Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Kwanza nianze kwa kusema kwamba kama Taifa tunahitaji mjadala mkubwa sana kwenye sekta ya elimu. Elimu yetu inapitia kipindi kigumu sana, elimu ya Tanzania inapitia kipindi kigumu na hili limethibitishwa hata na Rais wa awamu iliyopita Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete; na hili pia limethibitishwa na Rais ya awamu ya nyuma Mheshimiwa Benjamin William Mkapa. Tusiitazame elimu katika sura ya kutoa ajira peke yake ni vyema tukaitazama elimu katika sura pana hasa sura ya kichumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote ambazo ni magwiji kiuchumi siri kubwa wali-invest kwanza kwenye sekta ya elimu. Taasisi zote, mamlaka zote za kiuchumi na za kifedha zinathibitisha kwamba elimu ndiyo sarafu ya dunia. Kwa sasa tafsiri yake ni kwamba elimu ndiyo inayoshikilia uchumi wa dunia kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi nchi ambazo zimeshaendelea ambazo siri yao kubwa ni kwenye sekta ya elimu, wali-invest kwa kiwango kikubwa mfano ni China. Mwaka 1970 alikuwepo Rais mmoja anaitwa Deng aliwahi kupiga simu saa tisa usiku akampigia Rais wa Marekani Jimmy Carter akimuomba apelike wanafunzi 5,000 kwa ajili ya kupata mafunzo kwenye teknolojia kwenye vyuo vya teknolojia. Jimmy Carter kwa kuona umuhimu wa simu ile usiku akamwambia badala ya wanafunzi 5000 lete wanafunzi 1,00,000. Alifanya vile kwa sababu pia kwanza alihisi huenda kuna uvamizi kwenye nchi yake, lakini kwa umuhimu wa muda ule kupigiwa simu ile akaona yule mtu amethamini sana suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Trump analalamika kwamba China wanaiba teknolojia, anashindwa kujua kwamba ilikuwa ni mpango wa China wa miaka mingi baada ya wanafunzi kupelekwa Marekani kupata elimu. Dunia inakwenda kwa kasi sana, ni lazima tuende na kasi hiyo kwa sababu bila kufanya hivyo tutaendelea kuwa wasindikizaji. Nimesoma moja ya jarida la Harvard Business la Mei 2017 linaonesha kwamba kwa miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka jana kutakuwa na capital flight ambayo imeanzia Marekani ikaenda China sasa inatoka China inakuja Afrika, inakwenda kutengeneza ajira takribani milioni 85 mpaka milioni 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kama Taifa tumeandaaje vijana wetu kwa ajili ya fursa kama hii? Kwa sababu hii capital flight kwenye manufacturing sectors ambayo itakuja Afrika kama vijana wetu wangekuwa na uwezo ambao wakiwa skilled wakiweza ku-compete kwenye sekta ya ajira miongoni mwa vigezo vikubwa ambavyo vitaweza kutumika kwenye mitaji hii ambayo itakuja Afrika ni pamoja na wafanyakazi kwenye nchi husika wakiwa na wafanyakazi ambao watakuwa ni skilled. Ninasikitika kwamba kwa Tanzania tunaweza kukosa fursa hii kwa sababu ya kuendelea kupuuza sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali inapambana kutengeneza Stiegler’s Gorge, wakati Serikali inapambana kutengeneza standard gauge kama njia za ku-influence investment, don’t forget about education. Hii ni sifa mojawapo kubwa ambayo wawekezaji wengi wanaitumia wanapokwenda kuwekeza. Nisikitike zaidi kwamba elimu yetu imefikia hatua kwamba unaweza ukakuta kwamba graduate anashindwa kuandika hata sentensi moja kwa lugha ya kiingereza. Unaweza ukakuta graduate anashindwa kuandika barua ya kuomba kazi kwa Kiswahili anashindwa kuandika format haya ni majanga ambayo kama taifa tunaendelea kutia aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa ya kuishauri Serikali. Moja Serikali ni lazima muongeze juhudi za kufanya auditing kwenye education, mfanye ukaguzi wa kina, na uwe katika international standard kwa sababu kunaonekana kuna kizungumkuti sana kwa wakaguzi wetu hata hawa wakaguzi wanaofanya ukaguzi wanapashwa kufanyiwa ukaguzi pia, hii ni kwa sababu inaonesha kuna mapungufu makubwa sana katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo nataka kuishauri Serikali ni kwamba mchujo wa ufaulu wa wanafunzi ni lazima uzingatie uwezo wa wanafunzi, msifanye siasa kwenye hili. Leo division kesho GPA sijui kesho kutwa kitu gani!

Wale wanaostahili kufaulu wafaulishwe wale wanaofeli wafelishwe, tusianze kufanya siasa kwenye elimu. (Makofi)

Suala la tatu, Serikali lazima mu-invest kwa nguvu kubwa kwenye elimu ya kati, ile fedha ya skills development levy ambayo mmeitoa na kuipeleka kwenye mkopo wa elimu ya juu irudisheni VETA. Hii elimu ya kati inakufa, huu uchumi wa viwanda nani anaenda kufanya kazi hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu Serikali mnapaswa muwakumbuke. Moja ya vitu ambavyo Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Tano mnakosea ni kusahau walimu wetu. Serikali hii imepuuza walimu, Serikali hii inanyanyasa walimu, Serikali hii haioni mchango wa walimu, Serikali hii haioni kama kuna umuhimu wowote wa kuwasaidia walimu. Kenyatta hapa ameongeza asilimia tano mishahara ya walimu, ninyi mnaona walimu kama using machine, I don’t know mnawaonaje walimu wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba muwakumbuke walimu wetu hawa, muwakumbuke na muwathamni kweli kwa sababu wao ndio chanzo cha maendeleo yoyote ya kiuchumi kwa sababu kupitia elimu wanayoitoa tunaenda kupata watu ambao ni productive. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende sasa kwenye Chuo cha UDOM na na-decraire interest mimi ni mwanafunzi wa pale namalizia masters yangu pale. Hiki chuo kilikuwa kina mpango wa kusajili wanafunzi mpaka 40,000; lakini mpaka sasa wamesajiri wanafunzi 25,000 tu, na wanashindwa kufanya mwendelezo kwa sababu ya ninyi kwenda pale kuweka Wizara zenu sita. Haijulikani mnaondoka lini haijulikani mko pale, yaani hamjielewi. Chuo cha UDOM wakati kinajengwa planning yake haikuzingatia kwamba kuna Wizara sita zinakwenda kukaa pale, barabara ambazo ziko UDOM ninyi mnajua wanafunzi wanakoishi na madarasa yalipo kuna umbali wa kilometers… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)