Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Ally Yusuf Suleiman

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mgogoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu Subhannahu Wataalah aliyeniweka hai mpaka leo nimefunga Ramadhani, nimemaliza sita, kwa hivyo leo ni sikukuu kwangu Alhamdulillah. Pili namswalia Mtume Muhammad (Swalallah alayh wasalaam).

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sana nitakuwa ni mtu mwenye kushangaa shangaa lakini wewe usishangae. Jambo la kwanza ambalo linanishangaza sana ni kuangalia pande mbili za Muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika kwa upande mmoja, lakini upande wa pili tuangalie Zanzibar na nchi zote za Afrika Mashariki huo ni upande wa pili. Kipi cha kuangalia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tumeshuhudia kwamba bajeti za nchi za Afrika Mashariki zimesomwa siku ya Alhamis tarehe 14 Juni, 2018, lakini Bajeti ya Zanzibar imesomwa juzi tarehe 20/6/2018 hii ni kwa sababu gani? Je, Zanzibar haimo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki au vipi? Kwa nini Zanzibar inabaguliwa kiasi chote hiki. Sababu tunaijua, sababu ni kwamba kwanza ni lazima Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa upande wake awasilishe Wizara yake ijulikane marekebisho ya kikodi ndiyo baada ya hapo Zanzibar nayo waige, wafuate mfumo ule. Kwa hivyo, haiwezekani kabisa kabisa kwa Zanzibar kusoma bajeti siku moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baya zaidi ni kwamba kwa kawaida Bara huwa wanaunda vikosi kazi vya kushughulikia mambo ya kikodi na mambo ya kibajeti. Wakishamaliza wenyewe kwa wenyewe ndiyo wanaalika wadau kwa jumla waje na wao watoe maoni yao ikiwemo Zanzibar inaalikwa kama mwalikwa wa kawaida tu na siyo kama mshiriki wa Muungano. Ni kwa nini Zanzibar inafanyiwa hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka atakapokuja Mheshimiwa Waziri atueleze ni kwa nini Zanzibar isishirikishwe katika vikosi kazi badala yake ibaguliwe kiasi kikubwa namna hiyo. Kwa sababu kama tunakumbuka mwaka 1985, Zanzibar na Bara walipitisha bajeti siku moja. Bara wakashusha kodi, Zanzibar wakapandisha ikalazimu Zanzibar iitake Bara ilipe tofauti na ikalipa tofauti. Je, wanataka tuendelee na hali hiyo? Hakuna haja, tushirikiane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili Serikali iliunda Akaunti ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa Ibara ya 133 ya Katiba kupitia Sheria Na. 15 ya mwaka 1984 ili kila upande usimamie uchumi wake na masuala ya Muungano pia yasimamiwe na shughuli za Muungano. Ni miaka 34 tokea Tume hii ilipoundwa mpaka leo hii nilijibiwa wiki mbili zilizopita na Waziri wa Fedha kwamba akaunti hii haijafunguliwa miaka 34. Waziri atakapokuja jambo la kwanza atuambie hii akaunti itafunguliwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linatuonesha ni vipi Serikali ya Muungano ilivyokuwa haina nia njema kwa Zanzibar, kabisa. Serikali ya Muungano haina nia njema kwa Zanzibar kwa sababu kwa kuunda Tume hii au kwa kuunda akaunti hii matatizo mengi sana ya kifedha, ya kikodi yangelikuwa yametatuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uwoga huo wa Serikali tumeshindwa kuelewa mambo mengi sana kwa mfano, hivi sasa hatujui mahitaji halisi ya Muungano ni kiasi gani, matumizi ya Muungano hatujui ni kiasi gani, hatujui mchango wa kila upande katika Muungano ni kiasi gani, pia hatujui hata kodi zipi ni za Muungano, kodi zipi siyo za Muungano, nia njema haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, study iliyofanywa na PriceWaterHouseCoopers imeonesha kuwa vyanzo vya mapato vyenye vinasaba vya Muungano kwamba vyanzo hivyo vinatosha kabisa kuendesha Muungano kwa mambo ambayo ni ya Muungano. Pia pande mbili za muungano zikabakiwa na vyanzo vya kutosha kwa ajili ya kujiendesha kila upande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya mfuko huo mpaka leo hii haujaanzishwa na wala nia haipo, tunaambiwa tu kwamba majadiliano yanaendelea. Miaka 34 majadiliano hayajakamilika, hebu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango atuambie tumpe miaka hamsini na ngapi tena ili akaunti hii ya pamoja ianzishwe. Nataka kusema kwamba kama wanataka kujua kero za Muungano, basi hii ni kero mama katika kero za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa kweli nashangaa tena na napata mashaka makubwa sana juu ya nia ya Tanganyika kwa Zanzibar. Najiuliza ni faida zipi hasa za kiuchumi ambazo Zanzibar zinapata kutokana na Muungano huu kwa sababu jambo lolote ambalo ni la Zanzibar, Bara halitakiwi. Sukari ya Zanzibar imekataliwa, ukileta bidhaa kutoka Zanzibar tunaambiwa kwamba tulipie kama vile bidhaa inatoka Dubai. Jamani huu Muungano uko wapi? Muungano uko wapi ndugu zangu nataka kulijua hilo mnieleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha sana hata lile ambalo ni haki ya Zanzibar, hatupewi, kwa mfano katika suala la uajiri ni asilimia 79 Bara, asilimia 21 Zanzibar, hata hili halijatekelezwa mpaka leo hii, lini tuambie litatekelezwa suala hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yote yenye maslahi na Zanzibar basi tunanyang’anywa. Leo hii tumeambiwa kwamba usajili wa meli tunataka kunyang’anywa, jamani! Mnatutakia nini Zanzibar?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumze kidogo tu Kisiwa cha Fungu Mbaraka au kinaitwa Latham Island. Latham Island imepandishwa bendera ya Zanzibar pale tarehe 19 Oktoba, 1898, tokea wakati huo kisiwa hiki ni milki ya Zanzibar na hata siku moja bara haijawahi kusema kwamba ni chao, lakini waliposikia pale kwamba kuna block ya mafuta wamekuja mbio kwamba hiki kisiwa ni chetu. Nawa-challenge Mawaziri wote waliopo hapa waje hapa watuambie ni lini Bara imemiliki Kisiwa cha Latham Island, wote nawa-challenge waje hapa waniambie, lini wamekimiliki kisiwa hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bara zipo fursa nyingi sana. Tanzania Bara kuna madini, mbuga za wanyama, kilimo, mifugo na gesi, Zanzibar hakuna chochote lakini inapotokea tundu moja tu kidogo kwamba kuna heri inataka kuja haraka wanakwenda kuiziba, tukiuliza jamani kulikoni, wanatuambia atakayeuchezea Muungano tutapambana naye kwa thamani yoyote. (Makofi)

Ahsante.