Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Joseph Osmund Mbilinyi

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, wakati unaingia uliona kulikuwa na makelele kidogo ilitokana na Mheshimiwa Ali King kututukana na kutuita Mbwa. Sasa kiti kitaangalia namna ya kumrekebisha lakini kama rafiki yangu namsamehe kwa sababu ni rafiki yangu tunakunywa naye pombe na tunakula nae kitimoto Sheikh Ali King. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni mtu wangu wa karibu nakula naye sana kitimoto.

T A A R I F A . . .

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, nashukuru hajakanusha kwamba tunakula naye kitimoto ile yeye hapendi ya mafuta. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijiekeleze kwenye kuchangia kwa mara nyingine niwashukuru sana wana Mbeya kwa namna walivyosimama na mimi nilipofungwa gerezani. Nawashukuru sana wana Mbeya na sitaacha kuwashukuru kwa sababu katika changamoto ile waliweza kunipa projection ya mbele tunaendaje na wanaendelea vipi na Mbunge wao. Wakati niko gerezani nilisoma na nilipata taarifa kwamba uliagiza Wabunge wa upinzani tupewa Ilani za CCM ili tuzisome. Sasa sina uhakika kama agizo lako lilitekelezwa, lakini naomba nikuhakikishie sio tu tuna Ilani ya Chama chenu lakini pia tuna list ya ahadi zenu za mwaka 2015. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hatuwezi kukaa na kuongea mapungufu yenu wakati hatuwafuatilii kwa hiyo tunawafuatilia. Mfano wa list ya ahadi zenu ni laptop kwa kila mwalimu ni hewa, lakini kuna hili suala la shilingi milioni 50 kila kijiji na kila mtaa ni hewa, mmeng’ang’ana na suala


la elimu bure lakini wote tunajua elimu bure ni disaster, ni kitu kizuri ambacho hakijapangwa. Kuna watu wanasema kwamba mlirukia ajenda ya CHADEMA kwenye suala la elimu bure kwa namna mnavyotekeleza inaonekana kama ni kweli hili suala mlilirukia tu. Kwa hiyo, tunachoomba kwa msisitizo kwa leo kwa Wizara hii ya Fedha Waziri Mpango atakaposimama au Naibu wake atuambie ni lini utekelezaji wa shilingi milioni 50 kila kijiji na kila mtaa zitaanza kupelekwa kule kwenye mitaa kwa sababu kuna mitaa 181 Jiji la Mbeya ambalo wanasubiri hizi shilingi milioni 50 kila mtaa tuna kazi ya kuzifanyia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hii ni nchi yetu wote tunapozungumza tuwe serious katika masuala kuna masuala tunaongea kiutani utani tu mfano ni ujenzi wa hosteli za Chuo Kikuu cha Da es Salaam maarufu kama Hosteli za Magufuli, Mheshimiwa Rais. Tunaambiwa mnasema na mnang’ang’ania kwamba ujenzi wa zile hosteli ni shilingi bilioni 10 tu majengo 10 ina maana kila jengo moja lenye ghorofa nne ni shilingi milioni 500. Kama ingekuwa kweli hivyo hata mimi ningejitolea kujenga majengo mawili pale. Lakini niko kwenye Kamati ya Maendeleo na Huduma ya Jamii ambayo masuala ya elimu yako chini yetu tumeshakwenda pale kutembelea ule ujenzi ukweli ni kwamba pale zimetumika shilingi bilioni 54 plus na sio shilingi biloni 10 zilizotumika. Lakini nashangaa sijaona ripoti ya CAG katika suala hili, sijui ni nini au ni nani au ni maagizo kutoka juu ndio yamezuia hili suala watu wanang’ang’ana shilingi bilioni 10 wakati kitu ni uwazi kabisa hesabu zinasema shilingi bilioni 54 plus ndio zimetumika kujenga ule ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza hivi tunamdanganya nani hii nchi yetu sote tunamdanganya nani? Kama ni fedha, hizo fedha ni zetu sisi kama Taifa sio mali ya mtu binafsi. Sasa kwa nini tunapeleka mambo namna hii niliwahi kusema katika Bunge hili numbers don’t lie, women lie, men lie but numbers don’t lie na bahati mbaya tunapozungumza masuala ya fedha ni namba sio maneno maneno, fedha ni namba; shilingi bilioni 10 na shilingi bilioni 54 ni namba mbili tofauti. Tunakwenda masuala ya fedha


hizi fedha ni zetu wote sio fedha za mtu binafsi. Tunahoji kuhusu shilingi trilioni 1.5 ambazo matumizi yake hayajulikani hatujasema kwamba mmeiba tunasema tunata kujua zimeenda wapi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hakuna sehemu sisi tumesema kwamba mmeiba hizi hela sasa nyinyi mnasimama mnasema fulani! Simama eti! Kweli hela zimeibiwa? Hazijaibiwa Mheshimiwa! Hakuna mtu aliyesema kwamba hizi fedha zimeibiwa ila tunahoji kwamba hizi fedha shilingi trilioni 1.5 ziko wapi please explain shilingi trilioni 1.5 zimekwenda wapi hiki ndio kitu ambacho tunahitaji sisi kwa sababu hii nchi ni yetu sote na nchi sio sebule ya familia kwamba tu tunapelekana tu. Hii nchi mambo madogo yanatushinda, hili ni Taifa ambalo linashindwa kushonea uniform hata askari wake magereza pamoja na wafungwa, hili ni Taifa ambalo linashindwa kulisha na kutibu wafungwa wake, watu wanakufa kiholela na ukitaka kupima umaskini wa Taifa chunguza magereza zake, ukiingia katika magereza zetu utakuta taswira halisi ya umaskini wa Tanzania kupitia maisha yanayoendelea mle ndani. Watu hawana chakula, watu hawana madawa, mtu kafungwa unamwambia alete bima ya afya wakati haruhusiwi hata kutembea na shilingi 1,000 mle ndani, bima ya afya ataitoa wapi? Tunashindwa na mambo madogo sana . (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nchi hii leo tumefika mahali eti kubeba ndoo ya samaki kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam na maeneo mengine lazima uwe na kibali kweli mboga! Kitoweo! Na hii halafu mnasema mnakuza ajira. Kwa sababu unavyozuia ile biashara ya wale kina mama wengi wao wakiwa wajane pale Mwanza wanauza ndoo za samaki. Mheshimiwa Jenista wakati ule ukiwa Mwenyekiti wangu kwenye Kamati, tulikuwa tunakumbushana sana kubeba samaki tukitoka ziara Mwanza na Mara kubeba samaki kwenye ndoo. Lakini hii Serikali yako ambayo wewe ni Chief Whip inakataza inasema kwamba marufuku kubeba samaki hata watatu/wanne/watano ni lazima uwe na kibali kubeba Samaki wa Mboga kutoka Mwanza. Kweli Mheshimiwa tumefika hapo? (Makofi/Kicheko)


Mheshimiwa Spika, kulipa kodi ni wajibu, nashauri TRA iwe rafiki wa walipa kodi, iache kufanya utafikiri yenyewe ni polisi. TRA inafanya kazi kama polisi na sometimes inatumika kisiasa. Angalia walichomfanyia Kakobe. Kakobe katoa mawazo yake kama raia, Mtanzania na kiongozi wa waumini. Mara wamemwita, mara wanahoji kodi, mara sijui wanahoji nini, matokeo yake wamekosa kile walichokuwa wanakitafuta kwa Askofu Kakobe, wanakuja wanasema ooh, hana tatizo lolote na yeye hana hela ila Kanisa lake lina shilingi bilioni nane. Who asked you? Nani amekuuliza Kanisa la Full Gospel lina kiasi gani benki? Wanaingilia na kutoa ripoti za fedha za taasisi za watu bila kuulizwa na bila utaratibu. Kwa sababu kanisa sio Kakobe, kwa nini kama ulitaka kumchunguza Kakobe na umekuta hana kitu, unaanza kutoa taarifa za Taasisi ya watu?

Mheshimiwa Spika, sasa hayo mambo ya TRA yako mengi sana na tumeelezwa mengi sana. Mbeya Songwe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Naomba dakika moja tu, wanakata sana dakika hao. Hii ni namba yangu ya mfungwa jela, ambayo nitaendelea kuivaa kadri nitakavyojisikia. Kuhusu suti wewe unanijua, ni kawaida yangu kupiga suti kali.

Mheshimiwa Spika, mambo haya ya kuingiza siasa kwenye uchumi, TRA wanasababisha Mbeya na Songwe tumechoka. Sasa hivi tunapoongea, wafanyabiashara wa Tunduma wanahama, wanaenda kufanya biashara upande wa Zambia. Wanafanya biashara Zambia wanakuja kulala Tanzania. Hapa ndiyo tulipofikia na sisi yetu ni macho, lakini hii ngoma ishakwama inaonekana wazi kabisa.