Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ingawaje dakika tano ni kidogo, ngoja nijaribu tuone.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya na Naibu wake. Ziara zenu zinaleta tija Mwenyezi Mungu awape afya, muendelee kufanya kazi kama mlivyoagizwa. Nimpongeze Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu kwa kazi wanazozifanya. Vumilieni tu kwa sababu lazima tuwaseme kidogo kwa sababu kwenye Idara hiyo, lakini kazi mnachapa na Mungu anajua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie hapa, ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye eneo la maji tumesema kutakuwa na wakala wa maji, ndani ya ilani, leo tunaelekea mwaka wa tatu. Mheshimiwa Waziri kitu hiki ni muhimu sana kwa sababu kila ukiangalia Wabunge wanaosema wengi siyo wa mijini waliokuwa wengi ni wa vijijini, ni wa vijijini kwa sababu pesa zile ziko kule chini ndani ya Halmashauri ndiyo wanafanya nao kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hali ilivyo Wizara yako ni inaingiliana na TAMISEMI, Engineer aliyeko kwenye Halmashauri ukienda kesho kwenye ziara akiwa ameiba wewe huna file lake, file lake liko TAMISEMI. Chochote kitakachofanyika kule chini utaenda utafanya ziara, wanaoamua ni watu wengine. Wakala huu unakuja kukusaidia ninyi, kwa sababu leo ukija mijini tunazo zile taasisi kwa maana kuna bodi, kuna ile taasisi iliyoanzishwa, mjini hakuna shida, lakini wakala huu ukipatikana utakusaidieni sana ninyi Wizara. Kwa sababu unavyoenda kwenye Halmashauri Mhandisi yule unaweza kumuwajibisha, kama siyo hivyo utaenda kwa Katibu Mkuu Profesa, Profesa amwambie Mzee Iyombe, hapa kama hakuna mahusiano ya karibu nayo ni shida. Kwa hiyo, neno wakala hii ni muhimu sana. Muende kwenye meza mjipange, mliandae lije huku wabariki ili mpate wepesi wa kazi zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwa utaratibu wa Madiwani tulivyokuwa tunaishi huko Mkuu wa Idara kumshughulikia, siyo rahisi ukatoka maji ukamshughulikia aliyepo TAMISEMI ni kazi ngumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naiomba Serikali yangu suala hili kwa sababu, liko ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi muende mezani mkae nao tuanzishe wakala huo ili uwape wepesi katika kazi zenu mnazofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niseme dogo hapa, katika Bunge lililopita hapa katikati kabla ya bajeti ndani ya Bunge hili tulikubaliana tuunganishe DAWASCO na DAWASA, ndani ya Bunge humu, ilipita hapa kwamba, DAWASA mpya azaliwe, lakini wachangiaji wengi humu wanasema mara DAWASCO mara DAWASA, hapana. Tulishakubali New DAWASA ipatikane, tuwape nguvu suala hili litekelezwe kwa sababu lilishapita ndani ya Bunge. Kwa hiyo, nakuombeni sana Wizara wala msirudi nyuma, yale mliyokwishayafikia undeni taasisi ili watu wa Dar es Salaam wapate maji kwa urahisi na watu wa Mkoa wa Pwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam pale kuna shida moja, wakati wanaleta maji kutoka Ruvu Juu, Waziri ulishanijibu siku moja hapa ndani kuna watu wamekataa kutoka kwenye miundombinu ya maji pale, wameenda Mahakamani wameshindwa, lakini mpaka leo tunavyoongea hawataki kubomolewa, kunaingia siasa, ninyi ni Wizara, isaidieni DAWASA, wale watu wavunjiwe ili watu wa Chuo Kikuu wapate maji, kwa sasabu mtu ameshashindwa Mahakamani anatakiwa kutoka, mpaka leo hajatoka analindwa na nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, nani anamlinda tusaidieni tu? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati unakuja kwenye majibu yako, hebu njoo na majibu tunafanyaje kuwasaidia hawa watu?

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii inatengenezwa na watu kutoka nje, wameshalipwa akifika pale anasimama anaanza kutudai Serikali alipwe fidia kwa sababu mmemchelewesha kumaliza kazi. Naomba Wizara mkija hapa mtuambie, kama mnaruhusu kwa sababu alishashindwa Mahakamani kwa mujibu wa sheria abomolewe mtamke wazi, ikishatamkwa sasa kule waulizwe kwa nini wale watu hawajaondolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme hili la jumla, ajenda ya maji kuna watu wanasema Tume na kadhalika, hebu mpeni Mheshimiwa Waziri huyu nafasi, amekuwa Waziri mwaka mmoja mnamuundiaje Tume? Alikuwa Naibu Waziri, ukiwa Naibu Waziri kama Mheshimiwa Aweso siyo mwenye Wizara. Huyu anao mwaka mmoja ndani ya Wizara leo unamuundia Tume, unaenda kufukua kaburi au unaenda kufanyaje. Tumpe nafasi, afanye kama anavyofanya na umri wake anajitahidi ili tumuunge mkono. Mpitishieni bajeti ili kipindi kijacho sasa kama liko jambo muweze kumuuliza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dakika tano sina uwezo wa kuzipanga, acha niseme hayo machache, naomba kuunga mkono hoja tu.