Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na kesi ya miti, miti inalalamika inakatwa, tunamalizwa, tunamalizwa, mwisho wake ikakaa kikao ikabaini kwamba nani anatumaliza ni shoka. Baadae wakasema shoka hili nani analileta ni mpini. Mpini si ni sisi humu tuliomo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna tatizo Wabunge wanalalamika, wananchi wanalalamika pamba kuuzwa kwenye ushirika. Kwa hiyo, wananchi wamegundua wanaopeleka hili jambo kwenye ushirika ni akina nani, ni viongozi tuliowatuma kwa maana ya sisi Wabunge pamoja na Serikali. Maana yake ni nini? Badala ya kufika mahali tukaona kwamba tunapaswa kuwatetea wananchi lakini hatuwatetei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ushirika Wabunge wamelalamika wasikilizeni, viongozi wa ushirika waliochaguliwa si wale tuliokuwa tunawatarajia. Wahasibu waliochaguliwa ni wale waliotumia rushwa kupita. Maana yake ni nini? Maana yake wanakwenda kuwaibia wakulima pamoja na wanunuzi wa pamba, hili jambo halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba iliyoko kule ni ya kukopa wakulima kwamba washirika wakusanye pamba halafu ipelekwe kiwandani, baada ya kupimwa kiwandani ndipo mkulima alipwe, siku ngapi hizo? Kwa nini tuliweka soko huria? Tuliweka soko huria kwa sababu wananchi wetu waliteseka, hili jambo haliwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukaliangalia upya, wananchi wanalalamika sana na sisi ndiyo viongozi na sisi ndiyo watu wa kuwasemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niishauri sana Serikali kwamba tumechelewa kwa sababu washirika waliokwenda kuchaguliwa wamechaguliwa na bodi ya watu wachache, watu saba/kumi wale washirika wangeweza kuchaguliwa na mkutano wa hadhara tungepata watu wanaostahili. (Makofi)

Kwa hiyo, hili jambo tungelifanya mwakani halafu sasa tukaruhusu mfumo wa soko huria ukafanya kazi. Mtawapa shida ma-DC, mtawapa shida Wakuu wa Mikoa, hakuna kazi watakayokuwa wanaifanya bali kulinda tu wezi wa ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu katika mkokotoo wa soko ni kweli bei iko hivyo, lakini makato yameongezwa. Tunapokwenda kuulipa ushirika shilingi 45 halafu shilingi 33 inabaki kwenye AMCOS, shilingi 12 inakwenda ushirika (union), hivi tunawasaidia wakulima? Kwa nini hata hiyo shilingi 12 tusiiache kwenye kijiji? Kama kijiji kimeuza kilo 800,000 sawa na shilingi 9,600,000 hizo zitanunua madawati, zitajenga zahanati ili watu waone impact kweli hata ya kurudisha ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashauri, jambo hili tunalipeleka kwa kweli wananchi hawako tayari, wananchi hawa hatujawashirikisha, jambo hili limetoka juu halijashirikisha wananchi. Naomba tushauri tubaki na soko huria kama ilivyokuwa mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia uwezo wa ushirika, kama kituo kitanunua kilo 40,000 kwa siku tunazungumza shilingi ngapi? Tunazungumza shilingi 44,000,000 kwenye kituo kimoja; je, fedha hizo zina ulinzi na ni vituo vingapi, tuna polisi wangapi wa kulinda fedha hizo? Tunapeleka maafa kwa wakulima na benki, hili jambo linapaswa litazamwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tuliingia kwenye soko huria? Tuliingia kwenye soko huria baada ya Vyama vya Ushirika kushindwa. Hivi vyama kama nilivyotangulia kusema mwanzo vimejigeuza kuwa vyama ambavyo hata Waziri Mkuu hukuhitaji hivyo, Waziri Mkuu ulihitaji AMCOS ziundwe kutokana na wakulima wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa washirika tunaokueleza Mheshimiwa Waziri Mkuu wengine, hawana hata shamba wala pamba, sasa mtu anakwenda kumnunulia mwingine ambaye hata zao hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo msipoangalia Mheshimiwa Waziri na Serikali, wapo viongozi/watendaji wanashauri vibaya, wanataka ku-sabotage Serikali na hili litakuja litugharimu sisi kama wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kwenye mkokotoo; kwenye mkokotoo ni sahihi lakini ile shilingi 100 ingepungua. Mwaka jana tulikuwa na shilingi 30 ya kuendeleza zao la pamba, inakuwaje tunaweka mara nne/tuna-double mara nne kwa nini tusiende kwenye shilingi 60? Hii shilingi 60 tumeijaribu tukaona haiwezi kulipa madeni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali iliangalie hili, ione ili angalau tukokotoe vizuri tumuongeze mkulima ili angalu mkulima mwaka kesho aweze kulima vizuri kama ambavyo wameitikia mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanalalamika mahindi hapa, mahindi haya bila kuweka utaratibu mwaka huu yataoza. Ni vizuri Serikali ikafungua mipaka ikaachana na suala la vibali ili watu waweze kusafirisha nje ya nchi waweze kuuza haya mahindi na mahindi haya yakiuzwa ndio uchumi wenyewe unaozunguka… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)