Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Sixtus Raphael Mapunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara ya Kilimo. Nianze mchango wangu kwa nukuu maarufu sana iliyopendwa kutumiwa na Marais wawili wa Marekani kwa nyakati tofauti, Ronald Reagan na Abraham Lincoln naomba niisome hiyo nukuu; “You can not strengthening the weak by weakening the strong.” Kwa Kiswahili kisichokuwa rasmi ni kwamba “hauwezi ukamuimarisha mtu aliye dhaifu kwa kumdhoofisha aliye imara.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo ndiyo sekta imara kuliko sekta zote kwenye nchi yetu. Ni sekta pekee inayoongoza kwenye pato la Taifa kwa ripoti sahihi na statistics zinatuambia inaongoza pato la Taifa kwa asilimia 26.1 ikifuatiwa na viwanda asilimia 7.3, sekta ya madini asilimia 4.1 na sekta ya utalii asilimia 3.1 kwenye kuzo la pato la Taifa. Pia sekta hii ndiyo sekta inayoongoza kwa kuajiri Watanzania wengi zaidi ya asilimia 70, sekta hii ndiyo inayoongoza kwa export zaidi ya asilimia 85, sekta hii ndiyo inayoongoza kwa kutuhakikishia chakula kinapatikana nchini kwa asilimia 100. Pamoja na uimara wa sekta hii, tukaiangalia report ya Waziri mwanzo mpaka mwisho hatuoni sekta hii ikiimairishwa zaidi tukiona ikidhoofishwa kwa expense ya sekta nyingine, hii haiwezi ikawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa Tanzania wanahitaji matumaini, wamefikishwa sehemu wamekata tamaa kabisa. Wamekata tamaa katika eneo la uzalishaji, wamekata tamaa katika bei, wamekata tamaa katika mfumo mzima wa kilimo kuanzia mazao ya chakula mpaka mazao ya biashara hakuna zao hata moja ambalo tunasema hili ni salama, kila zao lina tatizo. Tulitarajia leo hii angalau tupate njia ya kutokea, lakini hatuoni matumaini katika sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri inasema kwa makadirio mwaka huu tunaweza tukazalisha mahindi tani milioni nane, maana yake itakuwa imepanda kwa tani milioni mbili kutoka mwaka jana milioni sita sasa tunakwenda milioni nane lakini uwezo wa NRFA kununua mahindi, wana uwezo na wamepanga kutumia tani 28,200 tu. Tafsiri yake tutakuwa na tani zaidi ya milioni saba hazitanunuliwa na NRFA, maana yake ili kiwepo chakula wakulima wa mahindi, lakini sisi kule kwetu nenda ukaanzie Rukwa, Katavi, Iringa, Mbeya, Njombe na Ruvuma wote katika ujumla wetu hatulimi mahindi tu kama chakula, tunalima vilevile mpunga unakubali, viazi vinakubali, ndizi zinakubali na mihogo inakubali. Ukituambia tule mahindi tu tusiuze maana yake unataka tufe kwa kwashakoo, kitu ambacho si sawa! Lazima hii sehemu iliyobaki ya mahindi tani milioni saba Waziri uje hapa na mchanganuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati za hizi tani 2,220 zitakazonunuliwa na NFRA utuambie una mpango gani wa soko la nje, una mpango gani kwa kiwango gani pia kwa kiwango kitakachobaki kitumike kama chakula ndani ya nchi yetu.Vinginevyo mimi sitakuunga mkono kwenye hoja hii na wakulima hawatanielewa nikikuunga mkono kwenye huo mchanganuo uliouweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la kahawa bado tunaendelea kuumia, tunaumia katika maana ya uhakika wa soko, tunaumia kwa maana ya uhakika wa pembejeo, tumeomba kwa muda mrefu sana Serikali ijaribu kutazama pembejeo kwenye zao la kahawa, kwa sababu ni zao la muda mrefu lilikuwa linatuletea fedha za kigeni kwa kiwango kikubwa sana, lilipoanza kusuasua vyama vya ushirika vilivyokufa na Serikali ilipoondoa mikono na miguu ndipo tulipoharibikiwa. Leo hii tunashukuru sana Waziri Mkuu kwa ziara alizofanya kwenye maeneo ambayo tunalima kahawa kwa kweli tumeona dhamira ya dhati ya Waziri mkuu kurudisha vyama vya ushirika viende kwenye mazao ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliopo site, mashaka tunayoyaona kwenye vyama vya ushirika ni makubwa, leo hii hawa watendaji wa vyama vya ushirika ndiyo walioshiriki kuviua miaka hiyo ya nyuma. Tunakwenda mwezi ujao kwenye msimu ujao, wakulima wa pamba wanalalamika watalaam hawapo, wakulima wa kahawa tunalalamika wakulima wa korosho tunalalamika, watumbaku tunalalamika, tutakwendaje? Katika huu muda mfupi katika crash program tunaiomba Serikali ipeleke watalaam kama kweli tunataka tufufue ushirika. Vyama vya Ushirika haya mazao ambayo mwaka huu tumeyahamasisha tumezalisha kwa kiwango kikubwa tunayahifadhi wapi? Kwa mfano pamba, consumption ya pamba yetu ndani kabla ya uzalishaji ilikuwa only 20% viwanda vyetu vya ndani vinaweza kuchakata, asilimia 80 tulikuwa tuna-export tumehamasisha pamba imezalishwa kwa wingi, tutaiweka wapi? Lazima kuwe na mkakati wa dharura vinginevyo tutakuja mwakani hapa tena tutaanza kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho naomba niseme kuhusu pembejeo, tumelalamikiwa sana kuhusu mawakala wa pembejeo wametiwa umaskini, wametoa huduma lakini hakuna tamko la Serikali linaloelezea haki yao watapataje? Kama hawajafanya kitu kizuri basi ieleweke, nani kakosea na nani kapatia, kuwaweka jumla tu kwa muda mwaka wa miaka miwili wakazika hela yao tunatengeneza umaskini uliokithiri, umaskini uliopitiliza. Lakini niseme neno moja Serikali ikiimarisha bei nzuri ya haya mazao hatutahiji mbolea ya rukuzu kwa sababu mbolea ya rukuzu inakuja kwa kuchelewa lakini muda mwingine inakuja hailingani na udongo wa eneo husika. Tungekuwa na utaratibu wa kununua mazao ya wananchi vizuri kwa bei nzuri tusingepata shida...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)