Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana mimi kuniruhusu nichangie hoja hii ya Hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwa muda huu mfupi niliopewa nitachangia mambo machache lakini muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa muhimu ni kuipongeza Wizara hii niliyofanya kazi nyingi sana kukuza elimu yetu nchini. Nampongeza sana Mheshimiwa Ndalichako na timu yake pia silisahau Baraza la Mitihani. Mimi nimefanya kazi Baraza la Mitihani kwa miaka 15 na naelewa kiasi gani tulipata taabu, miaka minne imepita hatujasikia mitihani imevuja. Jambo hili ni muhimu sana lieleweke kwamba Baraza limefanya kazi nzuri sana chini ya Mheshimiwa Waziri Ndalichako pamoja na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo ningependa kuchangia changamoto, mimi kwangu naona changamoto kubwa sana kwenye wizara hii ni lugha ya kufundishia. Mimi naelewa ziko nchi ambazo zimeendelea sana kwa sababu ya kutumia lugha ya kufundishia ambayo watoto wanaelewa. Kusema kiingereza sio elimu ni lugha tu. Mimi nimekaa Uingereza kuna watu hata kuandika hawajui wanajua kiingereza sana. Mfumo wetu wa elimu wa kufundisha darasa la kwanza mpaka la saba kiswahili halafu watoto wakahamia kiingereza secondary school au shule ya upili unaleta matatizo makubwa sana, wanafunzi hawaelewi masomo na hii ni kikwazo kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua sana kwamba kuendeleza kiingereza ni kuendeleza mambo ya kutawaliwa, kutumia lugha ya watu wengine. Sisi tumeweza kufanya vizuri sana kutumia kiswahili chetu pia tunasema kiswahili ni tunu ya Tanzania. Ningependa tunu hii ipewe heshima yake, ningependa mimi kuona watoto wanafundishwa kiswahili, wanaelewa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko nchi ambazo zimeendelea sana kwa mfano Uingereza wanatumia kiingereza, vile vile Uturiki wanatumia kituruki, Ufaransa wanatumia kifaransa, Ujerumani wanatumia kijerumani na wengine Waarabu wanatumia kiarabu na watoto wao wanaelewa vizuri sana. Lugha hii ni kikwazo kikubwa sana kwa kufundishia watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi hata kama tungepiga kura leo wangapi wangependa kusoma kiswahili. Watoto wanasoma kiingereza, shule ya upili na kuendelea huku chini msingi ni kiswahili wakimaliza shule na chuo kikuu, Bunge tunaongea kiswahili, Serikali inatumia kiswahili tunawaacha watoto hawa hawaelewi la kufanya. Pia liko tatizo na Mheshimiwa Ndalichako nimekuwa nasema mara kwa mara la kuondoa shule za ufundi. Tunaongelea Serikali ya viwanda hatuna mafundi, hatuna mfumo mzima mafundi sanifu na mafundi mchundo haupo. Watu wale wanaotoka VETA hawatoshelezi kufanya kazi ya ufundi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ndalichako nimekuwa nasema mimi ni zao la Chuo cha Ufundi Moshi (Moshi Technical College), Ifunda Technical College pamoja na Tanga Technical College.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ndilo jopo ambalo linafanya kazi viwandani. Itatupa taabu sana baada ya kuwaacha muda mrefu; fikirieni sasa hapa shule za kata na za sekondari, kila halmashauri itenge shule fulani zifundishe ufundi kwenye level ya form four itasaidia kupata mafundi vijijini hata wa kutengeneza mikokoteni ya ng’ombe na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya ufundi ndiyo key issue ya development ya nchi zote, hata Ujerumani wako vizuri kwa sababu wana mfumo huo wa ufundi ambao wanaweza kuongoza shuleni zao, sisi hapa tumepoteza nafasi hiyo. Mfumo uliokuwa unatumika zamani wa diploma engineers na engineers umekuwa ni kitu muhimu sana kwa Ujerumani, sisi tumeupoteza. Nimekuwa nikisema hapa, ilikuwepo system nzuri, imepotelea wapi? Naomba Serikali irejeshe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua ni jambo gumu kuishauri Serikali wewe mtu mmoja ikatekeleza lakini naongelea ndani ya Ukumbi wa Bunge hili, naomba Bunge lichukue umuhimu wake wa kuishauri Serikali. Serikali tafadhalini sana, nasema kwa uhakika, kwamba watu wote wanaofanya kazi viwandani sasa walitokea shule za ufundi ambazo sasa hazipo, imebakia Moshi Technical, Ifunda na nyingine zina masomo ya kawaida. Tumekwama hapo Mheshimiwa Ndalichako, naomba unisaidie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mimi napata taabu sana sana, nimetokea sekta binafsi, waajiri tumekuwa tunalalamika sana. Skill development training inatokana na uendelezaji wa ujuzi wa wafanyakazi. Kuiweka VETA chini ya Wizara ya Elimu ni misplacement, imepotoshwa kidogo, lakini najua inaingiza mapato Serikalini. Si vibaya hata kama VETA itabakia Wizara ya Kazi na Ajira, lakini hela ikaenda inapotakiwa kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi inakuwa vigumu sana sisi waajiri kufanya kazi ya kuchangia mfuko wa elimu ya juu ambao si hata tulilolenga ilipoanzishwa hii VETA. VETA ilianzishwa ku-develop skill za wafanyakazi wetu sisi tuliowaajiri si wanafunzi wenye elimu ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua tunasaidia lakini tume- misplace kitu kikubwa sana pamekuwa na ombwe kubwa ya tulichokitaka sisi. Mimi ningeshauri sana mjadili huko kwenye Serikali rudisheni hii VETA pale pale ilipokuwa zamani lakini hela kama zinatakiwa kwa ajili ya elimu ya juu ziende, lakini sisi tupeleke wafanyakazi wetu sehemu ambayo ni ya kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tungependa waajiri tupeleke wafanyakazi wetu VETA ambayo iko chini ya Wizara ya Kazi na Ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa muda huu siwezi kufanya jambo lingine tena. Nashukuru sana na ninaunga mkono hoja mia kwa mia.