Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii muhimu sana kwenye majimbo yetu. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na watendaji wao wote ndani ya Wizara hii ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu lina vijiji 61 lakini vijiji ambavyo vina umeme mpaka sasa ni 6 tu. Wengine wakisimama hapa wanasema wamebakisha vijiji 10, 5, tumuombe Mheshimiwa Waziri wakati mnapopanga mradi huu wa Awamu ya III wa REA tukuletea umeme, hebu sisi ambao hatuna umeme kabisa tuwe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliuliza hapa swali la nyongeza, kwa bahati mbaya ukachanganya Nguruka na Uvinza, ukasema kwamba mimi na wewe tuliambatana Nguruka kwenda kuwasha umeme. Mheshimiwa Waziri mimi na wewe tuliambata Uvinza kwenda kuwasha umeme. Umenichonganisha na wananchi wangu wa Nguruka. Sasa Mheshimiwa Waziri ili kuninasua na wananchi wangu wa Nguruka, naomba sana tuletewe umeme kwenye Vijiji vya Chagu, Ilalanguru, Mganza, Nyangabo, Nguruka, Itegula, Kasisi, Amriabibi na Mpeta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataja vijiji hivi kwa sababu kuna sintofahamu huko, kwamba Mheshimiwa Mbunge mbona Waziri amesema mliambatana kuja kutuwashia umeme Nguruka. Sasa hivi vijiji nilivyovitaja viko kwenye Tarafa ya Nguruka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aniletee umeme kwa sababu, umeme wa Gridi ya Taifa unaotoka Kaliua umekuja mpaka kwenye Kata ya mwisho ya Usinge. Nachomuomba Mheshimiwa Waziri watuongezee pale substation ya kutoka Urambo ifungwe Kaliua na substation nyingine iletwe Uvinza. Kwa kuyafanya haya, ina maana tutarahisisha sasa umeme wa kutoka Kaliua wa Gridi ya Taifa uweze kuingia katika hivi vijiji nilivyovitaja. Kwa kuingiza umeme kupitia Uvinza, itakuwa rahisi kuupeleka kwenye Vijiji vya Basanza na hatimaye kuingia kwenye Jimbo la Kasulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia kuzungumzia REA awamu ya II. Tunavyo Vijiji vya Kabeba, Mwakizega na Ilagara. Vijiji hivi umeme umeshamalizika kwa maana ya nguzo, transfoma na kila kitu lakini kutokana na mvutano baina ya Wizara ya Nishati na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi mkandarasi aliyekuwa anatekeleza mradi ule kwa maana ya Mkoa wa Kigoma na Katavi na Rukwa alisimamishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu kwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha bajeti yake anieleze au awaeleze wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini, hivi Vijiji vya Mwakizega, Kabeba na Ilagara, mradi wa REA mkandarasi ataendelea na taratibu zilizobaki kwenye mradi ule wa REA wa Awamu ya II? Kwa sababu tunapata kigugumizi, kama mkandarasi huyu tayari amefutiwa mkataba na hataendelea tena, nani anayeendeleza mradi ule wa REA katika Kata zangu hizi mbili za Mwakizega na Ilagara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie umeme kuingia Kata ya Kalia. Nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa kuwa kutoka Mwese mpaka Kijiji cha Lugufu kwenda Vijjiji vya Kashaguru, Chambusha, Kalia na hatimaye kumalizia Sibwesa ni karibu sana na Mwese kuliko kutoka kule kuja Ilagara. Sasa nimwombe Mheshmiwa Waziri hebu huu umeme ambao uko Mpanda unaelekea Mwese ndiyo mtuweke kwenye progamu ya REA Awamu ya III utoke Mwese, uingie katika hivi vijiji ndani ya Kata ya Kalia. Namuomba kwa unyenyekevu mkubwa na ndiyo maana leo wala siongei kwa jazba, natambua kwamba Waziri ni msikivu, Naibu Waziri ni msikivu lakini ndugu yangu Maganga naye ni msikivu, atanisikia na kwa faida ya wananchi wa Jimbo langu la Kigoma Kusini, wananchi wa Kalia nao watapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze kwanza Wizara kwa kuona umuhimu wa kuongeza megawatts 45 kutoka Malagarasi hadi Kidahwe. Nipongeze jitihada hizi ni nzuri, najua kwamba mradi huu mkubwa wa Malagarasi ukitekelezwa na njia ile ikijengwa ya kutoka Malagarasi kilomita 53 hadi kufika Kidahwe wananchi watanufaika na kupata umeme wa uhakika. Kwa sasa tunatumia majenereta, uendeshaji wa majenereta jamani ni mkubwa mno na hawa wenzetu TANESCO kama walivyoongea Waheshimiwa Wabunge mbalimbali, uwezo wao umekuwa wa chini mno ukilinganisha na siku za nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie TANESCO. Umeme kwenye vijiji sita kwa maana ya Vijiji vya Mlela, Kandaga, Uvinza, Kazoramimba na Mwamila umeishia barabarani na ukiwauliza REA wanakwambia wenye mamlaka ya kuuchukua ule umeme na kuuingiza kwenye vijiji vya ndani ni TANESCO. Sasa hao TANESCO ambao tunawasema leo tangu mradi wa REA wa Awamu ya II umekamilika, hakuna TANESCO walichokifanya kutoa nguzo barabarani na kuwapelekea wananchi wa Kandaga na Nyanganga. (Makofi)

Mheshmiwia Mwenyekiti, nimuombe sana Waziri, hawa TANESCO mbona wamebaki tu kama jina? Yaani tumebaki na TANESCO kama jina. Kama inaonekana TANESCO imefika mahali imekufa kabisa basi Serikali ituambie ili tusiwe tunasimama hapa kupiga kelele za TANESCO.

TAARIFA . . .

MHE. HASNA S. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko hapa kuishauri Serikali, hayo mambo ya mikataba na nini mimi sitaki kujiingiza sana huko. Ndiyo maana tunaishauri Serikali ikae chini ione ni jinsi gani ya kuiwezesha TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu, taasisi nyingi ndani ya jimbo langu hazijapata umeme. Kwa mfano, tunayo Shule ya Lugufu Boys na Lugufu Girls lakini tunazo zahanati na vituo vya afya vinashindwa kupata umeme. Mimi niliongea na Meneja wa TANESCO, akaniambia nguzo wanazo nadhani mia moja na kitu lakini hawana pesa ya kuwapa mafundi ili waweze kuchukua zile nguzo na vifaa ambavyo wanavyo wawapelekee wananchi umeme kwenye maeneo ambayo hatujapata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Waziri, Naibu Waziri na Mkurugenzi na pia niungane na wenzangu, huyu Kaimu Mkurugenzi wa REA, Ndugu Maganga jamani athibitishwe kama anaonekane anafaa. Kwa sababu unapokuwa unakaimu, mimi naelewa maana ya kukaimu,
nimefanya kazi Serikalini, ukikaimu unakuwa huna mamlaka, ukikaimu unakuwa huna sauti. Sasa tunabaki kusema mambo mengine akitaka kuyatolea maamuzi anashindwa kwa sababu bado yeye ni Kaimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimeona wakati Spika anawatambulisha kila aliyesimamishwa pale ni Kaimu. Sasa mtu anapokuwa Kaimu hapati ile confidence ya kufanya kazi yake inavyotakiwa. Kwa hiyo, tuombe Mheshimiwa Waziri umshauri Mheshimiwa Rais ili hawa wanaokaimu kama wamekidhi vigezo waweze kuthibitishwa na hatimaye tuweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nawapongeza zaidi hawa Mawaziri kwa kweli wanafanya kazi.