Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nami nichangie hotuba hii ya Bajeti ya Mapendekezo ya Serikali kuhusu Mapato na Matumizi yake kwa mwaka huu wa 2018/2019. Kabla ya kuanza kuchangia, nami nina utangulizi kidogo. Kwa muda mrefu sana tumekuwa tunapata lawama upande huu. Wenzetu upande wa barabara ya pili kule, wanaongea na kutusema kila tunapomsifu Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli, kwa mambo mazuri anayoyafanya kwamba wamefanya nchi siyo yeye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote viongozi wote wa nchi na viongozi wa Taasisi wanapata sifa zinazofanya na Taasisi zao kwa niaba ya Taasisi hizo. Tumekuwa na Viongozi kama Mheshimiwa Baba wa Taifa, Mheshimiwa Kwame Nkhuruma, Mheshimiwa Mao wa Uchina na wengine wote wamekuwa wanapata sifa za nchi zao za matendo yao kutokana na yale wanayoifanyia nchi. Pia kumekuwa na sifa mbaya, viongozi wanapata sifa mbaya ya matendo yao, kama vile sisi tulivyovamiwa na Iddi Amin. Yeye hakuchukua hata bunduki, waliotuvamia ni Askari wake, lakini lawama akapata yeye. Kwa hiyo, wenzetu upande wa pili wa barabara hii ya kuingilia Bungeni watuache tuendelee kumsifia Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa matendo yake, kwa sababu ndiyo sifa zake zilizomvaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya utangulizi huo, naomba niwashukuru sana na niwapongeze Mawaziri hawa wawili, Mdogo wangu Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mdogo wangu Mheshimiwa Dkt. Kijaji kwa kazi kubwa waliyoifanya kuandaa mpango huu wa Bajeti ya mwaka huu wa 2018/2019. Hawa ni Wachumi, wameonesha kwamba wamesomea kazi hii ya uchumi na ndiyo maana wanaitwa Madaktari wa Uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti yako hii, yako mambo mengi kwa manufaa ya wananchi. Hii ni bajeti ya wananchi kwa mara ya kwanza. Serikali ya Awamu ya Tano imeleta Bajeti ambayo sisi Sekta Binafsi tunaiunga mkono; watu wote Viwandani, wanaiunga mkono. Tangu tumeanza kuleta Bajeti hapa Bungeni, tangu nimeingia Bungeni, hakuna Waziri yeyote aliyeleta Mpango wa kusamehe madeni yanayotokana na riba za madeni ya wanaodaiwa na VAT. Hawa wameleta mfano mzuri sana, kwamba sisi, wale ambao tunadaiwa; mimi pia nadaiwa na VAT, naomba ku-declare interest. Nimefurahi sana na sio mimi tu na wafanyabiashara wote, Mheshimiwa Dkt. Mpango, tutalipa madeni hayo kwa kipindi cha miezi sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, bajeti hii imekuja na mapendekezo ya kusamehe ile kilichokuwa kinaitwa zamani kodi ya makampuni ya asilimia 30 na kwenda asilimia 20 kwa baadhi ya makampuni hasa yanayoanzishwa. Pia tumeona kwenye ngozi; na muhimu kabisa tumeona hata taulo za akinamama zimefikiriwa na ilikuwa adha kubwa sana na bei kubwa kwa watu kupata taulo hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninayo machache ya kusemea kama changamoto. Jambo la kwanza ni elimu. Elimu tumeona hapa Mzaramo, rafiki yangu Waziri wa TAMISEMI, ameongelea kwamba wanafunzi waliochaguliwa kwenda sekondari ni asilimia 75,000, lakini bahati mbaya sana wanaopata nafasi, wanabakia wanafunzi wengine 25,000 hawana pa kwenda. Kwa hiyo, njia pekee aliyopendekeza, tujenge madarasa ili tuweze ku-accommodate wanafunzi hawa kwa mwezi wa Nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mie nakuja na pendekezo lingine na naomba lifanyiwe kazi, linaweza likasaidia. Kwa nini tusiingie PPP na shule za watu binafsi ambazo zina miundombinu tayari, lakini tutoe hela ile ile ambayo ni unit cost ya kila mwanafunzi kwa mwaka huu waende kwenye shule zile wakati tunaandaa shule zetu, ziwe tayari kwa ajili ya intake ya mwaka kesho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, PPP inawezekana tunaiongelea ipo kwenye sera yetu; tuitumie kwa mara ya kwanza kwenye elimu, tupeleke wanafunzi hao kwa kuwalipia cost ile ile. Bahati mbaya au nzuri nimefanya research. Ziko shule nyingine za binafsi, cost unit ya mwanafunzi mmoja ni rahisi kuliko cost unit ya wanafunzi wanaolipiwa katika Shule za Sekondari za Serikali au za Upili. Napendekeza basi, Serikali ifikirie PPP na shule binafsi ambazo zitafanyiwa uchunguzi kwamba zinafaa, zinatoa mafunzo sawasawa na za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la pili ambalo pia ni muhimu kuliongolea, nalo ni Elimu ya Ufundi. Nimekuwa nasimama hapa mara kwa mara kwa maana mimi ni zao la Shule za Ufundi, lakini bahati mbaya Serikali inaongolea Sera ya Viwanda, lakini mafundi sadifu, nina maana technicians wa kuendesha viwanda hivyo hawapo, kwa sababu Shule za Ufundi hazitoshi na Vyuo vya Ufundi kipo kimoja tu cha DIT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mingi imepita, Serikali sasa ione umuhimu wa kuandaa chuo kingine ili kuzalisha mafundi sadifu (technicians) wengi badala ya kukazania VETA ambao wanatoa Artisans, ni kiwango cha chini cha Elimu ya Ufundi. Mafundi watakaoendesha mitambo hii viwandani wanatakiwa wawe na level ya FTC (Full Technical Certificate) au mafundi sadifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu atakapokuja ku-wind-up hii bajeti atuelezee mpango wa kuanzisha shule za ufundi; na ningependekeza shule za ufundi za Kata ili kwenye Kata kuanzishwe chimbuko la mafundi watakaoendesha ufundi wa viwanda vidogo vidogo huko kwenye kata na majimboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la Kiswahili. Kiswahili chimbuko lake ni hapa Tanzania, lakini hakuna sheria yoyote inayosema Kiswahili ni Lugha ya Taifa wala hakuna GN yoyote inayosema Kiswahili ni Lugha ya Taifa. Wenzetu Kenya wameitia ndani ya Katiba ya Kenya, kwamba Kiswahili ni Lugha ya Taifa. Sisi tulikuwa tunaandika hapa Katiba, ile Katiba inayopendekezwa, tuliweka suala hilomle; lakini wakati huu wa ombwe la Katiba Mpya, kwa nini Serikali isije hata na GN tu ili watu waongee Kiswahili badala ya kuongea lugha ambayo haieleweki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa Kiswahili imekuwa kitendawili mashuleni. Watoto wanasoma Shule za Msingi, mpaka darasa la saba Kiswahili. Wakifika Shule ya Upili, wanaanza kufundishwa Kiingereza, hawaelewi masomo, hawaelewi lugha. Nchi zote ambazo zimeendelea; Ufaransa, Uingereza, Marekani, Ufilipino na China wote wanafundisha kwa lugha ya kwao ambayo inayoeleweka. Hivi mwanafunzi akifundishwa Kiswahili, Serikali inaona tatizo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu inasema lugha ya kufundishia Shule za Upili na Shule za Utatu, ni Kiingereza, lakini huu ni Ukoloni. Nchi zote zote zilizojikomboa katika elimu zinafundisha kwa lugha zao. Naomba sana

Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind hili ili suala la mambo yanayohusu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, aongelee Kiswahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala lingine ambalo linaleta gharama kubwa sana katika Bajeti ya Mambo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Suala la nyumba za Mabalozi wetu; tumekuwa tunapanga nyumba kwa gharama; na asilimia 75 ya gharama zote za Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni pango za Balozi zetu; Ofisi na nyumba za wafanyakazi. Kwa nini tusiendeleze mpango uliokuwepo wa kujenga majengo ya Mabalozi wetu na nyumba za Makazi? Hata kama tutachukua miaka 10, lakini tutaweza kujenga nyumba hizo ili ziweze kuondoa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.