Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kazi nzuri inayofanya kuhakikisha kwamba inatatua kero za wananchi wake japo kwa muda ambao imejiwekea. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake na Makatibu Wakuu kwa namna ya pekee ambavyo wanajituma kwenda kuwaangalia wananchi huko vijijini wanavyotaabika na huduma hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote hapa kila linapoulizwa swali la maji wanasimama nusu ya Bunge. Maana yake ni kwamba hakuna hitaji muhimu tofauti na maji kwa wananchi. Wananchi hawa wanapata taabu sana hasa wakati wa kiangazi. Mimi nimekwisha kusema hapa kwamba sisi tunayo maeneo ambayo wananchi wanapata shida lakini maji yako karibu. Kwa mfano, kijiji changu cha mwisho kule Mahaha, Tarafa ya Ndagalu ni kilometa 58 kutoka Ziwa Victoria, lakini mpaka leo tunazungumza hapa hakijaweza kupatiwa maji. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu nimeshampelekea andiko mara nyingi, nimeshazungumza naye lakini bado sijaona njia sahihi ya kuweza kutatua kero ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma sana kwenye kitabu hiki nimeona Tarafa ya Ndagalu yenye wakazi takribani 80,000 imetengewa shilingi milioni 100. Shilingi milioni 100 ni visima vitano tu vya maji ambavyo ni vijiji vitano. Hii tarafa ina vijiji 21, ni kubwa kama ilivyo Wilaya na Jimbo la Mheshimiwa Waziri. Ni tofauti sana, tunapozungumza hapa kuna majimbo na vijimbo, sisi tunayo majimbo na wengine mna vijimbo, mtuelewe tunapozungumza jambo hili. Tarafa moja tu inameza jimbo lako, lakini haina maji, lazima mtuelewe vizuri Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niombe sana tusiwe tunalalamika hapa tusaidieni kutatua kero za maji. Tukitatua kero za maji ndipo tutakapokuza uchumi wa Watanzania, uchumi wa wananchi wetu kwa sababu akina mama ndiyo wazalishaji wakuu, lakini wanapoteza muda mwingi sana kuchota maji na wala hawaendi tena kuchangia shughuli za kiuchumi. Kwa hiyo, niombe sana tatizo hili lishughulikiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewahi kusema hapa kwamba asali ni tamu sana na kila mmoja anatamani kuinywa, lakini wako humu watu hawanywi asali lakini kila mmoja anakunywa maji.

Kwa hiyo, mimi niombe sasa pamoja na kwamba inaonekana katika makusanyo yetu hatuwezi kutosheleza miradi ya maji tuje na mpango. Kama tumekuwa na mpango wa kununua ndege, tumekuwa na mpango wa kujenga standard gauge, kwa nini tusije na mpango wa kumaliza tatizo la maji? Kama ni kukopa shilingi trilioni tatu tukaondokana na tatizo la maji kwa nini tusikope? Tuamue kama Taifa, tuamue kama nchi kwamba hivi tukimaliza tatizo la maji, tukasogeza huduma kwa wananchi tutakuwa tumepunguza mambo mengi sana. Magonjwa yote yanayowasumbua Watanzania wetu yanatokana na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana Serikali hata kama siyo leo ndani ya miaka mitatu au mitano tuje na mpango wa kukopa tumalize tatizo la maji ili Wabunge waendelee kusemea mambo mengine ambayo yanaweza kusaidia. Jambo hili likifanikiwa kama ambavyo tumefanikiwa kununua ndege, kama ambavyo tumefanikiwa kujenga standard gauge, litaleta matumaini mapya kwa Watanzania. Kwa hiyo, nikuombe hili liendelee kusisitizwa na Serikali na iweze kuweka mpango muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza maji tunazungumzia uhai. Mji wa Kisesa wangu wa Kisesa, Jimbo la Magu ni mji mkubwa sana na nimesoma kwenye kitabu hiki nilitarajia kwamba nitaona mpango ndani ya miji ambayo inatekelezewa miradi ya maji lakini sijaona Mji huu wa Kisesa ukiwekewa maji. Kwa hiyo, niombe kama ambavyo tumeshaendelea kuzungumza na Waziri, kama ambavyo tumeshaendelea kuzungumza na Katibu Mkuu muone mipango ya miaka ijayo hasa mwaka kesho kuja na mpango madhubuti kuhakikisha kwamba maji katika Mji wa Kisesa yanapatiwa majibu. Kwa hiyo, niombe tu kwamba vijiji vyote hivi ni vizuri tukahakikisha kwamba tunaweka maji ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu skimu za umwagiliaji, ripoti inaonyesha tunazo skimu nyingi sana za umwagiliaji lakini ni skimu ambazo zinategemea hasa wakati huu wa masika ambazo zinakinga maji yale yanayotiririka kutokana na mvua nyingi, mvua zikikatika skimu hizi zinakauka. Ni vizuri tukaandaa skimu ambazo zitatumia mito isiyokauka, mabwawa yasiyokauka na ziwa ambalo haliwezi kukauka ili hizi skimu ziweze kuleta impact. Skimu zilizopo sasa hivi hazileti impact kwa sababu wananchi hawamwagilii wakati ambapo mvua haipo, zinasaidia tu wakati wa mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe na hili Serikali iwe na mipango madhubuti ya kuweza kusaidia ili tuweze kukuza uchumi hasa uchumi wa kilimo ambao kila mmoja wetu unamgusa na mwananchi wa kawaida unamgusa. Badala ya kupumzika muda mwingi aweze kuendelea kulima mazao ambayo atatumia skimu hizi za umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo hata tukizungumza leo tupeleke maji ya Ziwa Victoria hayatafika, yanahitaji mabwawa. Mabwawa haya yakichimbwa maeneo hayo ambayo ni kame zaidi yanaweza kusaidia sana katika umwagiliaji, unyweshaji wa mifugo lakini pia katika matumizi ya binadamu. Kwa hiyo, tunapozungumza mabwawa mtuelewe vizuri wale ambao tuko maeneo ambayo yana shida na maji. Kwa mfano, Bariadi, Kwimba na Maswa yote haya yana shida na ukame mkubwa sana ni vizuri tunapojenga hoja mtuelewe kwamba hawa watu wanahitaji kupata maji yanayostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasikitika sana, kuna msemaji mmoja hapa amesema Serikali imefeli, juzi tu tarehe 1, yeye mwenyewe amempongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi haina ubaguzi wa chama chochote inapeleka maendeleo kwa kila jimbo. Leo amejifanya tena kuwa mnafiki, hawa watu ni vuguvugu. Hayuko baridi, hayuko vuguvugu, huyu anapaswa kutapikwa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.