Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Zubeda Hassan Sakuru

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo ni sekta ya muhimu sana katika ukuaji wa uchumi hasa katika mapinduzi ya viwanda. Ni ajabu sana kuona kuwa hakuna msisitizo mkubwa kwa sekta ya kilimo hasa ukizingatia kuwa hata mapinduzi makubwa ya viwanda duniani yaliyotanguliwa kwanza na mapinduzi ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo ni sekta muhimu, siyo katika uzalishaji wa malighafi, bali pia katika kutoa ajira hasa ukizingatia kuwa vijana ni wengi kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 ambayo imeweka wazi kuwa zaidi ya asilimia 52 ya idadi ya watu ni vijana. Hivyo Serikali ilitakiwa kutenga bajeti yake siyo tu kutekeleza sera yake ya viwanda, bali pia kuweka mkazo katika sekta ambayo inatatua changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado zipo changamoto kubwa ambazo zina athari kubwa na za moja kwa moja kwa sekta ya kilimo na ukuaji wake hasa miundombinu. Nchi yetu ina changamoto ya kijiografia. Kwa mfano, Mkoa wa Ruvuma una changamoto kubwa ya miundombinu hasa kwa Wilaya ya Mbinga, Nyasa, Namtumbo, Tunduru na hivyo kuleta changamoto ya masoko hasa kipindi cha masika. Hivyo Wizara hii inatakiwa kuweka mkakati wa pamoja na sekta ya miundombinu ili kuwezesha ukuaji wake na kuendeleza wananchi kiuchumi. Je, ukakasi wa kuweka miradi ya pamoja kukuza sekta hii muhimu unatoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa Mkoa wa Ruvuma ni mojawapo ya mikoa yenye kuzalisha kwa wingi mazao ya kibiashara na chakula. Hivyo tulitegemea iwe mojawapo ya mikoa yenye ukuaji mzuri wa kiuchumi, lakini hali ni tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kutoa majibu kuwa mbaazi ni nzuri kwa chakula, leo mwananchi wa Tunduru aliyewekeza kwenye mbaazi akitegemea soko la dunia, anadhihakiwa vipi kwa soko la mbaazi kushushwa na kauli za kisiasa? Ipo haja ya Wizara ya Kilimo kuwanasua wakulima hasa wanaotegemea jembe la mkono kwa kuwaunganisha na masoko na siyo kuwafanyia dhihaka pale wanapozalisha ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kuona kuwa Wana Ruvuma wanazalisha mazao ya kibishara na chakula lakini hawanufaiki na kilimo. Upo usemi unaosema kuwa mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe. Je, nguvu kiasi gani itumike ili Mtanzania aweze kunufaika na kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo linatakiwa kutazamwa kwa jicho la ziada ili kunusuru wakulima, nalo ni soko la mahindi. Nia njema ya Serikali iko wapi ikiwa NFRA haipewi fedha za kutosha na hivyo kupelekea kununua sehemu ndogo tu ya mahindi yaliyozalishwa nchi nzima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Ruvuma ambao kwa sehemu kubwa wakulima wamelima mahindi kiasi cha kuwa na ziada lakini kutokana na uwezo mdogo wa NFRA, leo mkulima anabaki na ziada ikumuozea shambani bila kuwa na uhakika wa soko. Hata kama Serikali inasema itajenga maghala kuhifadhi ziada (surplus), bado bei ya soko la mahindi haiwezi kumpa mkulima wa mahindi uwezo wa kurejesha gharama za uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa NFRA imeshindwa kununua mahindi, kuna ugumu gani wa Serikali kutoa kibali kwa wananchi kuuza mahindi kwa kuwa NFRA inanunua inachoweza kuhifadhi (ikiwemo kuwauzia WFP na private traders) lakini bado kiasi cha mahindi yaliyovunwa inabaki mikononi mwa mkulima na kuleta hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mkulima wa mahindi anufaike, ni aidha Serikali iongeze bajeti ya NFRA iweze kununua mahindi kwa bei nzuri ama/na kuamua kutoa uhuru kwa mkulima aliyezalisha ziada auze kwa bei ya soko la nje ambalo kwake ni nguvu yake mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. Siungi mkono hoja.