Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami niweze kuchangia Wizara hii ya kilimo, lakini naomba niseme tu kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi hatujajua tatizo liko wapi na ndiyo maana wakati mwingine tunamlalamikia Mheshimiwa Tizeba. Hiyo Wizara tukimweka hata Waziri Mkuu ndiyo awe Waziri wa Kilimo kesho tu mtamuondoa kwenye Wizara hiyo kwa sababu tatizo kubwa ninaloliona ni mtiririko wa fedha usioridhisha. Suala la mtiririko wa fedha usioridhisha si la kumlaumu mtu mmoja, mimi nailaumu Serikali ya Awamu ya Tano (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Tano, ukiangalia kuanzia bajeti ya mwaka 2015/2016 fedha za maendeleo zilizokuwa zimetengwa ni shilingi bilioni 32.7 lakini zilizotolewa ni shilingi bilioni 5.1 sawa na asilimia 16. Mwaka 2015/2016 aliyekuwa Waziri ni Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Bajeti ya mwaka 2016/2017, fedha za maendeleo zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge ni shilingi bilioni 101.5 lakini fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 3.3, sawa na asilimia 3.3. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018, bajeti hii ambayo tunaimalizia sasa, zilitengwa shilingi bilioni 150.2 zilizotolewa ni shilingi bilioni 27, sawa na asilimia 18. Hapa ndipo naposema kwamba hoja hapa si suala la mtu mmoja ni Serikali ya Awamu ya Tano tangu imeingia madarakani haina mpango, haina mkakati wa kuwasaidia wakulima wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize, tumesema kwamba mapato yanaongezeka, makusanyo yanaongezeka, haya makusanyo yanayoongezeka kwa nini hampeleki kwenye Wizara ya Kilimo? Makusanyo yanaongezeka hatuoni lakini kila siku tunaambiwa makusanyo yameongezeka. Serikali ya Awamu ya Tano naona ni tatizo kubwa na lazima tuchukue hatua sisi Waheshimiwa Wabunge wote bila kujali itikadi ya vyama vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niweze kuzungumzia hoja ya pili ambayo ni kununua kahawa kupitia vyama vya ushirika na nimesikia tunaanza msimu huu kwa kahawa, pamba pamoja na mazao mengine. Suala hapa ni kwamba vyama vya ushirika vilishakuwepo siku za nyuma, kulikuwa na ubadhirifu wa hali ya juu sana na kulikuwa na wizi, je, Serikali imewakamata wale wezi walioiba siku za nyuma? Je, hawa wezi kwa sasa hawapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye zao la kahawa kulitokea jambo moja ambalo ni la ajabu sana. Wakulima wanauza kahawa mwezi wa saba wanakuja kupewa fedha baada ya miezi sita wakati mwingine baada ya mwaka mmoja, malipo yanacheleweshwa. Je muarobaini wa matatizo haya umeshapatikana? Kulikuwa na mambo mengi sana ya ajabu. Watu waliuza majengo ya vyama vya ushirika, waliuza mali za vyama vya ushirika, kwa sababu Serikali hii ya Awamu ya Tano imekuwa ni Serikali ya mizuka, imekuja bila kufanya angalau tathmini, tumekimbilia jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na vikundi vya wakulima ambavyo vilikopa fedha Benki, wakanunua CPU kwa ajili ya kuboreshea zao la kahawa, hizi fedha atakayelipa ni nani leo tunakwenda kwenye vyama vya ushirika? Hizi CPU watapeleka wapi? Tusipochukua hatua makini kwenye hili tutakwenda kuangukia pua muda si mrefu. Nachoshauri katika hili, hivi vyama vya ushirika vinavyoanzishwa kwenye kahawa, pamba na mazao mengine tungesitisha kwanza, tuweke kipindi cha mpito, tuweze kufanya tathmini vizuri baada ya hapo tuvianzishe tukiwa tayari tumeshatafuta muarobaini wa matatizo ambayo yamewahi kujitokeza siku za nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu masoko ya mazao. Nimesikia Waheshimiwa Wabunge hapa wanalalamika sana mahindi, mahindi; ndipo sasa msingi wa ile hoja yangu ya kwanza kwamba shida ni Serikali ya Awamu ya Tano inapokuja. Ni kwamba, tatizo si mahindi peke yake, angalia kwenye suala la mbaazi. Mbaazi ilikuwa inauzwa kilo Sh.2,000, leo inauzwa Sh.150, Sh.120 hadi Sh.80 naambiwa hapa. Mbaazi inalimwa Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Lindi, Mtwara, Morogoro na maeneo mengine ya nchi, watu wengi wameshindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao lingine lenye changamoto ni tumbaku. Leo navyozungumza msimu wa tumbaku unakwenda mwingine lakini tumbaku iko kwenye maghala haijanunuliwa, hali ni mbaya sana. Tumbaku inalimwa Katavi, Tabora, Ruvuma pamoja na maeneo mengine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao lingine ndiyo hili la mahindi. Kule kwetu Mkoa wa Songwe mwaka mmoja na nusu uliopita tuliuza debe moja la mahindi Sh.20,000. Hivi navyozungumza na wewe debe la mahindi linauzwa Sh.3,000, kutoka Sh.20,000 limefika Sh.3,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ni mengi yenye changamoto, nenda kwenye kahawa hali ni mbaya, nenda kwenye ufuta, tuliuza Sh.3,000 leo ni Sh.1,000 na kitu . Kwa hiyo, hapa Serikali ya Awamu ya Tano ndiyo mliosababisha matatizo haya na mimi naamini mwarobaini wa haya ni
Serikali hii kuweza kupisha ili Serikali mbadala iweze kuingia na iweze kushika dola kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la pembejeo. Bei ya pembejeo ya mbolea imekuwa ghali sana. Hivi navyozungumza, Mkoa wa Songwe DAP inauzwa Sh.59,000, Urea inauzwa Sh.55,000 lakini bei elekezi ya Serikali mwaka jana, tuliambiwa Mkoa wa Songwe tungeuza Urea kwa Sh.41,500. Kutoka Sh.41,500 leo ni Sh.55,000.

TAARIFA . . .

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba umeniamuru nifute, nitafuta kwa sababu umeniamba nifute. Hata hivyo, naomba nimwambie tu ndugu yangu Mheshimiwa Mapunda kwamba kuna kitu kinaitwa Tatu Mzuka. Sasa ikiwezekana kama ingeweza kumpendeza waambie hata Vodacom wakafute neno Tatu Mzuka na inawezekana hajajua maana ya neno hili. Kwa hiyo, nimeshafuta kwa sababu umeniambia nifute lakini akaangalie maana ya neno hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia bei ya pembejeo, kwa mfano, mbolea kuwa ghali sana. Serikali imeweza kutoa bei elekezi kwenye mbolea ya Urea na DAP lakini bei hiyo elekezi haijafuatwa. Tunasema kwamba DAP kwa Mkoa wa Songwe na maeneo mengine iuzwe Sh.54,000 leo inauzwa Sh.59,000. Mbolea ya Urea kutoka Sh.41,500 leo inauzwa Sh.55,000. Mimi naona muarobaini wa suala hili ni kujenga viwanda vyetu, tuache sasa kuagiza mbolea na hapa ndipo tutakapoepukana na matatizo hayo. Tutakuja na mambo mengi sana, tutakuja na mikakati mingi sana lakini bila kujenga viwanda vyetu vya mbolea; kulikuwa na mkakati wa kujenga Kiwanda cha Mbolea kule Lindi kule Kuisni, kiwanda kile kimefikia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Taifa letu ni vipaumbele. Tunasema kwamba tunataka kuboresha kilimo tunapeleka pesa kwenda kununua Bombardier, fedha hizi tungeweza kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea. Tunajua kwamba bila kuanzisha viwanda vya mbolea, bila kuboresha kilimo hata viwanda vingine vitayumba kwa sababu malighafi ya viwanda vingine zaidi ya asilimia 70 inategemea kwenye kilimo. Nashauri tuanzishe viwanda vyetu vya mbolea kama nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu uchache au uhaba wa rasilimali watu kwenye sekta ya kilimo. Kwa utafiti walioufaya ANSAF mwaka 2013 watumishi wanaohitajika kwenye sekta ya kilimo ni 19,228, watumishi waliopo ni 8,756.