Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote kwa kunipa nafasi ya kusimama na kutoa mchango wangu katika hoja ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na hoja ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwa mwaka wa Fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na timu yote ya Serikali kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa Ilani ya CCM. Jambo ambalo limesababisha kila unapofanyika uchaguzi mdogo, CCM inapata ushindi wa kishindo, dalili hizi ni nzuri na kama kura zingepigwa leo ushindi wa Rais, Wabunge na Madiwani ungekuwa wa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huu naomba kujielekeza katika hoja nitakazozitilia mkazo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI: Mapitio ya utekelezaji wa Bajeti na ukusanyaji wa Mapato na Maduhuli. Upelekaji fedha katika Halmashauri; pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali Kuu kupeleka fedha katika halmashauri zetu kiasi cha trilioni 3.33, sawa na asilimia 50.63 fedha hizi hazikufikia lengo lililokusudiwa. Naiomba Serikali katika mwaka huu wa fedha tuiangalie sekta ya TAMISEMI katika macho mawili hasa katika kupeleka fedha za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na kwamba halmashauri zimekusanya zaidi, ukilinganisha na mwaka jana tofauti Sh.90/= ziliongezeka na makusanyo yote ni asilimia 50 kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri, ukurasa wa tisa (9). Bado kazi ya ukusanyaji wa mapato si ya kiwango cha kuridhisha katika baadhi ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri katika kukusanya mapato; naishauri Serikali kuzielekeza halmashauri zetu kuendelea na kubuni miradi ya uwekezaji na kubuni vyanzo vya mapato ambavyo havitaleta kero kwa wanawake na wananchi. Hapa pia ningependa Waziri atuambie je, Serikali imejipangaje kuzisaidia halmashauri zetu kufanya uwekezaji mkubwa utakaoleta tija na kuongeza vyanzo vya mapato na kuziondoa halmashauri katika tatizo la kuwa tegemezi kwa Serikali kuu hata kwa kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa fedha za Serikali za Mitaa; kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/ 2017 na Taarifa ya Waziri ukurasa wa 15 inaonesha kati ya Halmashauri 185 zilizokaguliwa, halmashauri 166 sawa na asilimia 90 zimepata hati safi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri na timu yake yote, Wakurugenzi wa Halmashauri zetu na Madiwani kwa kukubali maagizo ya Rais wetu ya usimamizi wa fedha za Serikali. Lengo likiwa kila kinachopatikana kiingie katika Mfuko wa Serikali na
kinatumika kwa kuzingatia taratibu za fedha za Serikali yetu. Hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tuendelee kuiwezesha Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani katika kila Halmashauri ili waweze kutekeleza wajibu wao kikamilifu na kuhakikisha wanapewa ulinzi wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao ili wasipoteze ajira zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa pia nipende kujua Serikali imejipangaje kuimarisha vitengo vya ndani vya ukaguzi ili watekeleze jukumu la kufanya ukaguzi wa ndani kwa uhuru na haki bila ya kuingiliwa na mamlaka zao za ajira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi; Mfuko wa asilimia 10 ya Wanawake na Vijana; pamoja na kuzipongeza halmashauri zilitengewa bilioni 15.6 na kutoa mikopo kwa vikundi 8,672 vya wanawake, vijana na walemavu kati ya 18,233.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema wazi kuwa bado lipo tatizo kubwa la baadhi yetu kutotenga, kutoa hata kufuatilia urejeshaji wa mikopo, ushahidi unathibitishwa na Taarifa ya Waziri kuwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Mfuko wa Wanawake ulitengewa Shilingi bilioni 61.6 kiasi kilichotolewa ni Shilingi bilioni 15.6 na ilipangwa vikundi 18,233, vikundi vilivyopata ni 8,672.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwa kuwa Mfuko huu wa Wanawake na Vijana katika Halmashauri ndio mfuko pekee ambao ndio mkombozi kwa mwanamke mnyonge asiye na uwezo wa kufikia taasisi nyingine za fedha kutokana na masharti yake, naomba hapa Waziri atupatie majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi huu Muswada wa Sheria wa kuweka utaratibu wa utekelezaji wa mpango wa kutaja na kutoa asilimia kumi ya wanawake na vijana utaletwa lini hapa Bungeni kwa sababu ni maoni ya Kamati mbalimbali hapa Bungeni. Je, Serikali Kuu ina mpango gani wa kupeleka fedha katika halmashauri kuunga mkono Mfuko huu kwa sababu fedha hazitengwi kikamilifu na hazitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa huduma za afya; kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri ukurasa wa 24 – 29 umeonesha kwa ufasaha kuwa hospitali za wilaya zilizopo 120 zinazohitajika 184 sawa na asilimia 65.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya afya vilivyopo ni vituo 696 sawa na asilimia 15.7 lengo likiwa ni kuwa na vituo vya afya 4,420 na Serikali iendelee na ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya 208.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Zahanati; kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri, Zahanati zilizopo nchini 6,440 sawa na asilimia 53, lengo ni kuwa na zahanati 12,543.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya kuendelea kujenga, kukarabati hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati. Tatizo la kusogeza huduma ya afya kwa wananchi bado ni changamoto kubwa sana, wanawake bado wanafariki kwa uzazi na watoto chini ya miaka mitano (5) wanafariki dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri; kabla ya kuja hapa Bungeni nilikutana na baadhi ya wanawake na wananchi na hasa wanawake ninaowawakilisha walinituma nije nilete kilio chao cha kuomba kusogezewa huduma za hospitali kama ambavyo Serikali imejenga shule kila kijiji na sekondari kila kata na ili niweze kuwasilisha maombi yao Bungeni nikianza na TAMISEMI kutaka kujua mipango yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya TAMISEMI chini ya Mtendaji wake mahiri Mzee Iyombe na Chaula walinieleza mipango yao ambayo ni mizuri sana, wanachohitaji Ofisi ya TAMISEMI ni kupatiwa fedha. Ofisi ya TAMISEMI wameishaandaa bajeti ya ujenzi wa zahanati 2,277, vituo vya afya 156 na ukamilishaji wa maboma yaliyojengwa na wananchi 1845 kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa vituo vya afya 156 na ununuzi wa vifaa tiba 156 x 850,000,000 = 132,600,000,000/=. Ukarabati wa zahanati angalau nusu ya mahitaji 2,277 x 100,000,000 = 227,700,000,000/=. Ukamilishwaji wa maboma 1,845 = 934,000,000,000/= hivyo Jumla kuu 1,294,300,000,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri; naiomba Serikali ya CCM itafute fedha hizo Sh.1,294,300,000,000 na kuzikabidhi TAMISEMI kwa ajili ya ujenzi wa miradi hii na kuboresha huduma za afya, kupunguza vifo vya watoto na wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sekta ya Elimu. Usimamizi wa elimu ya msingi na sekondari nchini; naishukuru Serikali kwa mpango wa kuendelea kuboresha elimu hapa nchini pamoja na pongezi nashauri yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke mpango mzuri wa kuwaandaa Walimu wa shule ya awali kwa baadhi ya shule wanaofundisha shule za awali hawana taaluma ya elimu ya awali. Serikali iandae vitabu vya kufundisha na kujifunza kwa wanafunzi wa shule ya awali. Shule za sekondari na msingi zina upungufu wa Walimu na hasa Walimu wa sayansi. Serikali kwa kushirikiana na wananchi wajenge madarasa yatakayopunguza msongamano wa watoto wetu katika shule zetu. Serikali kwa kushirikiana na wananchi itafute fedha kwa ajili ya matundu ya vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iimarishe Kitengo cha Ukaguzi ili kitekeleze wajibu wake kikamilifu. Serikali iendelee kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za Walimu. Ningependa kujua pia mpango wa Serikali wa kukabiliana na changamoto nilizozitaja hapo juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Utumishi; pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya kuajiri watumishi katika kada mbalimbali upo upungufu wa watumishi katika kada mbalimbali za umma mfano; Walimu wa shule za awali, Walimu wa shule za msingi na sekondari hasa Walimu wa Sayansi na Hesabu. Maafisa Ugani, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Sekta ya Afya, Madaktari, wataalam mbalimbali, Sekta ya Afya TAMISEMI, upungufu ni wafanyakazi 62,976 sawa na asilimia 55. Hapa ningependa kujua hawa wafanyakazi watakaoajiriwa mwaka huu wa fedha 2017/2018 ni wa kada gani na ni wangapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF); napenda kuchukua nafasi hii kuupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kwa kazi nzuri ya kutoa huduma za jamii na kuzitambua kaya maskini 1,363,448 tangu kuanza kwa mpango huu na kaya 1,118,751 zenye watu watano na shilingi bilioni 185 zilizotolewa kwa kaya maskini Tanzania Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi nashauri, Serikali ifuatilie kwa karibu viongozi wanasiasa katika vitongoji, vijiji na kata kwani yapo malalamiko ya baadhi ya wananchi kuwa baadhi ya viongozi wanasiasa wanatambua watu wahitaji kwa upendeleo bila kuzingatia vigezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo vya usalama na TAKUKURU: Usalama; nawapongeza kwa kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama na amani endelevu na kazi ya kuhakikisha usalama wa viongozi, wananchi na Taifa letu la Tanzania linaendelea kuwa salama na amani na kuwa mfano wa kuigwa katika mataifa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi, nashauri vyombo vyote vya ulinzi na usalama viendelee kuimarisha ulinzi na usalama na katika nchi yetu na Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani na utulivu, kwani amani itakapotoweka watakaoumia ni wanawake na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAKUKURU; nawapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya ya kudhibiti vitendo vya rushwa na kuwezesha kuokoa fedha nyingi ambazo zilipotea. Ushauri wangu waendelee na kazi ya kupambana na rushwa kwa nguvu na bidii zaidi kwa manufaa ya Taifa letu. Sisi wanawake wa Tanzania tunawaunga mkono katika jitihada hizo za kupambana na rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.