Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Dr. Adelardus Lubango Kilangi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja iliyoko mezani. Mimi nitajielekeza zaidi katika masuala ya kisheria kwa sababu katika michango mbalimbali iliyotolewa kwa maandishi na kwa mdomo umeonyeshwa wasiwasi tofauti tofauti kuhusu hasa hizi sheria mpya tulizotunga mwaka jana za Permanent Sovereignty na ile ya Review ya Mikataba. Kwa hiyo, kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali nafikiri ninao wajibu wa kutoa maelezo kidogo hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu katika maelezo yangu haya niirejee kidogo historia. Kuna wakati fulani hapa Waziri wa Katiba na Sheria aliwahi kuzungumza umuhimu wa historia ya sheria na mara nyingi mambo mengi tunakuwa hatuyaelewi kwa sababu historia ya kitu husika tunakuwa hatukifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria yetu ya Madini imeanza wakati wa Mjerumani. Mwaka 1895 Mjerumani alitunga sheria iliyokuwa inagusa masuala ya ardhi na akasema kwamba kwa sehemu kubwa ya ardhi ya iliyokuwa German East Africa, Tanganyika baadaye, iliwekwa chini ya Mfalme wa Ujerumani, lakini hiyo ikiwa ni pamoja na madini yote yaliyokuwa katika ardhi ile. Pia akatoa leseni za uchimbaji wa madini, palikuwa na uchimbaji tayari maeneo mbalimbali ikiwemo Geita na akayapa makampuni ya Ujerumani.

Mheshimiwa Naibu Spika, alivyochukua utawala Muingereza akatunga sheria na kati ya sheria za kwanza kabisa kutunga ilikuwa ni sheria inayogusa masuala ya madini. Kwa ufupi katika sheria hizo aliyaweka madini yote yanayopatikana Tanganyika wakati ule na kwa sasa Tanzania chini ya Mfalme wa Uingereza wakati huo. Pia aliweka taratibu ambazo zilihakikisha kwamba ni makampuni kwa kweli kwa sehemu kubwa ya Uingereza au ambayo yalikuwa na connection ya Uingereza ndiyo yangeweza kuchimba madini katika nchi hii. Kwa hiyo, kwa ufupi huo ndiyo ukawa msimamo wake wa kwanza katika sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1929 sheria ikabadilishwa na alikuwa bado Mkoloni ni huyo huyo Muingereza lakini ilibakiza misingi ile ile; kwamba madini yote ni mali ya Mfalme wa Uingereza na kampuni za kuchimba madini yale sehemu kubwa yanatoka Uingereza na huo ndio ukawa msimamo. Pia ulikuwa msimamo kwa ujumla katika sheria zinazosimamia uwekezaji kwa maana ya kwamba sehemu kubwa ya wale waliopewa nafasi ya kuwekeza katika nchi, hii ikiwa ni pamoja na kuchimba madini, walitoka Uingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1959 miaka miwili kabla ya Uhuru, World Bank wakijua kwamba Tanzania wakati ule Tanganyika itapata uhuru walifanya ziara ya kuja kumuona Mwalimu, wakamwambia Mwalimu tunafikiri ni vema nchi yako ikabadilisha sheria zinazohusu uwekezaji na ambayo ingegusa pia uwekezaji katika madini. Akawauliza mnataka nifanye nini? Wakasema inabidi uzirekebishe sheria hizi ili ziweze kuruhusu na kutoa uwazi kwa makampuni mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali waweze kuja kuwekeza hapa. Mwalimu akawauliza akasema mbona hizi sheria zimekuwepo toka Muingereza na Mjerumani alipokuwepo na zina shida gani sasa, kama ni hivyo basi tutaziacha hizo hizo sheria ziendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya uhuru nchi ilichukua hatua na kupitia katika Katiba ya TANU ya mwaka 1965 ilianza kuweka vipengele vinavyosema sasa hizi maliasili zilizoko Tanzania yakiwemo madini ni mali za watu wote, ni mali za Watanzania. Mwaka 1967 kama tunavyofahamu kulikuwa na Azimio la Arusha na katika lile Azimio baadhi ya athari zake ilikuwa ni kwamba uwekezaji mkubwa ni lazima urudi mikononi mwa wananchi, mikononi mwa Taifa na msimamo huo ukaathiri pia sekta ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1977 tulipopata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 walau vipengele vinavyohusu rasilimali vikaingia katika Katiba hasa katika Ibara ya 9 na Ibara ya 27. Mwaka 1979 tukafanya mabadiliko mengine makubwa ya Sheria ya Madini na haya ni baada ya uhuru. Katika mabadiliko hayo, maana shinikizo lilikuwa limeshaanza wakati ule basi tukaruhusu kampuni kuanza tena kurudi kuwekeza katika masuala ya rasilimali na hasa madini; maana mwaka 1967 msimamo wa sera ulikuwa kama unayaondoa yale makampuni lakini pia tukaruhusu wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya 80 na 90 mwanzoni kukatokea kitu kinaitwa Washington Consensus. Kwenye Washington Consensus ambayo ilisimamiwa na World Bank, IMF na Marekani pamoja na mataifa mengine makubwa uliwekwa mkakati wa makusudi wa kurudi Afrika na kuyadhibiti tena madini ya Afrika. Kwa sababu nchi nyingi za Afrika miaka ya 60 zilikuwa zimechukua misimamo ambayo ilikuwa inayanyima makampuni kutoka nje nafasi ya kuyaendeleza au kuya-exploit madini hayo. Hiyo ndiyo ilitupelekea kwenye Sheria yetu ya Madini ya mwaka 1998 ambayo kwa kweli kwa kiasi kikubwa ilikuwa na influence ya mtazamo wa World Bank. Baada ya hapo palikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kwa ujumla, ndiyo ikapelekea mabadiliko fulani ya msingi yaliyofanyika miaka ya 2010 hususani katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze kwa ufupi, hizi sheria mbili tulizotunga mwaka jana chimbuko lake ni nini, pamekuwa na maswali, sasa tumetunga sheria, tumebadilisha sheria, tumewa-discourage investors, tumewa- disappoint investors, hizo sheria zimetokea wapi? Sheria hizi kimsingi zilikuwepo kupitia maamuzi ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hayo Matamko ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1952, mwaka 1958, 1962, 1966, 1974 na kuendelea na baadaye yaliingia katika mikataba ya kimataifa ikiwemo zile International Covenant on Civil and Political Rights, International Covenant on Economic and Social Right ya mwaka 1966. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha msingi cha kuzungumza hapa na ambacho tunakipata sasa katika hizi sheria mbili za mwaka jana ni zile haki nne (4) kuu muhimu ambazo unazikuta katika haya Matamko ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na ile Mikataba ya Kimataifa iliyotungwa katika uelekeo huo. Ya kwanza, haki ya nchi kutambuliwa kwamba inamiliki maliasili. Nimeeleza Muingereza na Mjerumani walivyochukua nchi jambo la kwanza walisema rasilimali zote za madini ni mali ya Mfalme au yako chini ya Mfalme.

Mheshimiwa Naibu Spika, haki ya pili ni haki ya kusimamia na kudhibiti uendelezaji wa rasilimali hizi. Hii ni ya msingi sana kwa sababu kuna haki ya kutunga sheria, kuna haki ya kuangalia uendelezaji, kuna haki ya kuangalia processing, kuna haki ya kuangalia masoko, uuzaji na kila kitu. Hizi haki zote ziko humu ndani. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, haki ya tatu, ni haki ya nchi na watu wake kushiriki katika uendelezaji. Naweza nikasema kwa uhakika kabisa kwamba sheria na mfumo uliokuwa umewekwa wakati wa Muingereza na kwa mtazamo wa Washington Consensus ulikuwa umewekwa kwa namna ambayo hauipi nchi na watu wake nafasi ya kushiriki katika kuendeleza hizo rasilimali. Haki ya nne ni haki ya nchi kufaidika na rasilimali hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo manne utayakuta vizuri sana katika hizi sheria mbili tulizozitunga mwaka jana. Kwa hiyo, kimsingi sheria zilikuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee dakika moja na nusu kwa sababu nazungumzia masuala mazito ya kisheria, sheria hizi ni sheria msingi kwa maana kwamba zinakuwa na effect kwenye sheria nyinginezo za nchi hii ambazo zinagusa rasilimali na ndiyo maana zikawekwa chini ya usimamizi na uangalizi wa Waziri wa Katiba na Sheria. Baadhi ya misingi ile iko kwenye Katiba na baadhi ya misingi ile inatakiwa ifanye kazi katika sheria mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kwa kusema kwamba pana wasiwasi mwingi, tutashtakiwa, tutafilisiwa, sijui tutapata shida gani kwa sababu ya kutunga sheria hizi, tumezitunga kwa kuzingatia haki yetu iliyoko katika Sheria za Kimataifa. Kwa upande mwingine kama nchi hatupaswi sasa kuogopa. Bara la Afrika kwa ujumla limekuwa linatishwa sana, lakini kama nchi tumejipanga, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali sasa iko vizuri kabisa, tuna Ofisi sasa ya Wakili Mkuu wa Serikali na kama kunajitokeza jambo lolote nchi kama nchi hatupaswi kuwa na wasiwasi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.