Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kwanza hii niweze kuchangia katika hoja hii iliyoko mezani ya Waziri wa Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya elimu imekuwa inapitia mabadiliko makubwa sana katika kipindi cha miaka kumi mpaka 15 sasa. Kwa hiyo, ningependa kwa dhati kabisa nimpongeze Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya uamuzi ambao ni wa kijasiri wa kutoa elimu bure ya msingi. Huu ni uamuzi mkubwa sana kwa sababu katika hatua tuliyonayo sasa ya elimu Rais amekubali tupanue access na kwa kuanza ameondoa fees katika elimu ya msingi ambayo ni kuanzia darasa la kwanza mpaka form four. Kwa hiyo, pamoja na kupanua access kwa watoto wengi kupata elimu hii amepanua pia elimu ya msingi kutoka darasa la saba mpaka form four. (Makofi)

Napenda pia kwa nguvu hizo nipongeze viongozi wa Wizara ya Elimu na hasa binti yangu Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako kwa kazi nzuri sana anayoifanya katika Wizara ya Elimu. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Joyce, this is very good. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa labda ningetoa mfano huu wa access kwa sababu mwaka 2003 wakati mimi ni kipindi changu cha kwanza cha Bungeni hapa vijana waliomaliza O-Level (form four) walikuwa 46,000; mwaka jana vijana hao waliomaliza O-Level walikuwa wanakaribia 400,000; kwa hiyo, utaona access imepanuka kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza elimu hatua ya kwanza kabisa ni kupanua access, lakini sasa kilichoko mbele yetu baada ya kupanua access lazima sasa tujenge ubora katika elimu yetu, kwa sababu mahali tulipofika sasa tumefika mahali ambapo watoto wanafika darasa la saba wanaweza wasijue kusoma na kuandika. Watoto wanafika form four hawawezi kuandika barua, hivi sasa graduate lawyer hawezi kuandika judgment ya kiingereza. Kwa hiyo, hatua tuliyonayo sasa lazima tuweke mkakati wa kuboresha elimu yetu ili viwango vilingane na hii access ambayo imepanuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika level ya elimu ya msingi ukiangalia matokeo ya mitihani utakuta kwamba kwa miaka yote wala siyo miaka mitano wala siyo miaka sita, watoto wa darasa la saba wanaofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wanaofaulu mtihani wa hesabu hawazidi asilimia 17 kila mwaka ni hivyo na wanafunzi wanaofaulu mtihani wa Kiingereza katika ngazi hiyo ya msingi hawazidi asilimia 21. Kwa hiyo, kama watoto hawajui hesabu, kama watoto hawajui kiingereza ambacho sasa hatua inayofuata ndicho kinakuwa lugha ya kufundishia haiwezekani watoto hao waweze kupata elimu bora.

Kwa hiyo, jambo la kwanza ambalo tunatakiwa tufanye lazima tuangalie vitabu vinavyotumika, lazima tuwafundishe walimu wetu, tuwe na uhakika kwamba kweli Walimu hawa wanaofundisha wana stadi za kufundisha watoto katika ngazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano katika mwaka 2007 Wizara ya Elimu ilitoa mtihani wa hesabu wa darasa la saba wa mwaka 1994 ikawapa walimu wa Mkoa mmoja sitautaja ambao wanafundisha hesabu. Watoto wa Mkoa ule walifaulu kwa asilimia 17, lakini walimu waliokuwa wanafundisha hesabu wali-pass kwa asilimia 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi utaona kwamba tatizo siyo watoto peke yao na walimu hawana zile study zinazohitajika. Wizara sasa imefika wakati ichukue hatua katika kiingereza itengeneze vitabu vya kufundishia watoto. Sisi ambao tulifundishwa mwanzoni na vitabu vile vya kiada vinavyoitwa New Oxford English Course for Schools, tulijua kiingereza vizuri sana katika ngazi ile. Mimi sioni sababu gani vitabu vile visihaririwe upya na kuletwa vikafika level hii ya leo vikatumika kufundishia watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti umefanywa katika Wilaya ya Moshi Vijijini na umeonesha kwamba matokeo mazuri yanaweza kupatikana. Hivyo hivyo ni muhimu sana tuandike vitabu vipya vya hesabu vya kufundishia watoto, haikubaliki kwamba asilimia 17 tu ya watoto ndiyo wanaoweza kufaulu hesabu. Tuandike vitabu vipya, tunayo ile Taasisi inaitwa Institute of Education itumike na wataalam tulionao kwenye Vyuo Vikuu watumike kutengeneza vitabu hivi ili viweze kufundisha watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ngazi ya sekondari tumepanua sana na katika kupanua kuna vitu ambavyo tulifanya lakini bado. Katika ngazi hii wananchi walifanya juhudi kubwa sana ya kujenga zile shule za sekondari za kata. Walijenga kwa mikono yao wao wenyewe na walipata mafanikio makubwa. Ni muhimu tunavyoongea upanuzi wa elimu ya sekondari tuwapongeze sana wananchi wa Tanzania kwa kiu waliyokuwanayo na nguvu walizotumia kujenga shule za sekondari. Lakini bado ujenzi wa shule za sekondari haujakamilika, bado ujenzi wa shule za kata haujamalizika na hatua iliyofikiwa siyo hatua ya wanavijiji tena, hatua iliyofikiwa ni ya Serikali sasa kwa makusudi kabisa ichukue hatua ijenge maabara zote ambazo zimebaki katika shule za sekondari za kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu katika shule zangu 25, wananchi….

T A A R I F A . . .

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia.

Katika ngazi hizi za msingi maana yake, elimu ya msingi na elimu ya sekondari liko jambo lingine kuacha maabara ambalo ni muhimu sana na jambo hili ni Idara ya Ukaguzi wa Shule. Idara ya Ukaguzi wa Shule imekufa, hakuna ukaguzi maana yake kuna Wakaguzi lakini hawana bajeti, kuna ukaguzi lakini hawawezi kwenda shuleni kukagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu elimu ni kama bidhaa nyingine, sema hii ni bidhaa ya thamani kubwa kupita zote, wakati umefika sasa tungeunda commission wale walimu wote walioko kule kwenye ukaguzi wangekuwa kwenye Tume ya Ubora wa Elimu. Tungeunda Education Quality Control Commission ambayo itakuwa chombo huru chenye uwezo wa kuandikisha shule, chenye uwezo wa kukagua ufundishaji, chenye uwezo wa kuwasimamia walimu wanaofundisha na kama hawafanyi vizuri kuwateremsha cheo, wale wanaofanya vizuri kuwapandisha vyeo na shule zile ambazo zinafanya hovyo kabisa kuzifuta ili kuhakikisha kwamba elimu inapanda kutoka hapo ilipo inakwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu ya juu tumefanya maendeleo makubwa sana katika kupanua upatikanaji wa elimu ya juu. Sasa hivi tunavyo vyuo vikuu karibu 63, lakini hivyo vyuo vikuu sijui nisemeje maana yake viko very heterogeneous. Viko vyuo ambavyo ni vyuo vikuu kweli kweli, lakini viko vyuo vikuu ambavyo ungekuwa unahusishwa navyo ungesema jamani siyo mimi, mimi sitaki kukaa huko. Kwa maana hii vyuo vikuu ni lazima vikaguliwe very rigorously na hii commission yetu ya Vyuo Vikuu Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono lakini inaelekea yule dada alininyima dakika zangu sikupewa.