Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi kuchangia Wizara hii muhimu, Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ukweli, nimekuwa hapa Bungeni tangu mwaka 2000. Tumekuwa tuna migogoro mingi sana ya ardhi kuanzia mwaka 2000 mpaka sasa hivi ni mwaka 2018. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Lukuvi, amepunguza migogoro ya ardhi kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme ukweli Mheshimiwa Waziri William Lukuvi, anachapa kazi sana. Anafanya kazi kubwa sana, lakini sio kwamba achukue sifa zote peke yake, ana mke wake ambaye anamwangalia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa wa Kilimanjaro una wilaya saba. Ndani ya wilaya saba, Wilaya ya Same iko hapo ambayo katika ardhi inachukua takriban asilimia 40 ya ardhi ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wilaya ya Same asilimia 68 iko milimani, asilimia 32 iko tambarare. Tuna matatizo makubwa mawili ambayo ndiyo yamenifanya nisimame hapa, Nianze kwa kusema kwa Mheshimiwa Waziri; Same tunamwita aje aone matatizo yetu. Haya matatizo ni matatizo yako sehemu kubwa katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kata mbili, Kata ya Makanya ambayo iko Same Magharibi, kata hii tangu mwaka moja elfu mia tisa, kwanza population ya Kata ya Makanya ni takriban wananchi 15,000 kwa sensa ya mwaka 2012. Kwa hiyo, ni Kata yenye watu wengi sana. Kuna tatizo kubwa sana la ardhi pale kwenye Kata ya Makanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haya mashamba ya mikonge ambayo watu wengi tunayalalamikia kwamba yame-end up kutokuwa na tija kwa wananchi kwenye kata zetu. Kata ya Makanya ni kata yenye matatizo ya mafuriko ya mara kwa mara. Lile eneo zuri kwenye Kata hii ya Makanya ndilo eneo ambalo lina mkonge, la mwekezaji ambaye simjui ni nani lakini ni mwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 1994, wakati huo Waziri wa Ardhi akiwa ni Mheshimiwa Edward Lowassa, kama sikosei, wananchi wa Kata ya Makanya, Kijiji cha Makanya walileta maombi kwamba wapatiwe ardhi takriban hekta 30, kwa sababu ile ardhi wanayoishi wao ndiyo ardhi ambayo ina mafuriko mara kwa mara. Kwa hiyo, hili tatizo ni kubwa sana kwa Kata ya Makanya. Mheshimiwa Waziri, namnyenyekea, aje aione kata ile, aone wananchi wanavyoteseka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, hawana eneo la makazi, pili, ukiangalia kama unatokea Hedaru kwenda Same ardhi kbwa ya Makanya huku kando ya barabara ni kilimo cha mkonge. Vijana wa Kata ya Makanya nao wangependa kufanya biashara kandokando ya barabara ya lami, lakini kandokando ya ile barabara ya lami kuanzia Makanya mpaka Same ni mashamba ya mkonge ambayo nina uhakika hayana tija kwa wananchi wa Kata ya Makanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetumwa na wananchi wa Same nimwite Mheshimiwa Waziri aje Same na mimi nitakuwepo Same. Tuzunguke Kata ya Makanya aone ni kiasi gani wananchi wa Kata ya Makanya, Same ya Magharibi wanapata adha kwa ajili ya yale mashamba ya mkonge. Mheshimiwa Waziri nafikiri message ameipata vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Makanya ni kata ambayo mara kwa mara Watanzania mnasikia mafuriko, ni kwa sababu ardhi ile ambayo ni nzuri ndiyo yenye mkonge na ardhi ambayo ina mafuriko ndiko wanakoishi wananchi. Mheshimiwa Waziri nimalizie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi Kata ya Ndungu. Tangu Bunge zima la Kumi nimekuwa nalalamikia Kata ya Ndungu. Kata ya Ndungu asilimia kubwa ni mashamba ya mkonge pia; vijana wa Kata ya Ndungu hawana sehemu ya makazi, hawana sehemu ya biashara, ni mashamba ya mkonge. Mheshimiwa Waziri, nimemwona anazunguka Tanzania, anafanya mikutano mpaka saa sita usiku; namsihi aje kwetu Same, tunamsubiri, tunamsubiri atapata zawadi ya mpunga, atapata tangawizi, aje aone matatizo ya ardhi, mashamba ya mkonge yametuzidi, lakini hayana tija kwa Kata ya Makanya na Kata ya Ndungu. Karibu Same tunakusubiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.