Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote. Wizara yenu ni nyeti sana na mzigo mnapiga kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Mheshimiwa Waziri amenishtua, Jumamosi alikuwa Mkoa wa Songwe kwenye Wilaya ya mdogo wangu Mheshimiwa Mulugo na kwa Dada yangu Ileje ya Udinde kilometa 300 kutoka Mbeya. Jumatatu namsikia yuko Mtwara anafungua umeme, kwa kweli mnapiga kazi hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Wizarani kwako kuna watu zaidi ya watano (5) wanakaimu, siyo vizuri. Maana anapokaimu anafanya kazi kukufurahisha wewe ili usije ukamnyima cheo lakini ukim-confirm anafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kwa hiyo, naomba wawe-confirmed haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, REA I Wilayani kwangu Chunya ilipeleka umeme kwenye vijiji vingi sana lakini iliruka shule za sekondari zaidi ya saba. Mimi kama Mbunge na kama mzazi nilikopa hela benki nikaenda kulipa TANESCO niweze kupeleka umeme kwenye sekondari hizo. Nililipa pale TANESCO Chunya, Waziri anaweza ku-cross check na Meneja wa Chunya, nililipa pesa ndefu siwezi kuisema hapa kwa sababu sitaki kujisifu, kwa sababu vitabu vya dini vinasema mkono huu ukitoa sadaka huu usijue. Tatizo ni kwamba REA II imeruka Kituo cha Afya cha Kata ya Mtanila, cha zamani sana ambacho Mwalimu Nyerere alienda kuweka saini kwenye kitabu cha wageni mwaka 1966. Mheshimiwa Waziri sina uwezo tena wa kwenda kukopa benki kwa sababu bado nalipa ile ambayo nilikopa ya kupeleka umeme katika shule za sekondari. Naomba sana hii REA III inapoenda basi Kituo cha Afya cha Mtanila, Kata ya Mtanila ambacho kinachohudumia Tarafa nzima ya Kipambawe kipelekewe umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Wizara kwa kupelekea hiyo REA III ya sasa hivi, Jimboni kwangu iko kwenye Kata ya Ifumbo, Vijiji vya Ifumbo, Soweto, Mawelo na vijiji vingine. Kuna kijiji kinaitwa Itumbi, Wizara ya Nishati inataka kujenga kituo cha kuwahudumia wachimbaji wadogo (Center of Excellence) nikamuomba Mheshimiwa Waziri kwamba hii REA III Itumbi wapeleke umeme.

Mheshimiwa Waziri alinikubalia namshukuru sana Mungu ambariki, lakini naona bado Wahandisi wa REA hawajapewa hiyo taarifa kutoka kwake. Naomba anapowapelekea taarifa ya ombi langu la Kituo cha Afya cha Mtanila basi awapelekee na hii ya Kijiji cha Itumbi ambako itajengwa Centre of Excellence.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kidogo umeme wa maporomoko ya Mto Rufiji, ni wazo zuri sana litaikomboa nchi yetu naliunga mkono sana. Mto Ruaha unakauka, haukauki kwa sababu ya tabianchi hapana unakauka kwa sababu ya matumizi ya maji (management), unakauka kwa sababu wakulima wanachukua maji hawayarudishi, unakuka kwa sababu ya wafugaji, unahitaji tu utawala. Ndiyo maana Mheshimiwa Makamu wa Rais alienda Iringa akaliona tatizo hilo akaunda Tume ya kulishughulikia. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili alienda Kilombero aliona Mto Kilombero nao unaenda kwenye Mto Rufiji unakauka naye akaunda Tume. Rai yangu ni hii kwa Mheshimiwa Waziri, naomba yeye ambaye ndiye mwenye dhamana ya Nishati awe ndiyo kinara, achukue Wizara yake ya Nishati, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maliasili na Wizara zote zinazohusika muweze ku-manage mito hii miwili (2); Mto Ruaha na Mto Kilombero ili tupate maji mengi ya kwenda kwenye umeme wetu wa Stiggler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeishauri Wizara inasema, Kamati inaendelea kusisitiza Serikali kuwekeza zaidi katika nishati jadilifu (renewable energy). Mheshimiwa Waziri wakati anajibu maswali hapa alisema kwamba Tanzania ina-potential ya megawatt 5,000 katika geothermal, naomba nguvu ambayo Mheshimiwa Waziri ametumia kuunadi mradi wa Stiggler’s Gorge nguvu hiyo anadi hii geothermal, megawatt 5,000 ni nyingi mno. Tena hahitaji fedha nyingi Mheshimiwa Waziri, anahitaji tu anunue rig moja au mbili azileta hapa nchini na kuikabidhi hiyo Kampuni aliyounda ya Geothermal Development Company, yenyewe inatoboa mahali ambapo kuna potential inaleta juu kwenye well-head mnatangaza tenda waje wakezaji kuweka mitambo hapo. Kwa hiyo, naomba sana hii megawatt 5,000 potential ya Tanzania ni kubwa sana, naomba Mheshimiwa Waziri aishughulikie hii kama alivyoshughulikia Stiggler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niongelee kidogo miradi miwili ya Kiwira megawatt 200 na Mchuchuma megawatt 600 ya makaa wa mawe. Mheshimiwa Waziri ulipoingia Wizarani ulisikia kuna mradi wa Kiwira megawatt 200 Mchuchuma megawatt 600. Ulipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Wizara, Kiwira megawatt 200, Mchuchuma megawatt 600. Umekuwa Naibu Waziri Kiwira megawatt 200, Mchuchuma megawatt 600, sasa umekuwa Waziri bado Kiwira megawatt 200, Mchuchuma megawatt 600, Mheshimiwa Waziri do something, weka alama. Hii historia ya kwamba Kiwira, Mchuchuma iishe, fanya kitu, weka alama ili vizazi vijavyo viseme kwamba Mheshimiwa Dkt. Kalemani alikuwa Waziri wa Nishati alifanya kazi Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja.