Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

Hon. Ussi Salum Pondeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chumbuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo amewasilisha hotuba yake hii ya Wizara ya Nishati na Madini. Pia niwapongeze Watendaji Wakuu wa Wizara hii ya Nishati akiwemo Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Wakurugenzi wa REA, TPDC kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi vizuri na wanaweza kufikia yale malengo ambayo sote matarajio yetu ni kuiona Tanzania ya viwanda inakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema maneno haya kwa sababu tunaposema Tanzania ya viwanda tunaitaka bila umeme wa uhakika basi hatuwezi kuipata, lakini kwa kasi ambayo wanakwenda nayo Mawaziri hawa na Watendaji wao, tuna uhakika vission yetu ya 2020 tunao uwezo wa kufikia malengo haya. Tunachotakiwa ni sote humu ndani kama Wabunge kuishauri Serikali na kuwasaidia hawa katika juhudi zao ambazo wanaziendeleza katika kufanikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika ili tuweze kufikia malengo yetu yale ambayo tunayakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nishauri Wizara na Mheshimiwa Waziri kwa upande wa REA. Mimi ni Mjumbe wa Kamati tumetembelea miradi na tumekutana na matatizo mengi ikiwepo scope of work kwa maana kwamba maelekezo yanatolewa kwenye vitabu lakini mkienda field sivyo ilivyo. Hili ni tatizo kubwa ambapo wakandarasi wengi ambao tumewahoji hawana majibu mazuri, wanakwambia mimi scope yangu mwisho hapa, lakini wananchi wanalalamika wanasema katika kijiji chetu mradi umekuja lakini waliopata ni watu wanne, watano hawazidi 10. Kwa maana, hiyo upatikanaji au ile dhana kamili ya kusema wananchi wote watapata umeme wa REA inakuwa haifikiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine nataka nilizungumzie nalo ni kuhusu REA kupewa pesa kwa wakati. Sehemu zote ambazo tumetembelea, miradi tunaikuta imesimama au inasuasua tatizo kubwa ni fedha. Ukiwauliza kwa nini fedha hampati, tumejaribu kuwahoji REA na Wizarani, tatizo kubwa ni Wizara ya Fedha kutotoa fedha kwa wakati. Hili suala linazungumzwa karibu katika kila Wizara kwamba Wizara ya Fedha imekuwa kila pesa ambayo inatengwa lazima iwe inafanyiwa uhakiki, hatukatai kufanya uhakiki, lakini kuna mambo mengine ambayo kama hii REA ambayo iko ring fenced inachukua muda. Kuna time watu hawajalipwa imefika mpaka miezi nane, watu wanasubiri lini watalipwa ili waweze kupata material. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema sasa tuna matarajio ya kufika mpaka mwaka 2020...

TAARIFA . . .

MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sikubaliani naye na taarifa siipokei, hii tunajua ipo na akitaka ushahidi nafikiri kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameeleza, hiyo taarifa yake siipokei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maana kuwa REA lazima wapewe pesa kwa wakati ili tuweze kufikia malengo yetu yale ambayo tumekusudia ya kuhakikisha uchumi wetu unatoka uchumi wa chini na kuwa uchumi wa kati. Hapa kila Mjumbe ambaye amesimama, jambo kubwa ambalo tunalizungumzia ni jinsi gani pesa zitatoka Wizara ya Fedha kuja REA ili wakandarasi waweze kulipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie kwa ruhusa yako ni kuhusu tatizo la deni la Zanzibar. Kuna taarifa ambayo mazungumzo yameanza na yanaendelea kwa sababu imekuwa kuna sintofahamu katika suala la deni la TANESCO, katika taarifa zao wanasema wanadai hivi lakini reality haiko hivyo. Kwa sababu mazungumzo yameanza kufanyika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho naomba hili aliweke wazi limefikia hatua gani na kuna nini ambacho kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni tatizo kubwa sana kwetu Wazanzibar kila mwaka linajirejea hili na inafika pahali watu tunaonekana labda kama vile tunapata kitu cha bure au hatulipi, tunasaidiwa. Kwa sababu sisi tunajiamini na tuna uwezo wa kulipa current bill kabisa kama tunavyolipa sasa hivi, nakutaka Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa aje atoe taarifa hii ya kuhusu Zanzibar tunavyolipa umeme, deni na current bill ambayo tunatumia kila mwaka. Kuhusu suala la bei tutalizungumza baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, sitaki niendelee sana maana nitatoa utamu wa haya maneno yangu ambayo nimemalizia, naunga mkono hoja.