Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuweza kutimiza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na Sunnah ya sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze suala la korosho. Nimefuatilia mjadala wa asubuhi ulivyokuwa unaendelea na namna watu walivyokuwa wanataka kulipotosha jambo hili.

Mimi nilikuwa Lindi nimerudi jana, athari za pesa za export levy kutopeleka Bodi ya Korosho wataziona mwaka huu kwenye mapato ya korosho. Kwa sababu naamini labda Mheshimiwa Dkt. Mpango anachotaka ni asikie kwamba korosho zimeshuka uzalishaji atafurahi labla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka nimwambie Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango kwamba Bodi ya Korosho mwaka huu imeshindwa kutoa sulphur yenye ruzuku, hawajatoa hata mfuko mmoja. Mpaka sasa, nainapozungumza humu ndani ya Bunge sasa hivi mfuko mmoja wa sulphur unauzwa Sh.70,000 kutoka Sh.30,000 ya mwaka jana. Hivi ninavyoongea ndani ya Bunge chupa ya dawa ya viuatilifu ambayo ilikuwa inanunuliwa Sh.15,000 sasa hivi inauzwa Sh.51,000 wakulima wanakopeshwa kwa riba kubwa, yako makampuni nimeyakuta yako Jimboni yanakopesha wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango anachokitaka ni kwamba mazao yote yafe na korosho ife jibu litapatikana mwezi wa Kumi wala siyo mbali, korosho itakufa ili afurahi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu walitaka kutupotosha hapa kwamba export levy siyo fedha wakulima. Tunasema fedha ya wakulima kwa sababu korosho zimelimwa na wakulima, fedha ile kwa mujibu wa sheria asilimia 65 inakwenda kwenye maeneo yaliyolima korosho. Maana yake ni kwamba ile fedha ndiyo iliyokuwa inatumika kutengeneza ama kuandaa miche. Wataalam wa Hazina wapo pale wananisikia wamekwenda kule wamezunguka Lindi na Mtwara kwenda kuangalia wale watu waliokuwa wanaandaa miche na walikuwa wanasema wanakwenda kufanya tathmini, wamefanya tathmini wamemaliza wanawalipa lini, wale watu wanalipwa lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoongea hapa kuna watu leo nyumba zao zimewekwa bond na benki, Bodi ya Korosho iliingia mikataba na wazalisha miche, mpaka sasa hakuna. Nimezungumza na wale watu ambao walichukua tender Jimboni kwangu, nilikutana nao juzi, nikazungumza nao wanalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango anatakaje, tuache kulima korosho, atuambie? Anayesema kwamba asilimia 65 siyo fedha ya wakulima maana yake ni nini? Fedha hii ndiyo ilikuwa inafanya utafiti, wakumbuke kwamba Kituo cha Utafiti cha Naliendele ndiyo miongoni mwa vituo bora vya utafiti vya korosho Barani Afrika, imepata na tuzo, wao ndiyo wamefanya utafiti wa korosho wamepeleka korosho Nigeria, wamefanya utafiti wa korosho wamepeleka korosho Gambia, wamepeleka korosho Ivory Coast, jana nimewaona watu wa Naliendelea wanalalamika hawajapata fedha ya maendeleo hata shilingi kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umezuka ugonjwa wa mikorosho, wote wameona Waziri wa Kilimo alikuwa anahangaika hapa na Naibu wake, umezuka ugonjwa mikorosho inakauka kule Liwale, wanashindwa kufanya utafiti hawa hawana fedha hata shilingi tano, sasa kuna mtu anasisima anasema fedha za export levy siyo za wakulima ili iweje, mikorosho ife?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango nimemsikia Mwenyekiti wangu wa Wabunge wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Bwege ametangaza maandamano waandae Magereza watatufunga. Kama wameandaa Askari kuja kutukamata kutupiga watatupiga ikitokea mpaka tarehe Mosi tunatoka hapa fedha bilioni 200 hawajapeleka, tunakwenda kuandamana tunadai fedha zetu tutafunga barabara, hatutakubali kwa sababu ni fedha zetu, ni fedha za wananchi, wanataka kuua zao la korosho tubaki kuwa maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango ni Mchumi, Mchumi wa aina gani ambaye hafanyi affirmative action kwa watu maskini. Ninachojua Serikali kunapokuwa na gap kubwa la maendeleo baina ya walionacho na wasionacho, hawa wasionacho wanafanyiwa affirmative action. Watu wa Mikao ya Lindi na Mtwara mara nyingi tumekuwa maskini, kiwango cha umaskini Lindi na Mtwara ni kikubwa, kitu pekee kingeweza kutusaidia ni zao la korosho, leo wanataka kuliua! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili hatukubali kabisa, it is nosense to remain here wakati korosho wanataka kuiua, hatutakubali kubaki Bungeni wakati korosho wanataka kuiua hatukubali, kwa sababu ndiyo njia pekee ya kutokea wananchi wa Lindi na Mtwara. Huu mjadala ulioletwa wa kutaka kuja kubadilisha sheria, wanataka kuja kubadilisha sheria ili pesa hizo wazichukue, wakae nazo, wapange lini tuwapelekee na lini tusiwapeleke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoongea kama labla hawajui sasa hivi kuna maeneo korosho zimeanza kuokotwa. Mimi mwenyewe ni mkulima wa korosho ninasema hilo, nimekwenda shambani kwangu nimekuta korosho zimeanza, tayari, mpaka leo Bodi hawana hata mfuko mmoja wa sulphur hizi korosho watazipata wapi, shilingi trilioni 1.3 ya fedha ya korosho kama ya mwaka jana wataipata wapi? Mheshimiwa Dkt. Mpango huu ni uchumi wa aina gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tuseme labda watatuelewa, kwamba katika suala la korosho fedha shilingi bilioni 210 ambazo zimebaki zilikuwa bilioni 210, shilingi bilioni kumi mmepeleka, bado bilioni 200 fedha hii Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango apeleke. Apeleka kabisa wakulima wa korosho hatumwelewi na hatutamwelewa maisha yote. Hii habari tunaongea mchana wengine mpaka usiku tukilala tunaota kwenye ndoto, hii habari siyo ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wangekuwa wanajua huko wakulima wanasemaje wala wasingekaa hapa wakasema, kwa sababu ninachokiona kama wakishindwa kabisa wajue kwamba hicho Chama chenu ndiyo kinakufa Kusini na we are very serious! Watu wa Lindi tuna historia ya kufanya hivyo. Nawaomba sana hili jambo wali-take very serious. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nimesikia suala la Gaming Board, hii Bodi ya Michezo ya kubahatisha pia nimeona namna wanavyotaka kuongeza tax. Ukiwasikiliza wadau wa michezo ya kubahatisha wanasema wanachokipata wao ni 1.4 percent. Sasa hivi wanataka kuwaongezea kodi ya mashine kutoka Sh.32,000 mpaka kufika Sh.100,000 kwa mashine moja. Nimekutana na Taasisi moja wanasema wao wana mashine 1,550 kwa mwezi wanalipa kodi shilingi milioni 49. Leo wakiwaongezea kodi ya Sh.100,000 maana yake michezo yenyewe itakwisha watashindwa kabisa hata kupata hiyo kodi yenyewe. Sasa hivi kupata kidogo ambacho wanakipata kila mwezi, TRA wanakusanya na kukosa kabisa lipi ni jema? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii kama hawajui sasa hivi wamebatizwa jina badala ya kuwa ‘Hapa Kazi Tu’ wameitwa ‘Hapa Kodi Tu’. Wamekuwa ni watu wa kodi tu!

T A A R I F A . . .

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea taarifa, sijatetea kamali. Maana yake ukisema hivyo unasema kwamba watendaji wote kila mtu ana dini yake hapa ndani, maana yake tusifanye shughuli za Kiserikali hilo jambo halipo. Ninachokisema kwamba kama tunaamua ku-discourage, tu-discourage totally kwamba Tanzania hatutaki michezo ya kubahatisha. Kama tunaamua iwepo kwa ajili ya kutengeneza ajira za vijana, basi tuamue kwamba iwepo na itozwe kodi inayostahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho najua muda umekimbia sana, bajeti discipline. Mheshimiwa Dkt. Mpango tunaweza tukapanga fedha nyingi sana hapa, je, nidhamu ya utoaji wa fedha iko wapi? Changamoto ya Serikali tangia Mheshimiwa Dkt. Mpango umekuwa Waziri ni nidhamu ya bajeti. Bajeti discipline ni ndogo, kinachopangwa na Bunge sicho kinachoenda kufanyika. Leo wanaweza wakapanga shilingi fulani ziende huku hata fedha ambazo zimekuwa ring fenced wanazitumia kwenye matumizi mengine. Nidhamu ya kibajeti haipo na hili ndiyo tatizo kubwa ambalo linawapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini hii bajeti wanaosema inawezekana ikawa bajeti hewa ni kweli. Ukisoma kitabu cha bajeti inaonesha mapato ya ndani yatakuwa trilioni 18, maana yake ni kwamba kila mwezi watakuwa mnakusanya 1.5 trilioni, ukipiga mahesabu matumizi ya kulipa deni pamoja na watumishi wa umma ndo hiyo 1.5 trilioni, fedha za maendeleo ziko wapi au ndiyo wanakwenda kukopa kwenye hiyo mikopo ya kibiashara ambayo inasababisha riba kubwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na discipline ya kibajeti lakini changamoto nyingine walionayo ni kwamba namna ya matumizi ya fedha, sioni kama kuna dalili ya fedha za ndani zitatumika kwenye miradi ya maendeleo na kusipokuwa na fedha za ndani kwenye miradi ya maendeleo tukategemea wahisani na mikopo tu, mpaka Mheshimiwa Magufuli anatoka nchi hii ataacha deni kubwa kabisa ambalo litakuwa siyo himilivu na halitalipika na Rais ajae atakuta mzigo mkubwa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi.