hapa kifungu cha 16(1) mnamlinda huyu mtu ku-delay hata zaidi ya siku 30 au asitoe kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, atasema aah! mmeomba taarifa ya wafanyakazi hewa, Waziri wa Utumishi ametoa miezi sita tufanyie kazi, wewe unaomba ndani ya siku 30! atakwambia bado kuna taratibu hazijafuatwa hapa, kuna mambo hayajakamilika hapa! Mmempa mandate ya kuzuia hata hizo taarifa katika Kifungu cha 16(1). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, nenda Kifungu cha 18(1), matumizi ya taarifa, inasema, “Bila ya kujali masharti ya Kifungu cha 6 mtu aliyepewa taarifa kutoka kwa mmiliki wa taarifa hatatakiwa kuipotosha taarifa hiyo.” Hata kile ambacho kimetolewa kama kimepotoshwa kutoka kwenye chanzo, anayekuja kuadhibiwa katika Muswada huu ni yule mtumiaji wa mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii yote mmewabana Watanzania hata wakipata kile walichopewa waendelee, mpaka kifungo mmeweka, lakini aliyepotosha aliyetoa taarifa, yaani chanzo hakijapangiwa adhabu, mnampangia adhabu yule mtumiaji wa mwisho! Ndiyo maana nasema mmejificha kwenye Kifungu cha 6(2), yale ya kwenu yote ambayo hamtaki yaguswe mfunge watu midomo yako pale, mengine ni haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda vifungu vya 20, 21, 22, 24 ndiyo usiseme. Hata wale Maafisa wanaotoa zile taarifa wamepewa mamlaka whether watoe au wasitoe na wakifanya au wasipofanya, Kifungu cha 24 kwa nia njema! Haijawa defined hiyo nia njema! Hawatachukuliwa hatua, wanalindwa! Kwa nini mnataka mtumie Bunge hili kupitisha kitu kibaya kiasi hiki ambacho kiko against Katiba yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu, kama Serikali iko honest, walikuwa wana nia njema kuleta Muswada huu, nilifikiri huu Muswada base yake inakubaliana kwamba, ni Ibara ya 18(d) ya Katiba, lakini nilifikiri huu Muswada usingezidi vifungu vitatu. Kifungu cha kwanza kingeeleza jambo hili, njia za mtu kupata habari, mtaeleza pale kwamba Serikali itawajibika, Baraza la Madiwani litawajibika, Taasisi yoyote ya Umma itawajibika kutoa taarifa kwa wananchi hawa kama Ibara inavyosema. (Makofi)
Jambo la pili ingekuwa ni taarifa zipi ambazo raia hao wanatakiwa wapate kwa wakati kama ilivyoeleza kwenye Ibara hiyo ya 18(d); hamjaeleza mmekimbilia kujilinda kwenye Kifungu cha 6(2), mngeeleza ni taarifa zipi hasa na ni zipi ambazo Mtanzania hatakiwi kupewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ingekuwa ni adhabu ambazo angepewa huyu ambaye ni Afisa Habari au ni Mtumishi wa Serikali anayekataa kutoa taarifa hiyo kwa wakati, hamjasema adhabu. Mmesema tu anaweza aka-appeal, akaenda sijui kwa Mkuu wa hiyo Taasisi, akaenda kwa Waziri ndiye msemaji wa mwisho. Tena mnathubutu kusema Waziri ndio msemaji wa mwisho! Kwa sababu Mkurugenzi labda na Waziri wanawasiliana Mkurugenzi atamwambia sijamaliza kufanyia kazi, Waziri atatoa majibu hayo hayo. Mnathubutu kusema na Waziri ndiyo msemaji wa mwisho, ndiye mwenye maamuzi ya mwisho, lakini hamjasema adhabu ya mtu ambaye atakiuka ibara ya 18(d) ya Katiba kwa kushindwa kutoa taarifa kwa wananchi kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tuwaite mna nia njema? Kwa nini tuwaone mna mambo mazuri sana kuhusu Muswada huu, kwa nini tusiwaone kwamba lengo lenu kubwa ni kufunga vyombo vya habari midomo, ni kufunga whistle blowers, ni kuwatisha wananchi ambao hawajafuata taratibu kwamba hizi taarifa kwanza umezipataje achukuliwe hatua na mtafanya, kwani mangapi mmepitisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho naweza kuwashauri Serikali hii, hakuna marefu yasiyokuwa na ncha, na hakuna jambo ambalo halina mwanzo na mwisho, mnatumia wingi wenu vibaya, lakini yameanza kuwarudi taratibu. Hii ni movie tu ambayo mnacheza ila siku zinahesabika, kwa sababu hamuwezi mkawa mnakiuka Katiba kiasi hiki Watanzania waendelee kuwaangalia. Hawa Watanzania siyo wajinga hata siku moja, hata kama mnaona hawawezi kufikiria, lakini ipo siku watapata ufunuo kwamba haya mnayoyafanya kwa ajili yao siyo mazuri hata kidogo.
Mheshimiwa Waziri hayo ni maoni yangu, huu Muswada haufai kabisa na vifungu vyote vimetungwa kwa ajili ya kuwabana wale watumiaji siyo Serikali kuwajibika kwa wananchi kutoa taarifa vile ambavyo Katiba yetu inataka. Nawaomba tu kwa sababu mna muda mkatafakari, kama mmeona kwamba mtuletee mambo haya ndiyo tuyapitishe hiyo damu haitadaiwa mikononi mwetu, mtapitisha kwa wingi wenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawahakikishieni ipo siku haya mambo mnayopitisha yatawarudi. Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweke mawazo yangu katika hoja ambayo iko mbele yetu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kutupa afya njema ili tuendelee kutekeleza wajibu wetu ambao Watanzania wametukabidhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Jambo la kwanza ambalo Serikali imeona na naomba ninukuu na hili jambo limenishtusha. Ukurasa wa 22 katika kitabu cha Hotuba ya Waziri, anasema kwamba; “Mapato yote yatakusanywa na Wizara ya Fedha, mapato ambayo yanatoka katika Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa watatakiwa kuwasilisha mapato yote yatakayokusanywa yawasilishwe kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na yatagawiwa kulingana na bajeti za mafungu zitakazoidhinishwa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni kubwa sana, picha ninayopata hapa Halmashauri zetu zitakufa. Amesema mapato yote na kimsingi ukiangalia tunakwenda kuua Serikali za Mitaa. Leo tutakusanya mapato ushuru wa stendi, wa wafanyabiashara, chochote ambacho Halmashauri zetu wanakusanya tuweke kwenye Mfuko wa Serikali. Tukumbuke historia ya ugatuaji madaraka katika Serikali zetu (decentralization).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1982 Baba wa Taifa alijuta tulivyofuta mfumo mzima wa Serikali za Mitaa; barabara hazikwenda, hospitali zilikuwa mbaya na mwaka 1980 wanakumbuka wale waliosoma historia, kwamba ilifikia hatua hata outbreak ya cholera ilishindikana kuzuiwa huko chini kwa sababu kila kitu kilifanywa na central government.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunarudi kule ambako Muasisi wa Taifa hili aliona kulikuwa na tatizo na alijutia na akasema hili jambo halitojirudia tena. Serikali hizi za Mitaa wamepewa mamlaka kwa mujibu wa Sheria zetu za mwaka 1982. Wana mamlaka ya kuajiri, mamlaka ya kukusanya mapato na kuyatumia kwa kiasi fulani, lakini wana mamlaka pia ya kutunga sheria mbalimbali ambazo zinasaidia katika kukusanya ushuru huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapotaka pesa zote katika nchi hii tukusanye at central level, halafu tutengeneze bajeti zetu huku chini, tupeleke Serikali Kuu wao ndiyo waanze kutupimia, athari yake ni nini? Athari yake tutaua morali ya wale wanaokusanya hizo kodi ndogo ndogo huko chini, kwa sababu maendeleo hayataonekana; kutakuwa na ubaguzi wa kupeleka fedha hizo katika Halmashauri hizo, japo watu wengine wanakusanya, lakini pia hapatakuwa na maendeleo huko chini kwa sababu fedha haziendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wakweli; ukiangalia bajeti ya Serikali kwa muda mrefu, fedha za own source katika Halmashauri zetu ndiyo zinasaidia miradi ya maendeleo mbalimbali, miradi midogo midogo. Hizo fedha ndiyo zinasaidia kuchonga barabara zetu, lakini angalia fedha zinazotoka Hazina haziendi kwenye Halmashauri zetu kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia kwenye bajeti ya mwaka jana, mwaka juzi, hata katika hivi vitabu, inaonyesha fedha za wafadhili ndiyo zinakuja kuliko fedha zinazotoka Hazina. Nitoe mfano, katika Halmashauri yangu ya Mji wa Babati, 11% tu ya fedha za Hazina ndiyo zimeingia na ni miaka yote fedha zinazotoka Serikali Kuu haziingii. Kwa kubariki kila kifanyike at central level, huku chini watu wakusanye tu halafu watu wachache wapange, tupeleke sehemu fulani, tusipeleke sehemu fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo nakuhakikishia tunaua Halmashauri zetu, hakuna maendeleo yatafanyika, mtafanya mambo yenu makubwa makubwa katika central level, lakini yale yanayohusu maslahi ya wananchi wa hali ya chini na maendeleo yao nakuhakikishia tunarudi kwenye historia ya mwaka 1980 ya jinsi ambavyo decentralization, Baba wa Taifa Mwalimu aliona kwamba ni jambo muhimu sana kwa sababu central level hawawezi kufanya wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imebariki kwamba hizo sheria ziangaliwe, maana yake Sheria inayotajwa ni mwaka 1982 ya Serikali za Mitaa, kwamba sasa tunachukua uhuru wa Serikali za Mitaa kukusanya kodi zao na kuzifanyia matumizi, Serikali Kuu ndiyo inafanya. Naomba Bunge hili tusithubutu kufanya hivyo, bali tusaidie Serikali za Mitaa kubainisha vyanzo ambavyo hawakusanyi, tuviimarishe na Sheria hizo ziimarishwe badala ya Serikali kuu kuchukua madaraka yote. Sasa tunakusanya kila kitu at central level, hatuwezi tukapitisha kitu kama hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa retention premium ya ardhi 30%, hizo fedha huwa hazirudi. Tunauza viwanja huko, tunapeleka makusanyo yote ardhi, Wizara ya Ardhi hawapelekewi hizo pesa na Wizara ya Ardhi wao wakipata chochote na wanajitahidi chochote wanachopata kutoka Hazina wao wanapeleka 30% katika hizo Halmashauri, lakini Serikali Kuu, Hazina hawapeleki hizo fedha hata hiyo tu premium ya ardhi hawapeleki. Iweje leo tuwapelekee eti fedha zozote tunazokusanya kwenye Halmashauri zetu, tupeleke kwenye Serikali Kuu. Tunaua Halmashauri zetu na maana yake tunaua suala zima la Serikali hizi mbili Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, wanataka sasa kila kitu wafanye wao. Hiki kitu Bunge hili tusifanye vinginevyo maendeleo yatakwama katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la service levy. Wamezungumza hapa ushuru wa huduma na vitu kama hivyo. Kwa muda mrefu tumeishauri Serikali, suala la mitandao ya simu ni chanzo kimojawapo katika Halmashauri zetu. Leo mitandao hii wamiliki wa makampuni haya ya simu ushuru wa huduma wanaolipa haueleweki kwa sababu Halmashauri imefikia hatua wanakusanya sijui ushuru wa nguzo, sijui service levy, hiyo asilimia zero point three Wizara ya TAMISEMI mwaka jana na Wizara ya Mawasiliano walikaa chini wakasema watashauriana na wakaandikiana barua kwamba wakusanye katika central level. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pata picha mpaka leo hawajawahi kukaa, hawajawahi kupeleka kwenye hizo Halmashauri kwamba ni kiasi gani wanastahili kupitia kwa makampuni haya ya simu, hata hilo kama tulishindwa, tunathubutuje leo, eti kwenda kuchukua hata vile vyanzo ambavyo kidogo tunajitahidi Halmashauri zetu zinakusanya, lakini sisi at central level kitu ambacho Wizara mbili walitakiwa wakae wa-reconcile wapi ambapo haya makampuni hayalipi, halafu zile asilimia zigawanywe zipelekwe kwenye Halmashauri zetu equally hawapeleki.
Leo tunaua Halmashauri zetu tunasema tunafanya sisi, wakati ya premium ya ardhi mmeshindwa, hii service levy mmeshindwa, halafu Serikali Kuu, hivi kweli hiki kiburi kinatoka wapi cha kusema kwamba, sasa ninyi mnakusanya, halafu mtugawie sisi tuwaletee tu bajeti. Hili ni jambo kubwa sana na ninaona kama hatujalipitia na hatujalielewa vizuri, lakini kama tukipitisha jambo hili ambalo linapendekezwa katika ukurasa wa 22, tumeua Serikali zetu za Mitaa totally.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize sana kuhusu hili tusilipitishe na tuliangalie kwa upya, lakini suala zima la kurasimisha biashara zetu ni kwa nini sijaona Mpango unaoonesha vijana wetu ambao wanafanya biashara ndogo ndogo waweze kuboreshewa maeneo yao. Kwa muda mrefu hata kwenye Hotuba ya Rais alizungumzia suala zima la kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa vijana wetu, Wamachinga. Hawa wakipangwa pesa zikatengwa, zikajengwa shopping malls ambazo zitasaidia vijana wetu tukawapanga, watalipa ushuru katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea leo, hawa wafanyabiashara wanaokuwa taratibu, hawajawahi kupangwa kokote, hawajawahi kutengewa maeneo, lakini kingekuwa ni chanzo kizuri ambacho tukakaa tukawaangalia jinsi gani Serikali za Mitaa wakapanga maeneo kwa ajili ya hawa vijana, wakafanya biashara wakalipa ushuru mbalimbali na tozo mbalimbali, itasaidia sana kuongeza mapato ya Serikali. Kwa hiyo, nishauri kwamba inawezekana Serikali inawaza mambo makubwa, bandari, sijui ndege, sijui vitu gani wakati kuna watu ambao wakipangwa tu wanaweza wakasaidia kuleta marejesho katika Mfuko wetu na katika Halmashauri zetu ili tuone ni jinsi gani ambavyo tunaweza tukafanya maendeleo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda vidogo vidogo ambavyo vinaweza vikaajiri hawa vijana, limezungumziwa lakini…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru ili na mimi niweze kuchangia machache katika Wizara hii ya Elimu, Wizara muhimu sana na awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya ambayo anayoendelea kunijaalia ili niweze kutoa mchango wangu katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wananchi wa Jimbo la Babati Mjini ambao wamenipa dhamana ya kuwa Mbunge wao wa Jimbo na niwaahidi sitowaangusha na baada ya Bunge tutaendelea kuwa pamoja ili tuendeleze Jimbo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niombe Waziri anisaidie kwa sababu hapa tunazungumza suala zima la bajeti. Naomba tu anisaidie katika bajeti yake kabla sijaenda mbele zaidi katika kitabu chake cha Development, kwenye Vote 1003, amezungumzia suala zima la rehabilitation of the schools and colleges. Ametenga shilingi 8,153,000,000 lakini ukienda kwenye randama hii, Mheshimiwa Waziri ulichokiandika huku kwamba unafanya marekebisho ya shule zetu sicho ulichoandika, unaomba na nafikiri umefanya hivyo kwa sababu mkijua wengi Wabunge hatusomi randama, umeandika fedha hizo shilingi bilioni nane unajenga ujenzi wa ofisi ndogo ya Wizara Dodoma pamoja na ukarabati wa Makao Makuu ya Wizara shilingi 6,153,000,000 lakini ukaandika kwamba ni ukarabati na upanuzi wa Taasisi ya elimu ya Watu wazima shilingi bilioni mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo shilingi 8,153,000,000 huku ulivyotuandikia kwamba unafanya rehabilitation ya schools, sicho kabisa ni uongo na niombe majibu ya kina kwa sababu shilingi bilioni nane ukigawa kwa idadi ya madarasa ni zaidi ya madarasa 1,000 yanatakiwa yajengwe kwa fedha hizo na nasema hivyo kwa sababu mmekuja na sera ya elimu bure, watoto wanakaa chini Mheshimiwa Waziri kipaumbele chako ni kujenga ofisi yako kwa shilingi bilioni sita na shilingi bilioni mbili ilihali ukijua watoto wa Kitanzania wanakaa chini, chini ya Wizara yako.
Kwa hiyo, nahitaji uniambie ni kwa nini Waziri mwenzetu, mwanamke mwenzetu, mwenye uchungu kwa watoto wa Kitanzania unatenga fedha zaidi ya shilingi bilioni nane kwa ajili ya ujenzi wa ofisi yako ilihali watoto wanakaa chini na Wizara hiyo unaongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa la Kitanzania literacy level yetu ni asilimia 67. Watanzania wengi zaidi ya asilimia 30 bado kusoma na kuandika ni tatizo. Lakini kwa hali ya kawaida Taifa hili ambalo linapigana vita, maaskari hawa ambao wako vitani wamesahauliwa kwa asilimia zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu kama Mbunge wa Jimbo nilikaa na walimu wangu kuwafikia kwenye shule zote zaidi ya 30 katika Jimbo la Babati Mjini. Wala haya ninayoyachangia siyabahatishi na maaskari na walimu hawa ambao wanapambana na ujinga katika Taifa la Tanzania na naamini haya nitakayosema ambayo nimeambiwa na walimu wangu wa Babati ndiyo wanayopata walimu katika nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la madaraja walimu wetu. Mmetoa miongozo kwa miaka mitatu mnapandisha madaraja lakini walimu wanaofundisha huko katika shule zetu wanakaa miaka minne hawajapandishwa madaraja, lakini Mheshimiwa Waziri mnawapandisha madaraja kwa ceiling ya bajeti. Mimi naomba niishauri Serikali, kwanini mnawagawa walimu na maaskari hawa ambao wanapigana katika Taifa la Tanzania kuondoa ujinga? Kama hakuna fedha msiwagawe walimu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna walimu wanaajiriwa pamoja, kwenye madaraja wanatofautiana, kwenye mishahara wametofautiana, kwa nini? Mnapeleka wachache eti ukomo wa bajeti wengine wasubiri, nani kakwambia hivyo Mheshimiwa Waziri? Huu ni ubaguzi, walimu hawa kama hakuna fedha subirini mkipata muwapandishe hata kwa miaka mitano wote au miaka minne badala ya kuwagawa, hilo naomba majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wanaohamishwa kutoka Mkoa mmoja kwenda mwingine, Halmashauri nyingine kwenda nyingine akifika anaanza upya, daraja halipandi, anaambiwa huko ulikotoka ndiko ambako mambo yako yamekosewa, hebu Waziri tuambie leo hivi kuhamishwa ni dhambi kwenda kusaidia sehemu nyingine? Kwa nini walimu hawa wakihamishwa kwenda Halmashauri nyingine madaraja yao wanaanza upya, hawaendelei na madaraja waliyonayo? Unaongoza hiyo Wizara tupe majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti lakini lingine, hivi Serikali haina mpango kazi kwa walimu? Transport allowance? Leo anaibuka Makonda anasema walimu wapande mabasi bure. Msiwalipe transport allowance kwa nini? Yaani Serikali mmeacha walimu yeyote aamue kwamba hawa leo wapande bodaboda, hawa wapande mabasi bure, hawa wakejeliwe hivi kwa nini? Muwalipe walimu wetu transpot allowance. Sitting allowance hamuwalipi, yaani mwalimu hana shift yoyote, kwanza wanalalamika muda wanaingia saa moja wanatoka saa kumi, hawana wa kuwapokea wakati madaktari, manesi na fani zingine wana-shift lakini pia wanalipwa on call allowance, mwalimu halipwi housing allowance, sitting allowance wala transport allowance, umempeleka kijijini kule hakuna nyumba. Hivi kweli Mheshimiwa Waziri umekaa kwenye Wizara hiyo kwa muda mrefu, haya matatizo unayafahamu, leo nahitaji majibu kwa ajili ya walimu wa Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Waraka wa Elimu Bure, sawa, mmeiga kutoka kwetu UKAWA elimu bure mkakurupuka mkaanzisha. Haya mtuambie na mimi niliuliza swali kwa Waziri Mkuu, ni kwa nini mmekurupuka katika hili la elimu bure? Mnachokifanya sasa hivi shule zetu hakuna pesa. Shule ya wanafunzi 800 mnapeleka OC ya shilingi 200,000. Madeni katika shule zetu, Mheshimiwa Waziri tangu mwaka jana shule zinadaiwa pesa za ulinzi, za maji, za umeme kila shule yangu niliyopita inadaiwa zaidi ya milioni tano. OC ya shilingi 200,000 inaendeshaje shule? Mnaua elimu ya Tanzania. Mmetuachia huko kwa TAMISEMI mnasema kwamba huko tutafute pesa, hakuna. Mnabadilishia gear angani. Mlituambia kwenye waraka kwamba madawati wazazi hawatachanga leo wazazi wa Babati wanachangishwa Madawati, mnageuzia gear angani. Mtuambie kwanini mnatudanganya? Na hizi fedha mnapeleka lini tunahitaji mtuambie msitudanganye Watoto wetu wanakaa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa walimu wa sayansi. Mheshimiwa Waziri, zaidi ya walimu 30,000 wanahitajika wa sayansi katika nchi hii. Nimepita kwenye shule za sekondari, ninauliza hata mwalimu aliyesoma BAM (Basic Applied Mathematics) A-level aniambie kama yupo afundishe mathematics, hakuna mwalimu wa hesabu kwenye shule za sekondari halafu Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako unasema ujenzi wa maabara katika shule zetu za sekondari utakamilika mwaka 2018/2019 ndiyo vifaa vya maabara utapeleka huko. Tunapataje walimu wa sayansi ilihali hata maabara huko hakuna vifaa na hampeleki? Mnajenga ofisi zenu kwa shilingi bilioni nane, mnataka walimu wa sayansi wa mathematics, wa chemistry hawapo kwenye shule zetu, mnategemea mtabadilisha Taifa hili kweli elimu ya nchi hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha shule hatuna walimu wa sayansi. Mheshimiwa Waziri nikushauri tu, walimu wa arts tunao wakutosha. Boresheni VETA, pelekeni vijana wetu huko VETA muwadahili walimu wa sayansi, mtupelekee walimu wa sayansi kwenye shule zetu. Msitegemee watapatikana huku juu, huku chini hata hayo maabara mmeshindwa kujenga. Waziri nakupa tu ushauri wewe ni Mwananmke mwenzangu naomba tu nikupe ushauri labda utanielewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine niurejeshaji wa mikopo. Mheshimiwa Waziri Bunge lililopita tulikuwa tunalipa, mimi ni-declare interest, mimi nimelipa nimemaliza. Lakini Bunge lililopita tuliandaliwa mpango hapa, Wabunge wote tumelipa, tumekuwepo Bunge lililopita. Hivi nchi hii kodi mpaka ikusanywe mpaka Magufuli aende na polisi na mbwa kama alivyoenda bandarini ndiyo mkusanye? Ndiyo mtakusanya?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti mbona sijaona mkakati wa ninyi kukusanya fedha hizi, mtuambie wazi wazi, halafu mnasema mtu akichelewa kulipa eti mnampiga interest ya 10% kwa sababu amechelewa, ajira ziko wapi? Wamekaa mtaani hawana ajira baadae unampiga eti penalty ya 10%, kweli Mheshimiwa Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani muache kuimba Serikali ya Magufuli, hii nchi ni ya kwetu sote! Isiwe ni one man show kwamba Magufuli asipofikiria ninyi Mawaziri mnasubiri leo anaamkaje anasemaje, njoo na mpango kazi wako wa kukusanya hizo fedha, hata hapa basi ungetuita Wabunge wote hapa tujue nani anadaiwa, tulipe hizo pesa. Lakini pia utuambie na hao wengine ambao wameajiriwa kwenye sekta ambazo sio rasmi wanalipaje, sio tunamsubiri Rais akisema basi wote ndiyo tunaenda huko, hapana! Hatuwezi mkaendesha nchi kwa show ya kiasi hicho! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la shule za awali. Mheshimiwa Waziri najua utasema iko TAMISEMI, jamani mmechukua sera ya elimu bure, basi tembeleeni! Mtoke na Simbachawene muende hizo shule. Walimu kwanza hawana mitaala na watoto wetu wanakaa chini ya miti, hakuna darasa, mmewaambia Wakurugenzi watafute hizo fedha wajenge, hawana! Collection za Halmashauri ndiyo hizo mnasema mnaenda kukusanya wenyewe, mpaka zitoke lini? Watoto wananyeshewa na mvua!
Naomba leo mniambie Mheshimiwa Waziri, Wizara ya Elimu iko chini yako, sera na mambo mengine naomba leo utuambie kwenye hili Bunge, una mkakati gani kwa ajili ya watoto wetu wazuri? Wale wa miaka mitano ambao wanakaa chini, mkituachia Halmashauri tujenge hayo madarasa tutajenga kwa muda gani kama Serikali ya CCM mmejenga VETA kwa miaka 10 hata VETA moja kwa Wilaya haijakamilika! Mnategemea hao watoto…
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Mnategemea watajenga shule hizi za msingi….
MWENYEKITI: Mheshimiwa ni kengele ya pili hiyo!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ili na mimi nitoe machache ya kwangu katika Wizara hii ya Maji, Wizara muhimu sana katika maisha yetu ya kibinadamu na ni Wizara ambayo kwa kweli ina mgusa kila mmoja. Jana na juzi tulizungumzia Wizara ya Elimu jinsi gani inagusa maisha ya kila mmoja lakini maji kwanza, usipokuwa na maji hauwezi ukaenda darasani wala hauwezi ukaenda kazini wala hauwezi ukafanya chochote. Kwa hiyo, nitoe mchango wangu katika Wizara hii muhimu sana ambayo inagusa maisha ya kila Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nisemee yale ambayo wananchi wa Jimbo la Babati Mjini wamenituma kuyasema. Hadi sasa hali ya maji katika nchi yetu siyo nzuri na Mheshimiwa Waziri unazungumza kuhusu kufikia asilimia 80 katika miaka hii mitano maji katika vijiji vyetu katika nchi nzima. Lakini Mheshimiwa Waziri kinachokukwamisha ni bajeti ya Serikali na mimi niombe tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu hakuna sababu ya kukaa na kujadili bajeti ya Serikali wakati hazipelekwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtu anafanya vizuri ana nia njema lazima umpongeze. Mheshimiwa Waziri, tangu umeingia kwenye Wizara hii walau tumeanza kuona fedha zimeanza kufika katika maeneo yetu, bajeti iliyopitishwa ya Serikali ya mwaka huu inayotekelezwa kwenye shilingi bilioni 400 za maendeleo, zimeletwa tu bilioni 130 na kitu asilimia 28, hivi hata kama ungekuwa na nia njema ungefanyaje hiyo kazi? Ndiyo maana mchango wangu siku ya leo niwaombe Wabunge wote tujadili hii bajeti lakini tukijua adui mkubwa wa Wizara hii ni Wizara ya Fedha. Wizara ya Fedha hawapeleki pesa katika Wizara hii tunatenga bajeti pesa haziendi, na ndio maana miradi yetu haiendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru pia katika vijiji vyangu vya Nakwa, Malangi, mliniletea pesa yale maji yameanza kutoka Mheshimiwa Waziri, lakini kama ungeletewa pesa zote shilingi bilioni 400 maana yake miradi ingekamilika yote. Kwa hiyo, niiombe Serikali tusiiachie Wizara ya Maji tukawanyima fedha tukajua watu wetu kule wako salama. Kama mpaka sasa nusu ya Watanzania vijijini hawana maji mnategemea tunasongaje mbele na Serikali ya CCM mkae chini mfikirie hili. Watanzania hawana maji, na mkimyima Waziri huyu, siyo kwamba mnaikomoa Wizara hiyo, mnatukomoa sisi na wananchi wetu huko chini, kwa hiyo niiombe Serikali Wizara ya Maji tuipe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miradi viporo, tulikuwa na vijiji kumi kwa kila Halmashauri na Wilaya, kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Babati, zaidi ya vijiji vitatu sasa tumesubiri kwa muda mrefu sana. Mheshimiwa Waziri nimeona kwenye bajeti hii zaidi ya shilingi milioni 900 mnakwenda kunipatia kwenye kijiji cha Imbilili, kijiji cha Hala na Haraa. Ninaomba bajeti hii ya zaidi ya shilingi bilioni 900 unaoiomba kwenye Bunge hili, basi hivyo vijiji uvipatie kipaumbele kwa sababu tumekaa zaidi ya miaka minne watu hawana maji. Kata nzima kijiji kimoja tu sasa ndiyo naanza kuona kwamba kuna mwelekeo katika hizo shilingi milioni 900 lakini Kata nzima kina mama wanachota maji makorongoni, wanahangaika.(Makofi)
Mheshimiwa Waziri, shilingi bilioni 900 unaomba ni jambo jema, asilimia 75 ya fedha za ndani umetenga kwa mara ya kwanza kwa ajili ya miradi ya maendeleo, haijawahi kutokea, hizo asilimia 75 zikitoka za shilingi bilioni 900, shilingi bilioni 600 fedha za ndani basi zije moja kwa moja kwenye hivyo vijiji, haiwezekani miaka 55 wananchi wanachota maji kwenye makorongo. Kata nzima hawana maji, hawajui hata bomba la maji linafananaje, ndiyo sasa kijiji kimoja walau unaanza kuona mwanga kwa miaka 55 haiwezekani. (Makofi)
Kwa hiyo, ninaiomba Serikali kwa ujumla wake, angalieni suala la maji, suala la maji halisubiri, watu wanateseka. Walimu tuliokuwa tunawasemea juzi kwenye Kata hii Sigino anakuambia Mheshimiwa Mbunge ninakwendaje kufundisha wakati tu hata vyoo mlivyotujengea vya maji hakuna maji tunatoka na maji kwenye madumu. Naongea kwa masikitiko makubwa kwa sababu wananchi hawa wameteseka kwa muda mrefu, ninaomba Mheshimiwa Waziri hivi vijiji vyetu, ambavyo vimesubiri kwa muda mrefu uvipe vipaumbele hizo pesa zije mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la madeni ya taasisi. Wizara hii inadai zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa taasisi mbalimbali za Serikali. Mfano, katika Jimbo langu la Babati Mjini, Magereza tu tunawadai shilingi milioni 100, Polisi tunawadai zaidi ya shilingi milioni 30, Halmashauri yangu inadaiwa zaidi ya shilingi milioni 12 katika hospitali, kwa nini taasisi hizi wanashindwa kulipa, sababu ni hizi zifuatazo:-
Kwanza Serikali hampeleki pesa za OC. Kwenye Magereza hampeleki, Polisi hampeleki, hospitali zetu tunaendesha kwa shida hata madaktari na manesi wanashindwa kulipwa, fedha za OC na on call allowances, watalipaje maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu, naona leo dada yangu Susan Lyimo ndiyo amekaimishwa hongera dada, niombe Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu hebu taasisi na Wizara hizi waweze kulipa fedha hizi, mkiwapa Magereza na Polisi maana yake hizi shilingi bilioni 30 Mheshimiwa Waziri una uwezo kwamba hizi pesa sasa zinafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wezangu wa BAWASA Babati wameshindwa kufanya kazi kwa sababu wana nia njema, waliniambia Mheshimwa Mbunge tunapeleka Maji Gadueti, Managa, kila mahali kwenye vijiji vyako, lakini tunadai zaidi ya shilingi milioni 100 Magereza, Polisi tunawadai Halmashauri mmekata mpaka OC tunashindwa kuendesha, Serikali itupatie hizi pesa tukalipe.
Mheshimiwa Waziri, unasema solution ni prepaid meters, hivi unaweka prepaid meters hizi kwa pesa zipi yaani walipe kabla pesa ziko wapi OC haziko, hili ni la Serikali. Serikali tuleteeni pesa, lipeni hili deni la shilingi bilioni 30 ili tupate maji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la madeni ya wakandarasi, Mheshimiwa Waziri katika shilingi bilioni 200, shilingi bilioni 100 umeshalipa, ninakuomba hizi shilingi bilioni 105 zilizobaki ulipe ili nikamilishe mradi wangu wa Nakwa, mradi wa Malangi, mradi wa Kiongozi wa maji, kwa sababu kwenye hizi shilingi bilioni 100 naamini pia Wakandarasi wangu ambao wanaendesha mradi wa Nakwa wanadai zaidi ya shilingi milioni 252. Kijiji cha Malangi zaidi ya milioni 280 hizi pesa zikija shilingi bilioni 100 ambazo Wakandarasi wanadai na Serikali mkapeleka Wizara ya Maji, maana yake wananchi hawa wanapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Serikali bado, wala sina ugomvi na Waziri wa Maji, kwa sababu unagombanaje na mtu ambaye Serikali kwenye shilingi bilioni 400 inampelekea shilingi bilioni 100, nitakuwa mwenda wazumu! Mimi nahitaji Serikali pelekeni pesa Wizara ya Maji ili tuone kama Waziri anatosha au hatoshi. Lakini kwa kile alichokipata naamini kila mmoja hapa alikuwa anauliza walau kuna fedha zinafika kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe haya madeni Waziri wa Fedha naamini Mungu akitujalia tutachangia kwenye Wizara yako, kitu cha kwanza, tuone shilingi bilioni hizi 105 za maji za wakandarasi unalipa lini ili watu wetu waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvunaji wa maji, Mheshimiwa Waziri umesema taasisi za Serikali watengeneze matenki ya kuvuna maji. Hivi Halmashauri hazina pesa, OC haipelekwi unategemea hata kwenye fedha zile za miradi ya maendeleo watajenga matenki kwa fedha zipi? Serikali msirushe tu mpira Wizara ya Maji, hampeleki hata fedha za maendeleo, kama hampeleki mnategemea matenki hayo ya kuvuna maji kwenye maeneo ambayo visima haviwezi kujengwa, vinajengwa kwa namna gani? Kwenye package yenu hamuweki ujenzi wa hayo matenki ya kuvunia maji! Hili ni la Serikali, niishauri Serikali tatizo la maji ni kubwa sana, basi pelekeni fedha Wizara ya Maji ya matenki hayo maeneo ambako hakuna visima na maji ya mtiririko ili tuhakikishe kwamba maji hayo yanapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine muhimu sana ni suala la upangaji wa bei za maji. Mheshimiwa Waziri, utaratibu unajulikana kwamba wananchi wanahusishwa, lakini maji yamekuwa yakipanda katika taasisi za maji wananchi hawahusihwi, hata wakitoa maoni yao bado unit ya maji ni pesa nyingi sana. Hivi hawa Watanzania wanawezaje kulipa hizi bili?
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi nina mambo machache, naomba dakika zangu tano nimgawie Mheshimiwa Selasini, Mbunge wa Rombo, tembo wanamsumbua Jimboni kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni suala la chakula. Wakati Waziri wa Kilimo akieleza hali ya chakula nchini alisema kuna Wilaya zaidi ya 56 kama sikosei zina upungufu mkubwa, lakini Wilaya hizo hatujapewa list, ninaitake Serikali watupe majina ya Wilaya hizo tuzifahamu na ni lini sasa chakula kitaenda, kwa sababu wananchi wetu wana hali mbaya sana.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea wananchi wangu wa Jimbo la Babati Mjini debe moja la mahindi wananunua kwa shilingi 20,000. Naomba nifahamu mnapeleka lini hicho chakula kwa wananchi wetu kwa sababu hali ni mbaya na mliwambia kwamba wauze ng’ombe hata watatu wanunue debe moja, hao ng’ombe watatu hata bei haifiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeenda Karatu tumeona ng’ombe wamedondoka barabarani wamekufa, sasa hata ng’ombe kumi hawatoshi kupata shilingi 20,000. Mtuambie mnapeleka chakula lini hasa kwa wananchi wangu wa Babati wana hali ngumu kweli na mvua hazijanyesha. Wakati mwingine viongozi wa juu tuangalie kauli zetu, huenda hata Mungu anatuadhibu kwa ajili ya kauli zetu, mlisema hamtoi chakula, mvua ikaacha kunyesha, saa hizi hali mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Kamati iliyoundwa. Hii Kamati ya Migogoro ya Ardhi ya Wakulima na Wafugaji ni Kamati ambayo inahusisha Wizara zaidi ya tano, mpaka leo hamtuambii hiyo Kamati imefika Wilaya ipi? Hamtuhusishi Wabunge na Madiwani huko chini tufahamu hiyo Kamati, tuliuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, lakini huko kila tukizungumzia migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji mnatuambia Kamati iko site, mtuambie iko wapi? Imeanzia wapi? Imefikia wapi? Hiyo schedule mtupatie Wabunge ili tufuatilie, mkitujibu tu humu ndani mkatuambia Kamati iko site, watu wanauana haina maana yoyote Waheshimiwa Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtuambie iko wapi, mje na Babati huku, anzieni huko pia. Morogoro kule watu wanauana, Wabunge tushirikishwe hiyo Kamati tuipe ushirikiano mgogoro huo wa wananchi wetu kuuana uishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la kodi ya ardhi. Katika bajeti iliyopita Waheshimiwa Wabunge kodi ya ardhi tukasema TRA ikusanye, sasa hivi Halmashauri zetu hawakusanyi tena lakini TRA hawana manpower,haya maduhuli ya Serikali hayakusanywi tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri tu Wizara ya Ardhi, mlikuwa mnatuletea asilimia 30 retention ya premium, sasa hivi hizo pesa zingetusaidia hata kununua vifaa, Halmashauri zetu hatuna vifaa vya upimaji ndiyo maana ardhi kubwa ya Tanzania haijapimwa. Leo badala ya kuwezesha Halmashauri zetu wabaki na hizo retention za 30 percent mlipitisha kwenye bajeti mwaka jana, wakati mmetufukuza mkapitisha, mkasema TRA wakusanye. TRA hawakusanyi, hawana manpower. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali kwamba rudisheni sasa kazi hiyo kwa Halmashauri zetu ili kazi ya upimaji ardhi katika Halmashauri zetu iende sambamba na suala zima la upatikanaji wa fedha. Kwa sababu ile 30 per cent ilikuwa inatusaidia. Kama TRA hawakusanyi mwaka mzima kwa nini msifanye maamuzi? Kazi kwenu, wakati wa bajeti kaeni chini mfikirie siyo kodi tu ya ardhi, lakini pia hata kodi ya majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni suala la fedha za maji, fedha za maji kuna mlango wa Wizara ya Maji, mna bajeti yenu huko haiko wazi sana, lakini kuna TAMISEMI na kuna Halmashauri zetu. Kwenye Halmashauri mnatupa ceiling ndogo sana Mheshimiwa Waziri. Kaeni chini muweze ku-reconcile pamoja vyanzo vyote vya fedha za maji ili Wabunge tujue kwamba miradi mikubwa tupitishie milango ipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja Babati katika Jimbo langu, pale Kata ya Sigino, uliona Kata nzima hawana maji kabisa vijiji vyote vine. Tukiwafuata mnasema kuna fedha upande wa Wizara ya Maji, kuna TAMISEMI, wakati huo huo ceiling hazitoki mapema saa hizi Mabaraza wameshaanza kukaa kwenye bajeti, ceiling hazijulikani. Toeni ceiling mapema, lakini onesheni mapema kwamba Wizara ya Maji tunaweza tuka-access fedha hizo kwa kiasi gani? Kama tutaendelea kutokuweka mambo haya wazi, tutaendelea kuimba wimbo wa kwamba hakuna maji katika Taifa letu kwa miaka zaidi ya 50 na akina mama wanaendelea kuchota katika makorongo na ndoo hazijashuka katika vichwa vyao.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweke mawazo yangu katika muswada huu wa Sheria Huduma za Habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Kamati husika ilivyokuwa inachambua muswada huu, tulikuwa tunasoma mambo mengi na mapungufu yake, lakini mimi binafsi nilikuwa siamini kama kweli yako kwenye muswada. Nilipopitia muswada huu niliogopa sana kama Bunge hili tunakwenda kupitisha pamoja na marekebisho ya Serikali yale machache, kama Wabunge hatutasimama na tukawa wakweli kwa Taifa letu tukapitisha muswada huu tunakwenda kuzika tasnia ya habari katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu kwa hali ya kawaida, ukiufungua vifungu vyote vina mapungufu. Hakuna kifungu hata kimoja kina nafuu na nitaenda kwenye muswada, sitapiga porojo, kwa hiyo, mtulie siyo mnapiga kelele. Muswada huu kwa hali ya kawaida unakwenda kinyume kabisa na Ibara ya 18(d) ya Katiba; haki ya kila mtu kupewa taarifa kwa wakati. Huu muswada kama nia yake ni njema, kama nia yake tunataka tuwasaidie hawa wenzetu wanaotupa habari na waandishi wa habari na vyombo vyake, huu muswada leo ungekuwa unazunguzia maslahi ya waandishi wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu muswada umezungumzia tu suala la bima kwa waandishi wa habari, bima tu! Yaani, kama tunazungumza kwamba tumeleta kwa ajili ya kusaidia watu hawa na kuwalinda wapate haki zao, wawe huru walindwe katika Taifa hili ni uongo mtupu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii movie imeanza siku nyingi sana, Watanzania tulikua tukiangalia inaendelea na mnakaribia kuhitimisha hii movie, leo kwa kuleta muswada huu. Ninasema hivi kwa sababu gani, Serikali hii mlianza na movie ya kufungia Bunge hili tukawa gizani Watanzania wasituone mkafanikiwa. Hii yote mliwanyima Watanzania wasijue ni nini kinaendelea katika Bunge lao. Bunge ni mkutano wa Watanzania, tunakuja wawakilishi wachache tunajadili bajeti, tunatunga sheria Watanzana waone, mkaanza kizima Bunge hili tuko gizani mkafanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya hapo mkawanyima Watanzania haki ya kupata taarifa mbalimbali kupitia vyama vya siasa kwa kuwazuia wasiende kwenye mikutano. Leo katika Taifa hili katika Awamu hii ya Serikali ya Tano, vyama vya siasa hawana nafasi tena ya kuwapalekea Watanzania habari mbalimbali, mmewafungia wananchi, mmewanyima fursa hiyo. Lakini hamkuishia hapo mkaenda kwenye televisheni, redio mbalimbali magazeti mkayafungia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kupitia muswada huu mnakwenda kukamilisha azma yenu ndugu zangu Wabunge wa chama hiki tawala kama tutapitisha muswada huu; kufungia mitandao ya kijamii mbayo ndiyo ilikuwa pekee imebaki kuwapelekea Watanzania taarifa. Haya ninayosema yapo kwenye kifungu cha 3.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachilia mbali redio, televisheoni magazeti, mkazungumza suala zima la mitandao ya kijamii. Lakini wakati mnajadili kwenye Kamati, Mheshimiwa Waziri ulikua unabisha hata hili kwamba huku hatuendi, lakini leo iko kwenye kifungu cha 3 na inaeleza wazi kwenye hicho kifungu cha 3 katika kueleza maana mbalimbali kwamba mitandao hii ya kijamii ni mawasiliano yalianzishwa na watu hao kwa ajili ya kubadilishana habari. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, maana yake ni nini? Sisi Wabunge tuna group letu la whatsapp tunapashana habari mbalimbali, kuna facebook na ma-group mengine. Leo hata admin wa group la Wabunge inabidi apate leseni. Ndicho mnachopitisha kwenye kifungu cha 3. Chochote mtakacho…
Kifungu cha 3 hujasoma, tulia na wewe utachangia kwa wakati wako. Tulia na wewe utachangia kwa wakati wako, soma kifungu cha 3. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo huyo anaeongea ni admin wa group hilo. Kwa hiyo, tulia ukiwa hujui, sasa ndiyo nakwambia. Unajua hata hayo ma-group leo lazima wawe na leseni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lengo la muswada huu ilikuwa ni kuweza ku-impose fine mbalimbali ambazo mtataka kutoza kwa hao watu ambao angalau wanatoa taarifa mbalimbali kwa ajili ya Taifa la Tanzania. Kulikuwa hakuna hizo fine, leo mmeweka hizo fine za shilingi milioni tatu, shilingi milioni kumi, shilingi milioni 15 na shilingi milioni 25. Mnafungia Taifa la Tanzania kwenye giza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwneyekiti, huu muswada ni wa kuogopwa, wala siyo wa kupitishwa hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapitishe kwenye vifungu mbalimbali. Kifungu cha 7(1), yaani kwa hali ya ajabu kabisa ni kwamba watu wote wanatakiwa wapewe taarifa, lakini huu muswada haujazungumzia zile televisheni ambazo siku zote zimekuwa zikichuja taarifa mbalimbali. Televisheni ya Taifa (TBC) ambayo tunalipia kodi inaamua kutokurusha taarifa fulani, inarusha taarifa fulani, hawajaweka adhabu hata kidogo. Kama lengo lenu ni jema, kwa nini hamuelezi kwamba TBC kwenye kifungu hiki siku zote imekuwa ikionesha ubaguzi wa wazi kwa taarifa fulani fulani, mnasema kwenye kipengele cha 7(1) kwamba vyombo vya habari vina haki ya kutoa taarifa kwa wote bila kubagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nia yenu ni njema mbona msiseme TBC adhabu yake ni nini kutokutoa taarifa ambayo inachuja na kubagua vyombo vingine na taasisi nyingine? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 7(b)(iv), Muswada huu unazungumzia suala la Serikali kuchuja taarifa na iandikwe taarifa ambayo Serikali itakayoelekeza. Yaani televisheni za binafsi Serikali itaelekeza kwamba ni taarifa ipi waandike. Ninyi binadamu hii nchi ni ya kwetu sote, siyo yenu peke yenu. Mnataka muwafunge midomo televisheni na magazeti binafsi na vyombo binafsi mpaka Serikali ielekeze. Huu muswada ni mzuri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza kabisa, Ibara ya 7(2) mme-copy kifungu kinachotoka kwenye Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ya Namba 6 ya 2016. Mme-copy each and everything kutoka kwenye sheria ile tuliyopitisha juzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hiki kifungu cha 7 wakati tunapitisha sheria hii tulileta amendment vitu vyote vile; Taarifa ya Baraza la Mawaziri, hali ya uchumi, sijui Serikali imeyumba, isikosolewe, yaani kile kifungu kipindi kile tulipowaletea amendment, sasa hivi mmekileta kizima kizima. Mme-copy na ku-paste kama kilivyo, maana yake nia yenu ilikwama kipindi kile wakati tunapitisha ile sheria, leo mmeleta tena huku mnatuchosha tulete tena marekebisho wakati vile vitu tulishaviweka sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la muswada huu ndugu zangu ni kuingiza nchi yetu katika giza, Watanzania wasithubutu kuandika chochote, wasikosoe chochote; chochote unachoandika uwe na leseni na mlishaanza by the way. Vijana wetu wakikosoa tu kidogo, mmeshawakamata mnawapeleka Polisi wakatoe maelezo; wengine wako ndani. Umekosoa tu kwamba hapa hakijaenda vizuri, yaani mnatengeneza Serikali ya nchi hii Rais asikosolewe, Mawaziri msikosolewe, yeyote asikosolewe, ndiyo mnachotaka! Ndiyo maana mmepanga hizi fine humu ndani ambazo mnajua Watanzania hawawezi kuzilipa. Huu muswada ni wa ajabu sana! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Bodi; hii Bodi kwanza Waziri anateua. Mheshimiwa Waziri asubuhi umerekebisha umeingiza wale watu wawili; watu binafsi na taasisi nyingine ambazo ni za umma. Umeingiza tu hao wachache lakini the whole component ya watu saba wote ni wateule wa Waziri. Halafu huko sasa ndiyo unataka eti hii Bodi itoe vitambulisho. Wakitoa vitambulisho hivyo, mtu umenyimwa, hujui mahali pa kwenda kukata rufaa. Hata kama umenyimwa, hakuna popote unaweza kukata rufaa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 14 inasema hivi, itaajiri kwa idhini ya Waziri Mkurugenzi Mkuu. Waziri anaweza akaamua kufanya hata delay; si hajaamua. Mpaka atakapoamua! Hivi bado mnabisha kwamba Waziri sasa ndio ameweka miguu yake yote humo, chochote kinachofanyika, mpaka yeye awepo. Uhuru uko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa hali ya kawaida, hata kama mtapitisha, kama mlivyopitisha bajeti ya juzi, hatutakaa muda mrefu tu mtakuja kulia kama tunavyolia sasa hivi. Mnalia sasa hivi hakuna fedha huko; si mlipitisha kipindi kile? Kelele zote na kila kitu mkapitisha; lakini leo Halmashauri zenu hazina fedha miezi mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 18(1) kuthibitishwa kwa wanahabari. Hakuna vigezo vyovyote ambavyo vimewekwa hapa katika ibara hii. Kama ninyi mnataka fair play, kwa nini msiweke vigezo? Ili mimi nikijua kwamba kigezo ni hiki; maana kanuni hizo mnazozitunga, sio wote ambao wanaweza wakazi-access. Hapa tunatunga sheria, wekeni basi vigezo hapa tujue kwamba mtu anapoonewa kwa kigezo hiki, anajua kwamba hiki kigezo ndiyo kimenitoa mimi kwenye ligi. Hakuna vigezo, hamviweki. Mnataka Bodi yenu mliyoiteua ndiyo iweke vigezo. Hamwatendei haki Wanahabari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 20(2) ni mbaya zaidi, tena inaenda kinyume na Ibara ya 22 ya Katiba, kwamba mtu yeyote ambaye atakuwa amesimamishwa kufanya kazi hii, hataruhusiwa kufanya kazi hii tena. Yaani unamzuia kabisa asifanye hiyo kazi ya habari. Hicho kifungu cha 20(2) mnawanyima hata Watanzania ajira. Mmeshindwa kutoa ajira huko mtaani huku tena mnaendelea kuweka vifungu kwamba hata akionewa, basi hawezi akafanya kwenye chombo kingine. TBC mkimfukuza, ITV hawawezi kumchukua, ndicho ambacho mmeweka kwenye kifungu cha 20(2). Muswada huu kama utapitishwa na kwa wingi wenu mtapitisha…
Mheshimiwa Mwenyekiti, watapitisha tu, kwani walishapewa shilingi milioni kumi hizo! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 50(1)(d) cha muswada huu, adhabu ya kuchochea uasi na maneno ya kichochezi, fine kwa mtu atakayeandika huyo, ni shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni kumi au kifungo cha miaka saba mpaka 20. Mnaenda…
MWENYEKITI: Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie Finance Bill ambayo iko mbele yetu.Awali ya yote niombe wale wanaotunza muda watutendee haki upande wa pili. Kumekuwa na tabia ya kukata muda, last time nilichangia badala ya dakika 10 nilipewa dakika saba na nusu. Kwa hiyo, nami naona kabisa muda pale nimeanza ngapi, muache kutukata muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, sawa. Nategemea kuchangia mambo matano. Mafuta ya taa, kodi ya majengo, ushuru wa hoteli, ushuru wa mazao na vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya haya, niseme machache ambayo yamejitokeza juzi. Kwa hali ya kawaida naamini Bunge letu linaongozwa kwa Kanuni pia, kura ya bajeti ni kura ya imani na iko wazi. Ninyi ni Serikali ni Chama mnachoongoza sisi ni Wapinzani tunaotegemea kuingia madarakani, hatuwezi tukaunga bajeti yenu, ni Kanuni ni wazi, hata keshokutwa ninyi mkawa upinzani mnaweza mkawa na mawazo yenu mbadala na msiunge ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilishangaa sana kwa mara ya kwanza, huu ni mwaka wangu wa sita au wa saba, haijawahi kutokea mwongozo mtu mmoja akiomba wanapewa watu wengine sita nyuma yake, the same mwongozo. Ndiyo maana ilitushangaza sana na bahati nzuri mlifanya zile siasa mkiwa mmeachia television wazi, Watanzania wameona ubaguzi mnaoufanya wa wazi wazi. Hata kama mnakutana kwenye vikao vyenu vya caucus ni vizuri mkakumbuka critical thinking and argumentation, mmeletewa jambo lakini ni vizuri mkajiongeza, hivi kwa hali ya kawaida leo nchi nzima Miji mikubwa tunaongoza Wapinzani tukiamua kwa kauli zenu za ubaguzi ndugu zetu mlioko madarakani, tukaamua kukusanya zile kodi wenyewe, maendeleo tutashindwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ya majengo mnayochukua ninyi, kodi ya mabango mnayochukua ninyi, kodi ya ardhi mnayochukua ninyi ambayo hamrudishi tutafanya maendeleo na wananchi wetu watapata barabara, watapata hospitali, watapata kila kitu. Mkajisahau, mkaona mfanye siasa za kibaguzi, maana yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, mnawaambia Watanzania kwamba mtakusanya kwenye miji yetu hamtoturudishia na how if sisi tukaenda kwa Watanzania tukawaambia msilipe kodi, maana ninyi ndiyo mmeanza na waliwaona. Leo ukiwaambia kwamba wasilipe kodi, kwanza mlishawaambia kwa sababu mmesema hamtapeleka kwenye Majimbo ya Upinzani maana yake ni nini, mmewaambia wasilipe kodi. Ninyi ndiyo mnaleta matatizo kwenye Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfikirie ndiyo maana nikasema kwa wale ambao walisoma siasa; critical thinking and argumentation, ways and methods of decision making, maamuzi mliyofanya mmejichonganisha, mmejichora kwa Watanzania na ni aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu mlishaanza siku nyingi ndiyo maana hata hela za Mifuko ya Jimbo huku Wapinzani mmeanza kutukata, mmejiongezea ninyi. Mfuko wa Jimbo nikatolea mfano nikaombea mwongozo hapa, mmeshaanza iko wazi na hizi pesa mkianza kukusanya hamtotuletea, we are ready kwa hayo mnayotaka kuyafanya. Niwakumbushe tu, msifanye siasa za kitoto Watanzania wanawaona, inatia uchungu, mnaligawa Taifa hili. Naomba hayo yatoshe na Mawaziri wala msiendelee kuyaongelea hapo ni aibu kwenu, mnaligawa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mchangiaji amesema Serikali ni sikivu, eti ndiyo maana mkaleta sheria mkabadilisha badilisha sana, kwa sababu mmeya-accommodate mawazo ya Wabunge, kama ndivyo hili la mafuta ya taa, limewashindaje? Hayo mafuta ya taa nani asiyejua kwamba road licence haihusiani na mafuta ya taa? Hoja si ni kwamba Serikali ni sikivu, mmeya-accommodate mawazo ndiyo maana mkaleta yale marekebisho kwenye Finance Bill. Mafuta ya taa ndugu zenu wanawasha taa, vibatari, hakuna gari linalotumia mafuta ya taa, lipo? Mbona hili hamrekebishi kama Serikali ni sikivu! Nawashauri tu kama ninyi ni wasikivu toeni hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii na Finance Bill hii maana yake kila Mtanzania atalipa kodi, wala msijifiche, maana yake ni nini? Hata yale ambayo mnasema mmefuta sijui road licence, motor vehicle mmehamisha hata kwa watu ambao hawana hayo magari. Kwa hiyo, hili la mafuta ya taa naomba nipate ufafanuzi kama mlikuwa wasikivu kwa nini mpaka leo hamjafuta? Kwa hiyo, iondoke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la kuwatambua Wamachinga, MC, Mama Lishe, wauza mbogamboga, jamani! Lengo lenu ni jema kama mnavyosema, lakini siyo jema. Mmeshindwa tu kuandika mstari mmoja kwamba mnaenda kuwatoza kodi, hivi unaweza ukaniambia kwamba unataka kumtambua MC leo yuko kwenye kitchen party, kesho yuko kwenye harusi, kesho kutwa yuko kwenye msiba, kesho kutwa yuko kwenye ubarikio, eti unataka kumtambua! huyu movement yake unamtambuaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mama anayeuza mboga kichwani eti hata wauza mbogamboga hata aibu hamna mnaandika! Wengine, wanatembeza nyumba kwa nyumba unamtambuaje? Unampa kitambulisho ili iweje? Eti wauza mitumba hawa, mnataka kuwatambua muwape vitambulisho kweli? Semeni mmeamua kupeleka kodi kwa hawa wafanyabiashara wadogowadogo, Mama Lishe watalipa, kwa nini mnamumunya, mbona liko wazi, andikeni pia tujue? Tukienda kuwaambia Watanzania hao mmeshajiharibia sana kwenye bajeti hii. (Makofi)

T A A R I F A...

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa imetumia dakika tatu, muda wangu uwe pale pale. Kwanza sina sababu ya kubishana naye.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa siipokei kwa sababu hata Waziri wakati ana-wind up alisema lengo la kuwatambua ni nini, kwamba baadaye wakawe walipa kodi, kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge hakuwepo Hansard ipo itatafutwa, kama hakuwepo wakati ana-wind up tutatafuta Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kuwatambua mkawatambue, mkijua mmeshindwa kukusanya kodi kwenye makampuni ya madini, mnataka mkawalipishe hawa wanaotembeza mboga mboga, it is ok tutawaambia tu, tutakutana huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hoja nyingine ya ushuru wa hoteli. Mkanganyiko mwingine ni huu kwamba miaka sita niliyokuwa kwenye Bunge hili kulikuwa na mkanganyiko wa ushuru wa huduma kwa makampuni ya simu, mkasema mtakwenda kuyarekebisha, mtaangalia hilo mkashindwa, lakini hata huu ushuru wa hoteli, kulikuwa na mkanganyiko wa hoteli za five stars na hoteli zingine. Miaka mingi Halmashauri zikawa hazikusanyi, this time mmeleta tena mkanganyiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tu Mheshimiwa Waziri aangalie na mwongozo utoke mapema ushuru huu wa hoteli unakusanywa kwa kiasi gani na Halmashauri zikusanye, kwa sababu mlivyoandika maana yake hata ukusanyaji wake ni mkanganyiko mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Halmashauri zetu mmeondoa vyanzo vingi, hata hivi vingine vinavyobaki muwe mnaondoa mkanganyiko, haisaidii, mnasema isikusanywe, huku ikusanywe, sijui hoteli gani hampeleki mwongozo! Pelekeni mwongozo hili likae sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ushuru wa mazao, hili la ushuru wa mazao Mheshimiwa Waziri amesema kwamba tani moja imesamehewa mazao ya chakula, pia mmeshusha kwa asilimia mbili kutoka asilimia tano sasa ni asilimia tatu. Kimsingi Halmashauri zote zilikuwa zinakusanya asilimia tatu walikuwa hawajafika hata asilimia tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, toeni vitambulisho, kwa mfano Babati Mjini, wakulima wengi wanalima Babati Vijijini Galapo, lakini huu usumbufu siyo kwamba iwe ni tani moja, kama nimelima tani kumi ni mazao ya chakula yapitishwe kwa Halmashauri zote mbili, kukaa chini na kuwapa kitambulisho wakulima wanaotoka Halmashauri nyingine wanao-cross border. Hili la kusema iwe chini ya tani kumi haitosaidia wakulima wetu, kwa sababu pia kule wanakokodi mashamba wanakuwa wameshalipa fedha na wamechangia hiyo Halmashauri. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba wapatiwe vitambulisho sivyo ambavyo imekaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la kodi ya majengo, kuna watu wanasema kwamba Halmashauri za Wilaya ziko excluded, siyo kweli. Mmesema Miji Midogo, Miji Midogo iko kwenye Halmashauri za Wilaya! Mimi sijui uelewa wa watu ukoje? Hata huko wanasema nyumba ikiwa ya tofali na ya bati mtachaji. Kwa hiyo, Halmashauri za Wilaya zipo na huu mkanganyiko ulikuwepo hata juzi wakati mnahitimisha. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru kwa namna ya pekee Mheshimiwa Selasini Mbunge wa Rombo, kunipa dakika chache nami niseme machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza naunga mkono aliyoyasema kuhusu elimu sitaki kuyarudia ilikuwa niyasemee, lakini ni vizuri hiyo kauli ikatolewa ikaeleweka kwa sababu kama kuna kosa tutalifanya kama Taifa ni kuwafanya watoto wetu washinde kuanzia asubuhi mpaka jioni wasile chochote, kwa hiyo tunahitaji kauli ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ni suala la asilimia 10 ya vijana na akinamama. Nashukuru Wizara ya TAMISEMI Naibu Mawaziri walifanya ziara katika Jimbo langu la Babati Mjini lakini mkatoa mwongozo, kwamba sasa asilimia mbili ni kwa walemavu, halafu zile asilimia nane zigawanywe kwa akinamama na vijana. Naiomba Serikali ni vizuri mkatenga asilimia zingine mbili kwa ajili ya wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna timu kubwa sana ya wazee ambayo hainufaiki na hizi asilimia 10. Kama mliona busara kutenga asilimia mbili kwa ajili ya walemavu, sasa niiombe Serikali au niitake Serikali ione hitaji la wazee la muda mrefu ambalo wamekuwa wakiiomba Serikali iwatengee angalau kiasi fulani kwa kila mwezi wapewe. Sasa hizi asilimia 10 ukiwapatia vijana, akinamama na walemavu na hawa wazee muwakumbuke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni vizuri watu wengine wanapofanya kazi nzuri waweze kukumbukwa katika Serikali hii. Naishukuru sana timu ya wataalam katika Halmashauri yetu ya Mji wa Babati na Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba kama kuna miongoni mwa Halmashauri zinafanya vizuri kuhusu asilimia 10 ni pamoja na Halmashauri ya Babati Mjini. Ni vizuri wakawa-promote wale wataalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao wataalam ambao wanatusaidia zile fedha zinakuwa revolving fund, lakini Halmashauri zingine zile fedha zikiingia zinaingia kwenye consumption ya kawaida ya OC badala ya kurudi kwenye ule mfuko. Sisi kwa nini tumefanikiwa katika kutoa hiyo mikopo kwa asilimia 100 hiyo asilimia 10, ni kwa sababu tulikuwa na Mwanasheria mzuri sana, wale ambao hawalipi wanapelekwa Mahakamani, imesaidia watu kurejesha kwa sababu wanajua zile fedha lazima zirudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukawa na timu ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Mkuu wao wa Idara ambao zile fedha zikiingia wanaiweka kwenye account ambayo inakuwa revolving. Naomba vitu vingine hata kama vinafanywa na watu wengine ambao hamuwapendi sana kama ni vizuri basi mviige, njooni muone Babati tunafanya nini na tumefanikiwa kwa kiasi gani na nipongeze timu ya Babati Mkurugenzi na timu yake kwa sababu wanafanya kazi nzuri sana katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ninaotaka kuutoa ni kuhusu Pride Tanzania. Nimeona kwenye ripoti kwamba Kamati imeshauri Serikali iangalie kwa sababu hii Pride ilianzishwa kwa fedha za Serikali kipindi hicho. Naiomba Serikali pamoja na kwenda kuiangalia na kuibinafsisha irudi kwenye mfumo wa Serikali hii Micro Finance ni vizuri wale vijana wetu wasiathirike ajira yao na shirika likaendelea, kwa sababu kama kuna taasisi au kama Micro Finance ambayo imeajiri vijana wengi wa Kitanzania ni pamoja na Pride Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pamoja na kwamba huko nyuma mliuzianauziana kinyemela, lakini mwangalie pia ajira za Watanzania hata kama mnakwenda kuibinafsisha, lakini ni miongoni mwa Micro Finance ambazo zimetoa ajira nyingi kwa Watanzania na imefika katika vijiji na katika remote areas. Kwa hiyo, nitoe ushauri wangu kwamba msikimbilie kubinafsisha tu, sawa mtaangalia mtafanya audit ya kutosha, lakini mwisho wa siku muone jinsi gani ambavyo vijana wetu hawapotezi ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la OC, hebu niombe Serikali tunafanya bajeti, lakini bajeti hii hakuna sababu ya kukaa miezi mitatu au miwili hapa, tuka- budget fedha za maendeleo fedha za OC lakini mwisho wa siku Mheshimiwa Waziri wa Fedha, fedha zikawa haziji kabisa. Mmechukua vyanzo vikubwa vya Halmashauri zetu lakini hivyo vyanzo pia mvifanyie review, mfano nitoe chanzo kimojawapo, mmefuta ushuru wa machinjio katika machinjio zetu, pale Babati Mjini tumetengeneza machinjio mazuri, zaidi ya milioni 50 tumekarabati. Mmefuta ule ushuru at the same time mnamwachia Mkurugenzi alipe bili ya maji, bili ya umeme wakati kuna watu ambao wanachinja ng’ombe wao pale, mmefuta ule ushuru, angalieni…

(Hapa kengele ililia kuashiria muda wa mzunguzaji kwisha)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami nichangie machache katika bajeti ya Serikali ambayo ipo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Wabunge tunapokaa katika ukumbi huu kazi yetu ni kuisimamia na kuishauri Serikali, lakini kwa bajeti hii ambayo iko mbele yetu ni vizuri Serikali ikawa wazi ili tuishauri na tuisimamie. Hata hivyo, kama mtaleta vitu kwa mafungu na bila kufanya analysis ya kina maana yake hamtupi nafasi ya kuwashauri ili mfanye vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii ambayo tunaitumia sasa ni wazi kwamba Serikali imefikia malengo kwa asilimia 70 ya makusanyo, lakini kwenye makusanyo hayo ambayo mlikuwa mnategemea trilioni 29, trilioni 11 mmekusanya ya kodi lakini leo mnaleta trilioni 31 wakati makusanyo yetu yako asilimia 70. Mngetuambia tu ukweli, kwamba ni wapi mmekwama? Kwa sababu gani na mnarekebishaje? Kwa haya mnayotuletea kwamba kila mwaka mnakuza bajeti ambayo haitekelezeki mnawadanganya Watanzania siyo kweli. Ni bora mseme ni wapi mmekwama na tuishi according to bajeti ambayo tunaweza tukakusanya na tukapeleka kwenye miradi ya maendeleo, lakini kama mnataka tufanye biashara kama biashara mtapitisha bajeti hii lakini utekelezaji haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu ni bahati mbaya sana leo Serikali mnawaza kuzimisha kabisa Serikali za Mitaa. Makusanyo yenu yote mmekusanya huko mmeshindwa, mnakwenda kuchukua vyanzo vya Halmashauri zetu sasa ni kitu kinachosikitisha na nilishawahi kusema kwenye Bunge hili. Mwaka 1980 Baba wa Taifa alijuta suala zima la kufuta Serikali za Mitaa na kuondoa nguvu za Serikali za Mitaa. Wakati huo barabara zilikwama, zahanati zetu zilikwama kwa sababu fedha zilikuwa haziendi baada ya Serikali Kuu kukusanya. Hii bajeti mnayotuletea leo ni ya kuua Serikali zetu za Mitaa kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili mwaka jana mlitufukuza hapa mkapitisha bajeti, lakini mkaondoa chanzo cha kodi ya majengo. Mpaka hivi tunavyoongea mpaka leo Serikali haijakusanya, TRA haijakusanya kodi ya majengo ni bora mngetuachia Halmashauri tukakusanya. Kama hilo halikutosha hamkufanya tathmini ndiyo maana nasema mnaleta bajeti kama biashara tu kwamba muda wa kuleta bajeti umefika mnaleta bajeti hamjafanya tathmini. Leo Serikali mngekiri tu kwamba mlishindwa kukusanya na mlifanya maamuzi mabaya kuondoa chanzo hiki katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo haitoshi kodi ya ardhi mmechukua, kodi ya mabango mmechukua, uko kwenye minada mmefuta. Naomba Waziri wa Fedha aniambie ukweli wakati anajibu hivi wana mpango gani na Halmashauri zetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea mimi Halmashauri ya Mji wa Babati, nitoe tu mfano, wametuachia vyanzo viwili tu, ushuru wa soko na ushuru wa stendi. Wakati huohuo wanasema kwamba, Halmashauri zetu tuorodheshe idadi ya wazee, tuwalipie bima ya afya, wauna watu tunawalipa mishahara madereva na ma-secretary pale wasaidizi zile kada ambazo Halmashauri zetu zinaajiri, lakini hakuna chanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana hizi fedha tunazoambiwa kwamba, leo naomba tu nichangie hii sehemu ya Serikali za Mitaa. Hizi fedha ambazo Serikali mnasema mtakusanya mtatuletea ni uwongo mtupu. Ninavyoongea hivi Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nilikwenda nikamwona pale kwenye Kiti nikamweleza hata OC hawatuletei kwenye Halmashauri zetu, hivi ninavyoongea tangu bajeti hii imeanza ya trilioni 29 Halmashauri ya Mji wa Babati wametuletea OC ya milioni 26 tena ya mitihani! Hela ya Walimu wanaoenda kusimamia mitihani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Halmashauri ukienda watu wanaandamana hakuna fedha, hatuna makusanyo, fedha zote wamechukua. Ile asilimia 30 ya kodi ya ardhi ambayo tunakusanya hata hawarudishi tena kwa Wizara ya Ardhi hawatuletei tena! Halafu wao watu wa Mungu binadamu wanasema kwamba, kila kitu kifanyike kwenye Halmashauri, miradi ya maendeleo hawaleti fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha Mheshimiwa Waziri kwenye hiki kitabu, fedha zote wamepeleka zaidi ya milioni 500 kwa Jeshi. OC wanazopeleka ni za Jeshi, Polisi, ndiyo hela wanazolipa, lakini huku hawapeleki! Hakuna hela ambazo wanatuletea, leo tutawaaminije kwamba, wao tukiwaachia hivi vyanzo wataturudishia kwenye halmashari zetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu wajitafakari, ni bora wakaacha Halmashauri zikakusanya kwa sababu, wao vipaumbele vyao ni tofauti na walivyoviahidi. Kwenye Uchaguzi Mkuu wakaja wakatuahidi wakasema milioni 50 kwa kila kijiji, hakuna chochote huku Mheshimiwa Waziri. Tena hajaongelea chochote! Mwaka jana wakatenga mikoa sijui mingapi kama bilioni 59, hawakupeleka kabisa hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekaa Wabunge tunaulizwa, Serikali imeahidi milioni 50 kwa kila kijiji ziko wapi? Hata kuzisema tu wamekwepa, hata kuziandika tu, mwaka jana walithubutu kuandika, mwaka huu hawajathubutu hata kuandika kutaja. Wanavyoviahidi tofauti na wanavyotekeleza! Ni nini kinawaroga? Ni nini kinawasahaulisha? Ni kitu gani ambacho kinawafanya wasifikirie waliyoyaahidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zetu wametuachia kitu cha ajabu sana, wamepandisha faini za mtu ambaye ametupa takataka, labda kimfuko cha malboro amekidondosha chini, kutoka Sh.50,000/=, wamepandisha mpaka Sh.200,000/= mpaka Sh.1,000,000/=! Eti ndio chanzo wanachotuachia Halmashauri. Ni aibu kwa Serikali ambayo inawaza eti fine ndiyo iendeshe Halmashauri. Yaani wamepandisha eti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ile ni By Laws ya Halmashauri zetu, to be honest, tuwe wa kweli, wala hakiwahusu hicho chanzo, halafu Serikali wanakaa wanafikiria, halafu kingine, ada ya uchafu unapozolewa sokoni wamefuta, hata kuzoa uchafu hawataki tu-charge. Halafu wanaweka faini kwa kitu gani, wakati hata hizo ada za kuondoa tu huo uchafu wameondoa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana nasema wakae wafikirie. Waheshimiwa Wabunge kila mmoja hapa ana Halmashauri yake, Wabunge wa Majimbo, Wabunge wa Viti Maalum tunaingia, hii bajeti wale wanaosema ni bajeti ya karne, wanajidanganya na watapiga makofi watapitisha, lakini kwa upande wa Halmashauri, Serikali Kuu imeamua kunyonga Halmashauri zetu, kuchukua vyanzo vyote, wanatuachia eti tukakimbizane na wananchi, mtu ametoka hospitali kawekewa drip ameenda haja ndogo hapo tukam- charge laki mbili! Nani anaweza kufanya hayo? Hatuwezi kufanya hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri akae chini afikirie, ushauri wangu kwa Serikali na kwa bajeti hii, wakae chini wafikirie warudishe vyanzo vyote vya Halmashauri, ili tuwasaidie kufanya maendeleo kwa sababu barabara zetu hazipitiki, tunavyoongea hatuwezi kuchonga hizo barabara wala kukarabati. Tulishauri katika Bunge hili kwamba, asilimia 70 wanazopeleka TANROAD wapeleke kwenye Halmashauri, 30 iwe viceversa kwa sababu barabara

nyingi za mikoa wameshaunganisha kwa lami. Sasa hivi waturudishie hivyo vyanzo, wabadilishe, hawakutaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kinachotokea sasa kwa sababu wameona kwamba, hawakusanyi huku juu mambo hayaendi, wakaunda task force ile ya TRA ambayo wameweka Usalama wa Taifa, wameweka Polisi huko wanakimbizana na madeni ya nyuma huko, wakati walisema hawatafufua makaburi, leo wanafufua makaburi! Wanaenda wanadai kodi ya 2011 hata wao hawakuwepo kwenye hizo nafasi! (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee alikoishia mchangiaji aliyepita kwamba bajeti hii Serikali inyoongozwa na Chama cha Mapinduzi mmepoteana na Ilani ya Chama chenu lakini siyo tu kupoteana, mmepoteana na wapiga kura asilimia 80, waliowapigia kura ambao mnawaita ni wanyonge kila siku. Mheshimikwa Rais akisimama anasema Serikali ya Mheshimiwa Magufuli ni ya wanyonge. (Makofi)

Sasa kama ni ya wanyonge halafu bajeti ya wanyonge inapunguzwa kwa asilimia 34 bajeti ya development ya ajabu! Wanyonge gani wa nchi hii mnawaongoza wakati juzi tu kwenye maji mlipeleka asilimia 22, mkapitisha ile bajeti kwa caucus mkaitana mkaipitisha, lakini hii bajeti Mheshimiwa Waziri asilimia 18 tu ndiyo imepelekwa mpaka sasa, halafu mnajiita Serikali ya wanyonge, mlishapoteana zamani sana, siyo kupoteana na Ilani mpaka na wapiga kura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbaazi amesema Mheshimiwa Nape, Waziri kwenye kitabu chako mbaazi hata kuongelea ujaongelea kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali ya kawaida Mheshimiwa Waziri hata mbaazi hujaongelea kwenye kitabu chako, maana yake unatuambia watu wa Kanda hii yote tuliyolima mbaazi tukale na watoto wetu ndiyo Serikali ya wanyonge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natafuta kwenye kamusi nini maana ya laana, lakini nikaona tu niipotezee kwa sababu wakulima wa nchi hii wanawalaani sana maana wamekaa mazao yao, wamekaa na mbaazi zao na mahindi yao ninyi hamuhangaiki, unakuja hata huongelei suala la mbaazi Mheshimiwa Waziri, sasa unasema ni Serikali ya wanyonge asilimia 80 ya Watanzania hata huhitaji kuongelea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mahindi mmesema hivi mnataka muongeze production ifike tani milioni nane kutoka tani milioni sita iliyoko sasa, lakini Mheshimiwa Waziri unafahamu mliunda Bodi ya Mazao Mchanganyiko, ile bodi wanahangaika mmewakabidhi tu majengo ya National Milling mpaka leo Bodi ya Mazao Mchanganyiko wanaomba shilingi bilioni tisa kwenu hamjawahi kuwapatia hizo shilingi bilioni tisa, hao watu bodi ya mazao mchanganyiko wangetusaidia kununua mahindi yetu, mbaazi zetu wakachakata. Mnaita Tanzania ya viwanda mmeshindwa hata kufufua majengo ya National Milling mpaka leo. Bodi ya Mazao Mchanganyiko wanaomba shilingi bilioni tisa kwanye bajeti mnawanyima, wameomba mkopo NSSF shilingi bilioni tatu hata Serikali haitaki ku-endorse huo mkopo halafu mnasema mna mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye kitabu chako umesema eti mmefungua mipaka mahindi yapelekwe nje ya nchi, huku mnasema kwamba ninyi ni Serikali ambayo inafufua viwanda na nchi ya viwanda hivi viwanda ndiyo kupeleka mazao nje ya nchi? Kwa nini
hamtaki kutoa hizi fedha shilingi bilioni tisa National Milling hawa na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wakachukua mahindi yetu wakaweza kuyachakata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aibu zaidi katika Serikali yenu hii NFRA mliwapa fedha mwaka jana za kununua tani 18,000; mwaka huu mmewatengea fedha kununua tani 28,000 wakati mahindi tunazalisha tani milioni sita! Ninyi watu mmeshapoteana zamani sana, you are in the middle of nowhere! Hamjuani katika hili la wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaudhi mimi naomba niende kwenye solution naipongeza sana Kamati hii na hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo wameshauri solution mbalimbali... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Shirika la Posta takribani miaka 10 sasa hawafungui masanduku mapya? Imeleta matatizo makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, fidia ya bypass ya barabara ya Hangoni - Sigino kwa barabara ya Babati - Singida na Babati - Dodoma italipwa lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri TARURA wapewe 50% not 30%.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege Mkoa wa Manyara unajengwa lini? Eneo lipo Mamire Ngungu, Jimbo la Babati Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halotel waliahidi kuweka mnara wa mawasiliano katika Vijiji vya Himit, Imbilili na Chemchem Jimboni kwangu. Jamani, hadi lini ahadi hii itatimia?

Mheshimiwa Naibu Spika, niwatakie kila la heri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, posho za wazee wa Mahakama; Babati hawajawahi lipwa miaka miwili iliyopita, wazee wamehangaika bila mafanikio. Sasa naomba kufahamu wazee hawa wamehangaika sana watalipwa lini?

Mheshimiwa Spika, fidia ya wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa na jengo lao la Mahakama, Mkoa wa Manyara na Mahakama ya Wilaya ya Babati pale Mtaa wa Negamsii, Kata ya Bagara, Jimbo la Babati Mjini tangu 2004 hadi leo wananchi hawajalipwa fidia japo Mahakama imeshajenga majengo yao na wananchi hawajalipwa. Naomba kufahamu Mahakama kama chombo cha haki ni kwa nini imewanyima wananchi fidia yao na lini watalipwa?
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Awali ya yote nikitakie heri Chama cha Mapinduzi katika siku yake ya kuzaliwa, miaka 42 siyo mchezo. Naamini tutaendelea kuwaongoza Watanzania ili wafikie ndoto zao za maendeleo. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, niweze kutoka moyoni kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kauli ambayo ameitoa hivi karibuni kwa wananchi wetu ambao wanaishi katika hifadhi mbalimbali katika vijiji vyao, ambao walikuwa wakipata matatizo makubwa na hifadhi zetu, lakini pia wakulima mbalimbali ambao walikuwa wanatumia maeneo ya vijiji lakini walikuwa na migogoro na hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili halidhihirishwi tu na Wabunge tunaotokana na maeneo hayo, lakini limedhihirishwa na wananchi wetu ambao kwa namna moja au nyingine wamejitokeza hadharani kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kauli yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilichogundua ni kwamba kwa kauli hii, anayevaa kiatu ndiye anayefahamu ni wapi mwiba unamchoma. Kuna miongoni mwetu ambao wanabeza kauli ya Mheshimiwa Rais, lakini kwa wale ambao miaka yote tumekuwa tukiomba Serikali iangalie hili, kwa kweli tumepokea kwa moyo wa faraja na wa pongezi kwa Serikali na kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka mitano iliyopita, nilikuwa nikiongelea vijiji vya Gedhamaru, Gijedabung, Ayamango na maeneo mengine katika Mkoa wetu wa Manyara. Tumeona sasa wale wafugaji na wakulima jinsi ambavyo wameguswa na kauli ya Mheshimiwa Rais. Naomba nimtie moyo aendelee kutumikia Watanzania bila kuchoka, kwa sababu maamuzi anayofanya yanawagusa na yanagusa maisha ya wanyonge. Tunamshukuru sana. Ombi langu kwa Serikali, watusaidie mapema. Wizara husika waweze ku- identify hayo maeneo mapema ili wale wananchi sasa watulie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana kauli ya Mheshimiwa Rais ni jambo moja lakini pia utekelezaji ni jambo lingine. Nina imani na Serikali yangu na ninaamini kabisa kwamba hili litafanyika mapema na hatutamwangusha Mheshimiwa Rais kwa kauli nzuri aliyotoa kwa Watanzania ambao kwa kweli wamepokea kwa moyo wa shukrani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie kwa ufupi changamoto ambazo tumeziona kwenye hifadhi zetu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo, tunafahamu hifadhi zetu ambazo zinapatikana Kusini mwa Tanzania ukiachilia mbali za Kaskazini mwa Tanzania, zimekuwa na mchango kidogo kwenye Bajeti yetu ya Kitaifa lakini kwenye pato la Taifa ni kwa sababu ya changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo.

Mheshimiwa Spika, kwenye kitabu chetu cha Kamati, wamezungumzia au tumezungumzia changamoto za Hifadhi ya Mikumi, jinsi ambavyo ile barabara kuu wanyama wamekuwa wakigongwa zaidi ya wanyama 100, kwa mwaka tunapoteza wanyama hao. Pia hifadhi hizi au hii ya Mikumi imekuwa ikipata kuchafuliwa kwa sababu wanapopita panakuwa hapana doria ya kutosha na hata zile doria hazitoshelezi na wanaopita barabarani wanakuwa watupa uchafu na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Ruaha inahitaji kuangaliwa kwa karibu. Nafahamu kwamba hifadhi zetu zinachangia zaidi ya asilimia 17 katika bajeti yetu na katika pato letu la Taifa, lakini kama hifadhi hizi za Kusini zisipopewa kipaumbele na zikasaidiwa kwa karibu kwa kuondoa zile changamoto wanaweza wakawa wanaendelea kurudi nyuma katika mapato ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Hifadhi ya Ruaha, naiomba Serikali yangu na ninaamini ni Serikali sikivu, hii barabara kutoka Iringa mpaka hifadhini zaidi ya kilometa 100 ni ombi la muda mrefu kwamba sasa iweze kuwekewa lami. Naamini katika mpango mzima uliopo wa REGRO ambao unalenga kukuza utalii na kusaidia hifadhi zetu kwa upande wa Kusini, unaoendeleza ungeweza kusaidia. Naiomba pia Serikali waweze kuharakisha kusaini mkataba huo wa REGRO ili isaidie katika kuondoa changamoto ambazo ziko kwenye hifadhi zetu.

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara husika isaidie pia kuharakisha mfano miundombinu katika hifadhi zetu, Kwa Hifadhi ya Ruaha pamoja na Mikumi na hifadhi nyingine wanatamani sana ndege zitue katika hifadhi zetu ili watalii wale ambao wanatamani kufikia kule waweze kufikia.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu siyo watalii wote ni vijana ambao wanaweza wakastahimili kutembea katika barabara zetu. Kuna watalii ambao ni wazee, wao wanahitaji kutua moja kwa moja katika hifadhi zetu. Kwa hiyo, naomba pia Serikali iangalie kwa karibu sana ili waone pia tunakuwa na viwanja vya ndege katika hizo hifadhi.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, pia naiomba Serikali, sisi tuna hifadhi yetu ya Tarangire katika Mkoa wetu wa Manyara ambako geti la Babati – Tarangire kupitia Babati Mjini pale, sisi tumesharidhia na geti limeshafunguliwa. zaidi ya kilometa 20 ni za rough road. Naiomba Serikali na asubuhi pia mlinijibu swali la bypass, mmeahidi kushughulikia. Tukipeleka lami pale, tutasaidia watalii wetu waweze kufikia hizo hifadhi.

Mheshimiwa Spika, naamini changamoto ni nyingi katika hifadhi zetu, lakini Serikali yetu ni sikivu na inaweza ikafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nilitaka niipongeze Serikali kwa moyo wa dhati na ninampongeza Mheshimiwa Waziri pia, ni suala la mradi huu wa kurasimisha vijiji na upimaji ambao unafanyika kwa majaribio katika Mkoa wetu wa Morogoro na katika Wilaya za Malinyi, Ulanga na Kirombero, kwa kweli ni mradi uliosimamiwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa moyo wa dhati, huu mradi umesaidia wananchi kumilikishwa maeneo yao na wamepata Hati. Tumefika site, tumeona ni kwa kiasi gani hata akina mama wamepatiwa Hati, siyo wanaume tu. Tumeona ni kiasi gani wale wananchi wameshirikishwa.

Mheshimiwa Spika, nisipoipongeza Serikali kwa mradi huu, nitakuwa sijitendei haki. Nami naomba Serikali itusaidie, kuna fedha za ndani zaidi ya shilingi bilioni saba, lakini ni shilingi milioni 710 ndiyo zimetolewa. Mheshimiwa Waziri, pamoja na kazi nzuri, zikitolewa zile shilingi bilioni saba ambazo ni fedha za ndani, zitatusaidia kukamilisha ule mradi. Huo mradi sasa Mheshimiwa Waziri uweze kupelekwa kwa nchi nzima. Naamini nia ya Serikali ni njema sana, lakini tatizo lako ni bajeti.

Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tunapoelekea kwenye Bunge la Bajeti, Wizara hii tuipatie fedha kwa sababu wanapowapimia wananchi wakapata haki zao migogoro ya ardhi itakuwa imeisha katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweke mawazo yangu machache katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu anayetupa nafasi hii ya kusema kwa sababu siyo kwa nguvu zetu wenyewe lakini ni kwa neema zake. Pia tunapochangia, tunachangia yale ambayo tunayaona kwa macho yetu ambayo yamekuwa yakifanyika kwa nia njema tu ya kusaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nilivyokuwa Ukanda wa Gaza nilisema yafuatayo: “Ni nchi gani hii isiyokuwa hata na ndege ya kuazima, isiyokuwa na nia njema ya kuona kwamba Tanzania tunahitaji kuwa na uchukuzi wetu wenyewe lakini pia tukawa na ndege zetu wenyewe”, bajeti iliyopita nilikuwa mkali sana. Miaka mitano iliyopita nilivyokuwa Mbunge wa Viti Maalum na nilivyokuwa Mbunge wa Jimbo miaka kadhaa nyuma, nimekuwa nikichangia sana suala zima la Tanzania sisi wenyewe kuwa na ndege zetu. Leo nitazungumza tofauti na ile kauli niliyokuwa nikiongea wakati niko Ukanda wa Gaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kwa kunukuu, nukuu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo alimnukuu Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. Ukurasa wa saba katika hotuba yake, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameandika haya yafuatayo akimnukuu Mheshimiwa Rais, amesema: “Tumekuwa wakimya na hatuelezi kwa kina masuala tunayofanya. Niwaombe basi viongozi wenzangu wa Serikali, kila tunapopata nafasi tuseme mambo tunayofanya…tusipofanya hivyo yanayosemwa yataonekana kuwa ya kweli”. Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli hii na nukuu hii inatukumbusha kwamba lazima tuseme mambo ambayo yamekuwa yakifanyika katika nchi yetu ambayo hayajawahi kufanyika. Ni dhahiri kuna mahali tulikuwa tumekwama kama nchi, haiwezekani nchi kubwa tumejaliwa kila kitu lakini hatuna uchukuzi, hatuna ndege zetu na vitu kama hivyo. Kazi kubwa inayofanywa na Serikali hii, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu, wasiposema wengine, tutasema sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze sana hili la Serikali yetu, Mheshimiwa Rais kuhakikisha nchi yetu tunapata ndege zetu wenyewe, imetujengea heshima kubwa sana kama Taifa. Watu hawasemi lakini kipato kinaongezeka na watalii wanaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili niliseme kwa sababu nilisema sana nikiwa upande ule, nikiishangaa nchi hii, ni lini tutakuwa na ndege zetu wenyewe? Leo wametekeleza, hatutaki kupongeza. Naomba nipongeze na hizi jitihada ziendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili, uzalendo huu wa Mheshimiwa Rais Magufuli hata ajuzi tumeona anabadilisha ndege iliyokuwa inatumika kwa ajili ya kubeba viongozi, anaipeleka ibebe Watanzania. Inabadilishwa rangi ili iendelee kuongeza nguvu katika uchukuzi huu. Haya lazima tuyaseme. Naomba tusonge mbele, Mheshimiwa Rais asikate tamaa, amefanya mambo ambayo yalikuwa hayafanyiki na aendelee kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuwe wakweli tu, suala la barabara katika nchi zetu, hakuna mahali barabara na madaraja hayajajengwa. Nimekuwa nikiongea kwamba tuna barabara za lami kila mkoa umeunganishwa na mkoa mwingine, nimekuwa nikisifia ya Dodoma - Babati lakini juzi tumefika Kilombero tumekutana na daraja la Magufuli kule, wakati siku zote wale watu walikuwa wanahangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache Kilombero, twende Arusha; Mji mzima barabara zinajengwa kwa fedha hizi ambazo leo tunapitisha bajeti. Vile vile twendeni Dar es Salaam, Wabunge wa Dar es Salaam wanafahamu; mimi nimefika Dar es Salaam juzi, nimeshangaa sana; njia nne kwenda, njia nne kurudi, haijwahi kutokea. Haya mambo tusipoyasema tunamkosea hata Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwenye Bunge lililopita jamani eeh, hebu tusimsifie sana Mheshimiwa Rais, tuangalie, tukosoe kwa upendo. Nilikuwa nasema nikiwa najikaza tu, lakini ukweli unajulikana. Leo niseme kwamba hivi vitu vinaonekana, sisi ni Watanzania, tuache siasa, tuweke ukweli mbele, vitu vinavyofanyika Dar es Salaam kumaliza ile foleni, kumaliza msongamano wa magari barabarani njia nne hizo, upande mmoja mwingine nne, haijawahi kutokea na magari yako site na watu wanafanya kazi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema ya Jimboni kwangu naweza nikawa najipendelea, lakini kwa sababu ni bajeti ya nchi nzima, ni bora Watanzania tukaongea kazi anayofanya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tunabeza; wengi wanabeza, lakini sijawahi kuona ni Mbunge wa awamu ya pili sasa zinatolewa fedha nchi hii kwenda kukamilisha maboma ya sekondari ili watoto wetu wasome vizuri. Ndani ya miaka mitatu hii ya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kazi ya maendeleo aliyoifanya haielezeki. Hospitali zaidi ya 67 za Wilaya zimejengwa. Kwenye elimu hawaishii hapo, sasa hivi wanamalizia sekondari, ujenzi unaendelea, wanawaza kwenda kukamilisha maboma ya Shule za Msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo Watanzania wanajua. Hata kama kuna watu watasimama watayapinga kwenye Majimbo yao, wanafahamu mioyoni mwao kwamba maendeleo yanafanyika, isipokuwa tu hawawezi kutamka hadharani kama ambavyo mimi nilikuwa siwezi kutamka hadharani nilivyokuwa ukanda wa gaza. (Kicheko/ Vigelegele/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo maendeleo yanafanyika, hawaangalii, hawabagui, fedha za maendeleo zinatoka. Nenda SGR, zaidi ya shilingi trilioni 7.1 fedha za ndani. Collections zetu kwa mwaka siyo zaidi ya shilingi trilioni 14, lakini Mheshimiwa Rais huyu ambaye wengi wanasimama wanambeza, wanaibeza Serikali ana-commit zaidi ya shilingi trilioni 7.1 kwa ajili ya SGR tu. Hajasema mengine ambayo yanafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisimama le niseme, ingekuwa ni maamuzi yangu tu ningesema hatuna sababu ya kupoteza muda, tuwapitishie bajeti yao Serikali waendelee kufanya kazi, maendeleo yanaonekana. Kuna mtu hapa juzi alisimama akawa anazungumza hoja moja, mioyo ya Watanzania kwa maendeleo haya ambayo yanaendelea, tunatamani Mheshimiwa Rais huyu aendelee kuongoza nchi hii tupate maendeleo. Ninafahamu siyo kauli ya wote inaweza ikawa inakwaza kila mmoja, lakini kwa maendeleo haya yanayofanyika, kila mmoja anaweza akawa ana feelings zake moyoni kwamba hivi tunahangaika na uchaguzi kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifika Dar es Salaam nikasema, kwa kazi hii, barabara hizi, kazi zinafanyika site, tunakwenda kwenye uchaguzi kumchagua Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli awe Rais, kwa kitu gani tunachotafuta tena? Ni kumwambia endelea, chapa kazi ili Watanzania tupate maendeleo. Tunachotaka ni maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ungeniuliza leo mimi Pauline fedha za uchaguzi kwa nini tunakwenda; labda tuchague huko kwenye Serikali za Mitaa na maeneo mengine. Kwa Mheshimiwa Rais tunaenda kuchagua kitu gani? Sawa ni Katiba, tunaenda kuchagua kitu gani? Kwa sababu ambayo yamefanyika hayajawahi kufanyika na yanaendelea kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilirusha kwenye mitandao, Mji wetu wa Babati. Siyo fedha tu za barabara tunawekewa, jana nimerusha mpaka taa za barabarani tunawekewa sasa, Mji umewaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie hotuba hii kwa kusema Serikali yetu chapeni kazi, Waheshimiwa Mawaziri chapeni kazi, Mheshimiwa Waziri Mkuu chapa kazi, Mheshimiwa Rais usiwasikilize, kwa sababu hata wanaokutukana, kwenye Majimbo yao hawajatekeleza ahadi zao. Wewe umetekeleza nyingi. Chapa kazi, fedha ni hizi sisi tunakupitishia hizi fedha, wananchi wanataka maendeleo, hawataki maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi/ vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweke mawazo yangu katika Wizara hii ya Maji lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kutupa nafasi hii maana ni kwa neema yake tu tutimize wajibu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu na Katibu Mkuu na timu yake kwa jinsi ambavyo wanachapa kazi hongera sana. Nafahamu wanapambana sana, Wizara hii kila mmoja anatamani atendewe haki kwenye eneo lake na kila siku wako site. Pia niwashukuru wanatutembelea huko majimboni, Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Babati, akafika Imbilili kwenye mradi ambao umekuwa ukisumbua muda mrefu sana, lakini naona sasa kuna mwanga na mambo yanaendelea. Niwapongeze mno kwa kuwa wanapambana usiku na mchana ili wananchi wa Tanzania wapate maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Mradi huu wa Maji katika Mji wa Mtwara na Babati, ukurasa wa 90 kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri. Naomba tu watusaidie wawe wakweli, watuambie wapi wamekwama kwa sababu wameandika Mtaalam Mshauri anaendelea na usanifu wa kina wa mradi na ujenzi wa mradi utaanza baada ya kukamilika kwa usanifu huo. Sasa naomba nifahamu usanifu unafanyikia wapi Dodoma, Dar es Salaam au Babati na Mtwara. Kama ni Babati na Mtwara nafikiri warudi kwa wataalam wao wawaambie tu ukweli, huyu mtu wanayemsema Mtaalam Mshauri amefika, hayuko site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachofahamu Mradi huu wa KfW kati ya Serikali yetu na wenzetu wa Ujerumani ni mradi wa mwaka wa kumi na moja sasa ambao ungetusaidia kilomita 45 coverage pale tukapata maji, lakini ukatusaidia kujenga vyoo katika maeneo ya stand, masoko na maeneo mengine katika shule zetu. Maeneo mengine wameshatekeleza, Mheshimiwa Makamu wa Rais alikuja Babati tukaomba pia na hili, tukaomba kwa Mheshimiwa Waziri aliyepita na aliyepo sasa na Naibu Waziri wakatuambia tatizo Wizara ya Fedha ndio hawajasaini huu mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tu nisikitike kuwa Mheshimiwa Waziri leo anatuambia Mtaalam Mshauri yupo site Babati huko akiendelea na usanifu, nafikiri hizi taarifa zao waziangalie upya kwa nia njema tu, kwa sababu ni mradi wa miaka kumi na moja sasa. Sasa ni vizuri wakatuambia kwa sababu utatusaidia sana pale Babati Mjini na sijapoteza imani na Mheshimiwa Waziri, lakini natamani tuwe wakweli, kama tumekwama mahali tuambizane, hilo tu. Kwa huu mradi wakate mzizi wa fitina, wasituambie mkataba haujasainiwa, Mtaalam Mshauri yuko site, wakati hayuko site, naomba kwa hili watuambie ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niwapongeze walifika katika Kaya ya Sigino upande wa Imbilili. Usiposhukuru kwa kidogo pia maana yake utakosa kikubwa, wametulipia certificate za maji za Mradi wa Malangi na Mradi wa Haraa na unaendelea vizuri. Pia nimewapatia certificate ya Imbilili ambako wamefika, kwa kweli niwaombe wanafahamu ni viongozi wangapi wamefika pale, sitaki kuwataja, nawaomba watulipe hizo fedha za certificate ya Imbilili milioni mia mbili kama na arobaini ili ule mradi uende kwa sababu mradi ule ume-expire mara tatu, 2017 yule mkandarasi aliyeko site mkataba wake uli-expire. Mwaka 2018 tukaongezea tena ule mkataba uka-expire na mwaka 2019 ume-expire tena, lakini sasa anaendelea site kwa sababu fedha hazitoki na maeneo mengine pia anafanya miradi mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina tatizo na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, ninachoomba katika zile bilioni 40 walizosema zimesalia basi watulipe na ule mradi kwa sababu zifuatazo:-

Kwanza, ndio kijiji pekee kati ya vijiji vinne kwenye kata nzima ambako mradi ndio umeanza kidogo. Kwenye Kata ya Sigino Mheshimiwa Waziri wa Maji alifika baba yangu ambaye sasa yuko kwenye Wizara ya Ujenzi, akafika pale, akaongea na wale wananchi, akawaambia Kata ya Sigino tunawapatia maji umekuwa ni wimbo wa miaka yote. Naibu Waziri amefika ameona kata nzima ule mradi haujafika, naombeni Kata ya Sigino ndio mradi wetu wa kwanza Halmashauri ya Mji wa Babati hatuna mradi mwingine ni wa Kata ya Sigino, Kijiji cha Singu, Kijiji cha Sigino, Dagailoi na hicho cha Imbilili milioni 230 wakitulipa sisi hatuna ugomvi na wao, watupatie hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasahau naomba nishukuru sana pia kwa kitendo walichotufanyia watu wa Babati na Watanzania kwa kipindi hiki, wamefuta service charge kwenye bili zetu za maji, bili za mwezi wa Nne zimekuja, wananchi wa Babati walikuwa wanalia kuhusu Sh.2,500 kwa kila bili, kwa kweli nawapongeza na hii kauli ni ya wananchi wa Babati, wameondoa hiyo service charge, hongera sana. Sasa wanapopiga hatua mbele Mheshimiwa Waziri ni vizuri wakatuletea sasa prepaid meters, hizo wakitupatia kwanza zitatusaidia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji hayatapotea pia zile bili za maji ambazo zilikuwa hazikusanywi zitakusanyika sasa kirahisi, nawaomba wa-roll out mapema Waheshimiwa Mawaziri wetu, wameshafuta hilo wananchi wa Babati wamefurahi sana kwa sababu ilikuwa kila mkutano nikienda wanasema mama tunakuomba service charge iondolewe, wameiondoa hatuna cha kuwalipa tunawashukuru, lakini sasa watuletee prepaid meters itasaidia sana maji yasipotee na watu walipe bili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine katika Mji wetu wa Babati bili za maji imependekezwa na EWURA na mchakato kutoka chini kwamba ipandishwe kutoka unit moja kwa Sh.1,190 hadi Sh.2,000. Hivi imagine ongezeko la Sh.1000 niwaombe sana watu wa EWURA wasije wakathubutu kupokea hayo maombi ya kupandisha bili za maji katika Mji wa Babati kwa sababu hata hizo za sasa tu wanaona watumiaji wa maji sio wengi ni kwa sababu pia hizi bili ni kubwa kwa units tano mpaka 10 haitoshi kwa matumizi ya nyumbani, lakini units 10 na kuendelea wakaongeza kutoka Sh.1,100 mpaka Sh.2,000 Mtanzania wa Babati hawezi kumudu hiyo bili. Kwa hiyo chondechonde watu wa EWURA wasije na watu wa maji wakapandisha hizo bili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ni suala la usimamizi wa maji. Mheshimiwa Waziri amesema ana upungufu wa watumishi 3000, hao watumishi 3000 katika Wizara yake ambapo alitakiwa awe na watumishi 10,000, sasa una 6,000 lakini hiyo inashuka mpaka kwenye halmashauri zetu. Mimi nishauri kama hawa watumishi ni pungufu fedha za maji wanazotutengea waache mamlaka zisimamie kwa sababu hao ma-engineer wa maji wameshindwa kusimamia miradi ya maji katika halmashauri zetu. Utakuta usanifu mbovu, maeneo ambako mabomba ya chuma yanatakiwa yawepo kwenye makorongo wanaweka ya plastiki, tatizo ni kubwa kwenye mji wetu sisi miradi mingi ya halmashauri tumekuwa tukikabidhi BAWASA kwa sababu mradi unatekelezwa na halmashauri ukipelekwa kwa wananchi wau-test haufai hata kidogo. Mradi wa Managhat jana tumetoka kulipa, juzi kwenye kikao cha Kamati ya Fedha imebidi tutoe milioni 10 kwa ajili ya ku-repair ule Mradi wa Managa kukabidhi kwa BAWASA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mradi wa Nakwa milioni 800, umechakachuliwa ilibidi tulipe zaidi ya milioni 26 ndio BAWASA waupokee, kwa nini tupoteze fedha. Nashauri hivi, ni vizuri fedha wakatuletea halmashauri lakini wataalamu Experties wakasimamia watu wa BAWASA maana halmashauri zetu wameshindwa kusimamia hii miradi, inasababisha miradi inakuwa mibovu, kunakuwa na uchakachuzi mwingi, mwisho wa siku wananchi wanakosa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo niwatakie kila la heri, wanipatie fedha za Kata ya Sigino, certificate zetu watulipe, nawashukuru kwa kufuta service charge, tupo pamoja. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niseme machache katika Wizara hii kwanza niwapongeze Mheshimiwa Waziri na timu yako kwa jinsi ambavyo wanaipeleka Wizara hii iweze kusonga mbele. Piai niwape hongera sana hasa kwa kazi wanayofanya kwa ATCL wamekuwa na vituo tisa katika nchi lakini vitano katika kanda hongereni sana. Vile vile wamekuwa na destinations tano nje ya Nchi za Rwanda, Burundi, Zimbabwe, Zambia, Comoro, lakini mna matarajio ya destinations katika nchi tano Thailand, India, Afrika Kusini na China na haya wanayatekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia kwa sababu sasa wana mpango wa kuongeza ndege mbili tena dreamliner na bombardier tena ambazo zitaingia mapema mwakani hongereni sana. Pia wanafanya kazi kubwa ya kuwafundisha Marubani wetu 51, Wahudumu 66, Wahandisi 14, lakini abiria wameongeza kutoka 200,000 mpaka 300,000, hongereni sana. Naomba wasikate tama, hii kazi ni kubwa na wameitambulisha nchi yetu katika nchi zingine, jambo ambalo lilikuwa halijawahi kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, nimekuwa nikiongea kuhusu bypass ya Babati kutoka Arusha kuja Dodoma na Singida, sasa nimeona bilioni ambazo ametutengea kwa ajili ya fidia ya wale wananchi wa Babati, Mruki, Hangoni, Sigino na hii bypass inakwenda kutekelezwa, jambo ambalo lilikuwa halijawahi kufanyika hongereni sana na tunashukuru. Pia niwaombe kuhusu suala zima la uwanja wa ndege katika Mkoa wetu wa Manyara. Mheshimiwa Waziri Mkoa wa Manyara hatuna uwanja wa ndege, tumesema sana muda mrefu sana tunaomba watuwekee hata kwa changarawe, sio lazima lami kwa sasa, naomba hili walichukue kwa sababu mengi tumekuwa tukiyasema na wamekuwa wakiyachukua, naamini na hili pia watalichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri suala la malipo ya fidia kwa wale ambao mita za barabara zimeongezeka sasa, nimekuwa nikisema kwamba tunahitaji kuwafidia wale ambao nyumba zao sasa zimeathirika na zile reserve. Ni vizuri wakaliangalia hili kwa sababu neema tuliyoipata ya Babati kuunganishwa na barabara Singida-Arusha-Dodoma pia imezaa hili linguine, naamini watalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu watu wa TBA wako nao siku ya leo niwaombe pia maeneo ya National Housing yamekabidhiwa kwa TBA pale mjini, Mheshimiwa Waziri nilishamjulisha hili tunahitaji eneo la pale mjini kwa ajili ya matumizi ya halmashauri sasa na kuwapanga vijana wetu wale Wamachinga ambao wanahitaji kutumia eneo hilo naamini na hili watatupatia pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi pia barabara yetu ile inayoanzia Singe nishukuru wameiweka na inaendelea na ujenzi kila mwaka kwenda Kiteto, ni vizuri sasa wakatuongezea fedha kwa sababu itatupunguzia kilomita zaidi ya 78 kuja Dodoma. Sasa kwa sababu hii imekamilika ya Kondoa- Babati naamini hii ya Singe, Sukulo na maeneo mengine inaweza ikaturahisishia sana watu wa Babati kuelekea Dar es Salaam, hii barabara wakiikamilsha kwa kiwango cha lami jambo linaendelea sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwaombe barabara ya Dareda-Dongobeshi kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Hydom wamekuwa wakiweka, nashukuru pia wameweka hata mwaka huu, lakini sasa ni vizuri tukafikiria kuunganisha na hii inayotoka Karatu kuelekea Mbulu na Singida kwa kiwango cha lami. Nishukuru hiyo ya Karatu - Mbulu, Hydom - Singida mmeshai-cover lakini sasa hii ya Babati – Dareda – Dongobeshi - Hydom Mheshimiwa Waziri wakiweka pia itatusaidia sana. Otherwise wanafanya kazi nzuri hongereni na niwapongeze wamepokea zaidi ya asilimia 60 ya bajeti, nipongeze Wizara ya Fedha na Wizara yao na wanachapa kazi. Pia niwapongeze kwa kuwa wazalendo wameona kwamba wawe na bajeti ambayo inatekelezeka zaidi ya trilioni mbili mpaka 1.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Bima ya Afya iangalie utaratibu wa kupatia Bima Watanzania wote na bei ipungue.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Hospitali ya Mrara inahitaji ujenzi wa wodi ya wazazi na watoto. Tunashukuru kwa mkopo wa Bima ya Afya milioni 108 kwa hospitali hiyo. Tunaomba mtuongezee kwani bajeti yake ni zaidi ya shilingi milioni 800.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vituo vya Afya na Zahanati katika Kata zote za Babati Mjini vimejengwa na nguvu za wananchi, lakini hakuna fedha zozote za Serikali zimepelekwa kukamilisha maboma hayo. Tunaomba fedha za ukamilishaji maboma hayo ambayo ni Zahanati ya Singe, Sigimo, Mutuka, Himiti na Chemchem.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunaomba ambulance katika Hospitali ya Mrara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawawatakia kila la heri katika majukumu yenu.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii ambayo iko mbele yetu, na ninaomba nitangulie kuunga mkono hoja kwa asilimia 100, lakini pia niwapongeze Wenyeviti wa Kamati zote pamoja na Wajumbe ambao wametuletea taarifa hii ambayo imefanyiwa kazi kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba bado saa chache, Chama chetu Chama Cha Mapinduzi kuadhimisha miaka 43 ya kuzaliwa, naomba niendelee kuitakia kheri katika kuongoz anchi yetu na taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia mambo matano. Naomba niishauri Serikali yangu mambo matano ambayo nafikiri kwamba yanaweza yakawasaidia wananchi wetu, na nitachangia zaidi TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza niipongeze Serikali na TAMISEMI kufikia makusanyo ya zaidi ya asilimia 69 katika halmashauri zetu. Naamini halmashauri zetu zinajitahidi kukusanya. Niishauri Serikali yangu kwamba pamoja na makusanyo haya kuna sababu ya kukaa na wakurugenzi wetu ili kuangalia vyanzo vingine vya kuwasaidia zaidi waendelee kukusanya. Lakini kama tutawashauri, ni vizuri sasa TAMISEMI pia tukae na wakurugenzi tuhakikishe zile asilimia 40 za maendeleo zinapelekwa katika miradi ya maendeleo. Nasema hili kwa sababu tukikusanya tusipopeleka kwenye miradi ya maendeleo tukaiachia Serikali kuu iwe inapeleka fedha za kukamilisha maboma ya madarasa na zahanati nafikiri Serikali Kuu itazidiwa. Kwa hiyo pamoja na kazi nzuri hii inayofanywa ya kukusanya fedha hizi, lakini sasa zirudi kukamilisha maboma na zahanati ambazo wananchi wamezinyanyua zimebakia tu finishing. Kwa hiyo naamini Serikali, hili mtaliangalia kwa karibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo natamani sana niishauri Serikali. Hali za barabara zetu si nzuri sana; niombe, ifikie muda sasa wa Serikali yetu kufanya maamuzi ya dhati kwa TARURA kupewa asilimia 50 kuliko ambavyo sasa ni asilimia 30. Tunaiomba Serikali yetu iangalie hili. Sasa hivi TARURA wako site pamoja na hii hali ambayo si nzuri ya mafuriko; wamekuwa wakihangaika kutafuta moram na kuziba madaraja ambayo yamekatika. Ukweli ni kwamba kwa hizi asilimia 30 TARURA haitaweza kusaidia barabara hizi nyingi ambazo zimekatika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaelekea kwenye wakati wa bajeti. Tunaiomba Serikali iangalie gawio la 70 kwa 30, hizi asilimia zikirekebishwa naamini TARURA watafanya kazi nzuri; na hata sasa wanafanya kazi nzuri kwa asilimia 30; lakini Bunge hili tukiwasaidia TARURA wakapewa hata asilimia 30 itasaidia sana kukarabati barabara zetu. Niiombe Wizara ya TAMISEMI, sasahivi TARURA wameshaleta maoteo ya uharibifu ambao umefanyika huko kwenye barabara katika mitaa yetu, na Wizara ya Ujenzi na TARURA Taifa pia wanasema pia sasa TAMISEMI wao wameshapokea. Niiombe Serikali yangu response ya haraka sana kwa sababu katika mafuriko haya ambayo yanatokea, wananchi wameathirika, hawapiti na wanafunzi wanakwenda shule. Kwa hiyo TAMISEMI mtusaidie upesi kwamba sasa yale maoteo mliyoletewa mnaweza mkatupatia majibu lini ili wananchi kule kazi ziendelee na wanafunzi waendelee kwenda shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine la tatu ambalo nilifikiri kwamba niishauri Serikali ni suala la miradi ya kimkakati. Serikali yetu imefanya mambo mazuri sana. Niwashukuru, Mji wa Babati ni miongoni mwa miji ambayo tulipatiwa fedha za World Bank kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI pamoja na timu yako naamini si halmashauri zote wamefikisha zile kilometa 10, mfano sisi ni kilometa 10, lakini kwenye zile kilometa 10 tumetekeleza kilometa 8.2 bado 1.8. Tunaomba sasa fedha zile ziweze kufika mapema ili zile kilometa 10 ambazo ilikuwa ndiyo azma yetu tuweze kukamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, Serikali yetu iliomba tupeleke tena miradi ya kimkakati kupitia TAMISEMI kwenda Wizara ya Fedha. kwa taarifa ambazo ninazo kama ile miradi sasa haijaanza na imesimamishwa baadhi, sisi Mji wa Babati tulileta mradi wa kimkakati katika halmashauri yetu, mradi wa stendi kuu ya mabasi Babati. Tunaomba sasa tupate majibu ya haraka tuweze kujua kwamba ule mradi wa stendi unaanza lini itatusaidia sana kwa sababu pia ni hitaji letu katika mkoa wetu na halmashauri yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa ambao wamechaguliwa hivi karibuni. Nipongeze sana Chama Cha Mapinduzi kwa kushinda kwa asilimia 99. Niiombe sasa TAMISEMI kupitia waurugenzi, wahakikishe wenyeviti wetu hawa wanapatiwa semina. Wenyeviti hawa ndiyo wanaokaa na wananchi muda wote, wenyeviti hawa ndiyo wanaotatua kero mbalimbali za wananchi muda wote. TAMISEMI sasa tunaomba halmashauri zetu zielekezwe kwa sababu hao wenyeviti tukiwaacha wakafanya kazi bila kupata mafunzo inaweza ikawawia vigumu. Kwa hiyo kote nchini mafunzo haya tuiombe TAMISEMI wasimamie ndani ya muda mfupi waweze kupewa mafunzo wenyeviti na wajumbe hao wa Serikali ambao wamechaguliwa. Halmashauri wanaweza wakasema kwamba hawana fedha za kutosha lakini haop watu ni watu muhimu sana. Kwa hiyo niiombe Serikali yetu itoe kauli juu ya mafunzo ya Wenyeviti hao ambao wameweza kuchaguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo siku ya leo ningependa kuishauri Serikal yangu ni suala la TASAF. Fedha hizi zinasimamiwa vizuri katika halmashauri zetu na zinatoka kwa wakati; kwanza niwapongeze hili linafanyika lakini niombe sasa, si wazee wote au si kaya zote maskini zile zimeweza kuingia kwenye mpango. Kwanza niombe iharakishe suala zima la wale ambao hawajaingia na wanaingia katika bajeti na mpango wa mwaka huu na kuendelea huu mchakato ukamilishwe haraka ili wale wazee ambao walikuwa wamesubiri kwa muda mrefu waweze kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri pia kwa upendo kabisa kuhusu wazee wa Taifa letu. Niombe Serikali yangu tena wafikirie kuwaingiza wazee katika asilimia 10 za mkopo unaotolewa kwenye halmashauri zetu. Tumefanikiwa kwa vijana, akina mama na walemavu. Wazee hawa tukiwatengea asilimia mbili kama ambavyo tumetenga kwa walemavu, tukatenga kwa vijana na akina mama wazee hawa na wao wapate hilo dirisha naamini watafanya kazi na pia Watazalisha wataendelea kupata mitaji na wataendelea kuhudumia familia zao, kwa sababu si wazee wote ambao wanashindwa kufanya kazi. Umri wa mzee ni kuanzia miaka 60 na kuendelea; haimaanishi kwamba ukiwa mzee hauwezi kufanya kazi. Kama tumeweza kuwa-consider akina mama na vijana na walemavu, niiombe Serikali yangu kwa moyo wa dhati wazee sasa katika bajeti hii tunayoelekea waweze kupewa kwa sababu waliomba pension kwa muda mrefu lakini sasa kwa sababu hatukuwatimizia hili, tukiwaweka kwenye dirisha la mkopo wa halmashauri usiokuwa na riba itatusaidia sana kuondoa kero kwa wazee wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, mambo yangu matano nimemaliza. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba Kigosi Kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi pamoja na Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba la Igalla Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika maazimio haya mawili. Mimi naomba nijielekeze kwenye azimio hili la kupandisha hadhi mapori haya mawili ya Ugalla na Kigosi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze tu Serikali yetu kwa nia njema ya kukuza hii circuit ya Magharibi sasa kwa sekta ya utalii. Hili ni jambo jema sana kuona kwamba utalii katika nchi yetu unakuwa haubaki upande mmoja wa Kaskazini au Kusini lakini pia upande wa Magharibi wa nchi yetu unaangaliwa maana yake katika kukuza uchumi wa nchi yetu hili likipitishwa na Bunge letu tunakwenda kugusa uchumi wa wananchi wetu, lakini pia tunaongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hili kwa sababu utalii katika nchi yetu unatuletea forex zaidi ya asilimia 25 mpaka 30 forex inatokana na sekta ya utalii. kwa hiyo, tunapopandisha hadhi mapori haya mawili maana yake tunaongeza kiasi na circulation ya forex katika nchi yetu kwa sababu haya mapori sasa yanakuwa managed na TANAPA. Kwa hiyo, ni jambo jema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; katika Taifa letu, utalii inachangia Pato la Taifa zaidi ya asilimia 17.2 na mantiki yake ni nini? TANAPA wanapokuwa wana-manage sasa haya mapori ambayo yameongezwa kwa upande wa Magharibi inasaidia kukuza na kuongeza mchango katika Pato la Taifa kutoka ile 17 tunaweza tukafika 20 au 25. Kwa hiyo, ni jambo jema sana Bunge hili kupitisha mapori haya yawe chini ya TANAPA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu; utalii katika nchi yetu unachangia ajira kwa zaidi ya milioni mbili. Maana yake tutapata vijana wengi wa Magharibi na maeneo mengine ambao wataajiriwa katika sekta hii baada ya mapori haya mawili sasa kuwa chini ya TANAPA na kuwa managed. Kwa hiyo, ni jambo jema katika kuongeza pia ajira hili linaweza likawa linatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninafikiri ni la muhimu sana ni suala zima la kuboresha zile changamoto ambazo TANAPA wanapitia. Nafahamu mtu ambaye ana- manage kazi vizuri anaongezewa ndio maana TANAPA wameongezewa haya mapori mawili lakini nishauri sasa Serikali pia waangalie na zile tozo ambazo TANAPA wanakuwa wanazipitia kwa sababu tumewaongezea sasa hifadhi zinafika zaidi ya 20 sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vizuri zile tozo pia Mheshimiwa Waziri ukaziangalia zile ambazo TANAPA wanapokuwa wanatoa dividend kwa Serikali asilimia 15 wanakuwa-charged pia kodi ya asilimia 30 tena katika kile ambacho wanakichangia. Lakini wanapokuwa wanachangia miradi ya maendeleo ni vizuri pia Serikali iangalie na zile tozo zingine ambazo wamekuwa sasa wakizipitia kama changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, otherwise naunga mkono hoja, ni jambo jema sana na naamini kwamba hili litasaidia kukuza utalii katika Ukanda wa Magharibi na mwisho wa siku tuta-share keki ya Taifa kwa pamoja na vijana wetu pia watapata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho; nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri na Serikali wakati mmetuletea kwenye Kamati mlieleza kwamba wananchi wale hawataguswa na mipaka ile mlikuwa makini sana. Mimi niwapongeze sana, hili Serikali kuona kwamba wananchi wale wanakuwa hawaguswi, hawasumbuliwi na mkachora ramani kwa upya sasa ili wananchi wasisumbuliwe na naamini kwamba hili litafanyika kwa nia njema na wananchi wetu watafaidika, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) wa Mwaka 2021
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niungane na wenzangu kukupongeza sana kwa ushindi wa kuliongoza Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nifafanue maeneo machache. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia hoja za Wizara yetu kupitia marekebisho haya, lakini langu kubwa lilikuwa ni hoja ambayo imetolewa na Mheshimiwa Makamba kuhusu marekebisho tunayofanya.

Mheshimiwa Spika, nilipenda tu kuweka sawa kwamba marekebisho ambayo tunayafanya katika Wizara yetu kupitia marekebisho haya ya Sheria Ndogo, ni suala ambalo Bunge lako Tukufu lilitupitishia la Mfuko wa Maendeleo ya Michezo. Sisi kama Wizara tulilipokea kwa mikono miwili jinsi ambavyo mlitupitishia shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Michezo. Marekebisho haya yameshafanyika, ni kwamba sasa tunaingiza Mfuko huu kisheria chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT). Huko tuone kwamba Mfuko huu wa Maendeleo ya Michezo ambao Waheshimiwa Wabunge mlitupitishia wakati wa bajeti utumikaje, fedha hizi zitumike vipi, zinasaidia timu za Taifa, yaani Mfuko huu usimame kisheria na si kwamba marekebisho haya yanaendana na suala lolote la mirabaha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Salome hoja yake aliyoitoa ni nzuri, alipotoa maoni kwamba tuboreshe mirabaha na sisi tunapokea. Hata hivyo, kwa marekebisho ya leo ni suala la Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, lakini pia jambo hili tusilipuuze. Suala la mirabaha lilikuwa halijagawiwa kwa zaidi ya miaka saba ndugu zangu, wasanii wetu wamelipokea kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Spika, sasa, kama Serikali jambo hili tunalifanyia kazi na tuna mikakati mingi ya kuboresha, kwamba wasanii wetu basi wapokee gawio ambalo linastahili kulingana na kazi zao ambazo wanazifanya. Vyanzo ni vingi kama ambavyo kama ambavyo wameshauri, sisi kama Wizara tunaendelea kupokea mapendekezo, lakini hatuwezi tukapuuza jambo hili ambalo tumelifanya kwa sababu si wote ambao wanaweza wakawa wamejimudu. Kama Serikali tuna kazi ya kuhakikisha wasanii wetu wanapata haki zao, lakini pia tunawalinda tunawasaidia katika makusanyo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Salome kwamba Serikali hii ni sikivu na yeye mlango uko wazi muda wowote na Waheshimiwa Wabunge karibuni, mtuletee mapendekezo. Kwa mikakati tuliyonayo tukishirikiana, wasanii wetu watakuwa kwenye nafasi nzuri.

Mheshimiwa Spika, mwisho pia hoja hii ambayo imepongezwa ya wenzetu ambao wana uono hafifu kuweza kupata haki za kutafsiriwa vile ambavyo vimewekwa kwa njia ya vitabu pamoja na njia ya sanaa mbalimbali, ni jambo jema. Hili alilizungumzia Mheshimiwa Keisha. Naamini mapendekezo haya yakipita basi na wenzetu hao wanakuwa wako-considered. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niseme machache katika Wizara hii ya Maliasili. Niipongeze Wizara; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yake, toka moyoni niwapongeze. Mimi ni Mjumbe wa Kamati, nafahamu kazi kubwa wanayoifanya na Wizara hii imetulia. Hongera sana na hongera pia kwa ushirikiano, maana yake Mawaziri wanapowapa ushirikiano watendaji maana yake mambo yanakwenda. Hongera mno na ndiyo maana Wizara hii sasa imetulia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hili la Ngorongoro. Mheshimiwa Waziri ametuletea mchakato mzima ambao ulifanyika kwa mwaka mzima, tangu tarehe 23, Mei, 2018, ile timu aliyoiunda ya wataalam kuhusu Hifadhi yetu ya Mamlaka ya Ngorongoro. Nafikiri kwamba hata Kambi Rasmi ya Upinzani walikuwa hawana sababu ya kuandika katika ukurasa wa nane, kwa sababu Mheshimiwa Mchungaji, to be honest yeye ni Mjumbe wa Kamati, nilitegemea angempongeza kabisa wala asingeandika hiki cha Ngorongoro kwa sababu hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali yeye mwenyewe anazifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, wapitishe hiyo document mapema kwenye Baraza la Mawaziri, walete mapema tumalize mgogoro wa Ngorongoro ili mwisho wa siku ile hifadhi yetu tuiokoe. Kwa hiyo nimpongeze sana kwa hili ambalo wamelifanya na taarifa ameshaiandaa tunasubiri tu finishing.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze kwa Kamati hii ya Mawaziri ambayo Mheshimiwa Rais ameiunda na kazi inaendelea. Nafikiri ni vizuri sample size ikaongezeka, maeneo mengi hayajafikiwa kama ambavyo Wabunge wengine wamesema. Kuandaa hii taarifa ni jambo moja lakini naamini matatizo hayafanani; matatizo ya Tarangire na vijiji vile vitatu hayawezi yakafanana na maeneo mengine. Niombe kama taarifa hii sasa haijafanyiwa finishing, waongeze sample sizes zao ili vile vijiji ambavyo havijafikiwa viwe treated kwa maeneo yao na matatizo yao. Hilo naamini wanaweza wakalipokea maana ni concern ya Wabunge wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo nahitaji kuwapongeza ni suala zima la mchakato waliouanza wa kurekebisha Kanuni ya Fidia au Kifuta Machozi ya mwaka 2011. Nimekuwa nikilizungumzia hili kwa muda mrefu sana, nimwombe; kabla hajafikia finalization ya kanuni hizo waweze kufika Babati Mjini kuhusu wanyama ambao kwenye ile kanuni ya mwanzo walikuwa wanasema siyo wanyama waharibifu na siyo wakali, hawawezi waka-attack binadamu na boko wamekuwa kwenye kundi hilo, waje waone kwa sababu tuna watu zaidi ya 28 waliopoteza maisha, siyo kwenye Ziwa Babati tu, lakini wakiwa mashambani ambao wamekuwa attacked na wale viboko.

Mheshimiwa Nabu Spika, sasa niombe kabla hawajamaliza kanuni hizo, ambazo wako kwenye mchakato na nawapongeza, naomba wafike Babati waone waathirika na wahanga wa viboko ambao kwenye kanuni tunawa- define kwamba hawa hawana madhara na wananchi hawahitaji kufidiwa. Kwa hiyo kabla hawajamaliza niwaombe wafike ili tuone ni jinsi gani na hawa wahanga wanaweza kufidiwa. Nina majina yao nimeshapeleka ofisini kwao, tunafikiri kwamba sasa wana sababu ya kulitazama hilo kwa upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, na la mwisho kwa siku ya leo nikuombe Mheshimiwa Waziri; Hifadhi ya Tarangire inafanya vizuri hata kwenye collection tunaona, kwenye mapato inafanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spia, lakini tuna mageti matatu, kuna geti la kibaoni kilomita sita kuingia Hifadhini ambapo watalii wengi wanatoka Arusha wanaingia hifadhini na kutoka. Pia tuna geti la Sangaiwe ambayo ina kilomita nane, vilevile tuna geti la Babati mjini Mamire to Tarangire kilomita
17. Nikuombe Mheshimiwa Waziri kupitia hifadhi ya Tarangire na Wizara yako muone jinsi gani ya kufanya maintenance ya malango yote haya matatu kwa sababu wakiingilia kibaoni Minjingu wakatokea geti la Mamire wakaingia Babati Mjini, ni mahali salama zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Babati tuna hoteli nzuri ambazo naona hata Dodoma hazipo, nzuri kabisa, lakini pia hali ya hewa Babati ni nzuri, tuna ziwa Babati ambako hata hao watalii Mheshimiwa Waziri wanaweza kuja kutazama hawa viboko. Pia tuna mlima Kwaraa ambapo pale watalii wanaweza wakapanda. Tuna maji ya moto Kiru, tuna maji ya mungu Singu na wakilala pale Babati inaweza ikawa exit yao kuja Kondoa kuangalia mambo mengine hapa Kondoa ambako mnayo kwenye Wizara yenu. Kwahiyo niwaombe mlitazame hili kwa upya, badala kutumia milioni 600 kwenye barabara ya kilomita sita ya Kibaoni tu mkatumia milioni 600 ku-maintain ni vizuri pia mka-maintain malango haya matatu…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisa kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa afya njema siku ya leo na kupata nafasi katika Bunge lako Tukufu. Pia nitoe pole katika familia ya mwenzetu Mheshimiwa Nditiye kwa msiba ambao umetukumba. Nasi sote ni njia yetu, zaidi sana ni kuombeana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba nijibu hoja kadhaa za Wabunge ambazo wamezitoa wakati wanachangia Mpango na zaidi ya Wabunge 25 walichangia katika Wizara yetu. Sisi tumepokea kama Wizara, maoni ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wameyatoa kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa uvuvi, kwa sababu muda ni mchache, niende moja kwa moja; nitakuwa nakwenda kwa hoja zile ambazo zimesemwa kwa ujumla wake; lakini zile ambazo pia zinahitaji majibu, Wizara yetu iko tayari kujibu kwa maandishi na kuwapatia Waheshimiwa Wabunge pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kubwa kwa upande wa uvuvi ilikuwa ni kuboresha uvuvi wa bahari kuu. Katika Mpango huu, Serikali imejipanga; tunafahamu kwamba tuna Mpango wa Miaka Mitano na Mpango wa Mwaka Mmoja. Wizara yetu imebahatika katika Mpango huu wa Mwaka Mmoja kuingiza mambo kadhaa ambayo yakienda kuanza sasa yatakwenda kuboresha uvuvi wa bahari kuu. Jambo la kwanza ni suala la ujenzi wa bandari kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe, Serikali ilishaanza upembuzi yakinifu kuangalia maeneo mbalimbali ambayo Bandari ya Uvuvi itajengwa. Pia Serikali ikishirikiana na wenzetu wa Italia wameshaanza na zaidi ya Shilingi za Kitanzania bilioni 1.4 zilitengwa na shilingi milioni 700 zilishalipwa kwa kampuni hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upembuzi yakinifu, eneo la bandari ambalo sasa Serikali tunaenda nalo ni eneo la Bagamoyo pale Mbegani. Kazi hii inaendelea. Muda wowote upembuzi yakinifu ukikamilika sasa tunaenda kuwa na actual design ya bandari hii na kazi hii ianze ili tunapoenda kwenye uvuvi wa bahari kuu, bandari iwe imeshaanza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi walichangia ni suala la ununuzi wa meli, kwamba tunapokwenda sasa kwenye uvuvi wa bahari kuu Serikali ihakikishe kwamba tunajipanga kununua meli zetu. Bahati nzuri wenzetu wa IFAD katika Mfuko ule wa Maendeleo wa Kilimo pamoja na Mifugo na Uvuvi wameshatukubalia kwamba watatupatia fedha kwa ajili ya ununuzi wa meli hizo na meli hizi nane; nne zitakuwa upande wa Zanzibar na nne zitakuwa upande wa Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Zanzibar wameshatoa vigezo, wanahitaji meli za namna gani, nasi Bara tayari tunafahamu ni meli za namna gani, kwa vipimo vipi. Pia wenzetu hawa watatupatia Dola za Kimarekani milioni 58 ambazo sasa sisi Uvuvi tutakuwa na gawio letu hapo kwa ajili ya ununuzi wa hizi meli. Kwa hiyo, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba kazi hii inaanza sambamba ikiendelea na upande wa ujenzi wa bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kazi hii itakapoanza, pande zote mbili za nchi yetu watashirikishwa. Pia usimamizi huu utaendelea kufanyika na mamlaka ya uvuvi wa bahari kuu ambayo sasa inaendelea na kanuni zake tumeshazitunga, tunasubiri Mawaziri wa pande zote mbili waweze kusaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa jumla kuhusu uvuvi, kulikuwa na tatizo la tozo. Kwamba wavuvi wetu wengi wanahangaika na tozo, lakini maeneo mengine inawezekana hawatendewi haki. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kuhusu suala la kanuni zetu ambazo tumezitunga za mwaka 2020 ambapo maeneo mengi zimekwenda kugusa wavuvi na zimesababisha sintofahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijulishe Bunge lako Tukufu kwamba Wizara hii ni sikivu; Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara, tumeangalia kwa upya kanuni hizo, lakini pia yale maeneo ambayo yalikuwa yanasumbua wavuvi, mfano uvuvi wa ring net katika bahari kuu, tumeyafanyia kazi nanyi mmeona. Kwa upande wa Tanganyika, suala la wavu wa dagaa, tumefanyia kazi na tuliwashirikisha pia. Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha taratibu masuala ya uvuvi na tutawashirikisha Waheshimiwa Wabunge; na baada ya Bunge pia tutafika kwenye maeneo yenu ili pasiwepo na matatizo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwa upande wa mifugo. Kwa upande wa mifugo, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia kwa upana wake, suala la Serikali kuwekeza katika mifugo. Tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge katika maoni yao tuliyoyapokea wamehitaji Serikali iwekeze katika ujenzi wa miundombinu ya mifugo kote nchini. Sisi kama Serikali, tumejipanga, kwa kuanzia tu, tumeita kikao cha wadau wote ambao wanajihusisha na uzalishaji na uchakataji wa nyama. Tuna viwanda kama tisa katika nchi yetu. Nafahamu kwamba hoja kubwa ni kuangalia hizi tozo ambazo zinasababisha viwanda vyetu vinashindwa ku- perform waki-compete na nchi za wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeshapitia hizo tozo na katika Bunge lijalo la Bajeti, tutapendekeza mabadiliko mbalimbali ili kuhakikisha mifugo yetu inachakatwa ndani ya nchi. Haturidhishwi ng’ombe, mbuzi na kondoo kutoroshwa. Mwaka 2019/2020 tulikuwa na ng’ombe milioni 1.4 wanatoroshwa au wanasafirishwa wakiwa wazima kwenye nchi za wenzetu, halafu wao wanachakata, wanauza hizo nyama wakati ng’ombe wametoka kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi tozo tutazipitia kwa upya tuone kiasi gani tunaweza kuzirekebisha ili viwanda vyetu vya ndani viweze kufanya kazi sawa na viwanda vya nchi za wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwa upande wa mifugo ni suala la kuongeza malisho. Wizara katika kuhakikisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kutupa afya njema siku ya leo kutimiza wajibu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia kwa niaba ya Waziri wangu, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, nimshukuru Mheshimiwa Rais kuendelea kutuamini tuweze kuhudumu katika Wizara hii muhimu ya Sanaa, Utamaduni na Michezo. Mheshimiwa Rais tunakushukuru sana pamoja na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ni Wizara mtambuka, ina sekta tatu, inagusa maisha ya Watanzania lakini ajira kwa vijana wetu. Nishukuru Kamati yetu ya Bunge ya Huduma za Jamii chini ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti pamoja na Wabunge wenzetu, wamekuwa wakitushauri kwa dhati namna gani tunaweza tukafanya vizuri katika sekta hizi ambazo ni muhimu kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi nimshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wamekuwa wakituelekeza tufanye nini kwenye sekta ya sanaa, sekta ya michezo na sekta ya utamaduni. Nianze kwenye sekta ya utamaduni; Kamati kwa ujumla imezungumzia mambo matatu, imezungumzia suala la BMT, suala la Bodi ya Filamu na BAKITA, nami nitajikita huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa utamaduni nishukuru sana jitihada ambazo anazifanya Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan. Rais wetu wakati anakuza diplomasia ya uchumi pamoja na wasaidizi wake wametusaidia sana kwa upande wa utamaduni na kwa upande wa kukuza Kiswahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana UNESCO imetangaza Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 7 Julai. Hizi ni jitihada za Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan, pamoja na wasaidizi wake. Sisi Wizara tunawashukuru kwa sababu kazi yetu inakuwa imerahisishwa na viongozi wetu na wamekuwa wakitupa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo halitoshi, chini ya Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan tumeona juzi tarehe 6, mwezi huu wa Februari wakati Makamu wa Rais akituwakilisha, akimwakilisha Mheshimiwa Rais wetu katika vikao vya Wakuu wa Nchi na Serikali katika Makao Makuu ya Afrika, pale Ethiopia, Makamu wa Rais alipeleka maombi maalum kwa niaba ya nchi yetu na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wetu kwamba Kiswahili sasa iwe lugha ya kazi. Mheshimiwa Rais tunakushukuru sana na AU waliridhia hili. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu, hii ni hatua kubwa sana kwa Taifa letu lakini pia kwa sekta yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge na sisi tumefanya nini? Kwa kuwa mmezungumzia kupitia Kamati hii, kazi ambayo tumefanya, tumeielekeza BAKITA – Mheshimiwa Waziri Mkuu tunamshukuru sana, alikuwa BAKITA juzi, ametupa maelekezo mahususi. Sisi na BAKITA tumeandaa mpango mkakati wa kubidhaisha Kiswahili wa miaka kumi, kuanzia 2021 mpaka 2031 ambao una thamani ya bilioni 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii inaendelea chini ya BAKITA, dada yetu Consolatha na timu yake wanafanya kazi nzuri na hata balozi mbalimbali wameshaanza kupata wataalam kupitia BAKITA; Ubalozi wa Korea Kusini, Nigeria na Balozi zingine kazi hii imeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kazi hii tunaifanya kwa kasi kubwa na tunaamini pia kadri ambavyo wanatupitishia bajeti kazi hii itakuwa rahisi sana. Hii ni heshima kwa Taifa letu na tunaomba tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa kazi hii ya kubidhaisha Kiswahili na kutuelekeza na tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu na kubwa, tunamshukuru pia Makamu wa Rais kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine lilikuwa ni suala la Baraza la Michezo (BMT). Kamati imeshauri mambo kadhaa na wamekuwa wakitushauri sana kwa upande wa michezo. Wametushauri tuongeze mahusiano na Serikali za Mitaa, ma- DAS na ma-RAS wetu ni Wenyeviti katika Mikoa yetu kusimamia michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati wamezungumzia pia kuhakikisha utawala bora unapatikana katika vyama na vilabu vya michezo. Kwa niaba ya Waziri wangu, Mheshimiwa Mchengerwa, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba. kazi hii tunafanya, na tumekuwa tukifanya vikao na Maafisa Utamaduni na Maafisa Michezo, lakini ma-RAS na ma-DAS wetu tukipeana maelekezo nini cha kufanya kuboresha michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisipowapongeza Waheshimiwa Wabunge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikushukuru kwa nafasi, pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kutupa nafasi hii tena, kutupa afya njema kuendelea kutekeleza wajibu wetu katika wizara hii. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa maelekezo yake, Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameendelea kutupa imani sisi wasaidizi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nita-respond kwenye mambo machache. Jambo la kwanza nimshukuru Mheshimiwa Neema Lugangira kwa mchango wake. Ametoa ushauri mzuri kwa Wizara yetu; na kubwa zaidi ametoa ushauri kwamba wakati tunarekebisha sheria hizi za vyama vya siasa basi Tume yetu ifanye kasi kuleta marekebisho hayo na tuweze kuyaleta. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ukiangalia bajeti zetu hapa miongoni mwa kasma ambazo zimetuongezea fedha katika Tume yetu hii ya kurekebisha sheria ni pamoja na kazi hizi kumalizika na Tume yetu ilishamaliza utafiti katika sheria hizi za uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Neema, Mbunge, mawazo yako hayo ni mazuri na yataendelea kuzingatiwa pale ambako tutaleta sasa marekebisho haya basi tutaendelea kuboresha; lakini kwa sasa kama wizara tumechukulia serious na ndio maana katika bajeti ya Tume kumekuwa na ongezeko la fedha ili kazi hizi ziendelee. Pia tunawapa kipaumbele kwa kuwa tunaelekea kwenye mwaka wa uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu sheria hizi ziangaliwe kwa jicho la karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge pia ametushauri katika suala zima la katiba mpya kwamba ushirikishwaji wawe wazi, asasi mbalimbali zishirikishwe, NGO’s na taasisi zingine na wananchi kwa ujumla washirikishwe. Hili ni la msingi, ndiyo maana tumekuja kwenye Bunge hili mkiona kwenye bajeti zetu kuna ongezeko kwa ajili ya kazi hii ya mchakato wa katiba na ni fedha kubwa. Tushukuru Bunge hili kwamba mmeliona hilo kuanzia kwenye kamati lakini Mheshimiwa Rais wetu Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan. Kazi hii itakapoanza tutashirikisha kote Bara pamoja na zenzetu wa Zanzibar, wananchi watatoa maoni yao mchakato utakuwa wa wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la viongozi wetu wa Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Mbunge amelizungumzia; kwamba wasiondolewe kienyeji. Kwa sasa taratibu ziko wazi kabisa chini ya Serikali zetu za Mitaa, chini ya Ofisi ya DC akisadiwa na makatibu tarafa jambo hili limekuwa likifanyika kwa kufuata taratibu, Mwenyekiti wa Kijiji au Mtaa haondolewi tu bila utaratibu. Lakini katika marekebisho na maboresho haya ambayo yanaletwa na Tume basi tutaliangalia kama kuna mapungufu, lakini kwa sasa utaratibu uko vizuri na wananchi wanashirikishwa. Tunafahamu mkutano mkuu wa kijiji unakuwepo lakini taratibu hizo zinasimamiwa na ofisi zetu za wakuu wa wilaya na mambo haya yamekuwa yakifanyika kwa uwazi ili mtu pia ajitetee kama anatuhumiwa kwa jambo lolote lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jesca amechangia kwenye Tume yetu ya Haki za Binadamu na umuhimu wa Tume hii. Tume hii ni muhimu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema. Tume hii imekuwa ikifanya kazi zake. Naomba nimrifae (to refer) Mheshimiwa Mbunge katika ukurasa wa randama yetu kazi ambazo tume imefanya ukurasa wa sita mpaka saba, pale utaona kazi ambazo Tume imefanya. Pale ambako kuna ukiukwaji wowote wa haki za binadamu Tume hii haijafungwa mikono na imekuwa ikifanya kazi zake siku zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, good enough taarifa zake tumeshazikabidhi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu zitaletwa kwenye Bunge hili hakuna ambaye anazuia Tume hii isilete taarifa katika Bunge hili. kwa hiyo baada ya Tume kutukabidhi hizi taarifa kama Wizara taarifa hii tumekabidhi Ofisi ya Waziri Mkuu na taarifa hizi zitaletwa katika Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ni suala la bajeti ya Tume hii. Mheshimiwa Mbunge Agnesta amelizungumzia kwa kina, kwamba tume hii haipati fedha ipasavyo. Ukiona kwenye disbursement ya fedha kwa mwaka huu unaondelea Tume imepata zaidi ya asilimia 60, yaani kwenye disbursement wamepata fedha na ndiyo maana wamefanya kazi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika increment za bajeti kwa miaka mitatu mfululizo Tume hii imekuwa ikiongezewa fedha ili iweze kufanya kazi zake ipasavyo. Na tumeona, miaka mitatu mfululizo bajeti yao ilikuwa five billion, lakini mwaka uliofuata six billion, mwaka huu Bunge lako Tukufu litakaporidhia, na tunashukuru kamati zimeridhia bajeti hii ya ongezeko kwa Tume, Tume imepitishiwa zaidi ya eight billion ambayo kwa kweli sisi kama wizara tunafahamu umuhimu wake. Kimsingi ndiyo maana tunaona katika nyongeza za bajeti Tume hii haijaachwa. Kwa hiyo nimwakikishie Mheshimiwa Jesca kwamba Tume hii itaendelea kufanya kazi zake kwa umakini pia Serikali na Wizara tumekuwa tukiangalia kwamba inapata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwamba fedha za maendeleo ni kweli lakini Tume haisimami peke yake. Wizara hii tuna taasisi nyingi tumekuwa tukishirikiana katika miundombinu. Tume haijakwama kazi zake kwa kuwa haina miundombinu, ndiyo maana hata kwa upande wa Zanzibar Tume ina ofisi zake. Kwa hiyo kadri tunavyoendelea kupata fedha na kutenga fedha kwa ajili ya Tume hii na hata miundombinu tutaendelea kurekebisha vile ambavyo bajeti itaendelea kuruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kuunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuweka mawazo yangu katika muswada huu muhimu kwa maslahi ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye muswada nikihitaji ufafanuzi labda ni-declare tu interest, mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo, lakini kwa sababu hiyo sikatazwi pia kuweka mawazo yangu katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate ufafanuzi. Suala la kwanza, mwanzoni tulikuwa na utaratibu kwamba taarifa zie za uthamini zinapokuwa zimeshakwenda kwa ngazi za juu, kunakuwa na nafasi za Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa inaporudi wana-verify pia, lakini katika muswada huu hawajatajwa popote. Sambamba na hilo, naomba nifahamu tu kama sasa nafasi zao pia hazipo, lakini pia huyu mwananchi akate rufaa wapi pale ambapo anakuwa hajaridhika na uthamini ule?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Wizara itusaidie kujibu; kuna wananchi wengi ambao kwa muda mrefu sasa leo tunatunga hii sheria wao wamekuwa wakisubiri fidia zao hazijalipwa kwa muda mrefu na hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani imesema kwamba kuna wale ambao wanasubiri fidia katika maeneo ambayo yametengwa kwa akiba ya barabara na maeneo mengine; hawa watu wamekaa kwa muda mrefu hawajalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya sheria hii kupitishwa, sawa mtapata ule muda ambao unapandekezwa na baadaye Bunge tutapitisha, hao wengine wanachukuliwa wapi au wanakuwa wamesahaulika? Napenda kufahamu kwa sababu wako wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye vifungu vya Muswada huu, katika kifungu cha 7(1). Kifungu hiki kinasema; “Iwapo Mthamini Mkuu ameridhika kwamba uthamini haukufanyika ipasavyo, atapendekeza kwa mamlaka husika nidhamu na hatua zinazopaswa kuchukuiwa dhidi ya Mthamini aliyesajiliwa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mawazo yangu, ni vizuri sasa kwa sababu tunatunga sheria, tukaweka adhabu wazi wazi. Mheshimiwa Waziri ulikuwa umeeleza katika hotuba yako kwamba nia ni njema, kulikuwa na Wathamini wanafanya ndivyo sivyo na vitu kama hivyo, ndiyo lengo mahususi la muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini mnataka kumwachia Mthamini Mkuu apendekeze hatua na kwa nini tusiweke sasa kwenye muswada huu au kwenye sheria hii kwamba huyu ambaye amekuwa akifanya under valuation kwa watu wetu na mali zao; huyu mtu adhabu yake iwe ni kiasi hiki? Kwa nini tumwachie Mthamini Mkuu yeye apendekeze? Hiyo mamlaka husika inaweza isimwadhibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza tu au nashauri kwamba hii adhabu tuiweke kwa sababu tunatunga sheria hii pia kulinda watu wetu ili zile thamani za majengo yao na hadhi zao zisichezewe hovyo hovyo na hawa Wathamini. Kama lengo ni kuwabana hawa Wathamini, basi tupendekeze adhabu na tusiache hivi ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kifungu cha 52; Mheshimiwa Waziri amependekeza kutoka kile ambacho mwanzoni kiko kwenye kifungu cha 52 kwamba muda Waziri atabainisha, lakini umeenda kwenye miaka mitatu katika suala zima la kulipa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba huu muda ambao wananchi wetu wanasubiri fidia usiwe zaidi ya mwaka mmoja na tunafahamu kwa muda mrefu sana kwamba wananchi wamekuwa wakitwaliwa maeneo yao, lakini wanasubiri kwa muda mrefu, hawapati hizo fidia; tuwasaidie pia kwa sababu hii ardhi ndiyo rasilimali pekee Mtanzania anayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomwacha kwa miaka mitatu akisubiri fidia hiyo, anaweza akawa amesha-mess-up na hajui kwamba afanye nini. Baadaye unakuja kusema kwamba unamlipa au haumlipi, wakati huo umeshampotezea muda kama hao wa reserve ya barabara tumewaacha sasa, hawajalipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napendekeza kwamba endapo ardhi imetwaliwa, lakini huyu mtu baada ya mwaka mmoja hahitaji tena ardhi hiyo, basi alazimike kama ni ile interest ambayo ina-accrue baada ya miezi sita, ilipwe hata kama haihitaji ile ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hivi kwasababu zifuatazo: kuna baadhi ya watu binafsi ambao labda wanataka kujenga shule au taasisi fulani, wanataka kuwekeza kitu fulani, anahodhi ardhi ya wananchi kwa miaka miwili, mitatu au minne kama tutapitisha mwaka mmoja au kama mtapitisha pia kwa wingi wenu hiyo miaka mitatu mnayoipendekeza, lakini kuna watu watatumia ardhi hizo, atakaa nayo, hajalipa fidia, baadaye anasema siihitaji tena ardhi hiyo. Huyu mwananchi anakuwa katika hali gani? Miaka mitatu umempotezea muda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashawishi Bunge hili kwamba pia tuweke charge fulani kwa mtu atakayehodhi hiyo ardhi kwa lengo la kutaka kuendeleza, lakini baadaye aka-reject, akawarudishia wananchi, asiseme tu ardhi yenu hiyo hapo, sihitaji kuwalipa tena fidia kwa sababu siihitaji na siitumii tena. Tuwalinde hawa wananchi ambao watakuwa wamapotezewa muda, angalau awajibike hata some amount aweze kulipa ili tuepushe wimbi kubwa la watu ambao watahodhi ardhi, baadaye wanawarudishia wananchi wakati wameshawapotezea muda na wameshindwa kuendeleza ardhi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwamba miaka mitatu ni miaka mingi sana, kama lengo ni kuwasaidia Watanzania, Mheshimiwa Waziri akubaliane na maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba isiwe zaidi ya mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niende kwenye kifungu cha 55; hiki kifungu kinasema, Mthamini aliyesajiliwa endapo atataka kuingia kwenye eneo lolote au kwenye jengo lolote lile, hatakiwi kukataliwa. Pia Mheshimiwa Waziri akaleta marekebisho katika jedwali lake kwamba aweze kutoa taarifa; inaweza ikawa ya maandishi au taarifa yoyote ile. Niongezee kwamba iwe ni kwa ridhaa ya yule anayehodhi eneo hilo, iwe ni ardhi au jengo, kwa sababu taarifa inaweza isimfikie kama hajatoa ridhaa kwamba nakubali tukafanye uthamini wa haya niliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Waziri, kuna Wathamini watakwenda watasema mmiliki anafahamu, lakini hawa wamiliki hawafahamu. Nitoe mfano mzuri wa wananchi wa Jimbo langu la Babati Mjini eneo la Bagara Ziwani, Mheshimiwa Waziri analifahamu sana. Wale wananchi walithaminiwa maeneo yao bila wananchi wengi kufahamu hata kama Wathamini wameingia kwenye maeneo hayo, wakabaki kuwafukuza kwa silaha. Maana yake ni nini? Wakaja wakatoa taarifa ya uthamini ekari ifidiwe kwa shilingi 240,000. Wananchi wengi wakakataa kuchukua zile fidia kwa sababu haikuwa ridhaa yao pia na hawakushirikishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika kifungu hiki cha 55, iwe pia pamoja na taarifa ya maandishi, pawepo na ridhaa ya mwenye mali hiyo, iwe ni ardhi au jengo kwamba sasa hili lifanyike. Tusipofanya hivyo, taarifa zitapikwa mezani na baada ya hapo wananchi watakataa na mchakato wa fidia utachukua muda mrefu sana na matatizo yatakuwa mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upesi upesi kifungu 55(2), nipendekeze kwamba hiki kifungu tukifute kabisa na tufanye vice versa. Kinataka mtu ambaye amekataa kwamba eneo lake lisithaminiwe, hajatoa ushirikiano, kifungu 55(2)(d) inapendekeza adhabu, kwamba atatozwa fine isiyopungua shilingi milioni moja na isiyozidi shilingi milioni tatu au kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miezi 24 au vyote kwa pamoja; fine na kifungo. Naomba hii adhabu iwe nikwa hao Wathamini. Watakapokuwa wamekosea…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru nitaleta amendment.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2018
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika nakushukuru kunipa nafasi nichangie machache katika hii Miscellaneous Amendments. Nitachangia maeneo matatu naomba nijiekeze kwenye eneo la kwanza nalo ni eneo la
Amendment ya Statistics Act hiyo Cap ya 351 kwenye kifungu cha 31 ambacho kinarekebishwa hicho ambacho kinafanya marekebisho ya 24 A(1) na (2), mimi nijielekeze kwenye (2) inasema hivi: “A person shall not disseminate or otherwise communicate to the public any statistical information which is intended to invalidate, distort or discredit official statistics.” Pia hoja ni kwamba hizi statistical information ni zinatokana na census surveys or administrative data.

Mheshimiwa Spika, sikuona sababu sana ya Serikali kuleta marekebisho haya, binafsi naona labda Serikali inakuwa iko feared kwamba watu mbalimbali wanapotoa takwimu mbalimbali huenda haziwapendezi sana ndiyo maana wanataka kuweka kapini kuzuia haya. Sanasana hofu yangu iko kwenye administrative data ambazo zinatolewa mara kwa mara na huenda haziwapendezi sana wenzetu wa Serikalini ndo maana wanayaleta haya.

Mheshimiwa Spika, hizi statistical data ambazo zinatoka kwenye National Bureau of Statistics siyo kwamba zote wakati wote ni sahihi. Sasa wanapotaka kuleta marekebisho ya sheria kwamba mtu anapokuwa ana invalidate au ana distort au ana discredit official statistics wakati zina makosa Mheshimiwa Waziri sidhani kama ni solution sahihi sana kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri Serikali ikawa na open minded kwamba mtu anaweza akakosoa, lakini wakarekebisha kwa data zao. Niwape mfano kwenye National Bureau of Statistics ya kwenye Tanzania in figures ya mwaka 2016, naamini Mheshimiwa Waziri ata-refer na ata-confirm hili, Mlima Hanang na bahati nzuri ni mzaliwa wa Hanang nafikiri ana original huko, Mlima wa Hanang anaufahamu uliko Mheshimiwa Waziri. Kwenye National Bureau of Statistics wanasema mlima huu uko Arusha. Hizi ni data ambazo wamekusanya ziko kwenye figure zenu, lakini wanasema mlima huu upo Arusha. Mlima Hanang Mheshimiwa Waziri anaufahamu mwenyewe, ndugu zake wanakaa huko, uko Manyara, uko Kateshi, uko Hanang. Hata hivyo, kwenye hizi data ambazo ni official zimeshafanyiwa research na ziko chini ya hii Bureau wanasema Mlima Hanang uko Arusha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafikiri ni vizuri Serikali isiwe inaleta marekebisho kama haya kutafuta tu ku-pin Watanzania wasiongee na kutoa takwimu zao; ambazo kimsingi wao kama Serikali wanapaswa kuzirekebisha tu hakuna ugomvi wowote pale anapokosea. Siyo mpaka kuweka adhabu na vitu kama hivyo kuwatisha watu. Labda otherwise waniambie ni kwa sababu ya TWAWEZA walivyotoa takwimu kwamba umaarufu wa Rais umeshuka kutoka 90 mpaka asilimia 55, sasa hofu inaingia kuweka mazuio tu ambayo hayana maana yoyote. Kwa hiyo, binafsi naona sababu ya hili na sijui kwanini mnaleta.

Mheshimiwa Spika, nijielekeze kwenye jambo la pili ambalo nataka kuchangia kuhusu suala zima la haya Mabaraza ya Ardhi. Haya mabaraza yamesaidia sana kwenye maeneo mengi. Tatizo lililopo ukiachilia mbali hizo rufaa ambazo lazima waende juu zaidi, tatizo ambalo lipo kwenye haya mabaraza tunafahamu kwamba staffing yake hairidhishi. Pia Wenyeviti wa Mabaraza haya kwenye Wilaya siyo Wilaya zote, juzi tu wiki iliyopita Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi alijibu kwamba, hata kule kwetu Manyara mfano sasa wana mpango wa kuanzisha mabaraza haya Mbulu. Muda wote mkoa mzima ulikuwa unahudumiwa pale Babati.

Mheshimiwa Spika, Mabaraza haya kwenye Kata hayajawa strengthened, siyo Kata zote ambazo tuna Mabaraza haya ya Ardhi, lakini hata uendeshaji wao na mafunzo ndo tatizo; nilifikiri kwamba Serikali badala ya kufanya, hili ambalo wamelifanya binafsi sioni kama ni baya kwamba sasa wanataka Mahakimu Wakazi watusaidie katika kushughulika na hizo rufaa, sioni kama ni tatizo. Tatizo langu ni kwamba tunahangaika na vitu vidogo lakini hatu-address tatizo lililopo kwenye Mabaraza ya Ardhi.

Mheshimiwa Spika, kwenye mabaraza haya Wenyeviti wao hawana uhakika wa ajira zaidi ya uteuzi ambao unafanyika na Waziri. Hata hivyo, lakini pia tunachukua muda mrefu sana mfano kwenye Baraza letu la Wilaya ya Babati, Mwenyekiti amestaafu miezi kadhaa iliyopita mkataba umekwisha, lakini katika renewal ya mkataba wake kuna kuwa na umbea mwingi, kuna kuwa na fitina nyingi, kunakuwa na figisu nyingi, kuna kuwa na tuhuma nyingi, kuna kuwa kuchomekeana, kwa sababu labda Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa amesema hii kesi peleka hivi unavyotaka anapowakatalia kwa mujibu wa taratibu na sheria basi sasa katika uteuzi wake memo nyingi zinapelekwa kwa Waziri kwamba huyu asiteuliwe na wanachi wanakosa haki zao.

Mheshimiwa Spika, nafikiri niungane na Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba ni vizuri hao Wenyeviti ajira zao zikaangaliwa kwa upya wapewe katika terms za permanent badala ya hiyo mikataba ambayo wakati mwingine inasababisha kesi zinasimama, lakini wakati huohuo uteuzi unakuwa haufanyiki mapema. Ushauri wangu ni kwamba, ni vizuri kwa sasa Serikali itenge fedha nyingi ili ianzishe mabaraza haya katika wilaya zote itasaidia sana kui- easen haya matatizo ambayo tunayapata.

Mheshimiwa Spika, ushauri ambao nataka kutoa pia kama tatizo ni hizi kesi za ardhi, hebu Wizara ya Ardhi tuitengee bajeti ya kutosha ili maeneo mengi yapimwe, migogoro hii ni kwa sababu maeneo mengi katika nchi yetu haijapimwa bado. Hatimiliki za kimila zinatolewa kwa uchache sana, lakini hatimiliki za viwanja na maeneo mengine ni tatizo kwa maeneo mengi na upimaji unakuwa haujafika maeneo mengi. Kwa hiyo tatizo la kuwa-address pamoja na kwamba sasa referral wanazileta kwenye kwa Mahakimu Wakazi ni vizuri pia wakatenga fedha ili haya yakafika mwisho. Nilitamani kushauri mengi sana kwenye eneo hili lakini naona kama muda wangu hautoshi naomba niende kwenye jambo la tatu.

Mheshimiwa Spika, kwenye jambo la tatu, nataka nizungumzie hizi Mobile Courts au Special Courts wamechomoa kipengele hiki wamefanya vizuri; lakini ni vizuri watujibu. Zile gharama ambazo zilikuwa zimeshatumika kununua magari maana tunasikia walishayaandaa. Hayo magari sasa wanayapeleka wapi? Hii ni hofu yangu tu kwamba, ni vizuri wakati mwingine Bunge letu tukajiangalia kwamba Serikali inakuwa imeshafanya mambo yake, wanataka sisi tuwe rubber stamp, wanataka sasa walazimishe vitu kama hivi wakati wao walishafanya maamuzi na inasemekana na hizo van wameshazinunua na sidhani kama Bunge hili tuliwapitishia hiyo bajeti, sasa watuambie wanazipeleka wapi?

Mheshimiwa Spika, hofu yangu nyingine, kama walikubaliana nasikia huko wanavyojadiliana kwenye Kamati walishakubaliana mpaka kushusha zile small claims mpaka milioni 70, lakini mpaka wameshakubaliana hatua ya kuruhusu ma-advocate waweze kuhusika, sasa nini kimewafanya wachomoe? Kwa nini waondoe wakati walishakubaliana? Isije ikawa wanataka kutumia uchochoro wa Chief Justice kupitia kanuni wakaanza ku-practice hiki kitu wakati huo wameshatuambia kwamba sasa wameondoa, wanaangalia mlango mwingine wa ku- practice hiki kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ilifikia hatua ya nia mbaya kiasi hiki kwamba inafikia kwenye nchi hii mtu tu unaweza ukashtakiwa ukanyimwa haki ya kutokuwa na Wakili kukuwakilisha, yaani hata tu kuthubutu kuwa na nia mbaya kiasi hicho…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nami niweke mawazo yangu katika sheria hii, Finance Bill ya mwaka huu ambayo inakwenda kukusanya kodi katika vyanzo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Kamati ya Bajeti kutoka moyoni. Wamefanya kazi kubwa sana ya kizalendo usiku na mchana bila kuchoka. Kwa mara ya kwanza nimeona Kamati hii haikuleta tu taarifa yake, lakini imeleta na schedules za amendments.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa namalizia kuipongeza tu hii Kamati. Niseme kazi waliyoifanya ilikuwa ni kazi ya kizalendo kwa sababu, pamoja na tofauti zao na Serikali, wakabaki na msimamo kwamba hayo kwa maslahi ya wananchi tunatamani yawe hivi. Nawapongeza kutoka moyoni. Nami nafikiri pia Mungu tu anaweza akawalipa kwa haya waliyoyafanya.

Mheshimiwa Spika, naomba nami nitoe mapendekezo kadhaa katika hii Finance Bill. Katika Amendment of Land Act, Cap 113, Section 33, hii kuondoa au kusamehe kodi ya pango la ardhi, naomba nitoe mawazo yangu. Serikali imefanya jambo jema kusamehe Taasisi za Serikali, za Dini na nyingine, lakini imesahau private schools. Siyo shule zote ambazo zinatoa huduma na zahanati zote ambazo zinatoa huduma zinakuwa chini ya taasisi fulani fulani za kidini au organisation fulani fulani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kwa sababu muda mrefu wenzetu wenye shule binafsi wamekuwa wakilalamika kuhusu tozo nyingi na wanatusaidia kutoa elimu kwa watoto wetu, wawakumbuke pia hii tozo iondoke, kwa sababu hii tozo mwisho wa siku anayelipa ni yule mzazi ambaye amepeleka mtoto pale.

Mheshimiwa Spika, kama lengo ni jema, wanatoa elimu, wanatoa huduma za afya kwa watu wetu, tuwasamehe na hii kodi ambayo tumekuwa tukitoza taasisi nyingine ili angalau pawepo na equal ground ya hawa watu kutoa huduma. Kwa hiyo, vile ambavyo mmefungua huu mlango wa kusaidia taasisi mpaka za dini na taasisi nyingine na hawa watu wenye private schools, wenye private dispensaries, waweze kusamehewa na hii kodi isaidie. Hilo ni pendekezo Mheshimiwa Waziri natamani wakati wa kujibu atuletee majibu ambayo yanaeleweka.

Mheshimiwa Spika, kwenye Local Government Finance Act, Cap 290, Section 37A, kuhusu Mfuko wa Vijana na Akinamama, mimi bado niishauri tu Serikali kwamba tuna sababu ya kuongeza. Pamoja na nia njema waliyofanya ya kuongeza walemavu, hebu wafikirie kuhusu wazee. Tuongeze kipengele kingine cha wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wazee wa nchi hii wameomba muda mrefu sana pension, waliahidiwa katika Serikali iliyopita lakini hawakusikilizwa. Hebu wafanye wao sasa, kwamba, kwenye zile asilimia tuweke ya wanawake, vijana, walemavu na wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri wakati Mheshimiwa Waziri anatunga kanuni au wakati Waziri wa TAMISEMI anatunga hizi kanuni sasa tu-specify kwamba hawa wazee kuanzia labda miaka 60 mpaka 80 wana uwezo wa kufanya kazi. Hao wazee ninaowazungumzia ni wa jinsia ya kiume sasa, jinsi ya ‘me’, kwa sababu wazee wa jinsi ya ‘ke’ wao wanaingia kwa akina mama na wanapata hii fursa ya mikopo.

Mheshimiwa Spika, wale wazee, baba zetu na babu zetu ambao na wao wanahitaji wapate mtaji huu lakini hawapati. Tuwa-accommodate maana ndiyo tunatunga sheria. Isipokuwa wakati wa kutunga kanuni, tuki-limit age kwamba mpaka miaka 80, basi tu-limit ili tuweke kundi ambalo wanaweza wakafanya kazi, ni vizuri iwekwe kwenye kanuni. Ila kwa sasa tuwa-include wazee wa nchi hii, wamelia kwa muda mrefu sana na naamini hili Mheshimiwa Waziri atalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilipenda kuchangia ni suala la Tume ya Mipango. Kiukweli nchi hii bado Tume hii tunaihitaji. Kwa sababu, haiwezekani tu kila kitu kikawa chini ya Wizara hii. Leo tunavyoongea kuna Msajili wa haya mashirika yako chini yake, lakini huyu Msajili wa Hazina mpaka leo unaona hata bajeti yake juzi alipewa asilimia 17 tu na tuna mashirika zaidi ya 280. Kwa hiyo, kwa hali ya kawaida kuendelea kuiongezea mzigo inakuwa haifai. Hii Tume iendelee, ijitegemee, ipange mipango. Japo nchi hii hawafuati mipango na hapa wasitake kutudhihirishia kwamba sasa hii nchi wanaiendesha kwa asubuhi mtu ameamkaje, basi ndiyo hicho wanakuja wanaleta kwenye bajeti. Wawe honesty, hii Tume ibaki vile ambavyo Kamati imeshauri na naipongeza Kamati kwa msimamo wao huo.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu Public Finance Accounts, lakini suala la TSA. Mimi niseme hiki kitu bado hakijaiva. Ni vizuri wakakaa chini jinsi ambavyo wametofautiana mara nyingi sana kwamba kutakuwa na Sub-TSA, lakini wakati huo kutakuwa na voted na non-voted sources hizo, lakini wakati huo huo hii non-voted wamekuwa wakishindwa kutafsiri kwamba fedha zikishapita muda zirudi huko kwenye TSA Account halafu Katibu Mkuu sasa aweze kutoa go ahead tena.

Mheshimiwa Spika, kama Waheshimiwa Wabunge tunashauriwa na Kamati, Kamati hii imesema jambo hili lisubiri mpaka Septemba. Nashauri kwamba hatuna sababu ya ku- rush kwa sababu hiki kitu hakijafanyiwa kazi vizuri. Kifanyiwe kazi vizuri na tusi-rush hilo la Septemba, waende wakakae chini, watafute hizo sources ambazo zitakuwa zinaingia huko. Wanaona Kamati ilivyofanya kazi kubwa mpaka tukatoa own sources za Halmashauri zetu, walikuwa wameshaweka mpaka own sources, you can imagine that fight, mpaka own sources zikatolewa, sasa tumeingia kwenye contradiction ya voted na non-voted. wakae chini wa-settle. Where are we rushing? Kwa sababu, mwisho wa siku lazima tufanye thorough analysis ya maamuzi ambayo tunafanya kama Wabunge. Kwa hiyo, nashauri lisubiri na wala siyo hiyo Septemba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nataka kushauri, katika Tax Administration Act, Cap 438, Section 79(c), naomba kwa hili pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwamba amesamehe hizi interest ambazo wafanyabiashara walikuwa wameshindwa kulipa. Nimshauri, kwenye hiyo Section (c) kwamba anapoenda kutunga sasa zile kanuni, eligibility na duration ya ule msamaha namwomba wale wenye principle wasibanwe kutakiwa walipe leo ndiyo wasamehewe interest. Wapewe muda angalau wafanye installment within those six months ambazo Mheshimiwa Waziri amezisema ili wafanyabiashara wetu wengi waweze ku-qualify kusamehewa hizi interests.

Mheshimiwa Spika, kwenye kanuni ukienda akaandika anavyotaka wewe, maana yake hawa wafanyabiashara unaweza ukamwambia lipa ndani ya mwezi huu principle then usamehewe interest. Mimi naomba tu, hii nia njema ambayo Mheshimiwa Waziri ameionesha katika kuwasamehe aende sasa kwenye kanuni ambayo ame-provide katika ile Section 79(c) kwamba, kanuni itatungwa, lakini itaonesha eligibility na duration, azingatie suala la payment au installments za principles ili wafanyabiashara wetu walipe wakiwa wame-relax badala ya kuwa na stress. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri katika suala zima la Local Government Finance Act, Section 33 na 34. Hili najua limebaki kwenye Halmashauri zetu, hizi sources mpya ambazo Mheshimiwa Waziri amezi-introduce baada ya ule Mfuko wa Pamoja kukwama kwamba own sources zetu hazitaingia kule, maana hivi vyanzo tutakusanya. Wamependekeza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.