Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hoja hii muhimu sana ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati Dkt. Kalemani na Naibu wake Mheshimiwa Subira Mgalu kwa utayari wao wakati wote kuwasikiliza Wabunge na kupokea ushauri wao na kuufanyia kazi. Kiukweli Mheshimiwa Dkt. Kalemani na Mheshimiwa Subira Mgalu ni mfano mzuri wa Mawaziri ambao wanasikiliza Wabunge na kufanyia kazi kero za Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati REA awamu ya III inaanza, Waheshimiwa Wabunge tuliombwa tutoe mapendekezo katika maeneo yetu kwamba ni vijiji gani ambavyo tunadhani ni muhimu vipatiwe umeme. Waheshimiwa wote tulitoa mapendekezo yetu lakini orodha ya REA awamu ya III ilipokuja kulikuwa na mkanganyiko mkubwa sana, vijiji vingi vilikuwa vimerukwa, vimeachwa na vingine ambavyo siyo muhimu ndiyo vilikuwa vimewekwa. Niwapongeze tena Mheshimiwa Dkt. Kalemani alikuwa very flexible, alizingatia kwa umakini hoja za Wabunge na marekebisho makubwa yalifanyika karibu Wabunge wengi maeneo mengi ya vijiji ambayo yalikuwa yamerukwa au yameachwa yakawa incorporated kwenye REA awamu ya III.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu kwa mfano vijiji muhimu kama Vijiji vya Mwamala, Lububu, Kayombo, Sekondari ya Kili, Karitu na vingine vilikuwa vimeachwa kimakosa lakini baada ya kumfuata Mheshimiwa Waziri na kumuelezea umuhimu wa vijiji hivi alikuwa very flexible, aliwasiliana na REA na pia niwapongeze REA kwa sababu nao waliitikia kwa uharaka na sasa hivi tunavyoongea vijiji hivi vimo kwenye REA awamu ya III na kazi nzuri inaendelea. Mheshimiwa Dkt. Kalemani na Mheshimiwa Subira Mgalu hongera sana na naomba muendelee na ari hiyo hiyo ya kusikiliza Wabunge na kufanyia kazi hoja zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea suala la uwezo mdogo wa TANESCO kukidhi mahitaji. Hili jambo ni very serious, inabidi jitihada za makusudi zifanyike ili kuisaidia TANESCO iweze kukidhi mahitaji ya wateja. Hali ilivyo sasa hivi kwa TANESCO kwa kweli siyo ya kuridhisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ya Nzega, Ofisi ya TANESCO Nzega, leo hii kuna malalamiko makubwa sana. Wateja ambao wamelipia ili wapatiwe umeme tangu mwezi Januari mpaka leo hawajaweza kupatiwa umeme, tunakaribia miezi sita (6) sasa. Speed hii ni ndogo mno na kwa standard na level yoyote ile haikubaliki. Haiwezekani mteja alipie kupata huduma tangu Januari mpaka leo tunakaribia Juni hajaweza kupata huduma. Ni kipindi kirefu sana na wananchi wanakata tamaa na huduma ya namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba hiki kilio cha uwezo wa TANESCO, Serikali ikifanyie kazi. Kwa kweli TANESCO wamechoka na uwezo wao ni mdogo sana. Nitakupa mfano, Jimbo langu kuna Kata inaitwa Mambali ni kilometa 40 kutoka Nzega Mjini kina huduma ya umeme, ikitokea technical fault pale TANESCO Mjini Nzega hawana hata uwezo wa kufika kilometa 40, hawana hata gari lolote la kubeba nguzo, kubeba vifaa vya kujengea, hivyo, hawawezi ku-attend technical fault yoyote ambayo iko nje ya Mji wa Nzega na TANESCO Nzega inahudumia radius kama ya kilometa 40 ama 60 hivi. Kwa hiyo, hali TANESCO ni mbaya, hawawezi kukidhi mahitaji ya wateja. Haiwezekani mtu asubiri nguzo miezi sita wakati ameshalipia, hili kwa kweli lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema REA awamu ya III, tatizo ninaloliona hapa ni speed ndogo sana. Nikubaliane kwa sababu REA inachofanya ni kusambaza umeme, kinachotakiwa sasa hizi jitihada kubwa za kusambaza umeme vijijini lazima ziendane na ongezeko la uzalishaji wa umeme kwa sababu huwezi kusambaza bidhaa ambayo hujaizalisha, huwezi kusambaza kitu ambacho huna. Kwa hiyo, niunge mkono hoja aliyozungumza Mheshimiwa Simbachawene kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa na uzalishaji wa uhakika wa umeme wa kutosha ndipo tuusambaze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu REA wanachofanya ni kusambaza lakini huwezi kusambaza kitu ambacho hakijazalishwa. Kwa hiyo, jitihada kubwa bado nashauri kwamba Serikali iendelee na miradi yake ya kuzalisha umeme kwa wingi ikiwemo Stiegler’s Gorge ili tupate umeme wa kutosha ambao ndiyo sasa utasambazwa kwenye vijiji. Hatuwezi kukazania usambazaji wakati hatujui sasa utasambaza nini kama umeme huo haujazalishwa. Kwa hiyo hilo, naomba lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie bomba la mafuta…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.