Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa kusimamia mjadala huu na kunipa fursa ya kuhitimisha hoja niliyoitoa jana asubuhi kwa kutoa maelezo kuhusu masuala mbalimbali yaliyojitokeza na yaliyozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kutoa maelezo kuhusu hoja hizo ni vyema niwatambue Wabunge wote waliochangia kwa maandishi na kwa kuongea. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 117 wamechangia hoja hii, kati yao Wabunge 62 wamechangia kwa kuzungumza na Wabunge 54 wamechangia kwa maandishi. (Makofi)

Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu ya maandishi na kwa kuzungumza na kimsingi mmetoa hoja nzuri sana zenye malengo ya kuimarisha utelezaji wa majuku katika Wizara yangu. Hii inaonesha ni namna gani Wabunge wako tayari kutoa michango yao ya kimawazo kwa ajili ya kuendeleza sekta muhimu ya kilimo hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango iliyotolewa ni mingi sana. Ni ukweli pia kwamba muda niliopewa hauwezi kukidhi kujibu hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, naomba mtambue kwamba michango yote iliyotolewa ninaithamini sana na Serikali kwa ujumla kama mlivyosikia inaithamini sana na tutaifanyia kazi kwa umakini ili kuendeleza sekta hii ya kilimo. Majibu ya hoja zote yataandaliwa kimaandishi na Waheshimiwa Wabunge mtapatiwa kabla Bunge hili halijahitimishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kujibu hoja jumla zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Nianze na hoja za Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeishauri Serikali kuongeza bajeti ya kilimo. Ni kweli bajeti ya kilimo kama bajeti za Wizara zingine nyingi hazitoshi. Ukipewa unconstrained budget ni matrilioni ya pesa kwa kila bajeti, lakini kwa sababu ya resource envelope yetu tuliyonayo bajeti zetu karibu Wizara zote Waheshimiwa Wabunge zinaminywa, ndiyo maana kila Wizara imewekewa ukomo wa bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Wizara ya Kilimo haitekelezi majukumu ya kilimo yote yenyewe peke yake. Muundo wa Serikali yetu Waheshimiwa Wabunge umegawanya kilimo kitekelezwe katika Wizara nyingine kadhaa. TAMISEMI ndio watekelezaji wa shughuli za kilimo kwa asilimia 80 kwa sabau miradi yote ya wananchi ya kilimo iko katika mipango ya maendeleo ya kilimo ya Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kilimo kwa muundo wa Serikali yetu Waheshimiwa Wabunge kinatekelezwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Shughuli yote ya umwagiliaji; na nimewasikia humu Waheshimiwa Wabunge mkisema kwamba kilimo cha uhakika ni kile cha umwagiliaji na mimi nakiri, lakini kwa muundo wa Serikali yetu shughuli hiyo ya umwagiliaji inasimamiwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Tuna suala la masoko kwa mazao ya kilimo, ni sehemu ya shughuli za kilimo, hili nalo halisimamiwi na Wizara ya Kilimo, linasimamiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mambo ya maghala, mambo ya marketing ya masoko hili na lenyewe limewekwa kwenye Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, mamlaka ya maghala nchini iko Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, hata wale wanaosimamia minada ya korosho hawako chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna shughuli zingine zinatekelezwa moja kwa moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Miradi ya kujenga uwezo inatekelezwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tulikuwa na programu kubwa tu Waheshimiwa Wabunge ya MIVARF mnafahamu, hii imesimamiwa chini ya Ofisi ya Waziri, Uratibu na Sera, wamejenga barabara, masoko, wameweka viwanda vidogo vidogo vya kusindika. Yote haya ni sehemu ya kilimo cha nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wizara hii kimsingi ina mambo mawili makubwa, sera ya kilimo na uratibu wa kilimo chenyewe. Katika uratibu kuna mambo ya research, kuna mambo ya back stopping yaani kutoa msaada wa kiufundi pale unapohitajika. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge hili jambo la kwamba hela iliyopelekwa kwenye kilimo ni kidogo sana, ndiyo ni kidogo wala hilo si jambo la kubishania, lakini pia lazima tukumbuke kwamba kilimo hiki hiki tunachokizungumza kinasimamiwa pia na Wizara nyingine za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye jambo la Malabo au The Maputo Declaration. Azimio la Maputo linazungumzia kilimo kwa tafsiri ya FAO, halizungumzii kilimo kwa tafsiri ya Wizara moja ya Serikali hii, linazungumzia kilimo kwa tafsiri ya Shirika la Chakula Duniani yaani kilimo kwa tafsiri ya FAO ni kilimo cha mazao, kilimo uvuvi, kilimo mifugo, kilimo ushirika na kilimo misitu. Sasa ukichanganyna haya mambo matano unaona kwamba hilo tunalolisema asimilia kumi, asilimia sita au kumi kuelekea asimilia kumi halipo zoomed yaani siyo la kilimo mazao peke yake na ushirika ambalo linasimamiwa na Wizara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Waheshimiwa Waheshimiwa Wabunge tunawendelea kukokotoa, na nadhani Waziri wa Fedha atakapokuwa anahitimisha, atakapokuja na bajeti ataonesha sasa maeneo yote haya niliyoyataja yatakuwa yamewekewa au yametengewa kiasi gani cha fedha na hapo ndipo tutatazama sasa kwa tafsiri hiyo pana ya kilimo ni kwamba tumeelekeza kule fedha kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo mazao na ushirika peke yake, haiwezi ikatengewa asilimia kumi ya bajeti Waheshimiwa Wabunge hapana, kilimo kinachojumuisha mifugo, uvuvi, ushirika, misitu na mazao hicho ndicho Malabo au The Maputo Declaration kinachohitaji kitengewe angalau tufike kwenye asilimia kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imeishauri Serikali kuongeza kasi ya kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kuzalisha mbolea hapa nchini na kujenga viwanda. Ni kweli hili wala siyo suala la kubishana, huu ushauri wa Kamati tunaupokea moja kwa moja asilimia mia moja kwa sababu leo tunahangaika, mara vocha, mara BPS, mara sijui nini hii yote ni kwa sababu uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi ni mdogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Taifa tungekuwa tunazalisha mbolea haya mambo ya bei tungekuwa tuna fix wenyewe kwa sababu ni kitu product inayozalishwa hapa ndani, haya mambo ya ifike wapi, siku gani tungekuwa tunafanya haraka tu, lakini kwa sababu uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi ni wa chini kabisa ndiyo maana leo bado tuko katika tafrani hii ya mifumo ya namna gani tuwasaidie wakulima na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge ni rahisi sana nchi inayozalisha mbolea ndani ya nchi yake kuweka ruzuku kwenye hivyo viwanda vinavyozalisha hiyo mboela na mbolea ikawa rahisi au kuweka resume ya kodi ambayo inawezesha mbolea kuwa ya bei ya chini kuliko mbolea unayoagiza kutoka nje. Mbolea unayoagiza kutoka ni lazima uingie kwenye mfuko uchukue kule fedha ya kigeni uagize mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejaribu ruzuku na vocha, Waheshimiwa Wabunge ninyi wenyewe ni mashahidi, nilikuwa naongea na Mheshimiwa Flatei hapa ananiambia kule kwao utaraibu wa vocha ulikuwa ni miujiza, kijiji kizima wanasainishwa vocha halafu hata mfuko mmoja hauendi watu wanaenda NMB wanapiga pesa, kilimo hakibadiliki ingawa kwenye hesabu ya matumizi ya fedha inaonekana mbolea kubwa imepelekwa kule. Sasa hii yote ni matokeo kwa sabau wenyewe hatujawa na uzalishaji wetu wa ndani wa mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nifurahi tu kuwaambia kwamba ujenzi wa kiwanda cha mbolea kule Kilwa sasa angalau unatia matumaini. Yale mabishano na mazungumzo yaliyokuwapo kuhusu bei ya gesi itakuwa kiasi gani, wauzie bei kama mtumiaji wa nyumbani au wauziwe ile gesi kama malighafi, hilo jambo sasa limemazika na kwa hiyo hatua inayofuata ni wao kuanza ujenzi wa kiwanda. Hata hivyo kule Mtwara Kampuni nyingine pia ya Kijerumani na yenyewe kwa makubaliano hayo hayo taaraifa ya tariff gesi na wao wame- commit wataanza ujenzi wa kiwanda. Kiwanda chetu cha Minjingu pale Arusha kinazo sura mbili. Mwanzo walianza na mbolea ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wameisema haikufanya vizuri na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie watu hawa walijirekebisha wakafanya utafiti wamepeleka kwenye Taasisi za Utafiti (Seriani), kule utafiti umefanyika. Jambo moja lililopo mbolea ya Minjingu inabidi ufanye kwanza utafiti wa udogo kabla ya kwenda kuitumia. Hili jambo tunalitafutia na tumepata mwarobaini wake, tumepata msaada wa magari mawili yanayotembea na maabara ya kufanya analysis ya udongo. Haya magari tutayapata ndani miezi miwili ijayo, yatazunguka kijiji kwa kijiji nchini, yatapima udongo ule ni wa aina gani, na kwa hiyo recommendation ya aina gani ya mbolea inafaa kwa kijiji gani, inafaa kwa mkoa gani, wilaya gani, sasa habari hiyo tutakuwa nayo. Kwa hiyo mambo ya kupeleka DAP nchi nzima holela, kupeleka UREA nchi nzima holela, tutaachana nayo hivi karibuni, tutakuwa sasa tunajua kwa uhakika kwamba mbolea hii ukiipeleka Kanda ya Ziwa acidity kule iko kubwa sana haitafanya kazi. Hivyo kitu cha kufanya tuwashauri wananchi waweke chokaa (lime) kwanza ili tunapopeleka hii mbolea iwe na manufaa kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu niseme jambo moja hapa ndani ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi wanaweza kuwa hawalifahamu. Matumizi ya mbolea niseme tu ya kukuzia UREA tunayotumia sasa hivi nchini hapa, hii mbolea ukiitumia katika maeneo ambako tindikali imekwishafikia ile wataalam wanaita PH-5 unapoteza mavuno yako kwa asilimia 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mkoa wa Njombe hata wakiongeza matumizi ya mbolea ya UREA mara mbili bado mavuno yao hayawezi kuongeza kwa asilimia 30 kwa sababu ardhi ya eneo lile kwa kiwango kikubwa tindikali iko ya juu sana kiasi kwamba mbolea ikiwekwa inatengeneza ukame usiokuwa asilia yaani ukame ambao ni artificial, mizizi hairefuki ya mazao kwenda chini kuchukua virutubisho. Kwa hiyo uzalishaji unakuwa wa chini hata kama matumizi ya mbolea yanakuwa yameongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ndiyo maana tumekwenda kwenye hatua ya kutafuta haya magari. Mwaka 2017 mnafahamu watafiti wetu waliuwawa hapa Dodoma kwa sababu walikwenda wenyewe wenyewe tu vijijini wanachokonoa chokonoa udongo, wakatuhumiwa kwamba labda ni majambazi, wakapigwa wakachomwa moto. Sasa tumetafuta nyenzo (mobile laboratory) magari mawili yatazunguka nchini, yatapima udongo na kwa hivyo tutakuwa na uhakika wa aina ya mbolea na mahitaji ya wananchi kila eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imeshauri kuwa ni vyema ununuzi wa mbolea kwa pamoja ufanyike mara tatu au mara nne kwa mwaka kadri itakavyowezekana. Mimi nakubaliana na maoni haya ya kamati, lakini nitoe tu angalizo kwa sababu tumefanya hili jambo, tumeyaona mapungufu na changamoto zilizopo. Wakati ule tumewapitisha kwenye semina Waheshimiwa Wabunge tulisema kwamba bei ya mbolea kwenye Soko la Dunia inabadilika sana. Bei ya Mbolea kwenye Soko la Dunia jamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wahindi (India) na Brazil wanapoingia kwenye msimu wa kilimo mahitaji ya mblea duniani yanapanda, kwa hiyo na bei pia na yenyewe inapanda kwenye soko la dunia. Sasa tukitangaza zabuni yetu hapa katika kipindi hicho kwa vyovyote vile tutakwenda kukutana na bei kubwa. Halafu mwezi mmoja uliopita labda ulikuwa umewatangazia watu bei elekezi 47, unakwenda unakutana na bei kwenye bulk nyingine inayofuata inayokupeleka kwenye 55; sasa ile inakuwa inawachanganya watu. Wanaona kama vile mfumo huu haueleweki, kwa nini mwezi fulani bei ilikuwa hii, mwezi mwingine bei ilikuwa hii, hii sasa manufaa yako wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tunachokifanya tunavizia pale ambako bei ya mbolea katika Soko la Dunia iko katika minimum kabisa ndipo sasa tumesema tunatangaza na tunanunua ya mwaka mzima ili ikishaingia mbolea inakuwa na bei moja mwaka mzima kuliko hii ya
kununua mara nyingi nyingi, tukinunua mara nyingi nyingi bei haitakuwa moja mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunapoagiza kiwango kikubwa sana hata wauzaji wanapunguza bei, lakini tunapoagiza tani 29,000, tani 30,000, wauzaji wanaona hawa ni kama reja reja tu kwa hiyo wanatuuzia kwa bei ambayo ni ya rejareja. Kwa hiyo tunavyojipanga sasa hivi tunataka tutangaze zabuni na tunajua bei itashuka kwenye mwezi wa sita, itakuwa ndiyo iko chini kabisa duniani, tutaagiza hiyo mbolea itakayokuwa inatutosha mwaka mzima na tukishafanya hivyo Waheshimiwa Wabunge tatizo tutakalokutana nalo tu ni namna ya kuisambaza, kuifikisha vijijini na hili ndiyo tunajipanga nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge suala la kuingiza nchini mbolea si tatizo. Tatizo tulilonalo changamoto kubwa ni namna ya kuisambaza, kuifikisha huko vijijini. Tumejiwekea mkakati na hili naomba support yenu kwamba tutatumia nyenzo na mamlaka zote za Serikali. Tunayo Kampuni ya Mbolea ya Serikali wana warehouses mikoa na wilaya zote, hawa tutawapelekea kwanza mbolea huko. Wafanyabiashara wanaoshiriki katika mfumo huu tumewawekea sharti jipya kwamba ili ushiriki kwenye kuagiza ile mbolea tani 200,000 au 300,000 lazima uwe na mtandao wa kugawanya mbolea kwa eneo la nchi lisilopungua asilimia 60 ili mmoja tu akichukua ile amount aliyo-commit kuuza tunajua kwamba at least 60 percent ya nchi atakuwa amefikisha mbolea, sasa wakiwa watatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na jambo lingine katika hii issue ya mbolea wafanyabiashara wamekuwa na tabia ya kupeleka mbolea maeneo yanayotumia mbolea maeneo yanayotumia mbolea kwa wingi tu, kule ambako matumizi ya mbolea ni kiodgo hawaendi kabisa. Ndiyo maana utakuta eneo kama Kakonko kwa rafiki yangu Mheshimiwa Bilago, akipeleka anapeleka tani moja na akifika kule anaipandisha bei sana kwa sababu anajua hiyo mbolea itakaa miezi nane au miezi tisa haijanunuliwa, and that’s a business sense, wala mtu wa namna hii huwezi ukamlaumu atakuwa na storage charges, atakuwa analipa walinzi, atakuwa analipa nani, sasa akiweka bei ya chini badaa ya miezi tisa mfuko ule utakuwa bado unauzika kwa elfu ngapi hiyo? Atapata hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunachokifanya, ili tumpe leseni ya kuwa muuzaji mkubwa wa mbolea, tutawalazimisha wawe pia na maeneo ya kuuzia mbolea kwenye maeneo hayo ya namna hiyo ili tusiwe na pocket yoyote nchini ambako eti mkulima akihitaji mbolea hawezi kupata. Kwa sababu atakuwa anauza mbolea nyingi kwenye maeneo ya matumizi makubwa, hiyo itakuwa inafidia hata kule anakouza mifuko 10 au 20 kwa mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Kamati imetushauri ni kwamba minada ya kahawa iongezwe, na sisi tunasema minada ya kahawa itaongezwa, lakini kwa sababu tumeanza commodity exchange sisi Serikali tulikuwa tunadhani kwamba kahawa yetu ianze kuuzwa kwenye TMX, ianze kuuzwa kwenye commodity exchange. Infrastructure ya kahawa ya kuuza kahawa kwa mnada iko tofauti kidogo na ile flow ya commodity exchange. Kwa hiyo nimeshaelekeza kwamba TMX waende wakakodi ile facility iliyopo pale Bodi ya Kahawa-Moshi ili wao wawe ndio wanafanyia hiyo commodity marketing pale pale kuanzia Moshi, lakini isiwe tena huu mnada wa kahawa kama tuliouzoea ambako niseme tu ukweli kateli zilikuwepo kule, watu wanapanga bei nje ya mnada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiwaingiza wakulima wa kahawa kwenye commodity exchange kahawa yao itakuwa inajulikana tu duniani huko. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wanaotoka kwenye maeneo ya kahawa, kwamba kahawa ikishaanza kuuzwa kwenye commodity exchange habari hii ya ushirika ita-collapse tu yenyewe, yaani hakutakuwa na haja ya kutumia nguvu sana kuzungumza ushirika gani una nini, unakwenda kwa nani, No, kwa sababu suala lile ni la kimtandao wa dunia nzima kwa hivyo ushirika wamekwenda wao, imeenda AMCOS au imeenda union it doesn’t real make a big difference, watu watakwenda pale, kahawa yao itajulikana duniani kote, watauza, watagawana pesa, mambo yatakuwa mazuri.

Waheshimiwa Wabunge, sasa naomba hoja zingine za Kamati pia tutazijibu kwa maandishi. Naomba nizungumzie mambo ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge kwa hisia sana, naamini tukiwa na uelewa mzuri kwenye hili jambo na tukaweka commitment ya Serikali basi nina uhakika tutakwenda tu vizuri na Mungu atatusaidia.

Mheshimiwa mwenyekiti, nianze tu na hili jambo la soko la mahindi hapa nchini. Kwa kweli, naomba tu niwambie ukweli, mimi ni mkulima, naomba niwaambie huu ukweli kabisa yaani usiokuwa na mawenge mawenge, mimi nalima. Nalima mtama, nalima vitunguu na nalima mahindi. Hii adha na mimi inanipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lwenge hapa jana alipochangia alisema tunalima wote na mtama umetushika. Wamo humu Waheshimiwa chungu mzima waliolima na wao hawajauza mpaka leo. Wako wakulima wa vitunguu Singida kwa Mheshimiwa Monko, wako wakulima wa vitunguu hapa Kilolo kwa Mheshimiwa Mwamoto, wanalima mwisho wa siku hakuna soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu Waheshimiwa Wabunge mnisikilize vizuri kwa unyenyekevu sana nalisema hili jambo, seasonality, kilimo chetu ni cha kutegemea mvua kwa asilimia kubwa. Kilimo cha vitunguu kwa maeneo mengi huku nacho ni cha msimu, mvua ikiwa inanyesha huwezi kulima. Kwa hiyo, watu wanalima mvua hakuna au watu wanalima mvua ikiwa inanyesha. Kwa hiyo, watu wakiwa wanalima kwa pamoja si ndiyo? Watavuna kwa pamoja, mahitaji yanashuka, the low of demand and supply ina-setting, na kwa sababu hatuna miundombinu ya kutosha ya uhifadhi wa mavuno yetu tunajikuta tumeingia kwenye hasara, tunajikuta tumeingia kwenye kuuza kwa bei za kutupa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kama tungekuwa na miundombinu mizuri ya kuhifadhi, natoa mfano tu wa nyanya, mwaka jana watu wamelima nyanya nyingi sana hapa Dumila, hakuna storage facilities. Sasa hivi wanalima Parachichi nyingi tu Njombe, hakuna pack house. Kwa hiyo wakulima hawa wakivuna, akiona mazao yake yanaelekea kuoza ndugu zangu atauza tu kwa bei ya hovyo hovyo. Si kwamba mimi Tizeba nafurahia haya mambo. Kwa hiyo, Serikali tunachokifanya tunajitahidi ku-overcome hii situation, tunajitahidi sana ku-overcome hii situation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyotajwa hapa ni ya Serikali, bajeti iliyosomwa hapa ni ya Serikali, tofauti sana niseme kwa mfano na Wizara ya Afya ambao wadau wetu wa maendeleo wanapeleka fedha kwenye basket, si ndiyo? Sisi wadau wetu wameamua kwenda moja kwa moja ku- address issues kule. Tunayo programu na ADB ambayo itatengeneza complex ya kilimo kuanzia uzalishaji mpaka usindikaji na tayari timu ipo inafanya kazi, tumeshakubaliana na ndiyo maana Rais wa Benki ya Afrika alikuwa Tanzania hivi juzi, amefanya mazungumzo na Mheshimiwa Rais, wameshakubalaiana, timu ya wataalam nilikuwa nayo ofisi siku kabla ya jana, hili jambo tunaendelea nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari hii ya watu kuzalisha nyanya, anauza tenga shilingi 2,000 au mwisho wa siku unapita anakwambia chukua na wewe kawapikie watoto wako si sawa. Kwa hiyo, lazima tutafute suluhisho la haya mambo, one step ni Agro processing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge benki zetu za biashara; NMB, CRDB na Bank of Africa tumekwishafanya mazungumzo, wamekubali watakuwa wanatoa pesa kila mwaka kwa ajili ya kuingiza fedha kwenye value addition yaani kwamba mkulima akishalima, wananchi wengine ambao hawalimi, wa-takeover kwenye huo mnyororo wa thamani wale off takers wapate pesa, wanunue, wapeleke kwa wasindikaji, wasindikaji wasindike, wapeleke kwenye masoko na bidhaa zetu zikisindikwa masoko yake yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania leo, niwape mfano tu, juzi hapa ndani hapa debate kubwa kabisa ya mafuta ya kula, si ndiyo? Tunaagiza crude palm oil tani 600,000; lakini tuki-process mahindi tu kuyakamua na kupata corn oil, namshukuru sana Mheshimiwa Sokombi alilisema hili jambo. Tuki-process corn oil inaweza ikachukua nusu ya mahindi yanayolimwa hapa nchini na bado mafuta yake yasitoshe kwa matumizi hapa ndani. Kwa hiyo hizi benki zime-commit kwamba zitatoa fedha kwa Watanzania wanaotaka kufanya hiyo shughuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wafugaji wanahangaika na mifugo, kwa nini hatuwi na feed loads tukatuma mahindi yaliyokamuliwa yakatolewa mafuta, tukachanganya na soya tukapata chakula cha mifugo kizuri tu kabisa? Tumeanzisha programu ya uzalishaji wa soya nchini, Clinton Foundation wanatusaidia lakini pia tumeweka kwenye mipango yetu kwamba tuta-enhance uzalishaji wa Soya nchini ili tuanzishe utengenezaji wa chakula cha mifugo. Inawezekana watu wale ambao wanasumbuka na mazao yao wakapata masoko ya ndani hapa hapa kwa kuongeza thamani na tukafanya vizuri tu sana katika suala la masoko.

Lakini jambo lingine la masoko Waheshimiwa Wabunge, ziko nchi ambazo tuko jirani nazo lakini kwa hali ilivyo katika nchi zao hawawezi kuzalisha. Burundi, Sudan ya Kusini, Kenya nusu ya nchi hawawezi kuzalisha, hawa tunataka sasa wawe ndiyo soko letu. Kwa hiyo, nilikuwa ninazungumza hapa kwamba taasisi zetu za Serikali na za watu binafsi zichangamkie hizi fursa. Bodi yetu ya nafaka na mazao mchanganyiko; mimi nachelea sana kusema kwamba NFRA ndiyo ita-spearhead suala la biashara ya mahindi, hapana, wale wana jukumu lao la kisheria la strategic reserve.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili lilianzisha chombo kwa ajili ya shughuli hiyo ya biashara ya mazao. Kuna ule mkopo ambao niliwambiwa hapa ume-stack, hapana, mkopo ule utapatikana, hawajajidhatiti sana kwa hiyo huwezi kuwarushia bilioni mia moja. Hizo fedha walizopewa na NSSF watazipata, wataendeleza sasa shughuli ya kununua na kuuza mazao. Tulichokifanya, tunataka tuwatume waende Sudan, si wao ndiyo kazi yao kufanya biashara ya mazao? Tunataka tuwatiume waende Sudan ya Kusini, waende huko Mauritius, huko liko soko la mbaazi, waende wakazungumze na Wahindi wa Mauritus wakubali kununua mbaazi yetu, hela wanapata, kwa hiyo, wakishapata hizi pesa waanze biashara. Kibaya ni kuwaanzishia pesa nyingi ambazo hawatakuwa na uwezo wa kuzitumia halafu waishie kupanga matumizi ya kuzimaliza. Kwa hiyo, tuombe tu kwamba suala la biashara ya nafaka, wenye mandate ya kisheria wapo na sisi mtusukume tu kuhakikisha kwamba wanafanya kweli hiyo biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi na mazao yao, nimesema katika hotuba yangu na inavyoelekea haikueleweka sawa sawa. Hakutakuwa na kizuizi kwa mtu yoyote kuuza mazao yake nje. (Makofi)

Narudia tena, hakutakuwa na kizuizi kwa mtu yoyote kuuza m azao yake nje. Angalizo tu, wakulima wasiuze kila kitu mpaka cha kula wenyewe, uzeni. Yale mambo ya mpakani pale mtakutana na Afisa TRA atakwambia una kiasi gani humu ili aweke record unatoka na nini basi, uzeni tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale maeneo yanayofanya vibaya katika kuvuna chakula, kwa sababu Waheshimiwa Wabunge msisahau kwamba si kila sehemu ya nchi yetu wanavuna vizuri, yako maeneo Tanzania ambayo hayavuni vizuri na sisi kama Serikali hatuwezi kufumbia macho hilo jambo. Kuna mchangiaji mmoja amesema vizuri tu, suala la usalam wa chakula ni suala la usalama wa nchi. Ni vigumu sana Waheshimiwa Wabunge, hata kambi hii naomba mnielewe vizuri, ni vigumu sana kutawala watu au kuongoza taifa lenye watu wenye njaa, ni vigumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo NFRA itafanya hiyo shughuli ya kuhakikisha kwamba chakula cha dharura kinapatikana kwenye maeneo ambayo kisheria yatathibitika kwamba yanahitaji msaada wa chakula. Utaratibu tulioweka ni kwamba wata-maintain presence kwenye maeneo hayo, kwa sababu gani; mazao yaliyonunuliwa mwaka juzi, shelf life yake ni miaka mitatu kwahiyo lazima yatoke whether kuna dharura au hakuna dharura. si ndiyo? Sasa yake yatakayokuwa yana-approach shelf life yake kwisha tutayapelekea tu kwenye maeneo haya ambapo uzalishaji wao sio mzuri ili wananchi waendele kununua kwa bei himilivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na huu ndio mpango ambao nadhani utatutoa hata kwenye haya mabishano, mahindi yaende nje, au yasiende nje, mahinda acha yaende, ngano acha iende, mchele acha uende, chochote, as long as hatutafikia hali kwamba sasa eti nchi haina chakula halafu tena, kama ndugu yangu Mheshimiwa Zuberi siku moja alivyosema kwamba nchi imebakiza chakula cha siku tatu. Hiyo ndio situation ambayo tutajitahidi tu kama Serikali tusifikie hapo. Hakuna namna tunaweza tukasema eti tumefanya fanya mambo leo tumefikia nchi tuna chakula cha nane au saba. Vinginevyo niwatoe hofu Waheshimiwa kwamba wananchi watakaozalisha wanaruhusa tu ya kupeleka chakula chao huko nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa kwa hisia sana ni hili la uingizaji wa mbolea kwa pamoja. Nimeshalizungumza na kwa hivyo sitaki kulirudia tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa na wachangiaji ni hili la pamba. Pamba ndugu zangu, kwanza niweke clarification ya moja kwa moja. Ushirika hawanunui pamba, kwa hiyo Mheshimiwa Kiswaga, Mheshimiwa Ndassa, Mheshimiwa Mashimba, Mheshimiwa Njalu na wengine wote wanaozungumza hili jambo kwa mtazamo huo niwafahamishe tu kwamba ushirika kwa sasa, unless wana hela zao wenyewe, maana yake sheria haiwazuii kununua, unles wana hela zao wenyewe lakini hawatanunua eti watanunua pamba kwa fedha ya wafanyabishara, hili jambo halipo. Hili jambo ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge halipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ushirika ambayo Bunge hili limepitisha haizuii ushirika kununua pamba na ushirika umekuwa ukinunua pamba miaka yote Nyanza na SHIRECU ni washirika wale, lakini kwa msimu huu hawana fedha ya kununua pamba. Suala lililokuwa limezungumzwa hapa ni kwamba wawaweke pamoja wakulima wao na hili jambo Waheshimiwa Wabunge lilitokana na kilio cha wanunuzi wa pamba pia, walisema kwamba wanatumia gharama kubwa sana kuweka utitiri wa wale mawakala huko kwenye maeneo ya huko vijijini, wakaweka figure ya watumishi 22,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kutafakari pamoja nao ikaonekana labda inawezekana watu katika ushirika wao waka-aggregate halafu ninyi mkaenda kununua. Lakini inavyoonekana imani bado haipo ya kuwapa washirika hawa pesa. Kwa hiyo kama nilivyosema kwenye taarifa yangu na vyombo vya habari, watu wa ushirika wawaache wanunuzi waende na hela zao, wakakae pale, wapime pamba wao waweke record kwamba wakulima wao wameuza kiasi gani, wawaandalie maghala, wakute pamba iko kwenye maghala wawakodishie nyumba kama zinakodishwa huko vijijini, wawatengenezee mazingira ambayo wanunuzi wetu hawatasumbuka kununua pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachokisema niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, kwamba hela italiwa, itaenda kufanya nini, no, hela haitaliwa. Serikali yote, kuanzia Wakuu wa Mikoa nchi nzima huko pamba inakolimwa, Wakuu wa Wilaya, Wakurungezi wa Halmashauri wanaochukua cess kutoka kwa wakulima hawa ni lazima wawepo huko pamba inakouzwa kujiridhisha kwamba utaratibu unakwenda ambako si mkulima au mfanyabiashara anayepata hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo tutalisimamia Waheshimiwa Wabunge, si kwamba ni kitu impossible, kinawezekana, tutawasimamia. Msitie mashaka sana na dhamira ya Serikali, tumesema tutasimamia tutawasimamia, ushirika ule wa wizi ule hatuna namna ya kujiridhisha kwamba tumeukomesha kama hatuanzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tuna-fear of the unknown. Walishatuibia tunajua na namna walivyokuwa wanaiba, tukaja hapa Bungeni tukarekebisha sheria, sasa hivi wanafungwa. Zamani hakuna mtu alikuwa anaiba Nyanza anafungwa, sasa hivi jaribu kuchukua kitu cha Nyanza uone utakakoishia. Nimesikia hapa mchangiaji mmoja anasema huko TANECU sijui wapi wameiba pesa, wameiba pesa na watafungwa tu, si wameiba pesa? Imethibitika wameiba? Sheria tunayo mkono kwa nini tusiwapate hawa? Tutawapata watafungwa na kufilisiwa mali zao, ndicho kinakachofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mmoja Mkuu wa Mkoa wa Mara alisemaje, tunapenda kweli mtu ajaribu kuibia wakulima ili aone tutakachomfanyia. Hata mimi natamani nimpate mmoja atakayeenda kudokoa hela ya pamba aone, tumtoe mfano, kwani kuna tatizo gani kumtoa mfano? Tunamtoa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeiti, na jambo la pili kwenye pamba Waheshimiwa ni ile shilingi 100. Shilingi 100 ndugu zangu mtakumbuka tu Bunge lililopita hapa wakati wa kupulizia dawa Waheshimiwa Wabunge wote mnaotoka maeneo ya pamba mlikuwa mnadai viuatilifu vimechelewa, viuatilifu hakuna, jamani Wizara inafanyaje, pamba inakufa, pamba inakufa. Tumechukua hatua extra ordinary kupata hivyo viuatilifu, tumenunua chupa milioni saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Serikali ilikuwa bilioni tatu kwa viuatilifu vya mazao yote. Pamba tu iliyozalishwa kwa wingi namna hii msimu huu ilikuwa inahitaji viuatilifu vya bilioni 30. Sasa tungejifunga kwenye bajeti ya Serikali leo tungekuwa na pamba ambayo tunazungumzia? Tumeenda tumezungumza na benki yetu ya kilimo imetoa LC kwa makampuni ya kuagiza dawa, wameagiza dawa hiyo ni commitment ya benki, imetoa pesa zake sasa italipwaje hiyo pesa? Bajeti ya Serikali ilikuwa shilingi bilioni tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunahitaji pesa kutoka kwa waliotumia hiyo dawa ili tuilipe benki iliyotukomboa. Nataka niipongeze sana Benki ya Kilimo, kwa hili wametusaidia kweli kweli. Kwa sababu wangejielekeza na wao kama benki ya biashara nyingine yoyote wakasema tunataka collateral tunataka nini…, leo pamba ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tunayoizungumza isingekuwapo. Sasa tunataka pesa ya kuwalipa, Mheshimiwa Kiswaga shilingi 30 walikatwa wakulima mwaka jana ndiyo, makadirio ya zao ilikuwa ni tani laki moja, mwaka huu tumekwenda tani laki sita, mwaka kesho dhamira yetu ni tani milioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaweza kweli tukatoka kwenye shilingi 30 ya kuhudumia tani 100,000 tukaenda kwenye shilingi 60 ya kuhudumia tani milioni moja. Tunahitaji fedha na tuwe nayo mapema ili kuwaandalia wakulima mazingira ya kulima. Hakuna itakayempendeza hapa ikifika mweziJanuari, mwaka kesho hakuna dawa ya pamba nchini, nani atafurahi wakulima? Wetu tunawafahamu kutoa fedha mfuko kwenda kununua bomba ni issue. Kwa hiyo, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge, 30 zitatumika kulipa deni na hizo bilioni 20 tutaziweka tena benki kama cash cover ili watukopeshe fedha nyingi zaidi. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge, wakulima wanaelewa sana dhamira ya Serikali. Naomba niwahakikishie, mimi nilikuwa Igunga wakati tunazindua msimu, Mheshimiwa Kafumu ni shahidi yangu. Tulipoeleza haya wananchi walipiga makofi kwa sababu wanakuwa na uhakika. Si wananchi wetu wote wanao uwezo wa kutunza fedha kusubiria kuwekeza tena katika kilimo, lazima Serikali ichukue nafasi yake. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge hii hela haiendi kulipa madeni ya nyuma, sijui ya iliyokuwa mfuko wa pamba. Haiendi kulipa hayo, huko bado hatujaelewana nao nani alisababisha hayo madeni. Tunataka tumjue huyo alipeleka wapi hizo fedha. Kwa hiyo, hii pesa inakwenda kwenye hayo mambo matatu mbegu, dawa na mabomba, na kuna hela kidogo sana ambayo pia ni lazima tuipeleke kwa ajili ya watafiti wetu wa pale Ukiriguru. Vinginevyo hii hela inarudi kwa wakulima wenyewe kwa manufaa yao itasimamiwa na Bodi ya Pamba. Bodi ya Pamba ni chombo cha Serikali. Wanatumia fedha kwa kanuni za fedha za Serikali, akidokoa fedha tunaye. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge niombe sana mniruhusu tu niendelee na hiki kilimo, mipango si mibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo moja tu lingine labda ambalo kwa haraka haraka kwa ruhusa yako, naomba niwatoe hofu Wabunge wa eneo la kati hapa la nchi yetu. Ilisemekana kwamba korosho hapa haifai kulimwa na kadhalika. Watafiti wetu na tunao ushahidi, tulikuwa tumeomba mngeweza kuona kwenye screen pale jinsi korosho inavyostawi vizuri Mkoa huu wa Dodoma na Mkoa wa Singida. Korosho inastawi vizuri Kongwa kiasi kwamba inazaa mara mbili kwa mwaka. Hiyo ni korosho inayozalishwa huko Singida. Nimuombe tu mdogo wangu na swahiba wangu Mheshimiwa Ditopile anielewe tu kwamba mimi nina wataalamu waliobobea, a center of excellency ya korosho duniani iko Tanzania, dunia nzima wanakuja kujifunza kwetu korosho. Sasa tusiwakatishe tamaa watafiti wetu, wanafanya vizuri na nitumie nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru sana, wanachokifanya ndicho hicho wanachostahili kupongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho inastawi Singida, korosho inastawi Dodoma na hii tunawapa option wakulima wetu, wakilima mtama hali ya hewa ikawa mbaya wawe na pa kuangia, angalau kwenye korosho. Wakilima mahindi yakakauka wawe na angalau na kilo mia moja za kuuza waende sokoni wanunue mahindi. Tusiwaache tu kwamba wakilima zao moja likashindikana basi wao ni watu wa kwenda kupiga hodi kwa Mkuu wa Wilaya kuomba pesa au kuomba mahindi ya msaada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.