Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa dakika ulizonipa ni chache, lakini kwa kutumia taaluma yangu nitahakikisha nazitumia vizuri na naomba ridhaa yako nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutuwezesha kuwa hapa leo na kupata nafasi hii ya kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kikubwa zaidi, naomba ridhaa yako niweze kuishukuru Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisimamiwa na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo alichokifanya Waziri Mkuu leo humu ndani ni cha kihistoria cha kuhakikisha mafuta yanapatikana, sisi wengine ni wananchi tunaotokana na wazazi wenye kipato cha chini ambao tunatumia mafuta katika biashara ndogo ndogo na kutuwezesha kuishi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri Mkuu kila la kheri, Mawaziri wote kila la kheri pamoja na watendaji na Watanzania wote sasa


ambao tunakaribia kufunga mwezi wa Ramadhani na wale ambao hawatahitaji kuyatumia mwezi wa Ramadhani kwa kweli hii ndiyo nafasi yao.

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba unilindie dakika zangu. La pili, nadhani Mchungaji hajui lugha ya Kiswahili vizuri amezoea lugha ya Kichungaji, nimesema naomba nipongeze, sijasema naomba nichangie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia bajeti ya Wizara ya Maji. Nchi yetu awamu hii tunakwenda kwenye awamu ya viwanda, lakini pamoja na hayo tunahitaji maji ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu. Naomba Serikali iangalie uwezekano wa kutuletea maji maeneo mengi, Wabunge wengi humu ndani wamesimama wakielezea tatizo la maji kwenye maeneo yetu. Kwanza naomba wataalam wafike hadi kwenye miradi ya vijiji vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mradi wa Wilaya ya Kisarawe ambao umepata baraka za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba maji kutoka Ruvu Juu yafanyiwe utaratibu yaweze kwenda hadi Kisarawe. Mradi huo tayari taratibu zote zimeshakamilika, ni nini na ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa mradi huo na kitu gani ambacho kinakwamisha mradi huo mpaka leo usiweze kufanya kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji kwa Mkoa wa Pwani kwa kweli tukisema kwamba kuna maeneo maji hayapatikani inasikitisha sana kwa sababu mkoa wetu umezungukwa na mito mingi sana. Kwa mfano, Mto wa Rufiji maji yake yanamwagika hovyo, kwa nini usitengenezwe utaratibu wa kuutumia? Toka nimeingia ndani ya jengo hili nimekuwa nikiomba maji ya Rufiji yaweze kutumika maeneo mengine, haijawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna Mto Wami nao una maji mengi sana. Tatizo linakuja wakati wa mvua yale maji yanakuwa machafu kwa maana yanakuwa na tope nyingi. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu au itatengeneza utaratibu wa kuhakikisha maji yale yanasafishwa na kuweza kutumika kwa maeneo yaliyo jirani? Hakuna sababu sasa hivi maji ya kwenda Chalinze yatoke Ruvu Juu wakati Mto Wami uko jirani na Chalinze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kero ya maji ni kubwa sana kwenye shule zetu za msingi na maeneo ya huduma muhimu kama zahanati, vituo vya afya na hospitali. Kwa nini haya mashirika na idara za maji zilizopo zisipewe jukumu la kusimamia uvunaji wa maji ya mvua wakawezesha kuwapatia maji watoto wa shule, vituo vyetu vya afya na kwenye huduma muhimu? Maji ya mvua yakivunwa yanaweza kutumika kwa ajili ya wananchi na kuondoa kero ya maji na tumeahidi kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani japokuwa wanaume wakibeba maji wanauza, lakini shida ni ile ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la maji taka, mfumo wa maji taka Dar es Salaam siyo mzuri. Tunajua maji taka, mniwie radhi kwa kutumia hili neno, ni maji ya kinyesi au ya uchafu mwingine, lakini sasa hivi Dar es Salaam imefurika maji taka kweli. Machupa machafu yamo humo, mifuko ya rambo imo humo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)