Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wote wangetamani kupata nishati ya umeme popote walipo, wawe wa mjini au vijijini. Kwa hiyo, ushauri wangu kwanza ni kwamba, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri wa Fedha miradi ya umeme popote ilipo, iwe ya TANESCO au REA, fedha itoke ikamilike watu watoke gizani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna faida nyingi sana, kwanza kuna usumbufu mkubwa sana mtaani. Watu wa Dar es Salaam na maeneo mengine wanazuiliwa wasitumie mkaa na wanakamatwa sana, wanapigwa, wanateswa na watu wa Maliasili, lakini gesi ni ghali sana, umeme ni ghali na haupatikani. Kwa hiyo, mkitaka ku-save maliasili yetu kwa maana ya misitu lazima umeme upatikane kwa bei ya chini na gesi kwa bei nafuu, ili wananchi wa-opt waone kwamba, kununua gunia Sh.70,000 ni gharama zaidi kuliko kulipia umeme, kwa hiyo, misitu itabaki salama na hali yetu ya maisha itakuwa nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Dar es Salaam hasa Ukonga, kuna mitaa haina umeme kabisa. Sasa watu wakiambiwa waende mjini wanafikiri maana yake umeme upo, unafahamu katika mitaa tisa ya Kata ya Msongora ni mitaa miwili ambayo ina umeme, mitaa mingine haina umeme na hata maeneo ya shule. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifika mpaka usiku akaona hakuna umeme pale Ukonga Msongora, Chanika, Kidugalo, Vikongoro, Zavala, mitaa yote sita kati ya mitaa nane, hakuna umeme Buyuni, Kivule, Mvulege, Banguro, tuna mitaa mingi ambayo haina umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu TANESCO na hapa ndiyo nasema inatakiwa itengenezewe utaratibu mwingine, wananchi wana fedha mkononi wanalipia umeme zaidi ya miezi sita unaambiwa nguzo na mita hazipo, hili ni shirika la kibiashara, TANESCO wameshindwa kufanya biashara. Watu wana pesa zao, wanahitaji umeme, wanalipia, TANESCO haipeleki umeme. Ndiyo maana watu wanasema TANESCO hii kunatakiwa kuwe na chombo kingine washindane kama ilivyo kwenye mambo ya simu. Kama tungekuwa na shirika lingine ambalo TANESCO wakiweka bei Sh.320,000 mwingine aweke Sh.270,000, mwingine Sh.250,000, labda hao wangeamka kutoka usingizini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri alipokee hili. Kwenye taarifa mbalimbali inaonesha kwamba TANESCO inajiendesha kwa ma-trilioni ya fedha kwa maana ya hasara. Kwa hiyo, tungependa tupate taarifa halisi kwa nini TANESCO, Shirika la Umma kodi yetu, linajiendesha kihasara na nani anasababisha? Tuone tatizo ni nini? Watu wanahitaji umeme, kila mahali ukisoma taarifa za TANESCO kuna hasara wanaingia. Tungependa tujue kama Taifa na kama Bunge kwa nini kuna hasara TANESCO? Ni muhimu sana hili jambo likafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gharama ya umeme. Kuna hoja hapa maeneo ya mjini wanalipia Sh.321,000 hata kama huhitaji nguzo, vijijini Sh.170,000. Watu wa mjini siyo kwamba wana uwezo mkubwa, ambacho kingefanyika kuna watu mjini ni maskini kweli, ana kijumba chake anahitaji umeme hapati kwa sababu ya gharama kubwa, kwa hiyo, ninyi mngeangalia watu ambao hawana uwezo, Wenyeviti wa Mitaa, Wabunge, Madiwani wanajua mtu ambaye hana uwezo apewe bei nafuu, wale wenye uwezo wapewe bei ambayo inawezekana, lakini mkisema mjini na vijijini mtaumiza watu wengine. Mjini wengine wanakaa kwa sababu tu ya majina lakini hawana maisha mazuri, ni maskini, hawasomi na ndiyo maana TASAF iko mjini na vijijini na Ukonga kwangu Kivule ipo. Hivyo, hili jambo Mheshimiwa Waziri mliangalie vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ni ya umma. Kuna shule hazina umeme, wana visima vya maji, walimu wanahitaji photocopy wachapishe mitihani, hata kufeli mitihani kwa wanafunzi wetu ni mazingira. Kwa hiyo, hili suala la umeme ningekuwa mimi, kama ilivyo Idara ya Maji, Serikali ingekuja na mpango mkakati, wametuambia vijiji vyote watapata umeme, Wabunge wanatarajia, wananchi wanasubiri lakini umeme haupatikani, hili jambo lingeisha. Huwezi kwenda kwenye viwanda kama hata umeme majumbani hauna, haiwezekani. Hauwezi kwenda kwenye viwanda vikubwa umeme wa majumbani hauna, lazima mpango uwekwe mahsusi umeme upatikane mjini na vijijini, anayehitaji umeme awekewe ambaye hahitaji abaki kwenye giza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo mngeyafanya na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndiyo mngepata sifa. Kuna watu wanashauri hapa mahali ambapo kuna hasara watu washughulikiwe. Kuna mafisadi wengi, kuna mikataba mingi IPTL iko miaka nenda miaka rudi, ishughulikiwe, haya ndiyo maeneo Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli amulike atu wenye mikataba mikubwa. Watu wanaacha kutumia umeme wa bei nafuu wanatumia jenereta katika ofisi zao matokeo yake tunashindwa kujiendesha tunapata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha ni muhimu, hayumo humu Bungeni lakini taarifa anazo. Hii miradi ya REA, miradi ya umeme, Mheshimiwa Mpango kama kuna mahali umekwamisha bajeti yako inakuja hapa watu wanakusubiri. Kwa hiyo, tunaomba fedha itoke, kama fedha haipo mtuambie fedha haipo tupange mipango ya kupata fedha, umeme upatikane, tunataka umeme mjini na vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.