Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu, Subhannah-Wataalah.

Nianze kuuliza maswali kwa Wizara hii ya Fedha na swali langu la kwanza nilikuwa naomba kujua, kwa sababu Wizara hii ndiyo Wizara mama; na wakati tunachangia Wizara mbalimbali ambapo Wizara hii inaenda kutoa fedha; mara nyingi Mheshimiwa Waziri Mpango anakuwa hayupo ndani ya Bunge. Naomba kujua kwa nini Mheshimiwa Waziri Mpango huwa mara nyingi tukiwa tunachangia bajeti mbalimbali hizi ambazo yeye ndio kikwazo cha kutoa fedha kwenye miradi mbalimbali, ndani ya Bunge anakuwa hayupo? Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo naomba kujua kutoka kwenye Wizara hii, kuna suala hili la kutopeleka fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo. Hili limekuwa ni tatizo sana. Tulikuwa tunasikiliza taarifa ya Kamati hapa, ni asilimia tano tu ndiyo zimeweza kupelekwa mwaka 2017 kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo. Sasa tatizo nini? Tunaomba Mheshimiwa Mpango atueleze.

Mheshimiwa Spika, hapa naomba niongee kwa mifano kwamba miradi mbalimbali na hasa iliyopo maeneo ya Kusini mwa Tanzania, Mtwara na Lindi, Wizara ya Fedha imekuwa na kigugumizi kikubwa sana cha kupeleka fedha za maendeleo kwenye Mikoa hii ya Kusini.

Mheshimiwa Spika, mradi wa kwanza ambao naomba nizungumzie hapa ni mradi mkubwa ambao Serikali imekuwa inazungumzwa kabla hata hatujaingia kwenye mpango wa kujenga reli ya kati hii ambayo inaenda kujenga kwa kiwango cha standard gauge. Kusini kumekuwa kunazungumzwa mradi wa reli kutoka Bandari ya Mtwara kuelekea Mchuchuma, Liganga na Mbambabay na kule Kusini ili kuweze sasa kufunguka. Imekuwa inazungumzwa kwa muda mrefu sana na Mheshimiwa Waziri Mpango amekuwa anazungumza kila mwaka feasibility study na hizo pesa hajawahi kuzipeleka.

Mheshimiwa Spika, tunaomba atakapokuja kuhitimisha hapa, atueleze, kwa nini hataki kupeleka fedha za feasibility study ambazo kila mwaka wanaweka kwenye bajeti, wanaweka kwenye Mpango lakini hataki kuleta fedha hizi ili sasa ile Reli ya Kusini ambayo mwaka 1963 iling’olewa kwa makusudi kabisa na Serikali hii, ikapelekwa maeneo mengine, lakini hata kuirudisha mnakuwa na kigugumizi sana. Hata ile feasibility study hataki kuleta pesa. Mwaka 2017 tuliambiwa shilingi bilioni mbili zimetengwa kwamba Mchina sijui nani ameshapatikana, lakini mpaka leo zile fedha hazijaletwa na Mheshimiwa Mpango. Tunaomba atueleze wakati wa kuhitimisha bajeti, miradi hii ya Kusini anakuwa na kigugumizi sana kuleta fedha kwa ajili ya kufanya feasibility study.

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ambao naomba Mheshimiwa Mpango akija hapa atueleze, ni mradi wa maji ambao unatoka Mto Ruvuma. Hii ni bajeti ya tatu tunazungumza suala hili; na tatizo tunaambiwa ni Wizara ya Fedha haijapeleka fedha. Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma, vimechukuliwa zaidi ya vijiji 26 vya wananchi; wananchi wamechukuliwa maeneo yao, mashamba yao kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inasema itakuja kulipa fidia, lakini inasema Wizara ya Fedha haipeleki fedha kila mwaka. Sasa tunaomba akija hapa atueleze, kwa nini mradi ule mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvuma kuja Mtwara Mjini hataki kutoa fedha na kila mwaka anatenga Bajeti?

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ambao naomba Mheshimiwa Mpango aje atueleze hapa wakati wa kuhitimisha hii hoja, atueleze UTT PID ambayo ilichukua maeneo ya wananchi Mtwara, katika Mtaa wa Mji Mwema, mashamba yamechukuliwa pale, tangu mwaka 2013. Serikali ilikuja ndani ya Bunge hili ikasema kwamba inaenda kutoa fidia. Nina Hansard zaidi ya mbili ambazo Wizara iliahidi hapa kwamba itaenda kutoa fidia.

Mheshimiwa Spika, wananchi wamechukuliwa mashamba, wamechukuliwa maeneo yao ambayo walikuwa wanaendeleza kiuchumi, lakini mpaka leo tunavyozungumza, Wizara ya Mheshimiwa Mpango haitaki kupeleka fedha. Niliuliza kwenye Wizara ya Ardhi, nikauliza kwenye Wizara ya TAMISEMI nikaambiwa tatizo ni UTT PID ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha haitaki kupeleka fidia kwa wananchi hawa wa Jimbo la Mtwara Mjini. Naomba uje utueleze kwa nini hutaki kuleta fedha Mheshimiwa Mpango kwenye miradi hii iliyopo Mtwara na Lindi?

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze pia suala hili la EFD machines. Kuna hawa ambao wamepewa Uwakala (authorized dealers) ambao ndio wanaosambaza hizi mashine na wamechukua fedha kwa wananchi ambao ni wafanyabiashara wadogo wadogo maeneo ya Lindi na Mtwara hasa pale Mji wa Lindi. Wamelipa shilingi 690,000 lakini zile mashine hawazipeleki kwa wananchi. Wale mliowapa uwakala wa kusambaza EFD machines wanachelewesha kuzipeleka kwa wananchi, lakini kinachotokea sasa, TRA inaingia kwenye maduka yale na kufunga maduka na kuwabambikizia kodi wale wananchi, wakati Serikali haitaki kupeleka zile mashine kupitia dealers ambao mmewaweka ninyi Wizara ya Fedha. Tunaomba mkija mtupe maelekezo, kwa nini wananchi wanatoa fedha na wanakaa muda mrefu sana bila ya kuzipeleka zile mashine za EFD kwa wananchi, wafanyabiashara hawa wadogo wadogo?

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa naomba, Mheshimiwa Mpango hapa atakapokuja ku-wind up atueleze, ukija Mji wa Lindi na Mtwara miezi miwili iliyopita kulikuwa na hali ya ajabu sana.

Mheshimiwa Spika, naamini wakati nasoma historia niliweza kusoma kwamba wakoloni walivyokuja Tanzania, walikuwa wanakusanya capital kwa kutumia njia za ajabu sana. Walikuwa wanatumia njia inaitwa plundering, nyingine ni looting, grabbing and Kidnapping. Kitu hiki ndiyo kinachofanyika kwenye ukusanyaji wa kodi maeneo ya Mtwara na Lindi.

Mheshimiwa Spika, pale Lindi Mjini TRA wameweza kuwabambikia kodi wananchi, muuza matunda, ambaye anauza matunda, ndizi, nyanya, anauza embe akapelekewa kodi shilingi 700,000, anauza matunda ya shilingi 100,000 au shilingi 200,000 tu. Hili ni jambo la ajabu sana, akaambiwa afunge kibanda chake, asiuze, akapelekewa makadirio ya kodi shilingi 700,000; anauza matunda. Ni primitive accumulation of capital ambayo Watanganyika tulipigana kuondoa ukoloni huu kwa sababu ya kodi kandamizi.

Mheshimiwa Spika, kuna mtu mwingine ambaye alikuwa anauza vipodozi, akapelekewa makadirio ya kodi shilingi 8,000,000. Duka lake likafungiwa Lindi Mjini. Hata majina hapa ninayo, Mheshimiwa Mpango akiyataka nitampelekea. Ni jambo la ajabu sana. Tunaipeleka wapi nchi hii?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Mpango atakapokuja atueleze, ni kwa nini wafanyakazi wake katika maeneo ya Mtwara na Lindi wanatumia njia za kikoloni na kandamizi katika kukusanya kodi kitu ambacho ni kinyume kabisa na wananchi tulipigana na ukoloni kupinga mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu mwingine ni muuza chakula pale Lindi Mjini, stendi, anauza chakula (food vendor) akapelekewa kodi shilingi 4,000,000. Kama hatoi fedha hizo TRA mgahawa wake ulifungiwa, ni jambo la ajabu sana. Kwa hiyo, naomba sana kwamba hizi taratibu za kodi hakuna anayekataa kodi, watu wote sisi tuko entitled kulipa kodi, wananchi wako entitled kulipa kodi, lakini kodi ziendane kabisa na kipato. Tunasema pay as you earn; kadri mtu anavyopata ndivyo alipe kutokana na kipato chake na siyo kubambikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Mpango atakapokuja atueleze kwa nini maeneo haya ya Mtwara na Lindi kodi kandamizi zinakuwa ni kubwa? Maduka yamefungwa Mtwara, Lindi yamefungwa kwa kiasi kikubwa sana kuliko maeneo mengine ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie pia suala la miradi ya maendeleo. Taarifa ya Kamati imezungumza hapa, ni asilimia tano tu ya pesa za miradi ya maendeleo zimepelekwa mwaka 2017.

Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba maelezo ya kina, kwa nini? Kwa sababu tunahitaji pesa ziende ili maendeleo yaweze kuonekana na nchi yetu iweze kuwa na mapato. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa. kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Mpango atueleze kwa nini fedha za maendeleo zinapelekwa chache sana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa naomba nizungumze hapa na Mheshimiwa Mpango anipe maelezo, mwaka 2016 nilizungumza suala la ukaguzi wa CAG, ndani ya Bunge hili kwamba CAG amekuwa hakagui Taasisi fulani hivi za fedha. Kwa mfano, vile visima vile vya makusanyo ya gesi na mafuta CAG haendi kukagua na nikaomba kwamba uletwe muswada hapa kubadilisha zile sheria. Mwaka huu nashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wameniunga mkono, wamezungumza hilo, nami naomba nipate maelezo kwa sababu hata zile Taasisi za Kijeshi tunaona CAG anaenda kukagua, lakini taasisi hizi za fedha ambazo tunahitaji fedha zikusanywe….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nakushukuru sana, naomba Mheshimiwa Mpango atupe maelezo.