Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. OMARY M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo wa kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili niweze kusema machache katika bajeti hii ya WIzara ya Mambo ya Ndani. Awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu wake pamoja na uongozi mzima wa Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa sana. Sote Wabunge hapa katika Bunge hili tunakuja humu ndani na kutembea lakini amani na usalama wetu unategemea Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, mtu mwenye akili timamu na busara ni lazima asifie Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kesi chache chache tu ambazo kwa kweli kama Wabunge ni lazima tuziseme na ni jukumu letu kama Wabunge tushauri pale ambapo pana changamoto hizo. Kwa hiyo, ni ukweli usiopingika kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumza ni kulipongeza Jeshi la Polisi hususan Kitengo cha Magereza. Magereza wanafanya kazi nzuri sana hasa katika utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Viwanda.

Tumeona namna gani ambavyo wamefanya shughuli mbalimbali, mfano ni Karanga. Karanga wao wanatengeneza viatu, lakini tumeona katika hotuba hapa kwamba watu wa Jeshi la Magereza wanataka kuingia ubia na Mifuko ya Jamii kwenye Gereza la Mbigiri Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kuonesha kwamba Jeshi letu hususan Magereza na wao wako sambamba na Serikali yao kuonesha kwamba Sera ya Uchumi na Viwanda inakwenda vizuri zaidi. Hilo napongeza vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hotuba hapa nimesoma, nimeona kwamba mfungwa kwa siku gharama yake ni Sh.1,300/=, kum-retain mfungwa mmoja Gerezani kwa maana gharama ya chakula. Nasema, hivi kweli Magereza hawawezi kujilisha wao wenyewe? Tunao wataalam Magerezani mle; wanaweza kujenga majumba. Kuna kitengo hapa cha ujenzi. Hivi kwa nini hao wasi-compete tender na wengine kwa ajili ya kujenga shule, hospitali na kadhalika? Hili linawezekana. Magereza wana nafasi kubwa sana ya kuchangia uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Kamanda wa Magereza, hebu tuifanye Magereza iwe ni Magereza ya kisasa, iwe na wataalam, wawe ni sehemu ya kuchangia maendeleo ya nchi hii; wasitegemee sana ruzuku ili na wao waweze kusogeza gurudumu la maendeleo mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kuona hata baadhi ya Magereza, kwa mfano Ofisi za Magereza mikoani ziko katika hali mbaya sana. Nilipata fursa ya kwenda kwenye Ofisi ya Magereza Mkoa wa Tanga, nikawa najiuliza, hivi kweli hata kupiga rangi inahitaji ruzuku? Hii inachekesha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri kwamba tujiwekee utaratibu kutumia Magereza, wafungwa wetu waweze kufanya ukarabati wa Magereza yetu na taasisi mbalimbali. Tunawapa watu binafsi lakini nadhani Magereza wana nafasi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuzungumzia juu ya changamoto ya ukosefu wa Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi. Mheshimiwa Waziri, nilizungumza hapa siku moja kwamba Wilaya ya Kilindi ina takriban miaka 13 toka imekuwa Wilaya. Wilaya yetu haina Kituo cha Polisi, tunatumia kama post tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri na IGP yuko hapa, afanye ziara kuja Kilindi, aangalie ambavyo hata OCD hana nyumba ya kukaa; OCCID watumishi hawana. Hivi inawezekanaje, Polisi huyu aweze kuhudumia watu katika mazingira magumu kama haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, leo hii mahabusu pale hatuna. Leo mtu kama ana kesi pale inabidi apelekwe Handeni. Kutoka Kilindi hadi Handeni ni takriban kilometa 130. Maana yake tumewanyima haki wananchi hawa wa Kilindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye bajeti ijayo ahakikishe kwamba Wilaya ya Kilindi inatengewa kujengewa Kituo cha Polisi kwa sababu ni haki yao wananchi hawa kuwa na Kituo cha Polisi. Vile vile ni kwamba Wilaya ya Kilindi, tuna eneo takriban heka 100 ambazo tumetenga kwa ajili ya kujenga Gereza kwa sababu hatuna Gereza Wilaya ya Kilindi. Sasa eneo lile linaweza kutumika kwa ajili ya uzalishaji, pia litatupunguzia usumbufu wa kupeleka wananchi kutoka Kilindi kwenda Handeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo nimelizungumza mwaka 2017, nimeandika lakini namwomba Mheshimiwa Waziri, najua changamoto ziko nyingi, lakini nimeona hapa zimetengwa shilingi milioni 400 ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi. Namwomba sasa kwamba nasi mwakani kama siyo mwaka huu tuweze kutengewa kujengewa Gereza na Mahakama katika Wilaya ya Kilindi. Hilo linawezekana kwa sababu tunao mafundi, tunao wafungwa ambao wamefungwa katika Magereza yetu haya, ni mafundi wazuri tu maana yake tunaweza kutumia pesa hizo hizo kuhakikisha kwamba tunapunguza gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza ni suala la kulinda mipaka yetu. Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumza hapa, lakini ni ukweli usiopingika kwamba haiwezekani watu wa Home Affairs wasifuatilie wageni wanaoingia katika mipaka yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni kubwa, ni pana kwa hiyo lazima watu wa immigration wahakikishe kwamba wanatekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha kwamba kama wageni wanaingia lazima wafuatilie. Ni kitu cha kushangaza sana kama mtu anaweza kuhojiwa juu ya uraia wake, unasema kwamba watu wanafuatiliwa. Hilo jambo haliwezekani. Ni wajibu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba mipaka yetu inakuwa salama na watu hawaingii ovyo nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.