Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na pongezi kwa Waziri Mheshimiwa Angellah Kairuki; Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Doto Biteko na Mheshimiwa Stanslaus Nyongo; na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri na kuwasilisha hotuba yao ili tuweze kuijadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Serikali na kipekee nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuamua kufanyike marekebisho ya Sheria za Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nalipongeza Jeshi la Wananchi kwa ujenzi wa ukuta wa Mererani ambao umeweza hata kupandisha thamani ya madini ya tanzanite.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu elimu katika maeneo ya machimbo. Katika machimbo, wachimbaji wadogo hawana elimu ya kutosha kuhusu hatari zilizopo machimboni. Pia kuna maambukizi makubwa sana ya UKIMWI. Je, ni mkakati gani Serikali inaweka ili kuwanusuru vijana wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia yanapoanzishwa machimbo mapya kama machimbo ya Nyakavangala yaliyopo Jimbo la Ismani Mkoa wa Iringa, ni utaratibu gani unafanywa ili kuwaelimisha wananchi walio katika machimbo ili kujua fursa zilizopo katika eneo lao? Kwa sababu kuna watu wanakuja kutoka maeneo mbalimbali kufuata fursa wakati waliopo katika maeneo hayo wanakuwa hawajui.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika machimbo mapya kuna tatizo kubwa sana la huduma za kijamii kama ulinzi, vyoo, zahanati na kadhalika. Halmashauri hazina uwezo, je, Wizara huwa inawasaidiaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu fedha kutopelekwa katika vyuo vya madini. Vyuo vyetu ya madini vina changamoto kubwa sana ya fedha kutopelekwa kwa wakati. Naomba kama Serikali ina dhamira ya dhati ya kusaidia sekta hii, itoe fedha kwa wakati ili kuboresha vyuo vyetu ili viweze kuwa na mazingira mazuri ya kuzalisha watalaam wetu wa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni watoto wadogo kutumika katika machimbo. Pamoja na kuwa ipo sheria ya kumlinda mtoto kutoajiriwa au kutumika kufanya kazi, lakini tumeona umekuwa ni utaratibu wa baadhi ya wananchi na makampuni kuwatumia watoto wadogo kufanyishwa kazi migodini. Je, hatua gani zinawekwa na Serikali kukomesha tatizo hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua, je, Serikali inaisaidiaje STAMICO ili kuiwezesha kupata fedha ya kutosha ili shirika hili liweze kufanya kazi yake kama ilivyokusudiwa katika uanzishwaji wake?

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza tena Mheshimiwa Waziri na Manaibu wote. Nina imani kwa juhudi yao watainua sekta hiii ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.