Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Naomba nipate majibu ya haya mambo ambayo nitayaongea na sidhani kama nitatumia dakika zote kwa sababu mengi yameongelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasikia hapa wanasema kwamba kuzalisha umeme kwa njia ya gesi ni gharama kuliko kwa njia ya maji ndiyo maana wanakwenda kwenye Stiegler’s. Swali langu; wakati wanakwenda kukopa pesa nyingi, mabilioni kwenda kuwekeza kwenye bomba la gesi, wananchi wetu wa Mkoa wa Mtwara wamepigwa, wanawake wajawazito walijifungua kabla ya siku zao, walikwenda kukopa na kuwekeza wakati hawajafanya utafiti wa kutosha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate majibu ya swali hilo kwa sababu hiyo Stiegler’s ipo kabla hata hiyo ya gesi, ama vyote vilikuwa pamoja wakaenda kuwekeza kwenye gesi kwa pesa nyingi ambayo kama nchi tutatakiwa kulipa. Sasa hivi tunatumia kati ya asilimia sita mpaka saba, leo wanahamia kwenye Stiegler’s kwa mbwembwe nyingi wakisema huu huku ni gharama kuliko huu, waliingia bila utafiti? Tukiwaambia kwamba tunakwenda kwa mizuka wanakasirika, huu haukuwa mzuka? Naomba nipatemajibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho, lazima tu niiseme yaani hakuna namna. Unapozungumzia uchumi wa Mikoa ya Kusini, Mkoa ninaotoka mimi Mtwara huwezi kuzungumza bila ya kutaja korosho, yaani no way out. Sasa kama kuna mtu anafikiria hizo pesa tunazozizungumzia zaidi ya bilioni mia mbili si za wakulima, hivi kama wakulima wale wasingenyeshewa na mvua, wasingeng’atwa na nyoka, jua lisingewawakia, hizo trilioni moja nukta ngapi ambayo ilipatikana kwenye export levy ingepatikana kutoka wapi? Kwa hiyo hatuwezi kuona kwamba hizo pesa siyo za wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimezaliwa Mtwara mpaka leo ninavyokwambia naishi Mtwara, mimi si Mbunge wa Mjini, kwetu ni huko huko Mtwara. Wakati huo sisi tunakua, Bandari ya Mtwara ilikuwa inafanya kazi kutokana na korosho zikaanza hujuma. Mara meli haiwezi kufika hapo, mizigo hakuna na vitu hivi, Bandari ile ikaanza kudorora. Mama lishe, vijana ambao walikuwa wanafanya kazi pale wakawa hawafanyi kazi kwa sababu ya kutokuijali bandari ile na kuiendeleza kutokana na zao la korosho. Sasa tumeanza kurudi kidogo tunaonekana Wamakonde wale wanapeleka watoto wao shule ili waondokane na ile dhana ya watu wa Kusini hawakusoma kwa ajili ya kilimo cha korosho, leo hawataki kupeleka hela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kusikitisha kabisa, kama mnakumbuka, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mtu ambaye namheshimu sana; mnakumbuka mwaka jana alipita kuzindua miche kupanda, kuwahamasisha watu, ile miche mpaka leo haijalipwa, wale watu ambao wameotesha hawajalipwa, is it fair? Wanawatakia nini Waziri Mkuu na watu wake wa Kusini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate majibu na pia naomba nipate majibu ni nini mkakati wa Serikali, tuna kiwanda kinachozalisha cement pale cha Dangote, lakini kwa kiasi kikubwa cement ile inasafirishwa kwa barabara, hatujaona meli ya mizigo na barabara ile kila siku ukipita kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam kila siku ina viraka kwa sababu inabeba mzigo mkubwa. Maendeleo yoyote ni gharama. Sasa nataka nijue kama Serikali ina mkakati wowote wa kuleta meli ya mizigo ili kusudi bandari yetu itumike kusafirisha mizigo ikiwemo na ile cement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia madhumuni ya hiyo pesa ya wakulima, mimi sina namna nyingine ya kuiita hiyo pesa ya korosho, kuna madhumuni mengi kwa nini ikaanzishwa, wadau wa korosho wakafikiria ili tuliendeleze hili zao, tutenge pesa ambayo itasaidia. Dhumuni mojawapo tumesema ni kuwa na mikakati endelevu kuhusu zao la korosho ambapo mikakati hiyo inafanyika kwenye utafiti katika Chuo cha Naliendele ambapo 90 percent ya matumizi ya pale yanategemea hiyo export levy. Kwa hiyo kama hatupeleki tujue tumeua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kitu kingine, zao la korosho ukiliangalia, yaani wale Watafiti ukienda pale Naliendele wana mashamba ya mikorosho ambapo ile mikorosho inatunzwa vizuri ili iweze kutoa mbegu bora, hivi wanataka wale watafiti wetu waende wenyewe shambani wakalime ili watunze mikorosho wapate mbegu bora za kuendeleza hili zao ambao wanasema kwamba liende kwenye mikoa mingine ambapo sasa limesambaa katika mikoa 17?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu za korosho ni tofauti na mbegu zingine, kwamba unachukua shambani unaleta, hizi ni lazima kwanza uanze kutunza ile mikorosho iwe katika standard, unavuna then unakuja kuotesha, watu wanapata miche, wanakwenda kuiotesha kwa ajili ya kuendeleza zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhumuni lingine ni kufanya usimamizi na uratibu mzuri wa stakabadhi ghalani. Hawataki watu wauze Kangomba wanataka watu wauze korosho zao ghalani, hivi wale watu wote ambao watakuwa wanafanya hizo shughuli wanazifanya kwa kupata pesa kutoka wapi kama hawataki kutoa pesa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango ameitwa kwenye kikao si mara moja wala mara mbili, alikataa kuja. Angekuja, akatoa majibu watu wangemwelewa kwa nini alikataa kuja, pesa wamezipeleka wapi? Hilo ndilo swali la msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapoongea ni mwezi wa Sita, msimu kule umeshaanza hakuna sulphur, hakuna madawa, hakuna nini, hivi anategemea mwakani hata kama hiyo sheria yake ikapita na naamini itapita kwa sababu ni tumezoea, hakuna kitu kinachoingia humu ndani kikashindwa kupita. Hiyo Sheria yake imepita, anataka pesa zote zikusanywe ziwekwe kwenye huo Mfuko wa pamoja, atakusanya kitu gani kama korosho hakuna?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ni suala tu la kujiongeza, kwamba, tunahitaji tuhudumie vizuri ili mazao yawe mengi, aidha atakusanya yeye, atakusanya nani kwa sababu yote ni Serikali, hapa issue siyo kukusanya, issue pesa ikusanywe lakini pia itumike kwa matumizi yaliyokusudiwa. Atakusanya nini kama hakuna korosho? Atakusanya nini kama sulphur haijakwenda? Atakusanya nini kama madawa hakuna? Atakusanya nini kama kwenye taasisi ya utafiti hakufanyiki utafiti? Nafikiri hilo jambo wala halihitaji akili kubwa sana, ni jambo tu la kawaida, kwamba unahitaji uwekeze ili upate mavuno, sisi hatutaki kuwekeza, tunataka tupate mavuno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhumuni la tatu, tunasema kuendeleza ubanguaji wa korosho nchini, sasa hapo ndiyo majanga. Viwanda havieleweki, mashine hakuna, matatizo chungu mzima, Waziri wa Viwanda ukimuuliza kwamba kuna kiwanda gani kimetengewa eneo Mtwara Mjini? Anakwambia eti Chikongola kuna eneo, Chikongola hapo mnapopasikia ni katikati sokoni. Sasa sijui ametenga sehemu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya nimeuliza hili swali mwenyewe sikuwepo, nikajibiwa kwamba eti Chikongola sokoni wametenga eneo sijui sehemu gani. Kwa hiyo, yaani kuna vitu ambavyo ukikaa, ukivitafakari yaani ni lazima ushangae kwamba uelekeo wetu uko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimalize; tunachotaka watu wa Kusini ni pesa siyo maneno kama maneno tumeyasikia mengi tu. Hayo maneno aliyoyasema Mwenyekiti, Mheshimiwa Bwege wa Lindi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kangomba yaani kule kwetu kuna bakuli kubwa hivi ambalo lile wanapima kwa ujazo siyo uzito.