Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon Munira Mustafa Khatib

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MUNIRA M. KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kupata nafasi kuchangia jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake na timu yake yote, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa hotuba nzuri ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kauli yake ya kusema sasa suala la mafuta ndani ya nchi yetu siyo tatizo. Naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuwa katika ufunguzi wa Kiwanda cha Singida alisema kuwa viwanda vya kuzalisha mafuta anaondoa VAT kwa asilimia 18. Naomba Serikali iniambie, imetekeleza vipi agizo hili la Mheshimiwa Rais kwa kuondoa VAT katika mafuta ya alizeti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka tufikie katika uchumi wa viwanda basi la kwanza ni kuvilinda viwanda vyetu vya ndani. Siyo viwanda vya mafuta tu, hata viwanda vyetu vya maziwa, tunaiomba Serikali iweze kuangalia suala hili ya VAT ya asilimia 18. Tutapoondoa asilimia hii 18, kwanza tutaweza kuongeza uzalishaji ndani ya nchi yetu, tutaweza kupunguza kuagiza mafuta ndani ya nchi yetu, tutaweza kuwasaidia wakulima wetu kimaisha ndani ya nchi yetu, hata pia tutaweza kuondoa tatizo la wafugaji kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kuhusu SIDO. Katika taarifa ya CAG, SIDO inaonekana iko katika hali mbaya. SIDO inafanya vibaya ndani ya mikoa yetu na Tanzania kwa ujumla. Mwaka 2017/2018 imepangiwa shilingi bilioni 6 lakini ndani ya pesa hii haijapatikana hata asilimia 1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira nyingi za vijana zinapatikana katika viwanda vidogo vidogo. Kama tungeisaidia vizuri SIDO basi tungeweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetembelea SIDO ya Iringa ina wafanyakazi watatu tu ambao wameajiriwa na Serikali. Hivi tutafikiaje uchumi wa viwanda na tunawasaidiaje vijana? Naiomba Serikali iangalie namna ya kuajiri watumishi wa SIDO ndani ya mikoa yetu na wazisaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO ina wafanyakazi watatu, waliobakia wote wanajitolea mpaka Mnunuzi Mkuu na Mhasibu ndani ya SIDO wanajitolea, hizi kazi zinaendeshwaje? Naiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri uko hapo, uisaidie SIDO ili kuweza kufikia katika uchumi wa viwanda. Kama hatuwezi kuzisaidia SIDO zetu, basi hatutaweza kusaidia uchumi wa viwanda. Ndani ya SIDO kuna mashine za miaka 70 kabla mimi sijazaliwa ndizo zinatumika mpaka leo. Naomba hizi pesa ambazo zimetengwa kwa ajili ya SIDO, zifike na zitolewe kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii FCC imekuwa tatizo sana kwa wafanyabiashara. Wamekaa kwa ajili kupiga penalty tu. Naiomba Serikali wangekaa na hizi taasisi wakawapa wafanyabiashara elimu. Wakienda sehemu za kuchukua bidhaa wajue ni bidhaa gani ambazo zinatakiwa ziingie ndani ya nchi yetu ili wasiwe wanachukua mzigo ambapo kisa tu haukuandikwa Sumsung au haukuandikwa iPhone ukifika ndani ya Tanzania mzigo ule ikawa ni kuharibiana biashara kwa kuchomeana moto. Tungekaa tukafikiria, kuna wafanyabiashara mpaka wanaumwa, wengine wanakufa kwa sababu ya hii FCC. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri akae basi aangalie Watendaji wake aweze kuwasaidia wafanyabiashara wengi. Juzi kontena nzima ya chupi imechomwa moto na FCC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vimebinafsishwa ambavyo vilikuwa haviwezi kufanya kazi.

Naiomba basi Serikali viwanda vile virudi katika mikono ya Serikali. Viko ambavyo havijabinafsishwa lakini vinamilikiwa na sekta binafsi na zipo share za Serikali. Naiomba basi Serikali ikaangalie viwanda hivi ili viweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi niliuliza swali hapa kuhusu Kiwanda cha Nguo cha Urafiki lakini sikupata majibu ya kutosha na ndani ya kitabu cha Mheshimiwa Waziri sikuona maelezo yoyote kuhusu kiwanda hiki. Naomba basi wakati anahitimisha aniambie suala hili la Kiwanda cha Urafiki limefikia wapi kuhusu zile shares ambazo tunazo na wenzetu wa China? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kiwanda cha Nyama Dar es Salaam, naomba Mheshimiwa Waziri akiwa anahitimisha pia aje aniambie. Pia kuna Kiwanda cha ZZK Mbeya, kilikuwa kinatengeneza vifaa vya kilimo. Naomba Mheshimiwa Waziri akija aniambie, kwa sababu mpaka sasa hivi wakulima wetu kutumia majembe ya mkono wakati sisi wenyewe tulikuwa tuna kiwanda kikubwa tu na hakifanyi kazi, itakuwa ni aibu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aniambie kuhusu viwanda hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la vinywaji vikali ambapo Serikali inapoteza kodi nyingi. Vinywaji hivi vikali vinakosa kodi kwa kubandika sticker bandia na hili suala kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameliongea na ushahidi upo. Naomba basi Serikali iangalie inapoteza mapato kiasi gani katika suala hili la kubandika hizi sticker bandia katika vinywaji vikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vinywaji vikali Serikali ingekuwa ina-charge ile spirit wakati inaingia hapa nchini badala ya spirit ikiwa imeshatumika ndani ya vinywaji vikali ndiyo inakuja kuchajiwa. Hizi spirit zinapoingia tu nchini zichajiwe. Kwa sababu hizi spirit zinachajiwa kwa kiwango kidogo tu zinazokwenda kwenye hospitalini na sehemu nyingine lakini kiwango kikubwa kinatumika katika vinywaji vikali. Kwa hiyo, Serikali ingekaa ikaangalia vizuri kwa upande wa spirit inapoingia nchini. Tusi-charge ndani ya vinywaji, bali tu-charge inapoingia tu ndani ya nchi yetu.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.