Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutufikisha hatua hii.

Pia nichukue fursa hii kuwapongeza Mawaziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Waziri, Dkt. Tizeba, pamoja na Naibu wake, kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ndani ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa kusema machache katika mambo yaliyoonekana yako ndani ya Wizara yetu ya Fedha. Nianze na jambo la kwanza kabisa kusema kwamba kama Wizara ya Fedha tunatambua umuhimu wa Wizara ya Kilimo kwenye ukuaji wa uchumi wa taifa letu na tumekuwa tukiipa kipaumbele cha kutosha kabisa Wizara hii ya Kilimo kama ambavyo bajeti yetu imeonesha, kwa dhati kabisa tunatambua mchango wake na tutaendelea kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee tu kusema Waheshimiwa Wabunge, jambo la msingi tunalotakiwa kuelewa; katika mchakato wa kibajeti na katika theory ya uchumi ambayo ni ya kawaida kabisa, tunatambua mahitaji yako mengi kuliko rasilimali (resources) tulizonazo. Tukilitambua jambo hili tutaweza kwenda sambamba na bajeti ambayo Serikali imependekeza, la msingi tuweke nguvu kwenda kwenye utekelezaji wa bajeti tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende specific kwenye hoja, nayo ilisema ni asilimia kumi, Maputo Declaration au Malabo Declaration kwamba Serikali ifike huko. Nimeanza kusema kuwa resources ziko chache kuliko mahitaji tuliyonayo. Sote kwa pamoja tuko hapa tumeanza kupitisha bajeti hizi, tulianza na bajeti ya afya tukasema iongezwe, bajeti ya maji iongezwe, lakini la msingi tukubali tu kwamba Serikali inatambua umuhimu na inawapa kipaumbele cha uzito wa juu sana wakulima wetu wa taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tunafahamu kabisa kuwekeza katika sekta ya kilimo ni jambo la kwanza, lakini pia uhalisia uliopo. Sekta ya kilimo ni nani wawekezaji? Wawekezaji kwenye sekta ya kilimo ni wawekezaji binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini sana kama Mheshimiwa Dkt. Tizeba ana mashamba ya kupeleka pesa moja kwa moja. Tunachokifanya kama Serikali kuiwezesha sekta hii ni kuziwezesha sekta nyingine ambazo zinafanya kazi pamoja na sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tunasema Serikali ya vitu badala ya Serikali ya watu, si sahihi hata kidogo. Niliwahi kusema ndani ya Bunge lako tukufu kwamba barabara zetu zimewezesha sasa hivi chakula kinaweza kutembea kwenye mkoa unaozalisha kwenda kwenye mkoa ambao hauzalishi, na ndiyo maana limesemwa pia hili, kwamba tunazuia kuuza mahindi nje, na Mheshimiwa Waziri atalisemea vizuri ili ku-control mfumuko wa bei, hapana, mfumuko wa bei una-attributes zake ambazo zinachangia kwenye mfumuko wa bei, chakula ni sehemu moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa nini chakula ndani ya Tanzania kinachangia kwa kiwango kikubwa, ni kwa sababu Taifa letu limeweza kufunguka kwa miundombinu ambayo Serikali ya Chama cha Mapinduzi imewekeza kwa kiwango kikubwa. Unaweza ukasafiri kutoka Mbeya ukafika Arusha ndani ya siku moja kwa sababu ya miundombinu. Kwa hiyo, twende tu kwa pamoja tuelewe uchumi unafanya vipi kazi ili tuweze kwenda wote kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ya Kilimo ilisema kuhusu uwekezaji kwenye Benki yetu ya Kilimo (TADB). Tulianza kuwekeza shilingi bilioni 60 na mpaka sasa hivi niwapongeze uongozi wa Benki ya TADB, katika shilingi bilioni sitini waliyokuwa nayo, sasa hivi wana shilingi 66,785,790,000 wameweza kuongeza kiwango hiki katika utendaji wao wa kazi. Vilevile kama Serikali pia hatukuiacha wazi, tumechukua mkopokutoka TADB na kuonesha tunathamini wakulima wetu, bilioni mia mbili na sita zote tumezipeleka kwenye benki yetu ya kilimo. Dhamira ni ileile moja, kuwawezesha wakulima wa Tanzania ili waweze kufikiwa na benki yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama ambavyo nimekuwa nikiliambia Bunge lako tukufu kwamba Benki ya Kilimo inajiandaa mwezi huu wa tano inafungua tawi hapa Dodoma, mwezi wa sita inakwenda kufungua tawi Mbeya, mwezi wa tisa inafungua tawi Mwanza. Dhamira yetu ni ya dhati, kuwafikia wakulima wetu kule walipo ili waweze kupata huduma hii. Pia katika benki zinazofanya kazi na wakulima ni Benki yetu ya Kilimo. Popote mkulima alipo akishaonesha interest anahitaji mkopo anatembelewa kule alipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kengele imegongwa, naomba nilisemee jambo moja, nalo ni kuhusu Bodi ya Korosho na pesa ambazo zipo. Ni sahihi, pesa ipo na Serikali iko tayari kuitoa lakini lazima tukubali itolewe kwa mfumo upi na inakwenda kufanya nini, hilo ni jambo la msingi sana. Tunalalamika hapa kuhusu utendaji mbovu wa watendaji wetu, lazima tusimame imara wote kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoa shilingi bilioni kumi kwa sababu tumejiridhisha zinakwenda kufanya kazi ya Bodi ya Korosho, zilizobaki kama Wizara tunaendelea kuzihakiki, na kwa sababu tulishawapa Bodi ya Korosho mwongozo wa nini cha kufanya, wametuletea mahitaji yao na sisi tunaendelea kuhakiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape mfano tu ndugu zangu umuhimu wa hiki ambacho Serikali yetu inafanya, umuhimu wake ni huu, katika maombi tuliyoyapokea kutoka Bodi ya Korosho, nichukulie kipengele kimoja cha pesa za utafiti. Katika pesa za utafiti walikuwa wameomba shilingi bilioni 7.2, katika shilingi bilioni 7.2 kwa ajili ya utafiti, ndani ya pesa hizi kulikuwa na pesa ambazo haziendi kufanya kazi ya utafiti, sasa ni jambo la ajabu kusema kwamba Serikali tuachie, tupeleke tu kwa sababu sheria inatuelekeza hivyo. Tumepewa dhamana ya kuangalia pesa za nchi yetu. Mfano wa hizi shilingi bilioni 7.2 maombi yalikuwepo na shilingi bilioni 2.8 zinazokwenda kuwalipa honorarium watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo dhamira ya pesa ya utafiti kutumia shilingi bilioni 2.8 kwenda kuwalipa honoraria watumishi, lazima tumeaminiwa na Serikali yetu kusimamia rasilimali fedha ya taifa letu. Tujiridhishe, hii honorarium inayoenda kulipwa, kila mtumishi kwa honorarium hii anakwenda kulipwa shilingi milioni 19 kwa mwaka kwa ajili ya honorarium tu, hapana, tujiridhsihe anakwenda kufanya kazi gani ya ziada inayomuwezesha kulipwa. Tulianza kubana matumizi na mafanikio ya kubana matumizi tunayaona kwenye maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo moja nalo ni kuhusu malipo ya watu wa pembejeo. Waheshimiwa Wabunge wamesema vizuri sana; mchanganyiko wanaousema wao ndio ambao Serikali tuliupata, na ili kuondokana nao nani kaiibiwa Serikali katika maombi haya? Vyombo vya uchunguzi vipo kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waheshimiwa Wabunge, sisi kama wasimamizi wa rasilimali za taifa hili tusimame wote kwa pamoja. Vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yao. Mheshimiwa Kunti, vyombo vya uchunguzi ni muhimu sana, kama ni watumishi wa Serikali waweze kujulikana nani aliongeza sifuri kwenye shilingi milioni 20 ikawa shilingi bilioni mbili, lazima tuweze kukubaliana na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAKUKURU ikijiridhisha, tukipata taarifa yao, Serikali iko tayari. Pesa si tatizo kwa Serikali ya Awamu ya Tano, tutatoa pesa tutawalipa wote ambao wanaidai Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.