Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Ajali Rashid Akibar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Wizara hii nyeti ya Comrade Lukuvi kwani Wizara hii ni nyeti na ndiyo Wizara ambayo kwa kweli tunaitegemea kiuchumi. Bila ardhi tunaweza tusiwe na viwanda vya kiuchumi, tunaweza tusiwe na kilimo, viwanda wala mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ni muhimu na ndiyo maana inahitaji iwekwe kwa mtu ambaye ni makini tena mtu ambaye kwa kweli awe ni sahihi kweli kweli. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi amepewa yeye kwa kuwa ameonekana kwamba ni mtu makini. Ili aendelee kuwa makini, anatakiwa akemee baadhi ya Wizara. Wizara ambazo anapaswa kuzikemea ni pamoja na Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maliasili na Utalii wakitaka kujikatia eneo, wao wanaamua tu kwenda kujikatia, wanaangalia thamani ya tembo wao, lakini hawaangalii thamani ya binadamu. Naomba wafuate utaratibu kwamba pale anapostahili kuwepo mnyama aendelee kuwepo mnyama na pale ambapo panastahili kuwepo makazi yaendelee kuwepo makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wa Madini wakihitaji eneo lao, wao hawajali kama kuna watu ambao wapo ndani ama kuna mashamba ya watu. Wao wanachoangalia ni thamani ya yale madini yao. Kwa hiyo, tunahitaji watu wa madini wapewe eneo lao na wale watu wanahitaji wabaki katika eneo lao madini, waendelee kubaki katika madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyozungumza mwenzangu ambaye amepita, hii Wizara ya Ulinzi tunahitaji sana ulinzi, lakini tunapohitaji kupanua mipaka, basi wawepo ndani ya mipaka yao ili na wananchi waendelee kutumia maeneo mengine. Kwa hiyo, ni vizuri Wizara ya Ulinzi ikatengewa maeneo yao nje ya maeneo ya binadamu mahali ambapo wananchi hawawezi kuwa na mahitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale maeneo ambayo yamekuwa katikati sasa hivi, kwa mfano Jeshi ambalo lilo katikati, hatuhitaji tena kuwa na Jeshi katikati ya mji. Nadhani tuangalie uwezekano wa kuchukua Jeshi tuweke nje ya mMji, maana tuna maeneo mengi ili waweze kufanya mazoezi kwa nafasi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba ni kuhusu Wilaya ya Newala. Wilaya ya Newala ilitangazwa mwaka 1959 kwa GN ambayo ilitoka mwaka 2000. Tulitegemea kwamba kama Wilaya ilianzishwa mwaka 1959 na GN ikatoka mwaka 2000 kuna mpaka ambao unaanzia pale Chiwata, Ndanda, Mpanyani hadi kule Mwena; hiyo mipaka ilianzishwa tangu mwaka 1959 na wale wananchi ambao walikuwa wanabeba GPS za Wazungu wapo. Kwa hiyo, tunategemea ile GN ambayo ipo, kilomita moja kutoka Ndanda ndipo ambapo Wilaya ya Newala inapoishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mshangao kuna GN ya mwaka 2010 ambayo ilitangaza Wilaya ya Masasi. Hii GN ya mwaka 2010 inatofautiana na GN ya mwaka 2000 ambazo zote zinatoka katika Ofisi moja. Inakuwaje hizo GN ambazo zinatoka katika ofisi moja zinatofautiana? Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Comrade Lukuvi, aangalie GN ya mwaka 2000 inakuwa vipi tofauti na ile GN ya mwaka 2010?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii mimi naelewa kuwa kulitokea mgogoro mwaka 1994 juu ya mpaka, kwa hiyo, watu wakatumia advantage ya miaka sita ile baadaye kurekebisha ile GN na ndiyo maana hata tafsiri ya mpaka leo wa Masasi na Newala unatofautiana. Wananchi wanajua mipaka yao inaishia wapi na kila mmoja anafahamu, lakini watalaam wanatofautisha. Wale wataalam ambao siyo waadilifu wanafanya mambo ambayo siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi hapa kumetokea mgogoro kati ya watalaam wa Kanda ya Mtwara na wananchi pale Mpanyani. Haiwezakani mtu ambaye amekaa kuanzia mwaka 1918 yupo pale Mpanyani uende na approach umwambie bwana wewe upo Masasi, akwambie tu leo Mheshimiwa Lukuvi wewe ni mtu wa Mbeya. Kwa kweli namshukuru sana yule Diwani wa Chilangala, alitumia busara. Vinginevyo wale watu leo tungekuwa tunaongea hadithi nyingine. Yale mambo yaliyotokea Dodoma, yangetokea Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa kutumia busara zake aende akawaite wale wazee ambao walikuwa wamesimama na wanajua ile mipaka, awaite wananchi wa Masasi na Newala ambao wanajua mipaka yao na tumekuwa tukiishi kwa amani, sisi hatuna tofauti, isipokuwa kuna madini yatatusambaratisha, nchi hii itagawanyika katika vipande. Kuna wanasiasa wengine wanataka mashamba pale, wanahonga baadhi ya watalaam ambao siyo waadilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwamba tunapomaliza Bunge hili, yeye mwenyewe Comrade aje aangalie hali iliyoko pale. Haiwezekani leo mtu ambaye hakuwa anategemea kwenda Masasi au Newala asubuhi aambiwe kwamba leo wewe upo katika Wilaya ya Newala wakati ile mipaka wao wenyewe wanaifahamu au shamba lako unaambiwa lipo Masasi au halipo Masasi lipo Newala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, kwani naamini kwamba Mheshimiwa Waziri atakuja baada ya Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.